Mheshimiwa Spika, Awali
ya yote napenda kuchukuwa nafasi hii
kumshukuru Mwenyezi Mungu , ambae ametuwezesha sisi kukutana hapa katika
Baraza lako tukufu tukiwa katika hali ya uzima na afya njema. Lakini pia, ningependa kwa heshima na taadhima, nikushukuru wewe
binafsi kwa kunipa nafasi ya kusimama
mbele ya chombo hiki muhimu cha wananchi
kueleza maoni ya Kamati ya Maendeleo ya Wanawake, Habari na Utalii
kuhusiana na Bajeti ya Wizara ya Kazi, Uwezeshaji, Wazee , Wanawake na Watoto kwa
mwaka wa Fedha 2020/2021.
Mheshimiwa Spika,
kazi hii ya kupitia bajeti ambayo inalenga kuleta maendeleo katika nchi yetu, isingewezekana
kama tusingepata mashirikiano yako ya
dhati, pamoja na Wajumbe wangu wa Kamati
wakisaidiwa na Sekretariati ya Ofisi ya Baraza la Wawakilishi ambao kwa heshima naomba niwatambue kwa majina kama ifutavyo:-
1.
|
Mhe.
Mwantatu Mbarak Khamis
|
Mwenyekiti
|
2.
|
Mhe.
Mussa Foum Mussa
|
M/Mwenyekiti
|
3.
|
Mhe.
Makame Said Juma
|
Mjumbe
|
4.
|
Mhe.
Saada Ramadhan Mwendwa
|
Mjumbe
|
5.
|
Mhe.
Omar Seif Abeid
|
Mjumbe
|
6.
|
Mhe.
Mwanaidi Kassim Mussa
|
Mjumbe
|
7.
|
Mhe. Zaina
Abdalla Salum
|
Mjumbe
|
8.
|
Ndg.
Himid Haji Choko
|
Katibu
|
9.
|
Ndg.
Mussa Issa Mussa
|
Katibu
|
10.
|
Ndg.
Amina Abeid Hemed
|
Msaidizi
|
11.
|
Ndg. Azmina Hamad
Khamis
|
Msaidizi
|
Mheshimiwa Spika, Kamati ya Maendeleo ya
Wanawake, Habari na Utalii ya Baraza la
Wawakilishi , ilipata fursa ya kulifikiria kwa kulifanyia uchambuzi wa kina fungu la makadirio ya bajeti ya
Wizara ya Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Wanawake na Watoto ikiwa ni kutekeleza
matakwa ya Kanuni ya 96 (1) ya Kanuni za
Baraza la Wawakilishi Toleo la 2016.
Mheshimiwa Spika, kwa mantiki hiyo nachukuwa nafasi hii kukuarifu
kuwa kazi hiyo tuliifanya kwa umakini wa hali ya juu na leo hii tupo hapa
kukuwasilishia kazi tuliyoifanya kama
ilivyoelezwa katika Kanuni ya 96 (1) ya Kanuni
za Baraza la Wawakilishi Toleo la 2016 kwamba:-
Mheshimiwa Spika ,
kuanzia na ufafanuzi wa tathmini ya
jumla iliyofanywa na Kamati yangu kuwa
makadirio ya Makusanyo ya Wizara hii yamezidi
kutoka shilingi 1,039,464,000
kwa mwaka wa fedha unaomalizika hadi kufikia shilingi 2,108,555,000 kwa mwaka ujao
wa fedha wa 2020/2021. Hii ni dalili
kwamba Wizara imejipanga kuiongezea zaidi mapato Serikali, hatua ambayo Kamati yangu inaipongeza. Hata hivyo, Kamati yetu inaishauri wizara kuongeza bidii
zaidi ya utendaji ili kufikia malengo ya ukusanyaji wa mapato yaweze kufikiwa
kwani hadi tunapitia bajeti hii wizara imeripoti kufanikiwa kwa asilimia 58% ya makusanyo kwa mwaka huu wa fedha
unaomalizika.
Mheshimiwa Spika, Wizara pia imeonekana kuongeza makadirio ya
matumizi ya kazi za kawaida na kazi za Maendeleo , ingawa si kwa asilimia kubwa sana,
ambapo kwa mwaka wa fedha 2019/2020 ilikuwa ni shilingi 17,299,600, 000 ukilinganisha na makadirio ya mwaka wa fedha
2020/2021 ambayo ni shilingi 18,510,451,000
. Mheshimiwa Spika, ni imani ya Kamati kwamba ongezeko hili
la fedha limelenga kuleta ufanisi
katika kazi kwa Wizara hii na serikali yote kwa jumla.
PROGRAMU
YA UWEZESHAJI WANANCHI KIUCHUMI
Mheshimiwa Spika , Kamati
yangu inatoa pongezi za dhati kwa Wizara kwa kusimamia vyema utekelezaji wa
programu ya Uwezeshaji wa Wananchi Kiuchumi, kwani sote tumekuwa tukishuhudia uimarishwaji
wa mipango ya upatikanaji wa mikopo
nafuu ikiwa na lengo la kuimarisha kwa kuwajengea uwezo wajasiriamali
wetu. Aidha , Kamati inaridhika na juhudi za wizara za kuimarisha na kukuza hadhi za kiuchumi kwa
wazee, vijana, wanawake watoto na makundi mengine katika jamiii, suala ambalo limepelekea matokeo mazuri ya
viashiria vilivyowekwa katika utekelezaji wa programu hii.
Mheshimiwa Spika, Kamati yangu inaitakia
Wizara kila la kheri na kufanikisha mipango iliyojiwekea katika mwaka ujao wa
fedha ikiwa ni pamoja na kukusudia kutoa
mikopo 700 yenye thamani ya shilingi Milioni Mia Nane na Hamsini El (850,000,000) kwa lengo lile lile la kuwawezesha
wananchi wetu kiuchumi.
Mheshimiwa Spika, Kamati yangu pia inachukuwa nafasi hii kuipongeza Wizara kwa kusimamia mradi kwa vijiji
vilivyounganishwa kwa umeme wa jua ambapo tathmini ya mradi huo imebaini kwamba,
Mradi huo umewasaidia wananchi kung’arisha vijiji vyao na kuweza kuwasaidia
katika kuwawezesha watoto kudurusu masomo yao wakati wa usiku na kujiongezea
kipato kwa ‘Solar Mama’. Hata hivyo, Kamati inaishauri Wizara
katika malengo yake ya mwaka ujao wa
fedha, kuongeza idadi ya kinamama watakaowapatia mafunzo ya utengenezaji wa vifaa vya umeme wa
jua pamoja na idadi ya watakaowezeshwa
kujikwamua kimaisha kupitia kituo cha Barefoot Kinyasini Kibokwa, kutokana na umuhimu wa viashiria hivyo na
mafanikio yanayopatikana hasa vijijini.
PROGRAMU YA HIFADHI
YA JAMII NA MAENDELEO YA WANAWAKE NA WATOTO.
Mheshimiwa Spika, Kamati yetu pia imepata faraja kutokana na
azma ya Wizara ya kufuatilia uwezekano
wa kuanzisha Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi hapa Zanzibar. Kamati inaamini kwamba, uanzishaji wa mfumo
huo unaweza ukawa ni suluhisho la malipo ya Fidia kwa wafanyakazi
watakaoumia au kuuguwa wakiwa kazini. Mheshimiwa Spika, Kamati yetu iliwahi
kutembelea Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi wa Tanzania Bara na kubaini kwamba,
umekuwa ukiwasaidia sana wafanyakazi kwa
kugharamiwa matibabu kwa wanaoumia au kupata maradhi wakiwa kazini pamoja na
malipo kwa msaidizi wa mgonjwa.
Mheshimiwa Spika, Wizara
imeainisha viashiria kadhaa vinavyolenga matokeo mazuri ya Huduma za kuratibu masuala ya Kijinsia na Uendelezaji
wa Wanawake, ikiwa ni pamoja na kuendelea kuwapatia wanawake mafunzo ya kuelewa
haki zao, pamoja na kuwahamasisha kugombea
nafasi mbali mbali za uongozi na ngazi za maamuzi. Hili ni jambo zuri ukizingatia ya kwamba, hivi sasa tupo katika vuguvugu la kuelekea
Uchaguzi Mkuu wa mwezi Oktoba mwaka huu ambapo tutakuwa na chaguzi mbali mbali ikiwemo
Uwakilishi, Ubunge na Madiwani. Hapa tunachukuwa fursa hii kuiomba sana wizara kuifanya
shughuli hii haraka mara tu watakavyoingiziwa fedha, ili kuimarisha maendeleo
ya wanawake na kukuza muitikio wa kuelewa haki za mwanamke, ushirikishwaji na
uongozi. Tunawaomba waheshimiwa wajumbe sote tukubaliane na maombi ya Wizara
kwa kuidhinisha jumla ya shilingi 1,009,759,061
kwa ajili ya Programu ya Maendeleo ya Wanawake
na Kupinga Udhailishaji.
PROGRAMU YA
USIMAMIZI WA SHERIA ZA KAZI UKAGUZI
NA KAZI ZA STAHA KWA
WOTE
Mheshimiwa
Spika, Kamati ya Maendeleo ya Wanawake , Habari na
Utalii imeshangazwa na uamuzi wa Wizara wa kushusha makadirio ya matumizi kwa ajili ya utekelezaji wa Programu ya
Usimamizi wa Sheria za Kazi, Ukaguzi Kazi na Kazi za Staha kwa Wote kutoka shilingi 1,688,300,000 kwa mwaka wa fedha
unaomalizika hadi shilingi 1,484,900,000
kwa mwaka ujao. Kamati inadhani kuipunguzia fedha programu hii
wakati huo huo ikizidishiwa kazi ya kukusanya zaidi ni kuibebesha mzigo mkubwa
Kamisheni ya Kazi. Tunaishauri Wizara
iangalie tena mgawanyo wa fedha kwa taasisi zake ukizingatia ya kwamba Wizara
inategemea sana vianzio vya mapato vilivyochini ya Kamisheni ya kazi kwa ajili
ya mapato yake.
Mheshimiwa Spika, mwisho napenda nichukuwe fursa hii , kuipongeza Wizara ,
akiwemo Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri pamoja na Watendaji wake wote wa ngazi za juu, pamoja na wa ngazi
ya chini, kwa mashirikiano yao waliyotupa katika Muda wa wote wa kazi za Kamati
. Ni imani yangu kwamba mashirikiano haya yataimarishwa, ili kuleta ufanisi na kuweza kufikia lengo la
kuleta maendeleo katika jamii na Taifa kwa ujumla.
Nawashukuru
sana wajumbe wa Kamati yangu kwa kuniamini na mashirikiano makubwa waliyonipa
wakati wote nilipokuwa naongoza Kamati hii. Namuomba Mwenyezi Mungu awajaalie
mafanikio mema Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, ili kutimiza malengo yao
waliyokusudia na pia nawatakia kila la kheri wale wote tutakaojaaliwa kuendelea
kukitumikia chombo hiki muhimu cha wananchi.
Mheshimiwa Spika,
mwisho kabisa nakushukuru wewe binafsi kwa kuniruhusu nitumie muda wako adhimu ili kuwasilisha hotuba hii. Naamini
haya yote yanafanyika ili kuisaidia serikali
kufikia malengo iliyojiwekea ya kuleta maendeleo kwa wananchi wake.
Mheshiwa Spika,
naomba kuwasilisha.
(Mhe. Mussa Foum
Mussa)
Makamu Mwenyekiti
Kamati ya Maendeleo
ya Wanawake Habari na Utalii,
Baraza la Wawakilishi.
Zanzibar.
No comments:
Post a Comment