UTANGULIZI
1. Mheshimiwa
Spika; Naomba kutoa hoja kwa Baraza lako Tukufu likae kama
Kamati ya Matumizi ili liweze kupokea, kujadili na kuidhinisha Makadirio ya
Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Wanawake na Watoto kwa
mwaka wa fedha 2020/2021.
2. Mheshimiwa
Spika; Kwanza kabisa napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa
kutujaalia uhai na afya njema na kuweza kukutana tena kujadili Bajeti ya Wizara
ya Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Wanawake na Watoto. Kwa niaba ya Wafanyakazi wa
Wizara, Napenda kukupongeza Mheshimiwa Spika wa Baraza la Wawakilishi
kwa namna unavyoliongoza Baraza lako na kusimamia kwa dhati utekelezaji wa
Mipango ya Maendeleo na Bajeti za Serikali kufikia malengo yaliyokusudiwa ya
kuondosha umaskini kwa wananchi. Nachukua fursa hii pia kuwashukuru Naibu
Spika, Waheshimiwa Wenyeviti,
Waheshimiwa Wajumbe na Watendaji wote wa Baraza kwa namna wanavyotekeleza
majukumu yao kwa ufanisi.
3. Mheshimiwa
Spika; Napenda kumshukuru Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein kwa Busara, Hekima,
Maarifa, Weledi na Miongozo anayotupa katika kufanikisha utekelezaji wa
Shughuli za Wizara pamoja na kusimamia imara utekelezaji wa Dira 2020 na Ilani
ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi kwa vitendo ikiwemo kudumisha Amani na
utulivu. Sote ni mashuhuda wa namna Serikali ya Awamu ya Saba ilivyopiga hatua
ya Maendeleo katika kila nyanja.
4. Mheshimiwa
Spika; Kwa namna ya pekee napenda
kumshukuru Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Wanawake, Habari
na Utalii ya Baraza la Wawakilishi; Mheshimiwa Mwantatu Mbaraka Khamis; Mwanamke
Jasiri na Shupavu katika utekelezaji wa Majukumu yake pamoja na Wajumbe wake
wote, Makatibu wa Kamati na Wasaidizi wake kwa walivyofanya kazi na Wizara bega kwa bega bila ya kuchoka ili kuleta ufanisi wa kiutendaji. Michango na miongozo waliyotupa ililenga katika
kuimarisha ufanisi wa utekelezaji wa Programu zetu ili kuimarisha ustawi na
hifadhi ya jamii kwa wananchi na maendeleo yao.
5. Mheshimiwa
Spika; Aidha, Nampongeza kwa dhati Mheshimiwa Makamu wa
Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi na Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza
la Mapinduzi kwa jinsi wanavyozisimamia kwa ufanisi na umahiri mkubwa shughuli
za Serikali ikiwemo kumsaidia Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi kutekeleza Dira 2020 na Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha
Mapinduzi pamoja na kutupa maelekezo ya kitaalam katika kuimarisha ufanisi wa
utekelezaji wa kazi zetu. Maendeleo haya tunayojivunia ni kutokana na uongozi
wao imara, thabiti na mahiri. Namuomba Mwenyezi mungu awape umri mrefu Viongozi
wetu hawa Baraka, Busara na Maarifa ya kuendelea kutuongoza. Amin.
6.
Mheshimiwa Spika; Kwa niaba ya Watendaji wote wa Wizara ya Kazi, Uwezeshaji,
Wazee, Wanawake na Watoto napenda kutoa tahadhari kwa wananchi wote ya kuendelea
kujikinga na maradhi ya mlipuko ya Corona yaliyoingia hapa nchini na duniani
kwa ujumla. Nawasisistiza wananchi kufuata maelekezo yote yanayotolewa na
Serikali na Wizara ya Afya ya kujikinga na maradhi haya ikiwemo kunawa mikono
kwa sabuni kwa maji yanayotiririka kila wakati, kutumia visafisha mikono (hand sanitizer) na kudumisha usafi wa
miili na mazingira yanayotuzunguka na kuepuka
mikusanyiko isiyo ya lazima. Pia, napenda
kuwasisitiza wazazi na walezi kuwa karibu na watoto wao kwa kipindi hiki na
kutowaacha kuzurura ovyo mitaani kwani wanaweza kuathirika na maradhi haya.
Vile vile, Kuwasimamia kudurusu masomo yao.
7.
Mheshimiwa Spika; Mbali na Corona nawaomba wananchi waendelee na jitihada za
kupambana na vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa wanawake na watoto nchini. Jitihada zetu kwa pamoja zitatupelekea katika
kuvitokomeza kabisa vitendo hivi nchini. Tuendelee kushirikiana katika
kuelimishana, kuvipiga vita na kila mmoja atekeleze wajibu wake kwa nafasi
aliyonayo. Namuomba Mwenyezi Mungu atuondoshee mabalaa yote yaliyopo nchini. “Tushikamane! Kwa Pamoja Tutaweza”. Aidha nawaomba wananchi tuzidi kuchukuwa tahadhari za
kujikinga na maradhi ya miripuko ikiwemo kipindupindu na matumbo ya kuharisha
wakati huu wa mvua za masika zikiendelea kunyesha.
8. Mheshimiwa
Spika; Wizara ya Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Wanawake na
Watoto inaendelea kusimamia utekelezaji wa Sheria na Miongozo ya Kazi, kuratibu
upatikanaji wa ajira za staha hasa kwa Vijana, kuimarisha programu za
kuwawezesha wananchi kiuchumi na kuimarisha haki, ustawi, hifadhi na maendeleo
ya wanawake, watoto, wazee na watu wanaoishi katika mazingira magumu
zaidi. Pia, Wizara inasimamia na
kuratibu utekelezaji wa shughuli za hifadhi ya jamii na uzingatiaji wa masuala
ya jinsia katika Sera, Sheria, Mipango na Bajeti za Kitaifa, Kikanda na
Kisekta.
VIPAUMBELE VYA WIZARA
9. Mheshimiwa
Spika; Wizara ya Kazi, Uwezeshaji,
Wazee, Wanawake na Watoto kwa mwaka wa fedha 2020/2021 imejipangia kutekeleza
vipaumbele vifuatavyo:-
i.
Kusimamia
utekelezaji wa Sheria za Kazi na Kuratibu upatikanaji wa Ajira za Staha ndani
na nje ya nchi;
ii.
Kuimarisha
masuala ya Usalama na Afya Kazini katika Sekta Binafsi na za Umma.
iii.
Kukamilisha
Uandaaji wa Mfumo wa Taarifa za masuala ya Kazi.
iv.
Kukuza
Usawa wa Kijinsia, Kumwezesha Mwanamke na Kuendeleza Mapambano ya Kumaliza
Vitendo vya Ukatili na Udhalilishaji wa Wanawake na Watoto;
v.
Kusimamia
Ujenzi wa Kituo cha Kulea Wajasiriamali Pemba na kuimarisha uendeshaji kwa
Unguja.
vi.
Kuimarisha
Mfuko wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kwa kutoa mikopo yenye thamani ya hadi
Shilingi Milioni Kumi.
vii.
Kuanzisha
Mfuko wa Fidia Zanzibar.
viii.
Kujenga
Ukuta wa Nyumba ya Wazee Welezo.
ix.
Kuimarisha
uratibu wa Programu za Hifadhi ya Jamii na Hifadhi ya Mtoto.
x.
Kuimarisha Uendeshaji wa Kituo cha Kuzalisha
Vifaa vya Umeme wa Jua (Barefoot).
xi.
Kuimarisha uandaaji na utekelezaji wa Sera, Sheria,
Mipango, Uratibu na ufuatiliaji na tathmini wa shughuli za Wizara.
xii.
Kujenga Uwezo wa Wizara kutekeleza majukumu
yake kwa ufanisi.
MUHTASARI WA MATUMIZI KWA MWAKA 2019/2020
10. Mheshimiwa
Spika; Wizara ya Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Wanawake na
Watoto kwa mwaka wa fedha 2019/2020 iliidhinishiwa jumla ya Shilingi Bilioni Kumi na Saba,
Milioni Mia Mbili na Tisini na Tisa, Laki Sita (Tshs. 17,299,600,000) ambapo Shilingi
Bilioni Kumi na Tano, Milioni Mia Moja Thamanini na Tatu, Laki Tisa (Tshs. 15,183,900,000)
ziliidhinishwa kwa kazi za kawaida na Shilingi Bilioni Mbili, Milioni Mia
Moja na Kumi na Tano, Laki Saba (Tshs. 2,115,700,000) kwa kazi za Maendeleo.
Kati ya hizo, Shilingi
Bilioni Moja, Milioni Mia Nane Arobaini na Tisa, Laki Tatu Tisiini na Tisa
Elfu, Mia Mbili na Thamanini
(Tshs.1,849,399,280) ni kwa ajili ya kutekeleza Programu ya
Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi; Shilingi Bilioni
Kumi, Milioni Mia Nane na Thalathini na Saba, Laki Mbili na Thalathini Elfu,
Mia Nne na Arobaini
(Tshs. 10,837,230,440) kwa ajili ya kutekeleza Programu ya Hifadhi ya Jamii na
Maendeleo ya Wanawake na Watoto. Shilingi Bilioni Tatu, Milioni Sabiini na Nne, Laki Sita na Sabini Elfu,
Mia Mbili na Thamanini
(Tshs. 3,074,670,280) kwa ajili ya kutekeleza Programu ya Uendeshaji na Uratibu
wa Wizara ya Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Wanawake na Watoto na Shilingi Bilioni Moja, Milioni
Mia Sita Thamanini na Nane, Laki Tatu (Tshs.1,688,300,000) ni kwa ajili ya utekelezaji wa Programu ya
Usimamizi wa Sheria za Kazi, Ukaguzi Kazi na Kazi za Staha kwa wote.
11. Mheshimiwa
Spika; Hadi kufikia Mwezi Machi 2020, Wizara iliidhinishwa
matumizi ya jumla ya Shilingi Bilioni Kumi na Moja, Milioni Mia Nne Hamsini
na Saba, Laki Mbili na Thalathini Elfu, Mia Mbili Hamsini na Sita (Tshs. 11,457,230,256)
sawa na asilimia Sitini na Sita (66%) ya fedha zote. Kati ya hizo Shilingi
Bilioni Kumi, Milioni Mia Sita na Sitini, Laki Nane Sabini na Mbili Elfu,
Arobaini na Sita (Tshs. 10,660,872,046) sawa na asilimia Sabini (70%)
ya fedha zilizoidhinishwa zilitumika kwa Kazi za Kawaida na Shilingi Milioni
Mia Saba Tisini na Sita, Laki Tatu Hamsini na Nane Elfu, Mia Mbili na Kumi (Tshs. 796,358,210) sawa na asilimia Thalathini
na Nane (38%) ya fedha zilizoidhinishwa zimetumika kwa kazi za Maendeleo.
Mheshimiwa
Spika; Kati ya hizo, Shilingi Milioni Mia Nane na
Sabini na Mbili, Laki Nane Kumi na Nane Elfu, Mia Saba Sitini na Nne (Tsh. 872,818,764) zilitumika kwa ajili ya
kutekeleza Programu ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ambayo ni sawa na asilimia Arobaini
na Saba (47%) ya fedha kwa programu
hiyo. Shilingi Bilioni Saba, Milioni Mia Tano Tisini na Tatu, Laki Mbili Ishirini
na Tisa Elfu, Mia Tisa na Thamanini na Tatu (Tshs. 7,593,229,983)
zilitumika kwa kutekeleza Programu ya Hifadhi ya Jamii na Maendeleo ya Wanawake
na Watoto ambayo ni sawa na asilimia Sabini na Moja (71%). Jumla ya Shilingi
Bilioni Mbili, Milioni Ishirini na Mbili, Laki Tano Ishirini na Tano Elfu, Mia
Nne na Thalathini na Nane (Tshs. 2,022,525,438) zilitumika kwa kutekeleza
Programu ya Uendeshaji na Uratibu wa Wizara ya Kazi, Uwezeshaji, Wazee,
Wanawake na Watoto sawa na asilimia Sitini na Sita (66%) ya fedha za Programu
hiyo. Jumla ya Shilingi Milioni Mia Tisa Sitini na Nane, Laki Sita Hamsini
na Sita Elfu na Sabini na Moja (Tshs. 968,656,071) zilitumika katika
kutekeleza Programu ya Usimamizi wa Sheria za Kazi, Ukaguzi Kazi na Kazi za
Staha kwa wote sawa na asilimia Hamsini na Saba (57%) ya fedha kwa
programu hiyo. (Kiambatanisho namba 1
kinahusika).
MUHTASARI WA MAPATO KWA MWAKA WA FEDHA 2019/2020
12. Mheshimiwa
Spika; Wizara ya Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Wanawake na
Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 ilitarajiwa kukusanya mapato ya Shilingi
Bilioni Moja, Milioni Thalathini na Tisa, Laki Nne Sitini na Nne Elfu (Tshs. 1,039,464,000) kutokana na Ada za Usajili na Ukaguzi wa Vyama vya
Ushirika, Ada ya Ukaguzi wa Mikataba ya Ajira za Nje ya Nchi, Ada ya Ukaguzi wa
Maeneo ya Kazi na Vibali vya Kazi.
13. Mheshimiwa
Spika; Hadi kufikia Mwezi Machi 2020, Wizara
kupitia Kamisheni ya Kazi, Idara ya Ajira, Idara ya Usalama na Afya Kazini na
Idara ya Ushirika ilikusanya jumla ya Shilingi Milioni Mia Sita na Sita,
Laki Nne, Sabini na Tisa Elfu, Mia Nane na Saba (Tshs. 606,479,807)
kutokana na Ada za Usajili, Ada ya Ukaguzi wa Vyama vya Ushirika na Vibali vya
Kazi ambayo ni sawa na asilimia Hamsini na Nane (58%) ya Makadirio ya
Makusanyo (Kiambatanisho namba 2
kinahusika).
UTEKELEZAJI WA PROGRAMU ZA WIZARA KWA MWAKA WA FEDHA 2019/2020
14.
Mheshimiwa Spika; Kwa mwaka wa fedha 2019/2020, Wizara imetekeleza
Programu Kuu na Ndogo zifuatazo:-
PROGRAMU KUU PQ 0101: UWEZESHAJI WANANCHI KIUCHUMI.
Matokeo ya muda mrefu: Kila Mzanzibari anafanya
shughuli za kiuchumi za kumuwezesha kumudu mahitaji yake ya msingi.
Programu ndogo SQ010101: Mfuko wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi
Lengo
Kuu: Kuimarisha
upatikanaji wa Mikopo nafuu kwa Wananchi.
15. Mheshimiwa
Spika; Mfuko wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi unaendelea kufanya
shughuli zake za kutoa mikopo kwa Wananchi. Madhumuni ya Mfuko ni Kuwawezesha Wananchi wenye kipato
kidogo kupata mitaji ya kufanya shughuli za uzalishaji ili kujiajiri na kuinua
vipato vyao. Walengwa wakuu wa Mfuko ni Vijana, Wanawake, Wanafunzi waliomaliza
elimu ya vyuo vikuu, Vyuo vya Amali na Sekondari, Wastaafu na Watu walio katika makundi
maalum. Mfuko kwa mwaka wa Fedha 2019/2020 imetekeleza yafuatayo:-
·
Umetoa
mikopo 811 Unguja na Pemba yenye thamani ya jumla ya Shilingi Milioni Mia Saba Thamanini na Tisa, Laki Tatu na Arubaini na
Nane Elfu (Tshs. 789,348,000). Wilaya Nne za Pemba zimepata mikopo 330 yenye
thamani ya Shilingi Milioni Mia Mbili na
Thalathini na Laki Nne (Tshs. 230,400,000) na Wilaya Saba za Unguja
zimepata mikopo 481 yenye thamani ya Shilingi
Milioni Mia Tano na Hamsini na Nane, Laki Tisa na Arubaini na Nane Elfu (Tshs.
558,948,000). (Kiambatanisho namba 3
kinahusika).
·
Kati ya mikopo 811 iliyotolewa; Mikopo 461 yenye
thamani ya Shilingi Milioni Mia Tano na
Kumi na Moja, Arubaini na Nane Elfu (Tshs.
511,048,000) imetolewa kuendesha shughuli mbalimbali za kiuchumi kama vile
biashara za jumla na rejareja, utoaji huduma za kutuma na kupokea fedha, uuzaji
wa vinywaji baridi, uvuvi, viwanda vidogo vidogo, ufugaji, uchongaji na kazi za
mikono na Mradi wa kilimo cha Matunda na Mboga mboga umetoa mikopo 350 yenye thamani ya Shilingi Milioni Mia Mbili na Sabini na Nane na Laki Tatu (Tshs. 278,300,000).
·
Kati ya
Mikopo hiyo, Mikopo ya vikundi ni 223, na ya mtu mmoja mmoja ni 588. Kati ya
vikundi 223 vilivyopatiwa mikopo; vikundi 42 ni vya makundi maalum ya vijana,
wanawake na watu wenye ulemavu na vikundi vilivyobaki 181 ni vya mchanganyiko. Jumla
ya wajasiriamali 5,092 walinufaika na mikopo hiyo, Wanawake ni asilimia 53% na
Wanaume ni asilimia 47%. (Kiambatanisho
namba 4 na 5 kinahusika).
· Mfuko umefanikiwa kupata Shilingi Milioni
Mia Moja na Sitini na Moja (Tshs. 161,000,000) kutoka Mradi wa FEED THE
FUTURE wa Mboga Mboga na Matunda ikiwa ni moja ya mikakati ya kutunisha fedha
zake. Mikakati mingine ambayo imeuwezesha Mfuko kupata fedha za ziada ni uwekezaji wa sehemu ya fedha
zake katika Benki ya Biashara PBZ Ltd ambapo Mfuko ulipata faida ya Shilingi Milioni
Arobaini (Tshs. 40,000,000) na mkakati wa tatu ni kutoa mikopo midogo
midogo na ya muda mfupi wa miezi sita hadi tisa; hivyo kuwezesha kutoa mikopo
mingi kwa muda mfupi kutokana na kasi ya
mzunguko wa fedha za mikopo.
· Kwa ajili hiyo Mfuko umefanikiwa kuongeza kasi ya utoaji mikopo kufikia 811 yenye thamani ya Shilingi Milioni Mia Saba Thamanini na Tisa,
Laki Tatu na Arobaini na Nane Elfu (Tshs. 789,348,000) badala ya mikopo 650
yenye thamani ya Shilingi Milioni Mia Saba
(Tshs. 700,000,000) iliyojipangia.
Kwa kawaida Mfuko hutoa mikopo ya kuanzia 500,000 hadi Milioni 5,000,000 na
hutoa Mkopo kwa mujibu wa matakwa ya Muombaji baada ya kufanyiwa tathmini ya
biashara yake na uwezo wa kulipa Mkopo aliouomba.
· Jumla ya Shilingi Milioni Mia Nne
Kumi na Tatu, Laki Sita na Ishirini na Tisa Elfu (Tshs. 413,629,000) zimekusanywa
Unguja na Pemba katika kipindi cha Miezi Tisa kuanzia Julai, 2019 hadi Machi,
2020. Pemba imekusanya Shilingi Milioni
Mia Moja na Arobaini na Tisa, Laki Mbili Sabini na Sita Elfu na Mia Tano (Tshs.
149,276,500) na Unguja imekusanya Shilingi Milioni
Mia Mbili na Sitini na Nne, Laki Tatu Hamsini na Mbili Elfu na Mia Tano (Tshs.
264,352,500). Marejesho ni mazuri kwani kwa kila mwezi Mfuko umeweza kukusanya wastani wa Shilingi Milioni Arubaini na Sita (Tshs. 46,000,000) zaidi ya Milioni Sita
kila mwezi ya makisio ya kukusanya Shilingi
Milioni Arubaini (Tshs. 40,000,000).
·
Unaendelea kuwajengea uwezo wakopaji wote wanaopewa mikopo ili kuleta
ufanisi wa biashara zao. Pia, Mfuko umeandaa na kufanikisha ziara tatu za
wajasiriamali kujifunza (2 Unguja na 1 Pemba) ambapo wajasiriamali walipata
wasaa wa kuwatembelea wenzao waliofanikiwa katika shughuli zao za uzalishaji
kwa nia ya kujifunza kwa vitendo na kwa nadharia. Kwa upande wa Unguja
wajasiriamali 30 (Wanawake 19 na Wanaume 11) walitembelea wenzao wa Mkoa wa
Kaskazini kujifunza shughuli za kilimo cha viazi vidogo na kabichi na wengine
30 (Wanawake 17 na Wanaume 13) walienda Kibwegere Makunduchi Mkoa wa Kusini Unguja
kujifunza ulimaji wa tungule na matikiti maji.
· Vile vile,
ziara nyengine zilifanyika Kisiwani Pemba ambapo wakulima na wasarifu wa mazao
ya kilimo 31 (Wanaume 22 na wanawake 9) walitembelea wakulima wa Shehia ya
Chimba huko Micheweni. Wakulima walijifunza jinsi ya kutengeneza hodhi la
kuhifadhia maji kwa kutumia turubali na namna ya kuchagua mbegu kulingana na
hali ya hewa. Pia, walipata fursa ya kuiona mashine ya umwagiliaji maji
inayoitwa MWANAMEKA ambayo iliwavutia sana wakulima kwa kuwa haitumii umeme na
ina uwezo mkubwa wa kuvuta maji na kurahisisha shughuli za umwagiliaji.
· Kwa upande
wa mafunzo ya nadharia, Mfuko umetoa mafunzo ya kilimo bora (Good Agricultural
Practices) na masuala ya usimamizi wa Fedha, uwekaji wa Akiba, uimarishaji wa
bidhaa na elimu ya Masoko kwa wajasiriamali 1,061 (Unguja 446 na Pemba 615)
kati ya hao Wanawake 573 na Wanaume 488) kutoka katika Wilaya zote 11 za Unguja
na Pemba. Mafunzo yamewawezesha wajasiriamali kuzalisha bidhaa kwa wingi na
zenye ubora, hali iliyopelekea kuongeza mauzo na kurahisisha urudishaji wa
mikopo yao.
· Imewezesha
kikundi kimoja cha NURU TAILORING kilichopo Jumbi Wilaya ya Kati Unguja kuibuka
mshindi wa vikundi vinavyozalisha bidhaa za ushoni nchini yaliyoandaliwa na
Jumuiya ya Taasisi zinazotoa mikopo midogo midogoTanzania (TAMFI) na kupatiwa
zawadi ya US$1,000.
16. Mheshimiwa Spika; Kwa mwaka wa fedha 2020/2021; Mfuko
wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi umejipangia Kutoa mikopo 700 yenye thamani ya
Shilingi Milioni
Mia Nane na Hamsini Elfu (Tshs. 850,000,000) kwa vikundi vya kiuchumi na mjasiriamali mmoja mmoja katika
sekta zote za kiuchumi; Kuangalia fursa mpya za kiuchumi ambazo zinaweza
kutekelezwa na wananchi katika sekta mbali mbali; Kuhakikisha kuwa mikopo
inayotolewa inatumiwa ipasavyo na inarudishwa kwa wakati uliopangwa; Kuimarisha
uwekaji wa kumbukumbu za wateja wa mikopo; Kuendelea na juhudi za kutunisha
fedha ili Mfuko uendelee kuwasaidia wajasiriamali wengi
zaidi; Kuimarisha mashirikiano na uratibu wa shughuli za mikopo nafuu
hapa nchini; Kuimarisha mashirikiano na taasisi zinazotoa mikopo nafuu;
Kuimarisha uwezo wa watendaji ili kuongeza ufanisi wa kazi na Kuufanyia
mabadiliko madogo Muongozo wa Usimamizi wa Mikopo ili uende sambamba na
mabadiliko na mahitaji ya walengwa katika kipindi kilichopo. Kushirikiana na
Wizara ya Biashara na Viwanda (Kupitia SMIDA) na Benki ya Watu wa Zanzibar - PBZ Ltd kufanikisha uendeshaji wa Mpango wa Maendeleo ya
Wajasiriamali Wadogo wadogo na wa Kati utakaopata ufadhili wa Mfuko wa Khalifa.
17. Mheshimiwa Spika; Ili Mfuko wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi
uweze kutekeleza malengo yake kwa ufanisi kwa Mwaka wa fedha 2020/2021 naliomba Baraza lao kuidhinisha Ruzuku ya Shilingi Milioni Mia Mbili Thamanini, Laki Nne Arobaini na Sita
Elfu, Mia Saba Ishirini na Nne (Tsh. 280,446,724).
Programu Ndogo: SQ010102: Usimamizi na Uimarishaji wa Vyama vya Ushirika.
Lengo kuu: Kusimamia
mageuzi ya Mfumo wa Ushirika ili kuviwezesha Vyama vya Ushirika kuchangia
katika kukuza Ajira na Uchumi wa Nchi
18. Mheshimiwa
Spika; Programu
hii ina lengo la kusimamia Mageuzi ya Mfumo wa Vyama vya Ushirika ili viwe
imara, endelevu, vinavyoendeshwa kiujasiriamali na vinavyokidhi mahitaji ya
wanachama kiuchumi na kijamii. Pia, inachangia kukuza ajira na pato la Taifa.
Programu ilitekeleza shughuli zifuatazo:
·
Imesajili
vyama vya ushirika 860 (Unguja 100; Pemba 760). Kati ya hivyo SACCOS 2 na
vyama vya Uzalishaji na utoaji wa huduma ni 858. Idadi ya vyama vyote vya
ushirika vilivyosajiliwa hadi mwezi Machi 2020 ni 4,534 (Unguja 2,521 na Pemba
2,013).
·
Imekagua hesabu za vyama vya ushirika 186 (Pemba 104
na Unguja 82). Lengo ni kukagua hesabu za vyama vya ushirika 170 (Pemba 70;
Unguja 100).
·
Imefuatilia uendeshaji wa shughuli za vyama, utunzaji
wa vitabu na kutoa ushauri wa kitaalamu kwa vyama 671 (246 Pemba na Unguja 425).
Lengo ni kufuatilia vyama 840. Ufuatiliaji katika SACCOS umeonesha kuwa mitaji
imeongezeka kufikia Shilingi Bilioni Kumi
na Tano, Milioni Mia Tisa na Ishirini (Tshs. 15,920,000,000) kati ya hizo Unguja
ni Shilingi Bilioni Kumi na Tatu,
Milioni Mia Moja na Kumi (Tshs 13,110,000,000) na Pemba ni Shilingi Bilioni Mbili, Milioni Mia Nane na Kumi
(Tshs. 2,810,000,000)
·
Imetoa
leseni kwa SACCOS 22 kati ya 227 zilizopo. lengo ni kuhakikisha kuwa SACCOS zote zinaimarishwa na
zinaendeshwa kwa kufuata masharti kama yalivyoelekezwa katika Sheria ya Vyama
vya Ushirika Nambari 15 ya Mwaka 2018. Pia, imetoa leseni kwa taasisi 3 kutoa
Huduma za Ukaguzi kwa vyama vya ushirika Unguja na Pemba.
·
Imeimarisha uwezo wa watendaji, viongozi na wanachama
kwa kutoa mafunzo. Washiriki 2,410 (Wanawake: 1,608: Wanaume: 802) kutoka vyama
vya ushirika 168. Kati ya washiriki hao, viongozi walikua 284 na wanachama ni
2,126.
·
Pia mafunzo kwa waandishi wa habari 40 kutoka vyombo
vya Habari 20 (Pemba 8; Unguja 12) yalitolewa. Mafunzo hayo yaliwajengea uelewa
juu ya kuundwa kwa FARAJA Union Ltd. Matokeo ni kuwa vipindi 80 na Makala zilizosaidia
kuelimisha jamii viliandaliwa na kurushwa hewani kupitia vyombo vyao na Gazeti
la Zanzibar leo.
·
Imeimarisha
matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa kukusanya, kuchambua na kutoa taarifa za
vyama vya ushirika. Taarifa za vyama 2,258 kati ya vyama 4,534 vilivyomo katika Daftari la Usajili zimeingizwa.
Kati ya hivyo, vyama 1,141 vipo Unguja na 1,117 vipo Pemba. Pia, ipo katika hatua
ya kukamilisha zoezi la kuviingiza vyama
vyote vya Ushirika katika Mfumo wa Uwekaji wa Kumbukumbu za Vyama vya Ushirika.
·
Imeadhimisha Siku ya Ushirika Duniani katika Uwanja wa
Gombani Pemba tarehe 6/7/2019. Maadhimisho yalijumuisha shughuli za kuwaelimisha
wanaushirika juu ya uanzishwaji wa
FARAJA Union Ltd, kufanya usafi katika hospitali kuu tano za Pemba na kuchangia
Damu, Ujumbe ulikuwa “Ushirika kwa Kazi
za Staha”
·
Imeendesha mikutano 53 (Pemba 25 na Unguja 28) kwa
ajili ya kuitangaza Sheria mpya ya Vyama vya Ushirika Nambari 15 ya mwaka 2018.
Jumla ya vyama 783 (Unguja 598 na Pemba 185) vimefikiwa. Washiriki walikua
2,708 (Wanawake 1,735 na Wanaume 973) kutoka Wilaya zote za Unguja na Pemba.
·
Imekamilisha
uundaji wa Taasisi ya fedha ya kitaifa FARAJA UNION Ltd. Pia imejeijengea uwezo
wa taasisi hiyo kwa kuipatia ofisi na vitendea kazi vikiwemo, kompyuta, printa,
meza,viti, mtandao wa kielektroniki wa uendeshaji wa shughuli za fedha. FARAJA
UNION Ltd inaendesha shughuli zake kupitia ofisi zake zilizopo katika Shehia za
Kisiwandui kwa Unguja na Tibirinzi Pemba.
·
Imefanya ziara ya mafunzo iliyowajumuisha Maafisa wa
Wizara, viongozi na watendaji 16 wa FARAJA UNION LTD, kwenye Mikoa ya Dar es Salaam,
Dodoma na Iringa. Lengo la ziara hiyo ni kujifunza mbinu za uendeshaji na
uongozi wa taasisi za fedha za kitaifa.
19. Mheshimiwa Spika; Kwa mwaka wa fedha 2020/2021
Programu ya Usimamizi na Uimarishaji wa vyama vya Ushirika imepanga kusajili Vyama Vya Ushirika 400
(Unguja 250 na Pemba 150); Kusimamia uundwaji wa chama kimoja cha kisekta; Kukagua hesabu za Vyama vya Ushirika 200 Unguja (120) na
Pemba (80); Kufuatilia na kufanya uchunguzi kwa vyama vya ushirika 800 Unguja
(480) na Pemba (320) na Kuimarisha matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa
ukusanyaji Taarifa za Vyama Vya Ushirika.
20. Mheshimiwa Spika; Ili Programu ndogo ya
Usimamizi na Uimarishaji wa Vyama vya Ushirika iweze kutekeleza majukumu yake
kwa ufanisi kwa mwaka wa fedha 2020/2021 naliomba Baraza lako
Kuidhinisha jumla ya Shilingi Milioni Mia Tatu Sabini na Tisa, Laki Tisa
Sitini na Saba Elfu, Mia Moja na Kumi na Mbili (Tshs.
379,967,112).
Programu Ndogo SQ 010103: Uratibu na Uendelezaji wa Programu za Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi.
Lengo Kuu: Kukuza Hadhi ya kiuchumi kwa Vijana,
Wanawake, Wazee, Watoto, Watu wazima na Makundi maalum katika jamii.
21. Mheshimiwa
Spika; Programu hii inaongozwa na Idara ya Uratibu wa
Programu za Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na ina jukumu la kubuni na kuratibu
programu za uwezeshaji wananchi kiuchumi ili kuwawezesha Wananchi kujiajiri na kuwa
na kipato endelevu cha kuweza kumudu maisha yao. Msingi wa malengo haya ni
kuwawezesha Wananchi
kumiliki uchumi wao na kuchangia katika kuleta maendeleo ya nchi. Programu inasimamia
uendeshaji wa
vituo viwili; Kituo cha Kulea na kukuza Wajasiriamali kilichopo Mbweni na Kituo cha
Wanawake cha kutengeneza Umeme wa Jua kilichopo Kinyasini. Programu kwa mwaka wa fedha 2019/2020 imetekeleza shughuli kuu
zifuatazo:-
·
Imeanzisha vituo vya ushauri
wa kibiashara Pemba katika Wilaya ya Mkoani, Wete na Chake Chake na Unguja katika
Wilaya ya Kusini. Pia, imeviimarisha Vituo vilivyopo Unguja na Pemba katika
Wilaya za Kaskazini A, Kaskazini B, Kati na Micheweni ilikufanya kazi kwa
ufanisi ikiwemo kununua vifaa mbali mbali na mafunzo kwa ajili ya uendeshaji
wa vituo hivyo.
·
Imeandaa mafunzo ya huduma
za ushauri wa kibiashara kwa Maafisa watakaotoa huduma katika vituo hivyo
pamoja na wajasiriamali. Kwa Unguja, Jumla ya wajasiriamali 110
wamepatiwa mafunzo ya kuendeleza biashara zao kupitia Wilaya zao Kaskazini “A” 35,
“B” 35, Kusini 25 na Kati 25. Kwa Pemba, Maafisa na
Wajasiriamali 99 wamepatiwa mafunzo katika Wilaya za Chake Chake, Micheweni,
Wete na Mkoani.
·
Imeandaa ziara za kuwatembelea Wajasiriamali Unguja na
Pemba na jumla ya vikundi 70 (Unguja 40 na 30 Pemba) vinavyojishughulisha
na kazi za mikono, ufugaji wa nyuki, ng’ombe, umeme wa jua, ushonaji,
ufinyanzi, kilimo, salon ya kike na usarifu wa mazao, ambapo ziara hiyo kwa
upande wa Unguja zilihusisha vikundi vya watu wanaoishi katika mazingira magumu,
baadhi ya vikundi hivyo Unguja ni Sogea, Afraa Kijichi, Refasha, Sab Spice
Kijichi, Bau Business Group, Mtundani Metaring Work na kwa Pemba ni Makoongwe,
Kisiwa Panza, Zoyina Partnership na kikundi cha watu wenye mahitaji maalum.
Vikundi hivyo viliweza kupatiwa ushauri unaofaa juu ya kuviendeleza vikundi vyao.
·
Imeandaa vikao vya tathmini
ya maendeleo ya Idara na kuandaa Maonesho ya kutimia miaka 20 ya kuanzishwa
tena kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki yaliyofanyika Fumba Mji Mpya kuanzia
tarehe 16/11/2019 hadi tarehe 24/11/2019 ambapo yaliwashirikisha jumla ya wajasiriamali
183 kutoka Zanzibar, Tanzania Bara na Taasisi 17. Wajasiriamali waliweza
kutangaza na kuuza bidhaa zao.
·
Imesimamia uendeshaji wa
Kituo cha Wanawake cha Utengenezaji wa Vifaa vya Umeme wa Jua (Barefoot
College) na imetowa mafunzo ya ufugaji wa nyuki kwa wanawake 20 huko Pemba. Pia, Kituo kimeajiri vijana watatu katika masuala ya
ushonaji.
·
Imefanya ufuatiliaji na
tathmini ya Maendeleo ya mradi kwa vijiji vilivyounganishwa umeme wa jua pamoja
na kutembelea vijiji tofauti Unguja na Pemba kwa ajili ya kubaini
changamoto na mafanikio ya mradi. Tathmini imebaini kwamba Mradi unawasaidia
wananchi kwa kunga’risha vijiji vyao, watoto kuweza kudurusu masomo yao nyakati
za usiku na kuongeza kipato kwa sola mama.
·
Imefanya upembuzi yakinifu ili kuchagua kinamama ambao
watapatiwa mafunzo ya nishati ya umeme wa jua kwa muhula wa 3 wa masomo. Jumla
ya vijiji 6 (Kigongoni, Ukongoroni, Kendwa Unguja na Kukuu, Msuka na Matale
Pemba) vimeweza kuchaguliwa na wanawake 12 wameweza kupata nafasi ya kujifunza
masomo ya nishati ya umeme wa jua kwa Unguja na Pemba.
·
Kituo kimenunua vifaa kutoka nchini India kwa ajili ya
kufundishia wanawake ambao watajifunza nishati ya umeme wa jua kwa muhula wa 3 wa masomo vifaa
vilivyopelekwa ni pamoja na dayoda, tranzista na daiva.
·
Kituo kimeweza kuadhimisha siku ya Wanawake Duniani
kwa kutoa misaada ya vitu mbalimbali katika hospitali ya Kivunge, vifaa hivyo
ni pamoja na mito ya kulalia, mashuka, sabuni za kukogea na kufulia.
·
Katika kipindi hichi kituo kimeweza kutangazwa kupitia
njia mbalimbali zikiwemo, Makala katika Gazeti la Zanzibar Leo, semina, warsha
na mikutano ambapo kituo hupata fursa ya kualikwa pamoja na kutangaza na kuuza
bidhaa zinazozalishwa kituoni hapo ikiwepo taulo za wanawake, nguo na
asali.
·
Imesimamia uendeshaji wa Kituo cha Kulea na Kukuza
Wajasiriamali (ZTBI) ambapo mashine za maziwa zimefanyiwa matengenezo. Pia,
kituo kimeweza kufanya ukarabati wa vifaa mbali mbali vya ofisi. Pia Vipindi mbali mbali vya kukitangaza
kituo na huduma zinazotolewa vimerushwa kupitia redio za KISS FM, Bahari FM,
Hits FM na ZBC.
·
Vijana 40 wamepatiwa mafunzo juu ya usarifu wa mazao
ya kilimo kituoni kupitia mradi wa FAO, pamoja na kupewa tunzo kwa washindi
watatu (3) wa mpango wa biashara. Vile vile, Kituo kimefanya mafunzo ya bekari
kwa vijana 12.
22. Mheshimiwa Spika; Kwa mwaka wa fedha
2020/2021, Programu ya Uratibu na Uendelezaji wa Program za Wananchi Kiuchumi
imepanga kuendelea kutoa mafunzo ya ujasiriamali kwa Vijana 300, Wanawake na
Makundi maalum, itatekeleza Miradi ya kuwawezesha Wajasiriamali na Vijana ili
kutoa huduma na bidhaa zenye ubora; itawawezesha Wajasiriamali 25 kushiriki
katika maonyesho ya Afrika Mashariki (Jua Kali); itaendelea kuwawezesha Vijana
kujiajiri kupitia Kituo cha Kulea na Kukuza Wajasiriamali (INCUBATION CENTRE)
pamoja na kuwawezesha Wanawake kiuchumi kupitia Kituo cha Wanawake cha
utengenezaji wa vifaa vya umeme wa jua (BAREFOOT) Kibokwa.
23. Mheshimiwa Spika; Ili Programu ndogo ya
Uratibu na Uendelezaji wa Program za Wananchi Kiuchumi iweze kutekeleza
majukumu yake kwa ufanisi kwa mwaka wa fedha 2020/2021,
naiomba Kamati yako kuidhinishia jumla ya Shilingi Bilioni Moja, Milioni Mia Sita Ishirini na Nne, Laki Saba Ishirini na Mbili Elfu, Mia Saba na Kumi
na Mbili (Tshs.1,624,722,712/-).
24.
Mheshimiwa Spika; Ili Programu
Kuu ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi
iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi kwa mwaka wa fedha 2020/2021,
naliomba Baraza lako Tukufu Kuidhinisha jumla ya Shilingi Bilioni Mbili, Milioni Mia Mbili na Thamanini na Tano, Laki
Moja Thalathini na Saba Elfu, Mia Tano na Arobaini na Nane (2,285,137,548/-).
PROGRAMU KUU PQ0103: HIFADHI YA JAMII NA MAENDELEO YA WANAWAKE NA WATOTO
Mtokeo ya Muda Mrefu:
Kuimarisha Ustawi na Hifadhi ya Jamii na kupunguza kiwango cha umaskini kwa
wanawake wa Zanzibar.
Programu
ndogo SQ010301: Uratibu wa Huduma za Uhifadhi
wa Jamii.
Lengo kuu: Kuimarisha mifumo ya hifadhi ya
jamii na huduma kwa wazee na watoto wanaoishi katika mazingira magumu.
25. Mheshimiwa Spika; Programu hii
inatekelezwa na Idara ya Wazee na Ustawi wa Jamii ambayo ina jukumu la kuratibu
na kusimamia upatikanaji wa haki kwa makundi yanayoishi katika mazingira magumu
zaidi. Pia, programu ina lengo la kuimarisha Mfumo wa Hifadhi ya Mtoto, Kuimarisha
hifadhi ya wazee, Kusimamia ulipwaji wa fidia kwa wafanyakazi waliopatwa na
ajali kazini na Kusimamia malipo ya Pensheni kwa Wazee wenye umri wa miaka 70
na kuendelea. Pamoja na Mikakati ya Kitaifa na Mpango Mkakati wa Wizara,
Utekelezaji wa shughuli za Programu unaongozwa na Sheria ya Watoto Na. 6 ya
2011 na Sera ya Hifadhi ya Jamii ya Mwaka 2014. Programu imetekeleza
yafuatayo:-
· Imeendelea kupokea na kuyafanyia kazi malalamiko
yanayohusu ukiukwaji wa haki za watoto kupitia Kitengo cha Hifadhi ya Mtoto cha
Taifa ambapo jumla ya malalamiko 390
yalipokelewa na kufanyiwa kazi kwa Unguja ambapo Malalamiko 255 yalihusu
kunyimwa matunzo na 135 yalihusu mvutano
wa malezi. Kwa upande wa Pemba jumla ya malalamiko 289 yalipokelewa na
kufanyiwa kazi ambapo Malalamiko 194 yalihusu kunyimwa matunzo na 95 yalihusu
mvutano wa malezi. Takwimu zinaonyesha kuwa malalamiko ya matunzo na mvutano wa
malezi yanaendelea kuongezeka
kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo. Hii
ni aina mbaya sana ya ukatili dhidi ya watoto ambayo inatokea ndani ya familia
na kuwaweka idadi kubwa ya watoto katika hatari ya kupata aina nyengine za
udhalilishaji na ukatili. Sababu
kuu ya kuongezeka aina hii ya ukatili dhidi ya watoto ni talaka. (Kiambatanisho
namba 6a na 6b kinahusika).
·
Imeendelea kufuatilia kesi za jinai na madai 230 (72
Madai na 158 Jinai) katika Mahakama za Watoto za Mahonda, Vuga na Mahakama ya
Mkoa wa Kaskazini na Kusini Pemba. Jumla ya kesi 158 za jinai zilizofuatiliwa
zilihusisha makosa ya kubaka, kutorosha, kujaribu kulawiti, kulawiti, shambulio
la hatari, shambulio la kuumiza mwili, kukashifu na unyanga’nyi Unguja na Pemba.
Kesi 108 (Unguja 58 na Pemba 50) bado zinaendelea na kesi 24 zimepewa rufaa
kituo cha Marekebisho ya tabia. Aidha, kesi za madai 72 (Vuga 65 na Mahonda 7)
zilifunguliwa Unguja ambapo zinazohusisha kunyimwa matunzo na mvutano wa
malezi. Kesi 59 zinaendelea; Kesi 11 zimemalizika na 2 zimepatiwa rufaa (Kiambatanisho namba 7(7a na 7b) na 8 (8a,
8b, 8c, 8d) Vinahusika).
·
Imeendelea
kusimamia uendeshaji wa Kituo cha Marekebisho ya Tabia kwa Watoto Wanaokinzana na Sheria na Walio katika Hatari ya
Kukinzana na Sheria. Hadi kufikia Mwezi Machi, 2020 Kituo kimepokea watoto 21 (Wanawake 8 na Wanaume 13)
ambao wamefanya makosa mbali mbali ikiwemo; wizi, kukashifu na kuondoka
nyumbani. Watoto hao hupatiwa taaluma ya
mambo mbalimbali ikiwemo; stadi za maisha, ushauri nasaha, ufundi, ushoni,
uchoraji, kompyuta, sarakasi na maigizo.
Aidha, jumla ya watoto 13 (7 wanawake na 6 wanaume) wamemaliza muda wao wa
mafunzo na kuondoka kituoni katika kipindi hiki.
·
Watoto
wote hao wanaendelea vizuri ambapo 6 wamerudi Skuli kuendelea na masomo yao, 5
wanaendelea na Mafunzo ya Ufundi katika Taasisi ya Sayansi na Teknolojia Karume na 2 wamejiunga na Mafunzo ya ufundi wa uchomaji na uunganishaji wa Vyuma katika chuo
cha Mafunzo. Ziara katika familia za watoto hawa zinafanywa mara kwa mara na
Maafisa wa Kitengo ili kuhakikisha uendelevu wa marekebisho ya tabia zao.
·
Imefuatilia na
kusimamia uendeshaji wa vituo 6
vya kulelea watoto yatima vya binafsi Unguja na Pemba. Mpaka kufikia Mwezi Machi, 2020; jumla ya watoto 235 (wanaume 172
na wanawake 63) wanaendelea kutunzwa kwa kupatiwa huduma mbali mbali katika vituo hivyo. Wamiliki
wa vituo hivyo wameendelea kupatiwa maelekezo ya namna bora ya uendeshaji wa
vituo na kuimarisha malezi ya watoto wanaolelewa katika vituo hivyo.
- Inaendelea kuhakikisha kwamba
msisitizo unawekwa kwa familia kuzingatia jukumu la msingi la malezi na
ulinzi wa mtoto kwa ukuaji mzuri wa kimwili na kiakili na kwamba watoto kuwekwa
kwenye vituo ni suluhisho la mwisho baada ya mibadala yote ya malezi
kushindikana. Wizara imekuwa ikichukua juhudi kadhaa za kuhakikisha inadhibiti ongezeko la watoto
wanaolelewa katika vituo hivyo ikiwemo; kukamilisha kanuni za Makaazi yaliyokubaliwa
na hivyo kuanzisha utaratibu wa kuvipatia leseni vituo vyenye sifa tu,
kuhakikisha watoto wanaoingizwa katika vituo wanapata ridhaa ya Wizara
kupitia Idara ya Wazee na Ustawi wa Jamii. Jitihada hizo zimepelekea
kupungua kwa kiasi kikubwa idadi ya Vituo pamoja na wimbi la watoto
wanaolelewa katika vituo hivyo kutoka watoto 551 mwaka 2015 na kufikia
watoto 270 mwaka 2020.
(Kiambatanisho namba 9 kinahusika).
·
Imewajengea uwezo
Wakuu wa Vituo na Walezi 22 wa vituo vya binafsi vya Unguja na Nyumba ya Watoto
Mazizini juu ya Kanuni za Makaazi, viwango na mahitaji katika uendeshaji wa Vituo
hivyo pamoja na ulinzi na usalama wa watoto.
·
Wizara ipo katika hatua ya kuanzisha Programu ya
Malezi itayohusisha kuwepo kwa Walezi maalum wa kujitolea, watakaofanyiwa
tathmini ya kina juu ya malezi, kupatiwa mafunzo na kusajiliwa. Walezi hao
wataishi na Watoto wanaohitaji matunzo baada ya kufikwa na kadhia mbali mbali
ikiwemo ukatili na udhalilishaji. Pia, imeandaa Kitini cha mafunzo, nyenzo za
ufuatiliaji na tathmini pamoja na vipeperushi.
·
Imeendelea kuwatunza Watoto 37 (wanaume 19 na wanawake
18) wa Nyumba ya watoto Mazizini kwa kupatiwa huduma zote muhimu. Aidha, Nyumba
ya Watoto Mazizini imekuwa ikitoa hifadhi ya muda kwa watoto wanaofanyiwa
udhalilishaji na wanaopata matatizo mbali mbali ya malezi; ikiwemo mvutano wa
malezi au kukosa wazazi. Kwa mwaka wa fedha 2019/2020 jumla ya watoto 18
(wanawake 14 na wanaume 4).
·
Kituo cha Mazizini kimepokea Watoto watatu wote wa
kike, baada ya kutupwa katika maeneo tofauti Unguja na Pemba. Watoto hao
wanaendelea vizuri na malezi. Napenda kuchukua fursa hii kukemea vikali vitendo
hivi vya kinyama ambavyo vinaendelea kushamiri katika nchi yetu. Aidha, tunatoa
wito kwa jamii kuendeleza mshikamano wa kifamilia pamoja na kuwasaidia kwa kila
hali na kuwa karibu na wanawake wanapokuwa wajawazito ili kuwaepusha na msongo
wa mawazo unaopelekea kufanya vitendo vya kikatili.
·
Imeendelea kuwahifadhi wahanga 26 (wanawake 22 na
wanaume 4) wa ukatili na udhalilishaji katika nyumba salama ili kuzuia kupotea
kwa ushahidi na usalama wao.
·
Imeendelea kuratibu utekelezaji wa Sera ya Hifadhi ya
Jamii ya mwaka 2014 na imesimamia kufanya tathmini ya Sera hiyo kufuatia
kufikia nusu ya utekelezaji wa Mpango kazi wake ili kuangalia mafanikio na changamoto
zilizojitokeza katika utekelezaji huo. Tathmini ya awali imeonyesha kuwa Sera
imefanikiwa katika uanzishaji na uendeshaji wa zoezi la Pensheni Jamii kwa
Wazee wote lakini kumeonekana changamoto katika masuala ya uratibu. Tathmini
hii itakapokamilika itaota muongozo wa namna bora ya utekelezaji wa sera hiyo
kwa kipindi kijacho.
·
Imeendelea kuwapatia huduma muhimu ikiwemo Afya,
Chakula, Malazi na Mavazi wazee 80 wanaotunzwa katika Makao ya Wazee Welezo,
Sebleni na Limbani, Pemba ambapo katika Makao ya Welezo kuna wazee; 42 (wanaume 32 na wanawake 10) Sebleni Wazee 30
(wanaume 9 na wanawake 21) na Limbani Pemba
Wazee 8 ( wanaume 5 na wanawake 3). Aidha, waathirika wa maradhi ya
ukoma wa Makundeni 52 (wanaume 25 na wanawake 27) wanaendelea kupatiwa posho
maalum.
·
Kwa kushirikiana na Jumuiya za Wazee nchini
imeadhimisha Siku ya Wazee Duniani tarehe 1 Oktoba iliyofanyika kitaifa katika
Hoteli ya Zanzibar Beach Resort, Mazizini ambapo Mh. Waziri wa Kazi,
Uwezeshaji, Wazee, Wanawake na Watoto alikuwa Mgeni rasmi. Kauli mbiu ya mwaka
huu ilikuwa ni “Tuimrishe Usawa Kuelekea Maisha Ya Uzeeni”. Maadhimisho
yaliambatana na shughuli mbali mbali za kuwaenzi na kuwathamini Wazee.
·
Imeendelea kutoa misaada ya kiustawi kwa familia zenye
watoto wanaoishi katika mazingira magumu zaidi ambapo familia 152 (Unguja 86 na
Pemba 66) zimesaidiwa. Aidha, imewapatia msaada wa posho la maziwa kwa familia
zenye mapacha zaidi ya wawili; 14 (9 Unguja na Pemba 5).
·
Imeendelea kulipa na kusimamia malipo ya fidia kwa
Wafanyakazi walioumia wakiwa kazini. Jumla ya wafanyakazi 20 wamelipwa fidia
katika kipindi hiki, kati ya hao Unguja 11 na Pemba 9. Jumla ya Shilingi Milioni Ishirini na Moja, Laki
Mbili Thamanini na Tisa Elfu, Mia Nane na Tisini na Moja (Tshs. 21,289,891)
zilitumika kufanya malipo hayo. Aidha, madai 33 (Unguja Madai 21 na Pemba Madai
12) ya malipo ya fidia yenye thamani ya Shilingi
Milioni Arobaini na Saba, Laki Nne na Sitini Elfu, Mia Sita na Kumi na Moja
(Tshs. 47,460,611) yameshafanyiwa tathmini na yanasubiri malipo. Aidha, Wizara
inaendelea na hatua za kuanzisha Mfuko wa Fidia nchini.
· Hadi kufika
mwezi Machi, 2020; jumla ya Wazee 28,516 (16,565 wanawake na 11,951 wanaume)
wamesajiliwa katika Programu ya Pensheni Jamii; kati ya hao; Unguja ni 17,660
na Pemba ni 10,856. Jumla ya wazee wapya 2,380 (Unguja 1,434 na Pemba 946)
wamesajiliwa na Wazee 1,437 (Unguja 991 na Pemba 446) walifariki na kuondolewa
katika Programu katika kipindi hichi. (Kiambatisho
namba 10a na 10b Kinahusika)
· Pia, Mfumo
wa kuhifadhi taarifa za Wazee wanaopokea Pensheni unaendelea kuboreshwa na
taarifa za wazee zinaendelea kuchukuliwa kwa kufanyiwa usajili wa alama za
vidole na picha zao kwa kupitia ving’amuzi kila mwezi. Malipo ya kutumia
ving’amuzi kwa upande wa Unguja yameanza rasmi mwezi wa April, 2020 na kwa
upande wa Pemba malipo ya ving’amuzi yanaendelea. Mfumo huo utarahisisha pamoja na mambo
mengine utaratibu wa kupokea Pencheni za Wazee kwa njia ya kielekitroniki.
· Mpango
unaendelea vizuri kwa mashirikiano makubwa tunayoyapata kutoka kwa Wakuu wa
Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Masheha wa Unguja na Pemba yanayopelekea ufanisi wa
utekelezaji wa program hii. Aidha, tunaendelea kutoa wito kwa Taasisi na jamii
kuhakikisha kwamba wazee wote wenye sifa wanasajiliwa kwa wakati ili waweze
kupokea Malipo yao ya pensheni kwa wakati na kutoa taarifa kwa wakati kwa wazee
waliofariki ambao tayari wamesajiliwa katika Mpango huu.
26. Mheshimiwa Spika; Kwa mwaka wa fedha 2020/2021,
Programu ya Uratibu wa Huduma za Uhifadhi wa Jamii imepanga Kuendelea
kuimarisha Hifadhi ya Watoto
kwa mujibu wa Sheria ya Mtoto namba 6/2011; Kuratibu uendeshaji wa
Kituo cha kurekebisha tabia za Watoto; Kulipa fidia kwa Wafanyakazi wanaopatwa
na ajali kazini; Kufuatili uanzishaji wa Mfuko wa Fidia; Kusimamia
uendeshaji wa Makao ya Wazee Unguja na Pemba; Kusimamia uendeshaji wa nyumba ya
watoto Mazizini; Kuendelea kutoa misaada ya Kiustawi kwa familia zenye
Mazingira magumu zaidi; Kusimamia utekelezaji wa Mpango wa Pensheni Jamii;
kuratibu utekelezaji wa Sera ya Hifadhi ya Jamii na Kuzika maiti zisizokuwa na
wenyewe na Kuandaa Kanuni na kuratibu utekelezaji wa Sheria ya Wazee
27. Mheshimiwa Spika; Ili Programu ndogo ya
Uratibu Uratibu wa Huduma za Uhifadhi wa Jamii iweze kutekeleza majukumu yake
kwa ufanisi kwa mwaka wa fedha 2020/2021; naliomba Baraza lako kuidhinisha
jumla ya Shilingi Bilioni Kumi, Milioni Mia Tano Arobaini na
Nne, Thalathini na Tano Elfu na Thalathini (Tshs.10,544,035,030).
Programu ndogo SQ010303: Maendeleo ya Wanawake na Kupinga Udhalilishaji.
Lengo kuu: Kuimarisha
maendekeo ya wanawake na kuratibu mwitiko wa mapambano dhidi ya udhalilishaji
wa Wanawake na Watoto.
28. Mheshimiwa Spika; Programu hii inatekelezwa na Idara ya
Maendeleo ya Wanawake na Watoto ina jukumu la kuratibu na kusimamia utekelezaji
wa haki za wanawake na watoto ikiwa ni pamoja na kusimamia utekelezaji wa sera
na sheria zinazohusu maendeleo ya wanawake na watoto. Programu inatekeleza
majukumu yake ya kuwaendeleza wanawake kwa kuzingatia Sera na Mipango ya
Kitaifa, Mikataba ya Kimataifa na Kikanda. Programu kwa
mwaka wa fedha 2019/2020 imetekeleza shughuli zake kama ifuatavyo:
·
Imefanya
Kikao cha Kamati ya Viongozi wa juu na kujadili taarifa za utekelezaji wa
Mpango Kazi wa Kitaifa wa Kupambana na Vitendo vya ukatili na Udhalilishaji kwa taasisi zinazosimamia utekelezaji wa Mpango
huo. Pia, imeratibu vikao vitatu
vya Kamati ya Kitaalamu ya kupambana na vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa wanawake na watoto na
kupata taarifa ya utekelezaji ambayo iliunganishwa na kupatikana taarifa
iliyowasilishwa katika Kamati ya Viongozi wa Juu.
·
Imefanya
mkutano wa kutathmini na kujadili utekelezaji
wa mikakati ya kupambana na
vitendo vya Ukatili na Udhalilishaji iliyopendekezwa na wananchi kupitia programu ya uhamasishaji jamii
kupitia sanaa shirikishi. Wananchi
walichukua hatua mbali mbali za kujikinga ikiwemo kufyeka vichaka, kuondosha baadhi ya vigenge viovu, kuwaelimisha na
kuwapa mbinu watoto/ wanafunzi juu ya namna ya kujikinga na vitendo vya Ukatili
na Udhalilishaji, maboma kuwatafuta wenyewe kwa ajili ya kuyamaliza au kuyasafisha
ili kuweka udhibiti wa matukio ya ukatili na udhalilishaji yasitokee. Kudhibiti
uzururaji wa wanafunzi kwa mfano skuli ya Nungwi imejengwa ukuta, kuanzisha na
kuimarisha ulinzi shirikishi na doria katika Shehia, kudhibiti utizamaji wa TV
za nje (maskani) kwa watoto, kulifukia shimo liliopo eneo la Skuli ya Kibeni ambalo linatumiwa na
wanafunzi kufanyiana vitendo vya Ukatili na Udhalilishaji, kuondoshwa kwa
baadhi ya magesti na mabaa kwa mfano Donge Mchangani.
·
Imefanya mkutano wa Robo Mwaka kwa Timu ya Viongozi
wa Dini zinazojumuisha Viongozi wa Dini
88 za Wilaya kwa ajili ya kutathmini
utekelezaji wa shughuli wanazofanya katika kupambana na vitendo vya ukatili na
udhalilishaji dhidi ya wanawake na watoto pamoja na kutayarisha na kujadili
mipango kazi yao kwa robo mwaka unaokuja. Miongoni mwa shughuli walizozifanya
ni pamoja na kufanya mikutano ya hadhara, kutayarisha na kusambaza hotuba
katika misikiti mbali mbali ya Ijumaa, kuandaa vipindi kupitia redio ya ZBC,
Annur na redio jamii (Mkoani na Micheweni) na wamefanya uhamasishaji kupitia
Skuli na Madrasa. Jumla ya watu waliofikiwa ni 49,438 (wanaume 27,454 na
wanawake ni 21,984).
·
Imeziwezesha
Timu za Viongozi wa dini za Wilaya kwa kuwapa nauli na vitendea
kazi kama karatasi na kalamu ili
waweze kutekeleza shughuli zao za kutoa
elimu na kuihamasisha jamii juu ya kupambana na vitendo vya Ukatili na
Udhalilishaji dhidi ya Wanawake na Watoto.
·
Imetoa Mafunzo ya wasimamizi wa utoaji wa haki Unguja na Pemba na
kujadili Uwajibikaji wa Vyombo vya Sheria na Changamoto wanazokabiliana nazo
katika utoaji wa huduma. Mkutano huo uliwashirikisha Polisi, DPP, Mahkama, Kituo
cha huduma ya Mkono kwa Mkono. Washiriki hao walipendekeza kufanya mikutano
endelevu itakayoimarisha mahusiano kati ya vyombo vinavyosimamia masuala ya
Haki na kuanzisha mfumo wa uratibu katika masuala ya Sheria ikiwemo chuo cha
mafunzo.
·
Imeelimisha
na kuhamasisha jamii juu ya kupambana na vitendo vya Ukatili na Udhalilishaji dhidi
Wanawake na Watoto katika Shehia 37 (22 Unguja na 15 Pemba) kwa kupitia mbinu
ya sanaa shirikishi. Baada ya maigizo, wananchi walipata fursa ya kuibua na
kujadili sababu hatarishi za vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa Wanawake
na Watoto katika shehia zao na hatimae kupendekeza mikakati kwa ajili ya kuzitatua
sababu hizo.
·
Imehamasisha
viongozi wa Kamati za Kudumu za Baraza la Wawakilishi, Watendaji wa Wizara,
Viongozi wa Dini na Wandishi wa Habari kuhusu vuguvugu la malezi kwa watoto
ambapo jumla ya watu 120 wamefikiwa ili kuimarisha uwajibikaji wa malezi ya
pamoja na kuondoa vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa watoto. Wajumbe
wa Wawakilishi wanatarajiwa kutoa elimu hiyo katika majimbo yao ili kuimarisha
malezi bora ya watoto nchini. Aidha,
imeandaa vipindi vitano (5) vya uhamasishaji kuhusu vuguvugu la malezi kwa
watoto kupitia vipindi vya redio na Tv ikiwemo ZBC TV na Redio, Asalam FM,
Chuchu Fm, na Zanzibar Cable TV.
·
Imekiimarisha
Kitengo cha Ushauri Nasaha kwa kupatiwa vitendea kazi muhimu ikiwemo mafuta ili
waweze kutoa huduma madhubuti na msaada wa kisaikolojia kwa Wahanga wa vitendo
vya Ukatili na Udhalilishaji dhidi ya Wanawake na Watoto. Msaada huo ulisaidia
kitengo kufanya ufuatiliaji kwa wahanga wa ukatili na udhalilishaji pamoja na familia zao na kutoa
ushauri unaofaa.
·
Imeandaa na kurusha hewani vipindi 12 (8 Unguja na 4 Pemba) vya
kuhamasisha jamii kupinga vitendo vya Ukatili na Udhalilishaji na majukumu ya waratibu wa
Wanawake na Watoto katika Shehia. kupitia ZBC TV, Redio na redio jamii Pemba.
Kupitia vipindi hivyo wanananchi wamepata fursa ya kuzijua Sheria mpya
zinazohusiana na kupambana na vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa Wanawake
na Watoto pamoja na kujua utaratibu wa kutoa taarifa ya vitendo hivyo kupitia
ngazi mbali mbali. Aidha, Makala moja ilichapishwa na gazeti la Zanzibar leo inayohusu masuala ya
Udhalilishaji wa Wanawake na Watoto na vipeperushi vilichapishwa na kusambazwa
kwa wananchi kwenye maonesho ya chakula huko Chamanangwe.
·
Imefanya mikutano mitatu (3) ya kujenga uelewa juu ya Kuhamasisha
malezi bora na Matunzo kwa Familia kwa Watendaji kutoka taasisi za Serikali na
Binafsi zinazoshughulikia masuala ya Watoto, Waandishi wa Habari na Kamati ya Maendeleo ya Wanawake, Habari na Utalii ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar.
·
Imeratibu
Mkutano wa Kimataifa na Kikanda wa Huduma za Simu kwa Watoto ambao
ulizishirikisha Nchi 86 kutoka Afrika Mashariki ya Kati na Ulaya uliojadili juu
ya kuwekeza katika teknolojia ya kuwalinda Watoto dhidi ya vitendo vya Ukatili
na Udhalilishaji wa kingono. Aidha, Wajumbe walikubaliana kutumia Mfumo wa pamoja wa Kielektroniki wa
ukusanyaji wa taarifa za Udhalilishaji katika Nchi wanachama wanaoendesha
huduma za simu kwa Mtoto ili kukinga na kuripoti vitendo vya Ukatili na
Udhalilishaji. Pia, imeandaa
kikundi kazi cha kusimamia huduma za simu na masuala ya rufaa kwa watoto
waliofanyiwa masuala ya ukatili na udhalilishaji kwa kuwaunganisha na mifumo ya
utoaji wa huduma za hifadhi ya mtoto.
·
Imewajengea Uwezo Waratibu wa Wanawake na Watoto 209 (105
Unguja na 104 Pemba) kwa kupatiwa
mafunzo juu uelewa wa Sheria dhidi ya Ukatili na Udhililishaji wa
Kijinsia, Sheria ya Mtoto, Mambo muhimu ya kuzingatia katika kuwasaidia wahanga
wa ukatili wa kijinsia, kuelimisha jamii juu ya hifadhi ya mtoto na Kampeni ya
kitaifa ya kupambana na Udhalilishaji ambayo ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango
kazi wa Kitaifa wa Kupambana na Vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa
kijinsia.
Pia, Waratibu 319 walipatiwa posho la usafiri wa
kufuatilia (190 Unguja kwa Wilaya za
Mjini, Magharibi “A na B” na Kusini na Kati Unguja na 129 kwa Shehia zote za
Pemba).
·
Imefanya
maadhimisho ya siku 16 za wanaharakati wa kupinga Vitendo vya Ukatili na
Udhalilishaji Unguja na Pemba ambayo huadhimishwa kila mwaka Ifikapo tarehe 25
Novemba – 10 Disemba. Ujumbe wa mwaka huu ni “Imarisha Usawa Pambana na
Udhalilishaji, Pinga Ubakaji. Wizara ilitoa zawadi maalum kwa waratibu
wa Shehia wa Wanawake na Watoto pamoja
na Shehia zinazofanya vizuri zaidi katika harakati za kupambana na vitendo vya
ukatili na udhalilishaji wa Wanawake na Watoto ambapo jumla ya Waratibu 11 na
Shehia 11 zilipatiwa zawadi hizo ili
kuchochea ari ya uwajibikaji kwa Shehia na Waratibu wengine katika
Mapambano hayo.
·
Imeadhimisha
siku ya Mtoto wa Kike tarehe 11/10/2019 katika Ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdul
Wakil Wilaya ya Mjini ambapo ujumbe wa mwaka huu ni “Utekelezaji wa Sheria ni Jukumu Letu
Sote! Tuwajibike”. Pia, Imetoa mafunzo ya Watoto wa Kike ya kuandika Makala ya
Udhalilishaji wa kijinsia ambazo zitachapishwa katika Jarida la SEMA ambalo
linalenga kuhamasisha uzuiaji wa ukatili wa Kijinsia kwa Watoto na Kuimarisha
Malezi Bora.
·
Imeadhimisha
siku ya wanawake Duniani tarehe 8/3/2020 Ujumbe wa mwaka huu ni “Endeleza
Vuguvugu la Usawa: zingatia Haki na Maendeleo ya wanawake”. Kilele cha Maadhimisho hayo kilifanyika katika
Ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdul Wakil Kikwajuni Zanzibar kwa kufanya Kongamano la
Kitaifa. Lengo la Kongamano hilo ni
kutathmini mafanikio na changamoto za utekelezaji wa Azimio la Beijing kwa miaka 25 iliyopita.
·
Imefanya
ufuatiliaji wa vikundi vya wanawake 74
(14 Unguja na 60 Pemba) Vikundi hivyo vimepatiwa ushauri na maelekezo pamoja na
kuwaunganisha na fursa za ujasiriamali, mikopo na ushirika ili kuinua kiwango
cha uzalishaji.
·
Imepokea,
kuyasikiliza na kuyafanyia kazi malalamiko ya Wanawake 105 (41 Unguja na 64 Pemba) kwa kupatiwa
maelekezo na Ushauri nasaha, Malalamiko hayo yalihusu kutelekezwa na mume, madai ya mali,madai ya
mahari, dai la talaka, migogoro ya ndoa, shambulio la matusi kwa njia ya simu,
madai ya makaazi, kupigwa, huduma za ujauzito,
kudhalilishwa na madai ya mafao.
·
Imepokea
jumla ya simu 17 zilizorasmi za waathirika wa vitendo vya udhalilishaji kati ya
hizo, 1 kutelekezwa, 5 kubakwa, 2 kupigwa, 1 kutishiwa amani, 1 kukatishwa
masomo, 1 kulawitiwa, 1 kushikwa makalio, 1 kutumikishwa kazi za majumbani.1
kutukanwa, 1 mvutano wa malezi na 2 adhabu mbadala ya kutoleshwa pesa na
mwalimu. Malalamiko hayo yamefikishwa
sehemu husika kwa kuchukuliwa hatua za Kisheria kwa mujibu wa lalamiko.
29. Mheshimiwa Spika; kwa mwaka wa fedha
2020/2021, Wizara kupitia Programu ya Maendeleo ya Wanawake na Kupinga
Udhalilishaji inatarajia kufanya ufuatiliaji wa vikundi na kuviunganisha na
fursa mbalimbali zilizopo za kiuchumi pamoja na kuhamasisha wanawake kugombea nafasi
mbalimbali za uongozi; itaendelea kuwajengea uwezo wadau katika kupinga vitendo
vya ukatili na udhalilishaji dhidi ya wanawake na watoto pamoja na kuratibu
utekelezaji wa Mpango Kazi wa Miaka Mitano wa Kupambana na Vitendo vya Ukatili na Udhalilishaji
dhidi ya Wanawake
na Watoto
(2017/2022) na Kuimarisha uhamasishaji na utekelezaji wa Vuguvugu la malezi ya
familia na ushiriki wa watoto katika
kupambana na mimba za umri mdogo kupitia mabaraza na vilabu vya watoto.
30. Mheshimiwa Spika; Ili Programu ya Maendeleo ya Wanawake na Kupinga Udhalilishaji itekeleze
majukumu yake kwa ufanisi kwa mwaka wa fedha 2020/2021;
naliomba Baraza lako Kuidhinisha jumla ya Shilingi
Bilioni Moja, Milioni Tisa, Laki Saba Hamsini na Tisa Elfu na Kumi na Sita
(Tshs. 1,009,759,016).
31. Mheshimiwa Spika; Ili Progaramu Kuu ya Hifadhi ya
Jamii na Maendeleo ya Wanawake iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi
kwa mwaka wa fedha 2020/2021; naliomba Baraza lako Kuidhinisha jumla ya Shilingi Bilioni Kumi na Moja, Milioni Mia
Tano Hamsini na Tatu, Laki Saba Tisini na Nne, Arubaini na Sita
(11,553,794,046).
PROGRAMU KUU PQ0104: UENDESHAJI NA URATIBU WA WIZARA YA KAZI UWEZESHAJI WAZEE WANAWAKE NA WATOTO
Matokeo ya muda Mrefu: Kuwa na Mipango endelevu na
Sera sahihi zitakazoimarisha upatikanaji wa ajira zenye staha na ustawi wa vijana,
wanawake, watoto, wazee na makundi mengine yanayoishi katika mazingira magumu
zaidi.
Programu ndogo SQ010401: Uratibu wa Mipango, Sera na Tafiti za Wizara.
Lengo Kuu: Kusimamia
uandaaji na utekelezaji wa Sera, Mipango, Programu na Tafiti za Wizara itakayosaidia
kukuza uchumi endelevu nchini.
32.
Mheshimiwa Spika;
Programu ya Uratibu wa Mipango, Sera na Tafiti za
Wizara inalenga Kusimamia uandaaji na utekelezaji wa Sera, Mipango, Programu na
Tafiti za Wizara ili Kuwa na Mipango
endelevu na Sera sahihi zitakazoimarisha upatikanaji wa ajira zenye staha na
ustawi wa vijana, wanawake, watoto, wazee na makundi mengine yanayoishi katika
mazingira magumu zaidi. Programu hii iko chini ya Idara ya Mipango, Sera na
Utafiti na kwa mwaka wa fedha 2019/2020 imetekeleza shughuli zifuatazo:
·
Imekamilisha uandaaji wa Mswada wa
Sheria ya Masuala ya Wazee 2020 na tayari umepitishwa na Baraza la Wawakilishi.
Sheria pamoja na mambo mengine inatoa muongozo wa Uendeshaji wa Programu ya
Pensheni Jamii kwa Wazee wote na kutoa Muongozo kwa Jamii kusimamia malezi bora ya Wazee.
·
Imekamilisha
tafsiri ya Kiswahili ya Sera ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ya mwaka 2019
pamoja na nakala nyepesi ya Sera hiyo kwa lugha ya Kiswahili na vikatuni kwa
ajili ya urahisi wa kueleweka kwa wananchi. Jumla ya nakala 50 za nakala
nyepesi zimetolewa. Pia, imekamilisha Mpango Mkakati wa Wizara na kuchapisha
nakala 300 za Mpango mkakati huo na tayari zimeshanza kufanyiwa kazi.
·
Inaendelea
na hatua ya kutayarisha Rasimu ya Sera ya Mafunzo Kazi (Apprenticeship Policy)
ambapo imefanya vikao na Watendaji wa taasisi mbali mbali Unguja na Pemba juu
ya kuimarisha rasimu ya Sera ya hiyo na hivisasa iko katika hatua ya kujadiliwa
na Kamati ya Uongozi ya Wizara.
·
Imekamilisha
kutoa matokeo ya Utafiti wa ukatili na Udhalilishaji katika maeneo ya kazi
katika sekta binafsi ambapo matokeo yameonyesha kuwa waajiri wanaume wanafanya
ukatili na udhalilishaji kwa asilimia 44.2 ukilinganisha na waajiri wanawake
ambao wanafanya kwa asilimia 18.2. Vile vile, tatizo la kutoleana maneno mabaya
limeripotiwa na karibu asilimia 90 ya waliohojiwa. Pia, Asilimia 72.5 ya
wahojiwa wamesema kuwa mwenendo mzima wa kuzisimamia kesi za ukatili na
udhalilishaji wa kijinsia katika vyombo vya sheria hauridhishi na hakuna
kitengo maalum ndani ya taasisi binafsi zilizohojiwa, kinachoshughulikia
malalamiko ya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia. Vile vile, sababu zilizotajwa
zinazopelekea ukatili na udhalilishaji ni pamoja na kupungua kwa mashirikiano
baina ya wakuu wa taasisi na waajiriwa, kuwepo kwa watumiaji wa ulevi,
mazingira yasiyo salama, kiwango kidogo cha mshahara na kutopata mshahara kwa
wakati. Hivyo, imebainika kuwa mfumo maalum wa kushughulikia tatizo la ukatili
na udhalilishaji wa kijinsia katika sekta binafsi unahitajika.
·
Kwa kushirikiana
na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mjini magharibi imekamilisha zoezi la kufanya
tathmini ya tatizo la Omba omba kwa Mkoa wa Mjini Magharibi. Jumla ya omba omba
24 kati ya 42 walifanyiwa tathmini ya kina kwa kutambuliwa wanapotoka, sababu
za kujiingiza katika kuomba na hatua gani zichukuliwe. Tathmini imeonyesha
kwamba asilimia 87 ya Omba omba ni wanawake na walifanyiwa tathmini ya kina kwa
kutambuliwa Shehia wanazotoka ambazo ni Chumbuni, Kilimahewa juu, Mtopepo,
Kwaalinato, Mkele, Rahaleo, Mwembe makumbi, Mtoni Kidatu, Nyerere, Amani, Fuoni
Uzi, Tomondo na Kisauni. Pia, iliangalia sababu za kujiingiza katika kuomba na
hatua gani zichukuliwe. Imegundulika kuwa asilimia 17 (4) ya Omba omba
wanafanya shughuli ya kuomba kutokana na matatizo ya kimaisha na asilimia 83
walionyesha kuomba ni tabia yao lakini sishida za kimaisha. Wengine wanaomba
kwa kuiga watu na kutafuta njia rahisi za kujipatia kipato.
·
Kwa
kushirikiana na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali imeimarisha uaptikanaji wa
takwimu za matukio ya ukatili na udhalilishaji wa wanawake na watoto na imeanza
kutoa taarifa za takwimu za matukio ya makosa ya jinai ya ukatili na
udhalilishaji wa wanawake na watoto za mwaka 2017/2018 na 2018/2019 katika
vyombo vya habari mbali mbali ikiwemo ZBC redio na TV, Chuchu FM, Daily News,
Nipashe, The Guardian, Bahari FM. Zenj FM, Hits FM, Zanzibar leo, Majira,
Island, Mwenge, Uhuru, Mwananchi, Habari leo, Zanzibbar Cable, On line TV, TBC
redio na TV pamoja na ITV. Pia, imefanya kipindi maalum Mubashara na ZBC redio
kutoa takwimu hizo kwa wananchi.
·
Imeshiriki
katika Kikao cha Maandalizi ya Utafiti wa Taasisi za Kijamii na Jinsia Dodoma
ambapo utafiti huu utafanywa kuangalia ni namna gani taasisi za kijamii kama
familia, skuli, madrasa, mila, desturi n.k zinavyochangia au kupunguza masuala
ya ukatili na udhalilishaji wa wanawake na watoto nchini. Tayari nyenzo za
kufanyia utafiti huo za ngazi ya Kaya na Binafsi zimeshatayarishwa na kupitiwa
na wadau kwa kuimarishwa. Mafunzo kwa wakusanya data yatafanyika muda wowote na
zoezi la utafiti litaanza mara baada ya mafunzo Tanzania Bara na Visiwani.
·
Imetayarisha
vipindi 75 vya redio na televisheni ambapo vipindi 55 vimerushwa kupitia ZBC,
Hits FM pamoja na CHUCHU FM na Vipindi 20 vilirushwa kupitia ZBC TV na ZCTV.
Pia imetayarisha Makala 10 katika Magazeti mbali mbali na habari 103 zinazohusu
shuguli za Wizara ziliziandikwa na kurushwa hewani kupitia vyombo mbali mbali
vya habari. Documentary 2 zinazohusu masuala ya Wazee na Wanawake
zilitayarishwa pamoja na kipindi maalum cha utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi
kwa miaka 4 na utekelezaji wa miaka 9 wa kipindi cha awamu ya 7 ya Dkt. Ali
Mohamed Shein. Pia, imetayarisha tangazo maalum la Wazazi kufanya jitihada ya
kuwalinda watoto kuepukana na maradhi ya Corona kwa kutowaachia kuzurura ovyo
na kufuata maelekezo ya kinga yanayotolewa na kulirusha kwenye vyombo vya
habari.
·
Imekamilisha
zoezi la kuandaa taarifa ya utekelezaji wa Maazimio ya Ulingo wa Beijing kwa
upande wa Zanzibar na taarifa hiyo imewasilishwa Tanzania Bara na kutayarishwa
taarifa moja ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Taarifa hii imeshawasilisha
Umoja wa Afrika na pia imeshawasilishwa Umoja wa Mataifa. Pia, imemalizia
kuratibu uandaaji wa taarifa ya Zanzibar ya utekelezaji wa Mkataba wa Kimataifa
wa Kupinga aina zote za ubaguzi dhidi ya Wanawake (CEDAW) na taarifa imeshawasilishwa
Tanzania Bara na imeshatayarishwa Taarifa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
·
Imefanya
ufuatiliaji kwa maeneo tofauti ikiwemo Makao ya Wazee Welezo na Sebleni na
Nyumba ya Watoto Yatima Mazizini, Chuo cha Kulea na Kukuza Wajasiriamali na
Chuo cha Barefoot cha kinamama pamoja na kuwapitia wanufaika waliofungiwa umeme
wa jua. Aidha, imefanya ufuatiliaji katika shuguli mbali mbali za Wizara ikiwa
ni pamoja na vikundi vilivyopatiwa mikopo na Mfuko wa Uwezeshaji katika maeneo
ya Kaskazini Unguja ili kuona mafanikio yaliyofikiwa na changamoto zilizopo.
Changamoto zilizopatikana zimewasilishwa sehemu husika kwa kufanyiwa kazi.
·
Inaendelea
na hatua ya kuandaa Mpango Mkakati wa Takwimu wa Wizara kwa kushirikiana na
Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali. Imeshandaa viashiria vya Wizara ambavyo
vitatumika kuandaa nyenzo za kukusanya takwimu za Wizara. Mpango Mkakati
umeshakamilika na uko tayari kwa kutumika. Pia, imeandaa Mpango kazi (Roadmap)
ya Kuimarisha Takwimu za Wizara ambayo utekelezaji wake utaenda sambamba na
Mpango Mkakati wa Takwimu wa Wizara.
·
Imeratibu Kikao cha Mashirikiano baina ya Mfuko wa Uwezeshaji Kiuchumi
Zanzibar na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (National Economic
Empowerment Council (NEEC) na kukubaliana kushirikiana katika kubadilishana
taarifa, kutafuta rasilimali kwa pamoja, maonyesho ya biashara na mafunzo kwa
Watendaji wa pande zote mbili. Pia, Kikao cha mashirikiano ya utendaji baina ya
Wizara ya afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ya Tanzania bara na
Wizara ya Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Wanawake na Watoto kilifanyika Dodoma ambapo
Wizara zimekubaliana kuimarisha mashirikiano katika masuala ya Ustawi wa Jamii,
Wazee, Wanawake, Jinsia na Watoto.
·
Kwa
kushirikiana na Watendaji wa Wizara ya Fedha na Mipango imeshiriki katika
uandaaji na Uwasilishaji wa Taarifa ya Hiari ya Nchi juu ya Utekelezaji wa
Malengo Endelevu ya Ulimwengu katika kipengele cha Usawa wa Kijinsia, Ajira na
Uwezeshaji wa Wanawake. Ambapo tumejifunza kuwa mbali ya Mafanikio tuliyonayo
lakini bado tunahitaji kulisimamia imara suala la kuimarisha Bajeti
inayozingatia jinsia; suala la uwezeshaji Wanawake kiuchumi; kuwahamisha
Wanawake kushika nafasi mbali mbali za maamuzi; kupambana na mimba za utotoni;
ndoa za umri mdogo na ukatili na udhalilishaji hasa katika sehemu za kazi,
ajira hasa kwa vijana na suala la ukatili wa wafanyakazi wa majumbani.
33.
Mheshimiwa Spika;; Katika mwaka
wa fedha 2020/2021 Wizara kupitia Programu ya Uratibu wa Mipango Sera na Tafiti
za Wizara itafanya tathmini ya kuangalia mchango wa Mfuko wa Uwezeshaji katika
Kuzalisha Ajira na kuongeza kipato kwa wanachama wake; Itafanya tathmini ya
Kuangalia namna ya Kuanzisha Mfuko wa Fidia Zanzibar; Itafanya tathmini ya Mapitio
ya Utekelezaji wa Mpangokazi wa Kupinga Vitendo vya Ukatili na Udhalilishaji Wanawake
na Watoto kwa muda wa Kati; Itakamilisha na kuchapisha Sera ya Mafunzo Kazi;
Itaandaa taarifa ya mwaka 2019/2020 ya utekelezaji wa Mpango wa kitaifa wa
kupambana na vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa wanawake na watoto;
Itafanya Ufuatiliaji wa Shughuli za Wizara; Itaratibu utekelezaji wa Programu
na miradi ya Wizara; Itaimarisha mawasiliano ya Wizara na Itaimarisha
Mashirikiano ya Kitaifa, Kikanda na Kimataifa kwa shughuli za Wizara.
34.
Mheshimiwa Spika;; ili Programu ya Uratibu wa Mipango Sera na Tafiti za
Wizara iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi kwa mwaka wa fedha 2020/2021,
naliomba Baraza lako liidhinishe jumla ya Shilingi
Milioni Mia Tatu Thamanini na Nane, Sitini na Moja Elfu, Mia Mbili na kumi na
Sita (Tshs. 388,061,216).
Programu ndogo SQ010402: Utawala
na Uendeshaji
Lengo Kuu: Kuweka Mazingira bora ya kazi kwa
Wafanyakazi.
35. Mheshimiwa Spika; Programu ndogo hii ina
jukumu la kuratibu na kusimamia utekelezaji wa shughuli
za uendeshaji na utumishi za Wizara Unguja. Programu ilijipangia kutekeleza
yafuatayo:
·
Imekamilisha ujenzi wa
ghorofa ya pili ya jengo la Wizara lililopo Mwanakwerekwe na kwa sasa inatumiwa
na Kamisheni ya Kazi jambo ambalo kwa kiasi kikubwa limerahisisha upatikanaji
wa huduma zinazotolewa na Wizara.
·
Kwa kushirikiana na Tume
ya Utumishi Serikalini imekamilisha taratibu za uajiri wa Wafanyakazi wapya 73
kwa Unguja na Pemba, 35 wakiwa ni wanaume na 38 wanawake ili
kuongeza ufanisi katika Idara ya Uendeshaji na Utumishi, Idara ya Maendeleo ya
Ushirika, Idara ya Wazee na Ustawi wa Jamii. Kati yao 2 ni watu wenye ulemavu.
·
Imefanya malipo ya bima kwa gari zote
za Wizara kama agizo la Serikali linavyoelekeza, pamoja na kuzifanyia ukaguzi
wa kawaida wa kiufundi gari 8, likiwemo Basi linalotumika kusafirisha
watendaji wa kitengo cha Pencheni jamii kipindi cha uhakiki na ulipaji wa
pencheni hiyo. Aidha, imeendelea kulipia gharama za umeme, maji, vifaa vya
usafi, pamoja na kuimarisha kitengo cha TEHAMA kwa kununua CCTV Cameras za
kisasa ambazo kwa kiasi kikubwa zitasaidia kuimarisha usalama na kurahisisha
mawasiliano katika ofisi yetu.
·
Imesimamia ulipaji wa
posho la likizo kwa wafanyakazi 63 ( 40 kwa Unguja na 23
kwa Pemba), malipo ya muda wa ziada kwa wafanyakazi 15 na imefuatilia
malipo ya kiinua mgongo kwa wastaafu 10 kwa Unguja na Pemba.
·
Imeendesha mafunzo ya
ndani yanayohusu kupiga vita vitendo vya rushwa, utawala bora, maadili ya kazi
na kanuni za utumishi wa umma.
·
Imelipia ada ya mafunzo
ya awali “Induction Course” kwa wafanyakazi kumi na mbili (12). Aidha, inaendelea
kuwasaidia ada za masomo wafanyakazi watano (5) ambapo kwa ngazi za shahada ya
pili ni wawili (2) na wafanyakazi watatu (3) katika
mafunzo ya udereva.
·
Programu imeendelea
kukiimarisha kitengo cha Habari na Uenezi na kwa kushirikiana na vyombo mbali
mbali vya habari kimeweza kurusha habari zinazohusu shughuli za Wizara na kwa
mwaka 2019/2020 kimetoa jumla ya vipindi vya Redio 65,
Televisheni 20, makala 23.
·
Kupitia Mkataba wa Utoaji
wa huduma kwa Mteja Wizara imeendelea kutoa elimu kwa
wanananchi ili kuwapa uelewa juu ya fursa na huduma zinazopatikana katika
Wizara.
·
Imekamilisha upembuzi
yakinifu kwa wafanyakazi wa idara zote zilizomo ndani ya Wizara kwa mwaka wa
fedha 2019/2020 kwa lengo la kwenda sambamba na mpango mkakati wa
rasilimali watu (2017/2021) wa Wizara na Taasisi zilizopo chini yake.
·
Imeendelea kugharamia safari za ndani
na nje ya nchi kwa Viongozi na Maafisa wa Wizara ili kuweza kushiriki Mikutano
ya kikanda, Kitaifa na Kimataifa kwa manufaa ya Wizara na Taifa kwa ujumla.
36. Mheshimiwa Spika; Katika mwaka wa fedha
2020/2021 Wizara kupitia Programu ya Utawala na Uendeshaji itasimamia ulipaji
wa mishahara, posho la likizo, malipo ya muda wa ziada na kufuatilia malipo ya
viinua mgongo kwa wastaafu wetu, tukiwa na lengo la kuhakikisha wafanyakazi
wanapatiwa stahiki zao bila kuchelewa. Katika kuwajengea uwezo wafanyakazi
wetu, Wizara itaendelea kusimamia mafunzo ya awali (Induction Course) kwa
wafanyakazi wapya walioajiriwa. Programu itaandaa mafunzo yatakayolenga
kuhamasisha uwajibikaji ikiwemo kujiweka mbali na vitendo vya rushwa, pamoja na
kuratibu mafunzo ya muda mfupi na ya muda mrefu kwa wafanyakazi wake. Pia
Wizara itasimamia ununuzi wa jenereta la akiba ili kujihakikishia huduma
zinazotolewa na Wizara zinaendelea kupatikana kwa urahisi pale
umeme wa gridi ya Taifa unapokosekana.
37. Mheshimiwa
Spika; Ili Programu ya Utawala na Utumishi iweze kutekeleza
majukumu yake kwa ufanisi kwa mwaka wa fedha 2020/2021; Naliomba Baraza lako Kuidhinisha
jumla ya Shilingi Bilioni Moja, Milioni
Mia Tisa Thalathini na Nane, Thalathini na Tano Elfu, Mia Nne na Thamanini (Tshs.1,938,035,480).
Programu ndogo SQ010403: Uratibu na Utekelezaji wa shughuli za Wizara Pemba.
Lengo kuuu: Kuratibu
na Kusimamia Mipango na Uendeshaji wa shughuli za Wizara Pemba.
38. Mheshimiwa Spika; Programu ndogo hii ina
jukumu la kuratibu na kusimamia utekelezaji wa shughuli
za Wizara Pemba na inahusisha Idara ya Utumishi na Uendeshaji pamoja na Idara ya Mipango,
Sera na Utafiti. Programu kwa mwaka wa fedha 2019/2020 imetekeleza yafuatayo:-
· Imeendelea kuwasaidia wafanyakazi
watano (5) kwa mafunzo ya ndani.
Kati ya hao Wafanyakazi wawili (2) (mwanamme 1 na mwanamke 1) katika mafunzo ya
muda mrefu wa ngazi ya shahada ya pili katika fani ya Teknolojia ya habari na
ngazi cheti katika fani ya utunzaji wa kumbukumbu na Wafanyakazi watatu (3) (mwanamme 1 na wanawake 2) wa Mafunzo ya muda mfupi katika fani
ya Ununuzi na ugavi na uandishi wa miradi.
· Imelipa fedha za likizo kwa
wafanyakazi 24 na wafanyakazi 12 wamelipwa posho la masaa ya ziada. Pia,
imelipia gharama za safari za ndani ya nchi ili kushiriki katika vikao na
shughuli mbali mbali za wizara Unguja.
· Imefanya manunuzi ya magazeti pamoja
na kulipia gharama za umeme, maji, mafuta, na huduma za mtandao. Pia, imefanya
matengenezo vyombo vya moto (5) pamoja na kulipa bima gari (1) na vespa (6).
· Imefanya ziara 4 za ufuatiliaji na
tathmini kwa madhumuni ya kuboresha utendaji wa shughuli mbali mbali za Wizara
ikiwemo Wanufaika wa Mikopo, maendeleo ya Vikundi vya Ushirika, Nyumba ya Wazee
Limbani, zoezi la pencheni jamii, mabaraza ya watoto ya Shehia, Kamati za
Shehia za kupinga Udhalilishaji na utekelezaji wa Sheria za Kazi na usimamiaji
wa Sheria ya Usalama na Afya Kazini katika sekta binafsi. Changamoto mbalimbali
zilzobainika katika maeneo haya zimeweza kufanyiwa kazi. Aidha imewajengea
uwezo watendaji 30 (wanawake 13 na wanaume 17) wa Wizara katika masuala ya
Ufuatiliaji na tathmini wa shughuli za Wizara.
· Programu imefanya vikao viwili (2)
kwa watendaji 30 (wanaume 11 na wanawake 19) wa Wizara juu ya maswala Mtambuka
kama Udhalilishaji, UKIMWI na umuhimu wa lishe kwa jamii.
· Imeratibu uandaaji wa ripoti mbali
mbali za utekelezaji ikiwemo ripoti ya utekelezaji ya Bango kitita, ripoti za
utekelezaji za Ilani za Uchanguzi ya mwaka 2015/2020, pamoja na utayarishaji wa
mpango wa Bajeti wa muda wa kati wa Wizara (MTEF) ya mwaka 2020-2023.
39. Mheshimiwa Spika; Kwa mwaka
wa fedha 2020/2021, Wizara kupitia program ya Uratibu na Utekelezaji wa
Shughuli za Wizara Pemba itasimamia upatikanaji wa maslahi na mafao ya
wafanyakazi yakiwamo mishahara, posho la likizo, malipo ya viinua mgongo,
malipo ya muda wa ziada, itawaendeleza wafanyakazi, itafanya ununuzi wa
Pikipiki 1, na kufanya matengenezo ya vifaa na pamoja na kusimamia upatikanaji
wa huduma muhimu za uendeshaji wa ofisi; itasimamia shughuli za ufuatiliaji
na tathmini, itawajengea uwezo watendaji katika masuala ya takwimu,
utayarishaji wa ripoti za utekelezaji wa kazi za Wizara pamoja na kuratibu
masuala mtambuka na kusimamia utekelezaji wa sera na mpango mkakati wa Wizara.
40. Mheshimiwa Spika; Ili Programu
ya Uratibu na Utekelezaji wa Shughuli za Wizara Pemba iweze
kutekeleza majukumu yake kwa mwaka wa fedha 2020/2021; Naliomba Baraza lako
Kuidhinisha jumla ya Shilingi Milioni
Mia Nane Sitini na Sita, Laki Tano Ishirini na Tatu, Mia Sita na Sitini
(Tshs. 866,523,660).
41.
Mheshimiwa Spika; Ili Programu Kuu ya Uendeshaji na Uratibu wa Wizara ya Kazi,
Uwezeshaji, Wazee, Wanawake na Watoto itekeleze majukumu yake kwa ufanisi
kwa mwaka wa fedha 2020/2021; naliomba Baraza lako Tukufu Kuidhinisha jumla ya Shilingi Bilioni Tatu, Milioni Mia Moja
Tisini na Mbili, Laki Sita Ishirini Elfu, Mia Tatu Hamsini na Sita
(3,192,620,356).
PROGRAMU KUU PQ 0105: USIMAMIZI WA SHERIA ZA KAZI, UKAGUZI KAZI NA KAZI ZA STAHA KWA WOTE
Matokeo
ya Muda Mrefu: Upatikanaji wa Kazi za Staha kwa
Vijana na Kufuata Kanuni na Sheria za Kazi
Programu ndogo: SQ010501: Uratibu wa Upatikanaji wa Ajira za Staha
Lengo kuu: Kuongeza kiwango
cha Ajira zenye Staha na kupunguza kiwango cha ukosefu wa Ajira kwa Vijana
42. Mheshimiwa Spika; katika
kutekeleza majukumu yake ya uratibu na usimamizi wa Sera ya Ajira ya Zanzibar
ya mwaka 2009. Kwa mwaka wa fedha 2019/2020, Programu ilitekeleza yafuatayo.
·
Imeweza kuratibu upatikanaji
wa ajira 659 (421 Wanaume na Wanawake 238) katika Sekta Binafsi nchini na Ajira
909 (Wanaume 83 na Wanawake 826) nje ya nchi, na kwa sasa imo katika kuboresha
mfumo wa soko la Ajira ili uweze kukusanya na kuchambua mwenendo wa fursa za
ajira kwa ufanisi kwa lengo la kubainisha maeneo muhimu yenye fursa na mafunzo
yanaohitajika.
·
Kwa kushirikiana na Ofisi ya
Ubalozi nchini Qatar imeweza kuratibu upatikanaji wa fursa za mafunzo kazi kwa
vijana wa kike nchini Qatar, vijana 16 wamefaidika na fursa hio na kuanza
masomo katika chuo cha malezi ya watoto nchini Qatar, chuo kinachojulikana kwa
jina la Qatar Nanny Training Academy (QNTA). Fursa hizo zinatarajiwa kuongezeka
zaidi katika kipindi kijacho ambapo wahitimu wa mafunzo hayo wataunganishwa na ajira
mara tu baada ya kumaliza masomo yao.
·
Imeendelea kuratibu vyema Taasisi zote za Wakala Binafsi wa Ajira
ambapo kwa sasa zimefikia taasisi 15 zilizopatiwa leseni ya wakala wa Ajira
Binafsi.
·
Imefanya mikutano na Kamati za Kisekta za Uzalishaji na Ukuzaji wa
Ajira za Wilaya kwa Unguja na Pemba ili kuibua fursa mpya za ajira zinazoweza
kupatikana katika wilaya zetu kupitia sekta za Kilimo, Utalii, Mazingira, Ujenzi,
Sanaa na Michezo.
·
Imefanya mikutano miwili na
wadau wakuu wa sekta ya usafiri wa nchi kavu (Magari ya Abiria) ili kujadili
hatua ya urasimishaji wa sekta ya Usafiri wa Umma hususani wa Daladala kwa
lengo la kufikia ajira za staha kwa wote.
·
Inaendelea na uratibu wa programu ya majaribio awamu ya pili ya Mafunzo
Kazi ambapo jumla ya mikutano minne ya uratibu huo imefanyika na jumla ya
vijana 120 wamejiunga na mafunzo hayo kutoka wilaya zote za Unguja na Pemba,
aidha Sera ya Mafunzo Kazi inategemewa kukamilika.
·
Imeendelea na maandalizi ya Mafunzo Kazi kwa vijana ambao hawatambuliwi
na mfumo wa elimu, hawana ajira na hawaajiriki (NEET) ili kufikia lengo la kutomuacha
mtu yeyote nyuma kwenye upatikanaji wa
fursa za Ajira
·
Imetoa mafunzo kwa Vijana 40 wanaotafuta ajira ili waweze kukabiliana
na mbinu mbali mbali zinazotumika katika usaili wa kutafuta Ajira.
·
Imeandaa programu tatu za
Ajira ili ziweze kuongeza fursa za ajira na hatimae vijana waweze kuzitumia kwa
kuajiriwa na kujiajiri wenyewe.
43. Mheshimiwa Spika; Programu
ya Uratibu wa Upatikananji wa Ajira za Staha kwa mwaka wa fedha 2020/2021,
imepanga kuwawezesha na kuelimisha jamii juu ya upatikanaji wa ajira za staha
kwa kutangaza nafasi za fursa za ajira zitakazopatikana kupitia Mfumo wa
Taarifa za Soko la Ajira na vyombo vya habari; itaimarisha mashirikiano na
wadau wa nje na ndani katika kutafuta fursa za ajira kwa vijana; itatoa mafunzo
kwa watafuta kazi juu ya kujiajiri na kuajirika; itaendelea kusimamia program
ya mafunzo kazi kwa wanagenzi.
44. Mheshimiwa Spika; Ili Programu ya Upatikanaji wa Ajira za Staha iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi kwa mwaka wa fedha 2020/2021; naliomba Baraza lako
kuidhinisha ruzuku ya Shilingi Milioni
Mia Mbili Ishirini na Nne, Laki Nne Hamsini na Mbili Elfu, Mia
Tatu na Thamanini (Tshs 224,452,380).
Programu Ndogo SQ010502: Usimamizi wa Usalama na Afya Kazini.
Lengo Kuu: Kuimarisha masuala ya Usalama na
Afya katika sehemu za kazi
45. Mheshimiwa
Spika; Programu hii inatekelezwa na Idara ya Usalama
na Afya Kazini na inasimamia utekelezaji wa Sheria Namba 8 ya Mwaka 2005 ya
Usalama na Afya Kazini. Kwa mwaka
wa fedha 2019/2020; Programu
imetekeleza yafuatayo:-
·
Imefanya usajili wa sehemu za kazi 78 (57
Unguja na 21 Pemba) ili kuzitambua na kuweka taarifa zao kwenye daftari la
usajili wa sehemu za kazi. Hii itarahisisha shughuli za ukaguzi kwa kutambua
mapema mazingira ya kazi zao, hatari zinazoweza kutokea katika sehemu hizo na
hivyo kutoa ushauri na maelekezo yanayofaa, kabla ya kutokea tatizo.
·
Imefanya ukaguzi wa sehemu za kazi 137 (84
Unguja na 53 Pemba) ili kuangalia hali ya usalama na afya katika maeneo hayo.
Ushauri ulitolewa juu ya kurekebisha kasoro zilizobainika. Ufuatiliaji
uliofanywa baada ya ukaguzi, umeonesha kuwa kasoro nyingi zimerekebishwa baada
ya kufuatwa ushauri uliotolewa.
·
Imefanya uchunguzi wa matukio ya ajali na
maradhi yatokanayo na kazi katika
sehemu (5) za kazi ambazo ziliripotiwa kutokea kwa ajali
hizo wakati wafanyakazi wakiendelea na kazi. Wafanyakazi 2 walifariki kwa
kufukiwa na udongo katika ujenzi wa mtaro wa kupitishia maji ya mvua na mfanyakazi 1 wa kampuni ya CCE alifariki
baada ya kukanyagwa na gari wakati wa ujenzi wa barabara.
·
Katika kukuza uelewa wa masuala ya usalama
na afya kazini, Idara imeandaa na kurusha hewani vipindi vitatu (3) vya radio
na vipindi vinne (4) vya televisheni kupitia Shirika la Utangazaji la Zanzibar
(ZBC). Vile vile Idara imetoa mafunzo
kwa wawakilishi 80 (50 Unguja na 30 Pemba) wa masuala ya usalama na afya kazini
kutoka kwenye Wizara na taasisi za umma ili waweze kufahamu majukumu yao na
wajibu wao wakiwa kwenye maeneo yao ya kazi kwa mujibu wa Sheria ya Usalama na
Afya Kazini.
·
Ili kukuza mashirikiano na uratibu wa
masuala ya usalama na afya kazini, imewajengea uwezo watendaji wake kwa kuweza kuhudhuria mikutano na
makongamano mbali mbali ya mashirikiano Kitaifa, Kikanda na Kimataifa juu ya
Masuala ya Usalama na Afya Kazini katika sekta ya Mafuta na Gesi Asilia na
Virusi vya Ukimwi na Ukimwi na TB sehemu za kazi. Pamoja na hayo, Uratibu wa
shughuli za usalama na afya kazini unaendelea kufanyika ili kupata mashirikiano
kwa taasisi zote zinazotakiwa kufanya kazi kwa pamoja.
46. Mheshimiwa
Spika; Katika mwaka wa fedha 2020/2021, Programu imejipangia kuendelea
Kuimarisha utekelezaji wa Sheria Nambari 8 ya mwaka 2005 ya Usalama na Afya
Kazini; Itafanya ukaguzi wa sehemu za Kazi 300; Itafanya
usajili wa sehemu za kazi 120; Itatoa elimu kwa waajiri na wafanyakazi 170
(Sekta ya Umma 90 na Sekta Binafsi 80); Itaimarisha mashirikiano na uratibu wa
masuala ya usalama na afya kazini na itakuza uelewa wa jamii kupitia vyombo vya
habari.
47. Mheshimiwa
Spika; Ili Programu ya Usimamizi na Usalama wa Afya Kazini iweze
kutekeleza majukumu yake kwa mwaka wa fedha 2020/2021; naliomba Baraza lako kuidhinisha jumla ya Shilingi Milioni Mia Mbili na Sita, Laki Tatu
na Saba na Mia Tatu na Ishirini (Tshs
206,307,320) kwa ajili ya matumizi ya kazi za
kawaida.
Programu Ndogo: Q010503: Usimamizi wa Viwango vya Kazi vya Kitaifa na Majadiliano ya Pamoja Kazini
Lengo
Kuu: Kuhakikisha Kunakuwepo
Utekelezaji Mzuri wa Sheria za Kazi.
48. Mheshimiwa
Spika; Kamisheni
ya Kazi ina jukumu la kusimamia utekelezaji wa Sheria za kazi katika sekta za
binafsi kwa hapa Zanzibar. Pia, Kamisheni ya Kazi inajukumu la kufanya ukaguzi
kazi kwa taasisi hizo, kusimamia ajira za wafanyakazi wa kigeni, kuthibitisha
Mikataba ya Wafanyakazi wazalendo na
wageni na kuimarisha mahusiano mema kati ya waajiri na waajiriwa sehemu za
kazi. Kwa mwaka wa fedha 2019/2020, Programu imetekeleza
shughuli kuu zifuatazo:-
· Imefanya ukaguzi kazi kwa Taasisi 380 (Unguja ni 314 na Pemba ni 66). Ukaguzi huo unafanyika ili kusimamia ipasavyo
utekelezaji wa Sheria za Kazi kwa taasisi zote.
· Pia, imefanya ukaguzi maalumu kwa Taasisi 403 kati ya hizo (Unguja ni 324 na Pemba ni 79)
ili kuona utekelezaji wa ulipaji wa kima cha chini cha mishahara tokea
kilipotangazwa mwezi Julai 2017.
·
Imethibitisha mikataba ya kazi 2,329
(Unguja ni 2,082 na Pemba ni 247) kwa wafanyakazi
ili kuhakikisha inaendana na Sheria za Kazi ikiwa ni miongoni mwa haki yao ya msingi kwa mujibu wa
Sheria za Kazi. Wakati wa uthibitishwaji wa Mikataba hiyo wafanyakazi husika
husomewa Mikataba hiyo na Maafisa Kazi ili kupata uelewa mzuri juu ya
haki zao.
·
Imepokea
migogoro ya kazi 288 iliyowasilishwa (Unguja 236 na Pemba 52). Migogoro 52 ilitatuliwa
kwa njia ya upatanishi (mediation)
(Unguja 50 na Pemba 2),
Migogoro 84 ilitatuliwa kwa njia ya usuluhishi (arbitration)
(Unguja 61 na Pemba 23), Migogoro
67 imepelekwa
Mahkama ya kazi kwa taratibu nyengine za kisheria. Migogoro 6
iliamuliwa nje ya kitengo. Aidha,
Migogoro 24 imefutwa kutokana na
sababu za kutokufika kwa pande zote mbili pamoja na kuchelewa kufungua shauri
na Migogoro
55 inaendelea katika ngazi
ya usuluhishi
na uamuzi.
Migogoro yote hiyo iliyowasilishwa inahusu kukatishwa Mikataba ya Kazi kwa wafanyakazi, kutokulipwa
kwa kiwango cha mshahara stahiki kwa mujibu wa sheria, na kufukuzwa kazi.
· Imewapatia
Vibali vya Kazi jumla ya wafanyakazi
wa kigeni 1,441 kutoka Mataifa mbali mbali (Italy, India, China, Uingereza na
Nchi za Afrika ya Mashariki) kufanya kazi nchini. Idadi kubwa ya wafanyakazi waliopatiwa
vibali hivyo ni kutoka Sekta
Binafsi (hoteli na Vyuo) na Sekta za Umma (Afya, Ujenzi na Utalii).
· Imeanza hatua ya kuandaa database ya
Kamisheni ya Kazi ambapo Hadidu Rejea ya utayarishaji wa Database imekamilika
na hatua inayoendelea ni kutangazwa kwa wakandarasi ili kupata wataalamu wa
kuitengeneza.
·
Imefanya
Ukaguzi wa Vyama vya Wafanyakazi kwa matawi 5; matawi mawili (2) Mkoa wa Kaskazini Unguja, Matawi mawili (2) Mkoa wa Kusini
Unguja, na Tawi moja Mkoa wa Kusini Pemba.
·
Imetoa
elimu ya Sheria za Kazi kwa Taasisi 26 (Unguja 17 na Pemba 9). Pia, imerusha vipindi tisa (9) kuhusu elimu hiyo kupitia
vyombo vya habari. Kati ya vipindi hivyo 4 vilirushwa ZBC TV, ZBC Redio
3 na 2 Chuchu FM. Lengo hasa la kutoa taaluma hiyo ni kujenga uelewa kwa Waajiri,
Wafanyakazi na jamii kwa jumla juu ya Sheria za Kazi.
49. Mheshimiwa Spika; kwa mwaka wa fedha 2020/2021 Kamisheni ya Kazi kupitia
programu ya Usimamizi wa Viwango vya Kazi vya Kimataifa na Majadiliano ya Pamoja mbali na majukumu mengine Itafanya ukaguzi kazi kwa Taasisi 700;
Itathibitisha mikataba ya kazi kwa wazalendo 6,000; Itakagua vyama vya waajiri
na wafanyakazi 16; itatoa elimu ya Sheria za Kazi kwa taasisi 45 na itarusha
vipindi 25 kupitia vyombo vya habari.
50. Mheshimiwa Spika; Ili
Programu ya Usimamizi wa Viwango vya Kazi vya Kimataifa na Majadiliano ya Pamoja iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi kwa mwaka wa fedha 2020/2021; naliomba Baraza lako Kuidhinisha Ruzuku ya jumla ya Shilingi Bilioni Moja, Milioni Arobaini na Nane, Laki Moja Arobaini Elfu na Mia Tatu (Tshs.1,048,140,300)
51.
Mheshimiwa Spika; Ili Programu Kuu ya Usimamizi wa Sheria za Kazi, Ukaguzi Kazi na Kazi za Staha kwa wote
itekeleze majukumu yake kwa ufanisi kwa mwaka wa fedha 2020/2021; naliomba
Baraza lako Tukufu Kuidhinisha jumla ya Ruzuku ya Shilingi Bilioni Moja, Milioni Mia Nne Sabini na Nane, Laki Tisa
(1,478,900,000).
MAOMBI YA FEDHA KWA PROGRAMU ZILIZOPANGWA KUTEKELEZWA MWAKA WA FEDHA 2020/2021
52. Mheshimiwa
Spika; Ili Wizara ya Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Wanawake na
Watoto iweze kutekeleza Programu zake kwa ufanisi kwa mwaka wa fedha 2020/2021,
naliomba Baraza lako Tukufu iidhinishe jumla ya Shilingi Bilioni Kumi na Nane, Milioni Mia Tano na Kumi, Laki Nne na
Hamsini na Moja Elfu,
(Tshs.18,510,451,000/-). Kati ya hizo,
Shilingi Bilioni Kumi na Tano, Milioni Mia Mbili Hamsini na Moja, Laki Tatu
(15,251,300,000/-) ni kwa ajili ya Kazi za Kawaida ambapo Shilingi Bilioni Kumi, Milioni Tisini na Tano, Laki Mbili (10,095,200,000/-) ni matumizi ya Uendeshaji
wa Ofisi; Shilingi Bilioni Tatu, Milioni Mia Tano Thalathini na Tatu,
Laki Tatu (3,533,300,000) ni kwa ajili ya Mishahara na Shilingi Bilioni Moja, Milioni Mia Sita Ishirini na Mbili, Laki Nane (1,622,800,000)
Ruzuku. Pia, Shilingi Bilioni Tatu,
Milioni Mia Mbili Hamsini na Tisa, Laki Moja Hamsini na Moja Elfu
(3,259,151,000/-) ni fedha za maendeleo
53. Mheshimiwa Spika; Kati ya Fedha hizo, Shilingi
Bilioni Mbili, Milioni Mia Mbili na Thamanini na Tano, Laki Moja Thalathini na
Sita Elfu, Mia Tano na Arobaini na Nane (Tshs. 2,285,137,548) ni kwa ajili ya kutekeleza
Programu ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi. Shilingi
Bilioni
Kumi na Moja, Milioni Mia Tano Hamsini na Tatu, Laki Saba Tisini na Nne Elfu,
Arobaini na Sita (Tshs.11,553,794,046)
kwa ajili ya kutekeleza Programu ya Hifadhi ya Jamii na Maendeleo ya Wanawake
na Watoto. Shilingi
Bilioni Tatu, Milioni Mia Moja na Tisini na Mbili, Laki Sita Ishirini Elfu, Mia
Tatu Hamsini na Sita
(Tshs. 3,192,620,356) zimetengwa kwa ajili ya kutekeleza Programu ya Uendeshaji
na Uratibu wa Wizara ya Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Wanawake na Watoto na Shilingi Bilioni Moja, Milioni
Mia Nne Sabini na Nane na Laki Tisa (Tsh.1,478,900,000) ni kwa ajili ya utekelezaji wa Programu ya
Usimamizi wa Sheria za Kazi, Ukaguzi Kazi na Kazi za Staha kwa wote (Kiambatanisho namba 11 kinahusika).
54. Mheshimiwa
Spika; Wizara katika kipindi cha mwaka wa fedha 2020/2021 inatarajiwa kukusanya
mapato ya Shilingi Bilioni
Mbili, Milioni Mia Moja na Nane, Laki Tano Hamsini na Tano Elfu (Tshs. 2,108,555,000) kutokana
na Ada za Usajili na Ukaguzi wa Vyama
vya Ushirika, Ada ya Ukaguzi wa Mikataba ya Ajira Nje ya Nchi, Ada ya Ukaguzi
wa Maeneo ya Kazi na Vibali vya Kazi (Kiambatanisho namba 12 kinahusika).
HITIMISHO
55. Mheshimiwa
Spika; Wizara inatekeleza majukumu yake kwa kushirikiana na Watendaji mbali mbali ikiwemo
taasisi za Serikali, taasisi za kiraia na Washirika wa Maendeleo zikiwemo UNICEF,
UN WOMEN, UNDP, UNIDO, UNFPA, ILO, SAVE THE CHILDREN, FHI, MIVARF, HELP AGE
INTERNATIONAL, CSEMA, Milele Foundation, COSTECH, na Jumuiya ya Afrika
Mashariki.
56. Mheshimiwa
Spika; Pia,
Wizara inafanya kazi na Taasisi
za Kiraia nazo ni ZAFELA, ZLSC, UWAWAZA, UWT, ACTION AID, TAMWA, CUZA, Madrasa
Resource Centre, JUMAZA, ZANEMA, ZATUC, Male Network na Pathfinder. Pia, nazishukuru
Taasisi zote za kifedha, ikiwemo PBZ kwa mashirikiano yao mazuri kwa Wizara.
57. Mheshimiwa
Spika; Napenda kuvishukuru vyombo vya habari vya Serikali na
binafsi kwa jitihada kubwa wanayoichukua ya kuelimisha jamii juu ya shughuli
zinazofanywa na Wizara ikiwemo kupiga vita suala la ukatili na udhalilishaji wa
Wanawake na Watoto na mapambano dhidi ya ugonjwa wa Corona ambao kwa njia moja
au nyengine umeathiri wanawake, watoto na sekta ya kazi nchini. Vyombo hivyo ni pamoja na ZBC redio na
televisheni, Gazeti la Zanzibar Leo, Zanzibar Cable televisheni, TBC, AZAM TV,
Zenj FM, Island TV na Hits FM, Redio Jamii za Mtegani, Micheweni, Mkoani na
Tumbatu. Ni vigumu kuvitaja vyote lakini napenda kuvishukuru vyombo vyote vya
habari vilivyoshirikiana nasi.
58. Mheshimiwa
Spika; Mwisho kabisa napenda kuwashukuru watendaji wote wa Wizara ya Kazi, Uwezeshaji,
Wazee, Wanawake na Watoto kuanzia Naibu Waziri Mheshimiwa Shadya Mohammed
Suleiman, Katibu Mkuu Ndugu Fatma Gharib Bilal, Manaibu Makatibu Wakuu Ndugu
Maua Makame Rajab na Ndugu Mwanajuma Majid Abdallah, Kamishna wa Kazi, Ofisa
Mdhamini Pemba, Wakurugenzi na Watendaji wa ngazi zote kwa mashirikiano makubwa
ya kiutendaji wanayonipa katika kutekeleza majukumu yetu Wizara. Wamekuwa
mstari wa mbele kuhakikisha kuwa tunatekeleza majukumu ya Wizara kwa ufanisi
ili kuleta maendeleo endelevu kwa walengwa wetu wote. Yote niliyoyaeleza katika
kitabu hiki ni mafanikio tunayoyapata kutokana na utendaji wao mahiri na thabiti.
Nawaomba waendeleze mashirikiano haya na kuendelea kuwatumikia wananchi wetu.
Namuomba Mwenyezi Mungu adumishe mapenzi na mashirikiano baina yetu katika
kutekeleza majukumu yetu.
59. Mheshimiwa Spika; Naomba kutoa hoja.
Ahsanteni.
MHE.
DKT. MAUDLINE CYRUS CASTICO (MBM)
WAZIRI WA KAZI, UWEZESHAJI, WAZEE, WANAWAKE NA WATOTO
ZANZIBAR
No comments:
Post a Comment