Habari za Punde

Mukhtasari wa hotuba ya Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa, Serikali za mitaa na idara maalum za SMZSERIKALI YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR

MUKHTASARI WA HOTUBA YA WAZIRI WA NCHI,
OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA, SERIKALI ZA
MITAA NA IDARA MAALUM ZA SMZ
MHE. HAJI OMAR KHERI (MBM)
KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI KWA
MWAKA WA FEDHA 2020/2021
KATIKA BARAZA LA WAWAKILISHI LA ZANZIBAR
MEI, 2020
1


MUKHTASARI WA HOTUBA YA WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA, SERIKALI ZA MITAA NA IDARA MAALUM ZA SMZ, MHE. HAJI OMAR KHERI KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA WA FEDHA 2020/2021

UTANGULIZI

1.       Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba Baraza lako Tukufu likae kama Kamati kwa madhumuni ya kupokea, kujadili na hatimaye kuidhinisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha kwa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ kwa mwaka wa fedha 2020/2021.
2.       Mheshimiwa Spika, awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu Muumba Mbingu na Ardhi kwa kutujaalia uhai na uzima na kutuwezesha kukutana hapa leo katika Baraza hili Tukufu tukiwa salama katika hali ya amani na utulivu. Tunamuomba Mwenyezi Mungu atuzidishie neema zake za uhai, atuzidishie amani na utulivu na atuondoshee janga la maradhi ya corona.
3.       Mheshimiwa Spika, baada ya kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu, naomba kutumia nafasi hii adhimu kupitia Baraza lako Tukufu kumshukuru na kumpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dk. Ali Mohamed Shein kwa uadilifu na uongozi wake wenye busara na hekima ambao umeiwezesha nchi yetu kuwa katika hali ya amani na utulivu. Uongozi wake mahiri umekuwa dira sahihi katika kuleta mabadiliko ya kweli ambayo Wazanzibari sote tunayashuhudia katika nyanja mbali mbali ikiwemo Elimu, Afya, Kilimo, Miundombinu na kuongezeka kwa pato la Taifa na maslahi ya Watumishi.
4.       Mheshimiwa Spika, pongezi maalum kwa Mheshimiwa Rais kwa jinsi alivyoweza kutoa maelekezo na kufanya maamuzi magumu katika kupambana na janga la maradhi ya corona kwa faida na maslahi ya Taifa. Napenda kumuahidi Mimi Binafsi na Viongozi wenzangu katika Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum tutaendelea kumuunga mkono  na kufuata maelekezo yake katika kuhakikisha  ugonjwa huu  hauenei na  unaondoka  kwenye Mikoa, Wilaya na Shehia. Aidha, nawasisitiza wananchi kufuata maelekezo ya Serikali na Wataalamu wa afya ili kuyashinda maradhi haya.
5.       Mheshimiwa Spika, nachukua nafasi hii pia kumpongeza Makamu wa Pili wa Rais, Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi kwa kuendelea kumshauri vyema Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi sambamba na kuendelea kuongoza vyema shughuli za Serikali katika Baraza la Wawakilishi na kusimamia vyema utekelezaji wake. Nichukue fursa hii kukupongeza wewe Mheshimiwa Spika kwa jinsi ulivyo mahiri kuliongoza Baraza hili Tukufu kwa hekima, busara na uweledi mkubwa. Uongozi wako umeliwezesha Baraza hili kutimiza kikamilifu jukumu lake la kusimamia na kuishauri Serikali. Nimpongeze pia Mheshimiwa Naibu Spika na Wenyeviti wa Baraza kwa kukusaidia kuliongoza vyema Baraza la Wawakilishi. Aidha,  natoa pongezi maalum kwa Kamati ya Sheria, Utawala Bora na Idara Maalum chini ya Mwenyekiti wake Mheshimiwa Machano Othman Said Mwakilishi wa Wananchi Jimbo la Mfenesini.
6.       Mheshimiwa Spika, wakati nchi yetu ikiwa katika taharuki ya kupambana na kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona (COVID 19), naomba nichukue fursa hii kuwanasihi wananchi wote wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huu, naomba tuendelee kufuata maelekezo yanayotolewa na Serikali ili kujikinga na madhara yatokanayo na ugonjwa huu. Aidha, naomba kutoa salamu zangu za pole kwa wananchi wote ambao wamepoteza jamaa zao kwa madhara ya maradhi
ya corona, sote kwa umoja wetu tumuombe Mwenyezi Mungu kwa rehema zake atuondoshee maradhi haya ili tuendelee kuijenga nchi yetu.
7.       Mheshimiwa Spika, baada ya utangulizi huo, sasa naomba uniruhusu niwasilishe utekelezaji wa Programu za Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ kwa kipindi cha Julai hadi Machi 2019/2020.

MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA BAJETI KWA MWAKA WA

FEDHA 2019/2020

8. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2019/2020, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ kwa ujumla imetekeleza mambo yafuatayo;

           A.          TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA

9.       Mheshimiwa Spika, katika kusimamia utekelezaji wa Mpango wa Upelekaji Madaraka kwa wananchi (Ugatuzi), Ofisi imefanikiwa kukamilisha muundo wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, muundo huo unajumuisha uanzishaji wa Idara tano zinazounda Sekreterieti za Mikoa, Idara sita za Mamlaka za Serikali za Mitaa na Mabaraza ya Wadi na Kamati za Mashauriano za Shehia. Kwa upande wa Rasilimali watu Ofisi imeweza kuongeza watumishi wapya 932 wakiwemo walimu 673, wahudumu wa afya 93 na Mabwana shamba na Mabibi shamba 166. Aidha, uteuzi wa Wasaidizi Makatibu Tawala  Mikoa 25 na Wasaidizi Wakurugenzi 66 umefanyika na wameanza kutekeleza majukumu yao katika Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Kwa upande wa fedha, Serikali kuu imeongeza kiwango cha ruzuku kwa matumizi mengineyo katika Serikali za Mitaa kutoka shilingi 8,702,800,000 kwa mwaka 2018/2019 na kufikia shilingi 11,014,260,000 kwa mwaka 2019/2020 sawa na ongezeko la asilimia 27.
10.    Mheshimiwa Spika, mafanikio ya ugatuzi kwa wananchi yamezidi kuimarika ambapo Serikali za Mitaa zimetekeleza miradi 61 ya maendeleo yenye thamani ya shilingi 1,697,359,323 katika maeneo ya wadi mbali mbali. Miradi hiyo imehusisha ujenzi wa madarasa mapya 72, matengenezo ya skuli 43 na ujenzi wa matundu ya vyoo 133. Kwa upande wa huduma za Afya, Ofisi imesimamia matengenezo ya vituo 29 vya afya, matengenezo hayo yanajumuisha uwekaji wa maji, umeme na mapaa. Huduma za mama na mtoto zimeimarishwa ambapo kinamama wanaojifungulia katika vituo vya Afya wameongezeka na kupunguza idadi ya vifo vinavyotokana na uzazi kutoka asilimia 55 hadi asilimia 41. Aidha, katika kuimarisha huduma za ugani jumla ya wananchi 19,912 wamepatiwa mafunzo ya kisasa ya kilimo, mifugo na uvuvi.
11.    Mheshimiwa Spika, katika kuendeleza matengenezo ya barabara za ndani, Ofisi imewasilisha Serikalini Mpango wa miaka mitano wa matengenezo ya barabara za ndani pamoja na makisio yake ya bajeti ambapo Serikali imeridhia asilimia 40 ya bajeti ya Mfuko wa barabara kutumika katika matengenezo ya barabara za ndani na utekelezaji wake unatarajiwa kuanza katika mwaka wa fedha 2020/2021. Mpango huu utasaidia kutatua changamoto za matengenezo ya barabara za ndani na kuiwezesha Ofisi kuongeza idadi ya kilomita za barabara za ndani zitazojengwa katika Wilaya. Vilevile, Ofisi imeajiri Mshauri Elekezi kwa ajili ya kuzifanyia tathmini barabara zote za ndani za Zanzibar na kuzigawa kwa mujibu wa madaraja ya Wilaya na Vijiji.
12.    Mheshimiwa Spika, Hadi kufikia Machi, 2020 Ofisi imekamilisha matengenezo ya barabara ya Tume ya Uchaguzi yenye urefu wa kilomita 0.22 na barabara ya Skuli ya Kinuni yenye urefu wa kilomita 0.95. Kwa upande wa Pemba, ujenzi ya Barabara ya Gombani – Pagali yenye urefu wa kilomita 1.8 unaendelea katika hatua ya mwisho ya kuwekewa lami.
Aidha, Ofisi inakamilisha matengenezo ya Barabara ya Fuoni Mambosasa hadi Mwera Wilayani yenye urefu wa kilomita 3.4 kwa kiwango cha lami. Barabara hizo zinapitia katika maeneo ambayo yanaishi idadi kubwa ya watu, hivyo kukamilika kwa ujenzi huo wa barabara utarahisisha upatikanaji wa huduma za kijamii na kiuchumi, kupunguza msongamano wa gari katika barabara kuu, kuongeza haiba ya mji na kupunguza masafa kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyengine.
13.    Mheshimiwa Spika, Tawala za Mikoa zimeratibu utoaji na usimamizi wa huduma za ustawi wa jamii kwa makundi maalum ya watu wakiwemo wazee wasiojiweza 5,492 ambapo jumla ya shilingi 319,670,000 zimetumika katika kuwasaidia wazee. Aidha, kupitia kifungu maalum cha bajeti cha Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa, watu wenye ulemavu, wenye kuishi mazingira magumu na waliofikwa na matatizo mbali mbali ya kifamilia wameweza kupatiwa misaada mbalimbali ya matibabu, vifaa vya skuli, vifaa vya ujenzi na kujikimu kimaisha.  
14.    Mheshimiwa Spika, Mikoa imeendelea kudhibiti na kusuluhisha migogoro ya ardhi kwa kuhakikisha kuwa masuala yanayohusiana na migogoro ya ardhi yanashughulikiwa na kupatiwa ufumbuzi kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na taratibu zilizopo. Kwa kipindi cha Julai hadi Machi 2019/2020, jumla ya migogoro 196 ya ardhi iliyohusisha umiliki wa mashamba, viwanja na mipaka imeripotiwa katika Ofisi za Mikoa na Wilaya Unguja na Pemba. Kati ya migogoro hiyo, migogoro 105 imepatiwa ufumbuzi katika ngazi ya Wilaya na Mikoa, 14 imepelekwa Mahakama ya Ardhi na 77 inaendelea kupatiwa ufumbuzi kwa kushirikiana na Kamisheni ya Ardhi, Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi na Kamisheni ya Wakf na Mali ya Amana.

15.    Mheshimiwa Spika, suala la kupambana na udhalilishaji wa kijinsia limeendelea kupewa umuhimu mkubwa katika utekelezaji wa majukumu ya Tawala za Mikoa. Jitihada mbali mbali zimeendelea kufanyika katika ngazi za Mikoa, Wilaya na Shehia ili kuhakikisha matukio hayo yanapungua na hatimae yanaondoshwa kabisa. Miongoni mwa jitihada zinazofanyika ni pamoja na kutoa elimu kwa jamii na kufuatilia matukio yaliyoripotiwa katika ngazi mbali mbali za kisheria. Kwa kipindi cha Julai hadi Machi 2019/2020, jumla ya matukio 1,060 ya udhalilishaji yameripotiwa ndani ya Mikoa. Kati ya hayo, matukio 501 yapo katika hatua ya upelelezi wa Polisi, 119 yamepelekwa Mahakamani ambapo 45 yameshatolewa hukumu, matatu yamefutwa na matukio 71 yanaendelea kusikilizwa. Aidha, matukio 29 yamepelekwa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), 343 yamepatiwa ufumbuzi katika ngazi za Wilaya na 23 yanaendelea na ufumbuzi Wilayani.

           B.       IDARA MAALUM ZA SMZ

16.   Mheshimiwa Spika, Maofisa 187 wa Idara Maalum wamejengewa uwezo kwa kupatiwa mafunzo ya msingi kwa mujibu wa vyeo vyao na nafasi zao kazini pamoja na mafunzo maalum (msasa). Kati yao, Maofisa 49 (32 KVZ na 17 JKU) walipewa mafunzo ya ‘Platoon Commander’ ambapo maafisa wanne hawakufaulu mafunzo hayo; Maofisa 53 (28 KZU na 25 MF) walipatiwa mafunzo ya ‘Special Course’; Maofisa 35 (22 KZU na 13 MF) walipatiwa mafunzo ya ‘Advanced Course’ na Maofisa 50 wa KMKM walipatiwa mafunzo ya ‘Specialization’ ambapo Afisa mmoja hakufaulu mafunzo hayo. Mafunzo yaliyotolewa yamewawezesha Maofisa kuwa na uwezo wa kutekeleza vyema majukumu yao kama ilivyokusudiwa kuanzishwa kwa mpango huu maalum wa mafunzo katika Idara Maalum za SMZ. Aidha, mafunzo hayo yameimarisha utayari wa Idara Maalum katika kusimamia majukumu ya ulinzi na usalama nchini.


17.   MheshimiwaMwenyekiti,Ofisi imeratibu uajiri wa askari wapya 3,000 wakiwemo wataalamu wa fani mbali mbali 600 na kupatiwa mafunzo ya awali ya uaskari kwa muda wa miezi sita katika vyuo vya Idara Maalum za SMZ. Askari 2,990 waliweza kumaliza mafunzo yao ya awali na kugaiwa katika kila Idara Maalum. Hatua inayofuata ni kupata mafunzo ya miezi mitatu kulingana na majukumu na utendaji kazi wa Idara Maalum husika. Uajiri huu utaziwezesha Idara Maalum za SMZ kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kuongeza wataalam wapya kwenye Idara na Vitengo vya Idara Maalum za SMZ. Aidha, uajiri huo umesaidia kupunguza changamoto za ajira kwa vijana na kuwawezesha vijana hao kutumika katika kuimarisha shughuli za ulinzi na usalama katika
Taifa.
18.   Mheshimiwa Spika, katika utekelezaji wa miradi  ya maendeleo  katika  Idara Maalum za SMZ, Ofisi imesimamia ujenzi wa Mahanga,  nyumba na Ofisi  uliotekelezwa  kwa kila kikosi.  Kwa upande wa KMKM imefanya ujenzi wa Kambi ya KMKM Micheweni ambapo ujenzi huu upo katika hatua ya kuezeka paa. KVZ imejenga  hanga moja na nyumba ya Mkuu wa Zoni Pemba katika kambi ya Ndugukitu ambapo ujenzi upo hatua ya kuezeka paa.  Majengo manne katika Kambi ya Chuo cha Mafunzo Kangagani yameezekwa upya na kazi za uwekaji wa milango, madirisha pamoja na miundombinu ya maji zinaendelea. Ujenzi wa Majengo ya Kambi za JKU Msaani upo katika hatua ya kuezeka kwa mahanga mawili na bwalo moja la chakula. Aidha, ujenzi wa jengo la Kituo cha Zimamoto Kijichame umekamilika ghorofa ya kwanza na kazi ya uwekaji wa mfumo wa maji na umeme inaendelea. Kukamilika kwa ujenzi wa mradi wa mahanga, nyumba na Ofisi katika kambi za Idara Maalum utasaidia kuimarisha mazingira bora ya kazi na makaazi ya Maofisa na Wapiganaji wa Idara Maalum za SMZ.

           C.                  MAMBO MAALUM YALIYORATIBIWA

19.    Mheshimiwa Spika, katika kuanzisha Jiji la Zanzibar, mnamo tarehe 6 Agosti, 2019 Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alimteua Mkurugenzi wa Jiji na hivyo kuanzisha rasmi Jiji la Zanzibar kwa mujibu wa kifungu cha 18 (1) cha Sheria Namba 7/2014 ya Mamlaka za Serikali za Mitaa. Zanzibar kwa mara ya kwanza baada ya Mapinduzi Matukufu ya Januari 1964 imeanzisha Jiji lake ambalo litaipandisha hadhi Zanzibar katika nyanja tofauti hususan utalii. Zanzibar ilikosa uwakilishi mzuri kwenye sura ya Kimataifa ya Majiji na hivyo kupoteza nafasi ya uwakilishi mpana kwenye mambo mengi ya kimaendeleo yanayofanywa kwenye Mataifa duniani. Hongera kwa Mheshimiwa Rais Dkt Ali Mohammed Shein kwa kuliona jambo hili na hivyo kuanzisha Jiji la Zanzibar. Hii ni hatua muhimu ya kuiweka Zanzibar katika ramani ya dunia yenye mnasaba wa kutatua changamoto za maendeleo ya nchi na wananchi wake. Uwepo wa Jiji ni kiashiria cha ukuaji wa uchumi, upatikanaji wa huduma muhimu za kijamii, upanuzi wa huduma na miundombinu ya kiuchumi na utayari wa Serikali kuendeleza mipango mipana na miradi mikubwa zaidi ya maendeleo kwa wananchi wake.
20.    Mheshimiwa Spika, katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, Ofisi imeendelea kufanya malipo ya kila mwezi ya Mradi wa Mji Salama kwa mujibu wa masharti ya mkataba. Kupitia mradi huu jumla ya matukio ya kihalifu 214 yalibainika na kuchukuliwa hatua za kisheria. Matukio 80 yalihusu wizi, matukio 122 ajali za barabarani, saba utapeli wa mali na matano yalihusu matumizi haramu ya dawa za kulevya. Aidha, shughuli za uendelezaji wa Mradi wa Mji Salama kwa Miji ya Mkoani, Chake Chake na Wete zimekamilika kwa kuchimba mashimo na ujenzi wa kangriti kwa ajili ya uwekaji wa nguzo za kamera za usalama. Kazi inayoendelea kwa sasa ni matayarisho ya uwekaji wa waya na kusimamisha nguzo za kamera.
21.    Ofisi imeendelea kuviimarisha vituo vya uokozi viliopo Kibweni, Nungwi na Mkoani. Vituo hivyo vimefungwa vifaa maalum vya mawasiliano na kuweza kuwa na mifumo mitatu ijulikanayo kwa majina ya VMS, Sea Vision na Find Ship. Mifumo hii imekuwa na faida nyingi zikiwemo upatikanaji wa taarifa kwa urahisi kutoka kwenye vyombo vya baharini na  wananchi na kuimarisha mashirikiano baina ya KMKM na ZMA, MRCC pamoja na vyombo vya ulinzi vya Jamuhuri ya Muungano Tanzania hususan Jeshi la Wananchi Tanzania na Uhamiaji. Hivyo uwepo wa vituo vya uokozi kunahakikisha upatikanaji wa huduma za uokozi, uzamiaji na ulinzi wa nchi na kuepusha majanga ya uzamaji wa vyombo vya baharini na athari za maisha ya wananchi.
22.    Mheshimiwa Spika, Ofisi imesimamia utaratibu ulioanzishwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wa kusimamia upatikanaji wa rasilimali ya mchanga kwa wananchi. Utaratibu huo unawataka wananchi wanaohitaji mchanga kujaza fomu maalum za maombi ambazo zinapatikana kwenye ngazi ya Shehia wakielezea malengo, mahala, na kiwango cha mchanga. Lengo la utaratibu huo ni kupunguza uharibifu wa kimazingira, kuweka usimamizi bora wa upatikanaji wa mchanga na kusimamia matumizi bora ya mchanga nchini. Mkoa kwa kushirikiana na Idara ya Misitu na Maliasili zisizorejesheka umeendelea kusimamia mpango wa Serikali katika kudhibiti rasilimali ya mchanga kwa kufanya operesheni maalum na kukagua magari yanayobeba mchanga kwa lengo la kuhakikisha taratibu zinafuatwa.
23.    Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ imeshiriki kikamilifu katika kupambana na maradhi ya Corona (COVID19) kwa kushirikiana na Wizara ya Afya na Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar. Ofisi imetekeleza mikakati ya kupambana na COVID19 ikiwemo kuanzisha kambi za karantini katika kila Wilaya ambapo jumla ya wananchi 715 walioingia kupitia bandari zisizo rasmi waliwekwa karantini na vyombo saba vilivyobeba abiria kinyume na utaratibu vimekamatwa. Aidha, Ofisi kupitia Tawala za Mikoa imesimamia wafanyabiashara kuweka vitakasa mikono katika maeneo yao ya biashara, kupunguza misongomano katika masoko na shughuli za kijamii ikiwemo maziko na harusi, kuwafuatilia wageni wote wanaoingia na kutoka katika Shehia na kuelimisha wananchi juu ya kujikinga na maradhi kupitia njia za radio, televisheni, vipeperushi na matangazo.

           D.      UPATIKANAJI WA FEDHA

24.    Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2019/2020, Ofisi iliidhinishiwa kiasi cha shilingi 208,218,000,000. Kati ya fedha hizo, shilingi 80,113,100,000 mishahara, shilingi 26,919,660,000 matumizi mengineyo, shilingi 77,390,000,000 ruzuku kwa Tume ya Utumishi ya Idara Maalum za SMZ, Wakala wa Ulinzi JKU na Mamlaka za Serikali za Mitaa na shilingi 23,795,240,000 kwa kazi za maendeleo ikijumuisha shilingi 785,240,000 mchango kutoka kwa Washirika wa Maendeleo. Hadi kufikia Machi 2020, Ofisi iliingiziwa shilingi 161,172,240,898 sawa na asilimia 77 ya makadirio ya mwaka. Kati ya fedha hizo, shilingi 65,346,633,845 sawa na asilimia 82 ni mishahara, shilingi 19,351,608,936 sawa na asilimia 72 matumizi mengineyo, shilingi 59,166,932,761 sawa na asilimia 76 ni ruzuku kwa Tume ya Utumishi ya Idara Maalum, Wakala wa Ulinzi JKU na Mamlaka za Serikali za Mitaa na shilingi 17,471,441,356 sawa na asilimia 73 kwa kazi za maendeleo.
25.    Mheshimiwa Spika, kwa upande wa mapato, Ofisi iliidhinishiwa kukusanya shilingi 1,867,667,000 kwa ajili ya kuchangia Mfuko Mkuu wa Serikali na kukusanya shilingi 1,018,557,468 sawa na asilimia 55 ya makadirio ya mwaka. Kwa upande wa Mamlaka za Serikali za Mitaa zilikadiriwa kukusanya shilingi 13,260,003,546 na kukusanya shilingi
9,781,317,531 sawa na asilimia 74 ya makadirio ya mwaka.
26.    baada ya utekelezaji wa ujumla wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ, nawaomba Waheshimiwa Wajumbe waangalie ukurasa wa 12 hadi wa 87 katika kitabu cha Hotuba ya Bajeti kwa utekelezaji mahsusi wa programu za Fungu D01 hadi Fungu D12.

MWELEKEO KWA MWAKA WA FEDHA 2020/2021

27. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2020/2021, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ imepanga kutekeleza vipaumbele vifuatavyo;

A.       TAWALA ZA MIKOA NA MAMLAKA ZA SERIKALI ZA MITAA

i.         Kuimarisha Amani, Utulivu na Usalama katika Mikoa, Wilaya na Shehia hasa ikizingatiwa Taifa linaelekea kwenye uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.
ii.       Kuimarisha mfumo wa ukusanyaji wa mapato ya Serikali za Mitaa kwa kuhakikisha kila Halmashauri inakuwa na “electronic database” ya vyanzo vyote vya mapato na Walipa Kodi.
iii.     Kusimamia utekelezaji wa majukumu ya Jiji la Zanzibar ili kuufanya mji wa Zanzibar kuwa mji wa kisasa na kivutio cha utalii.
iv.      Kuondosha msongamano na vurumai kwenye masoko ya Mwanakwerekwe, Mombasa na Darajani na kuwahamishia baadhi ya wafanyabiashara katika Soko la Saateni na maeneo mengine.
v.       Kuhamisha daladala Michenzani na kuzipeleka katika Kituo cha daladala Kijangwani kwa kushirikiana na Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji.
vi.      Kuajiri Makatibu wa Wadi na Shehia ili kuwezesha Mabaraza ya Wadi na Kamati za Mashauriano za Shehia kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria.
vii.    Kuendeleza uwekaji wa anuani za mitaa (postcode) katika maeneo ya Miji.

           B.       IDARA MAALUM ZA SMZ

i.        Kuimarisha Kambi na Makaazi ya Idara Maalum za SMZ kwa kuendeleza ujenzi wa majengo ya Ofisi, nyumba za Maafisa na Mahanga ya Wapiganaji.
ii.       Kuimarisha Vyuo vya mafunzo vya Idara Maalum za SMZ ili kuviwezesha kutoa mafunzo kwa Maafisa na Wapiganaji wa ngazi zote.
iii.     Kuimarisha Kiwanda cha kushona sare na viatu cha Idara Maalum KVZ – Mtoni kuanza kazi na uzalishaji.
iv.     Kuanza ujenzi wa Kituo cha Mafunzo ya Uzamiaji KMKM Kama.
v.       Kuendelea na utekelezaji wa mradi wa Mji Salama kwa upande wa Pemba katika Miji ya Chake Chake, Wete na Mkoani na maeneo mengine ya Unguja.
vi.     Kuimarisha huduma za zimamoto na uokozi kwa kununua gari za zimamoto pamoja na kufanya upembuzi yakinifu wa uanzishaji wa Chuo cha kisasa cha Zimamoto na Uokozi.
vii.    Kuimarisha uzalishaji wa chakula na kuanzisha mashamba ya mifugo kwa Chuo cha Mafunzo na Jeshi la Kujenga Uchumi-JKU

           C.          MAMBO MAALUM KWA OFISI

viii.  Kuandaa rasimu ya sera mpya ya Serikali za Mitaa yenye kuzingatia kiukamilifu dhana ya ugatuzi na ushirikishwaji wa wananchi katika Serikali za Mitaa.
ix.     Kuandaa Mpango Maalum wa Utafiti wa Ofisi kwa kushirikiana na Taasisi za Utafiti za SMZ na COSTECH.
x.       Kuimarisha Mfumo wa Usajili na Uratibu wa Jumuiya zisizo za Kiserikali (NGOs) kwa lengo la kuwa na NGOs zenye tija na maslahi ya Nchi na Wananchi.
xi.     Kuimarisha mfumo wa usajili wa matukio ya kijamii kwa kuhakikisha huduma ya usajili wa vizazi, vifo, ndoa na talaka vyeti vyake vinapatikana katika Ofisi ndogo za kila Wilaya.
xii.   Kuendeleza ujenzi wa barabara za ndani kwa kiwango cha

lami pamoja na kuandaa andiko la mradi litalochambua na kuainisha barabara zote za ndani Zanzibar.

28.    Mheshimiwa Spika, baada ya mukhtasari huo wa mwelekeo wa vipaombele vya Ofisi, naomba kuwasilisha mwelekeo wa bajeti ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ kwa mwaka wa fedha 2020/2021 kwa kila fungu.
29.    Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2020/2021, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ itaendelea kutekeleza Programu Kuu 18 kupitia Mafungu 12 yaliyoanzia D01-D12. Fungu D01 limepangiwa kuetekeleza programu kuu tatu; Mafungu (D02–D06) yamepangiwa kutekeleza programu kuu mbili kwa kila mmoja; Mafungu (D07-D11) yamepangiwa kutekeleza programu kuu tatu kwa kila mmoja na Fungu (D12) limepangiwa kutekeleza programu kuu mbili.

PROGRAMU ZA OFISI KUU FUNGU-D01

30.    Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2020/2021, Fungu D01 litatekeleza Programu Kuu tatu ambazo ni Programu ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ, Programu ya Uratibu wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Programu ya Usimamizi wa Utumishi na Uratibu wa Idara Maalum za SMZ.
31.    Mheshimiwa Spika, kwa maelezo zaidi ya mwelekeo wa Programu za Fungu D01, nawaomba Waheshimiwa Wajumbe waangalie ukurasa wa 90 hadi wa 93 katika kitabu cha Hotuba ya Bajeti.
32.    Mheshimiwa Spika, ili programu zilizo chini ya Fungu D01 ziweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi, kwa mwaka wa fedha 2020/2021, naliomba Baraza lako Tukufu liidhinishe jumla ya shilingi 28,451,630,000. Kati ya fedha hizo, shilingi 1,740,900,000 kwa ajili ya mishahara, shilingi 11,025,800,000 kwa matumizi mengineyo ikijumuisha shilingi 261,100,000 mchango kutoka kwa Washirika wa Maendeleo, shilingi 1,288,700,000 kwa ajili ya ruzuku  ya Tume ya Utumishi ya Idara Maalum na Wakala wa Ulinzi JKU na shilingi  14,396,230,000 kwa kazi za maendeleo. Aidha, naliomba Baraza lako Tukufu liidhinishe makusanyo ya shilingi 832,800,000 kuchangia Mfuko Mkuu wa Serikali.

PROGRAMU ZA IDARA MAALUM ZA SMZ - FUNGU

(D02-D06)

33. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2020/2021, Idara Maalum za SMZ zitaendelea kutekeleza majukumu yake kupitia Programu Kuu mbili zitakazotekelezwa kwa kila Fungu kuanzia Fungu D02 hadi D06 na kufanya jumla ya Programu  zitakazotekelezwa na Idara Maalum zote kuwa 10. Maelezo yafuatayo yanahusu mwelekeo wa utekelezaji wa Programu za Idara Maalum za SMZ kwa kila Fungu.

JESHI LA KUJENGA UCHUMI (JKU)- FUNGU D02

34.    Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2020/2021, Jeshi la kujenga Uchumi litatekeleza Programu kuu mbili ambazo ni Programu ya Mafunzo kwa Vijana na Uzalishajimali na Programu ya Utawala na Uendeshaji wa JKU.
35.    Mheshimiwa Spika, kwa maelezo zaidi ya mwelekeo wa Programu za Fungu D02, nawaomba Waheshimiwa Wajumbe waangalie ukurasa wa 94 katika kitabu cha Hotuba ya Bajeti.
36.    Mheshimiwa Spika, ili Jeshi la Kujenga Uchumi kwa mwaka wa fedha 2020/2021 liweze kutekeleza Programu zake kwa ufanisi, naliomba Baraza lako Tukufu liidhinishe jumla ya shilingi 31,557,600,000. Kati ya fedha hizo, Shilingi 24,066,000,000 kwa ajili ya mishahara, shilingi 2,991,600,000 kwa matumizi mengineyo na shilingi 4,500,000,000 kwa kazi za maendeleo. Aidha, naliomba Baraza lako Tukufu liidhinishe makusanyo ya Shilingi 87,224,000 kuchangia Mfuko Mkuu wa Serikali.

CHUO CHA MAFUNZO-FUNGU D03

37.    Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2020/2021, Chuo cha Mafunzo kitatekeleza Programu kuu mbili ambazo ni Programu ya Urekebishaji Tabia kwa Wanafunzi na Programu ya Utawala na Uendeshaji wa Chuo cha Mafunzo.
38.    Mheshimiwa Spika, kwa maelezo zaidi ya mwelekeo wa Programu za Fungu D03, nawaomba Waheshimiwa Wajumbe waangalie ukurasa wa 95 katika kitabu cha Hotuba ya Bajeti.
39.    Mheshimiwa Spika, ili Chuo cha Mafunzo kwa mwaka wa fedha 2020/2021 kiweze kutekeleza programu zake kwa ufanisi, naliomba Baraza lako tukufu liidhinishe jumla ya shilingi 21,865,600,000. Kati ya fedha hizo shilingi 17,276,200,000 ni mishahara, shilingi 3,089,400,000 matumizi mengineyo na shilingi 1,500,000,000 kwa kazi za Maendeleo. Aidha, naliomba Baraza lako tukufu liidhinishe makusanyo ya shilingi 75,720,000 ili kuchangia Mfuko Mkuu wa Serikali.

KIKOSI MAALUM CHA KUZUIA MAGENDO (KMKM)-FUNGU D04

40.    Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2020/2021, Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo (KMKM) kitatekeleza Programu kuu mbili ambazo ni Programu ya Ulinzi na Uzuiaji wa Magendo na Programu ya Utawala na Uendeshaji wa KMKM.
41.    Mheshimiwa Spika, kwa maelezo zaidi ya mwelekeo wa Programu za Fungu D04, nawaomba Waheshimiwa Wajumbe waangalie ukurasa wa 95 hadi wa 96 katika kitabu cha Hotuba ya Bajeti.
42.    Mheshimiwa Spika, ili Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo kwa mwaka wa fedha 2020/2021 kiweze kutekeleza Programu zake kwa ufanisi, naliomba Baraza lako Tukufu liidhinishe jumla ya shilingi 35,630,700,000. Kati ya fedha hizo shilingi 24,543,900,000 kwa ajili ya mishahara, shilingi 5,586,800,000 kwa matumizi mengineyo na shilingi 5,500,000,000 kwa kazi za Maendeleo. Aidha, naliomba Baraza lako Tukufu liidhinishe makusanyo ya shilingi 60,542,000 ili kuchangia Mfuko Mkuu wa Serikali.

KIKOSI CHA ZIMAMOTO NA UOKOZI (KZU)-FUNGU D05

43.    Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2020/2021, Kikosi cha Zimamoto na Uokozi kitatekeleza Programu Kuu mbili ambazo ni Programu ya Uzimaji moto na Uokozi na Programu ya Utawala na Uendeshaji wa KZU.
44.    Mheshimiwa Spika, kwa maelezo zaidi ya mwelekeo wa Programu za Fungu D05, nawaomba Waheshimiwa Wajumbe waangalie ukurasa wa 96 hadi wa 97 katika kitabu cha Hotuba ya Bajeti.
45.    Mheshimiwa Spika, ili Kikosi cha Zimamoto na Uokozi kwa mwaka wa fedha 2020/2021 kiweze kutekeleza Programu zake kwa ufanisi, naliomba Baraza lako Tukufu liidhinishe jumla ya shilingi 16,795,900,000. Kati ya fedha hizo, shilingi 11,852,000,000 kwa ajili ya mishahara, shilingi 2,443,900,000 kwa matumizi mengineyo na shilingi 2,500,000,000 kwa kazi za maendeleo. Aidha, naliomba Baraza lako Tukufu liidhinishe makusanyo ya shilingi 45,700,000 na kuchangia Mfuko Mkuu wa Serikali.

KIKOSI CHA VALANTIA ZANZIBAR (KVZ) – FUNGU D06

46.    Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2020/2021, Kikosi cha Valantia Zanzibar kitatekeleza Programu Kuu mbili ambazo ni Programu ya Ulinzi wa Nchi, Raia na Mali zao na Programu ya Utawala na Uendeshaji.
47.    Mheshimiwa Spika, kwa maelezo zaidi ya mwelekeo wa Programu za Fungu D06, nawaomba Waheshimiwa Wajumbe waangalie ukurasa wa 97 hadi wa 98 katika kitabu cha Hotuba ya Bajeti.
48.    Mheshimiwa Spika, ili Kikosi cha Valantia kwa mwaka wa fedha 2020/2021 kiweze kutekeleza Programu zake kwa ufanisi, naliomba Baraza lako Tukufu liidhinishe jumla ya shilingi 20,135,000,000. Kati ya fedha hizo, shilingi 15,975,100,000 kwa ajili ya mshahara, shilingi 2,659,900,000 matumizi mengineyo na shilingi 1,500,000,000 kwa kazi za maendeleo.

PROGRAMU ZA TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA

MITAA - FUNGU (D07-D11)

49. Mheshimiwa Spika, kutokana na kufanana kwa majukumu ya Mikoa, Wilaya na Mamlaka za Serikali za Mitaa, Mikoa yote imepanga kutekeleza shughuli zake chini ya Programu Kuu tatu ambazo ni Programu ya Kusimamia Shughuli za Serikali katika Mkoa; Programu ya Uratibu na Uendeshaji wa Tawala za Mikoa; na Programu ya Usimamizi na Uendeshaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa. Maelezo yafuatayo yanahusu mwelekeo wa utekelezaji wa Programu za Tawala za Mkoa kwa kila Fungu kuanzia fungu D07-D11.

MKOA WA MJINI MAGHARIBI– FUNGU D07

50.    Mheshimiwa Spika, kwa maelezo zaidi ya mwelekeo wa Programu zitazotekelezwa na Fungu D07 la Mkoa wa Mjini Magharibi pamoja na Jiji la Zanzibar, Baraza la Manispaa Mjini, Baraza la Manispaa Magharibi ‘A’ na Baraza la Manispaa Magharibi ‘B’ nawaomba Waheshimiwa Wajumbe waangalie ukurasa wa 98 hadi wa 101 katika kitabu cha Hotuba ya Bajeti.
51.    Mheshimiwa Spika, ili Mkoa wa Mjini Magharibi kwa mwaka wa fedha 2020/2021 uweze kutekeleza Programu zake kwa ufanisi, naliomba Baraza lako Tukufu liidhinishe jumla ya shilingi 35,826,000,000. Kati ya fedha hizo, shilingi 1,653,600,000 ni mishahara, shilingi 1,749,650,000 matumizi mengineyo na shilingi 32,422,750,000 ni ruzuku kwa Jiji la Zanzibar, Baraza la Manispaa Mjini, Baraza la Manispaa Magharibi ‘A’ na Baraza la Manispaa Magharibi ‘B’. Aidha, naliomba Baraza lako Tukufu liidhinishe makusanyo ya shilingi 125,000,000 ili kuchangia Mfuko Mkuu wa
Serikali.

MKOA WA KUSINI UNGUJA – FUNGU D08

52.    Mheshimiwa Spika, kwa maelezo zaidi ya mwelekeo wa Programu za Fungu D08 la Mkoa wa Kusini Unguja pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Kusini na Halmashauri ya Wilaya ya Kati nawaomba Waheshimiwa Wajumbe waangalie ukurasa wa 101 hadi wa 103 katika kitabu cha Hotuba ya Bajeti.
53.    Mheshimiwa Spika, ili Mkoa wa Kusini Unguja kwa mwaka wa fedha 2020/2021, uweze kutekeleza programu zake kwa ufanisi, naliomba Baraza lako Tukufu liidhinishe jumla ya shilingi 14,068,800,000. Kati ya fedha hizo shilingi 1,369,900,000 ni mishahara, shilingi 758,630,000 kwa matumizi mengineyo na shilingi 11,940,270,000 ni Ruzuku za Halmashauri ya Wilaya ya Kusini na Halmashauri ya Wilaya ya Kati. Aidha, naliomba Baraza lako Tukufu liidhinishe makusanyo ya shilingi 50,750,000 na kuchangia Mfuko Mkuu wa Serikali.

MKOA WA KASKAZINI UNGUJA – FUNGU D09

54.    Mheshimiwa Spika, kwa maelezo zaidi ya mwelekeo wa Programu za Fungu D09 la Mkoa wa Kaskazini Unguja pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Kaskazini ‘A’ na Halmashauri ya Wilaya ya Kaskazini ‘B’ nawaomba Waheshimiwa Wajumbe waangalie ukurasa wa 103 hadi wa 105 katika kitabu cha Hotuba ya Bajeti.
55.    Mheshimiwa Spika, ili Mkoa wa Kaskazini Unguja kwa mwaka wa fedha 2020/2021, uweze kutekeleza Programu zake kwa ufanisi, naliomba Baraza lako Tukufu liidhinishe jumla ya Shilingi 15,365,100,000. Kati ya fedha hizo, shilingi 1,397,700,000 kwa ajili ya mishahara, shilingi 770,500,000 kwa matumizi mengineyo na shilingi 13,196,900,000 kwa ajili ya Ruzuku ya Halmashauri ya Wilaya ya Kaskazini ‘A’ na Halmashauri ya Wilaya ya Kaskazini ‘B’. Aidha, naliomba Baraza lako Tukufu liidhinishe makusanyo ya shilingi 27,500,000 ili kuchangia Mfuko Mkuu wa Serikali.

MKOA WA KUSINI PEMBA – FUNGU D10

56.    Mheshimiwa Spika, kwa maelezo zaidi ya mwelekeo wa Programu za Fungu D10 la Mkoa wa Kusini Pemba pamoja na Baraza la Mji Chake Chake na Baraza la Mji Mkoani, nawaomba Waheshimiwa Wajumbe waangalie ukurasa wa 105 hadi wa 107 katika kitabu cha Hotuba ya Bajeti.
57.    Mheshimiwa Spika, ili Mkoa wa Kusini Pemba kwa mwaka wa fedha  2020/2021, uweze  kutekeleza Programu zake kwa ufanisi, naliomba Baraza lako Tukufu  liidhinishe jumla ya  shilingi 14,682,500,000. Kati ya fedha hizo, shilingi 1,124,200,000 ni mishahara, shilingi 994,690,000 matumizi mengineyo na shilingi 12,563,610,000 ni ruzuku kwa Baraza la Mji Chake Chake na Baraza la Mji Mkoani. Aidha, naliomba Baraza lako Tukufu liidhinishe makusanyo
ya shilingi 25,700,000 na kuchangia Mfuko Mkuu wa
Serikali.

MKOA WA KASKAZINI PEMBA – FUNGU D11

58.    Mheshimiwa Spika, kwa maelezo zaidi ya mwelekeo wa Programu za Fungu D11 la Mkoa wa Kaskazini Pemba pamoja na Baraza la Mji Wete na Halmashauri ya Wilaya ya Micheweni, nawaomba Waheshimiwa Wajumbe waangalie ukurasa wa 107 hadi wa 108 katika kitabu cha Hotuba ya Bajeti.
59.    Mheshimiwa Spika, ili Mkoa wa Kaskazini Pemba kwa mwaka wa fedha 2020/2021 uweze kutekeleza Programu zake kwa ufanisi, naliomba Baraza lako Tukufu liidhinishe jumla ya shilingi 13,408,940,000. Kati ya fedha hizo, shilingi 1,226,400,000 kwa ajili ya mishahara, shilingi 1,078,340,000 ni matumizi mengineyo na shilingi 11,104,200,000 ni ruzuku kwa Baraza la Mji Wete na Halmashauri ya Wilaya ya Micheweni. Aidha, naliomba Baraza lako Tukufu liidhinishe makusanyo ya shilingi 25,476,000 na kuchangia Mfuko Mkuu wa Serikali.

WAKALA WA USAJILI WA MATUKIO YA KIJAMII –FUNGU D12

60.    Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2020/2021,
Ofisi ya Wakala wa Usajili wa Matukio ya Kijamii itatekeleza Programu kuu mbili ambazo ni Programu ya Usajili wa Matukio ya Kijamii na Programu ya Utumishi na Uendeshaji.
61.    Mheshimiwa Spika, kwa maelezo zaidi ya mwelekeo wa Programu za Fungu D12, nawaomba Waheshimiwa Wajumbe waangalie ukurasa wa 108 hadi wa 109 katika kitabu cha Hotuba ya Bajeti.
62.    Mheshimiwa Spika, ili Ofisi ya Wakala wa Usajili wa Matukio ya Kijamii iweze kutekeleza Programu zake kwa ufanisi, naliomba Baraza lako tukufu kuidhinisha jumla ya shilingi 4,909,600,000. Kati ya fedha hizo shilingi 1,475,000,000 kwa ajili ya mishahara, shilingi 2,434,600,000 kwa matumizi mengineyo na shilingi 1,000,000,000 kwa kazi za maendeleo. Aidha, naliomba Baraza lako Tukufu liidhinishe makusanyo ya shilingi 626,512,000 na kuchangia Mfuko Mkuu wa Serikali.

SHUKURANI

63.    Mheshimiwa Spika, namshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia kuwasilisha hotuba hii mbele ya Baraza lako Tukufu kwa hekima na utulivu.
64.    Mheshimiwa Spika, napenda kutoa Shukrani zangu za dhati kwa Waheshimiwa Mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Watumishi wa Baraza la Wawakilishi kwa mashirikiano yao ya dhati waliyoyaonyesha katika kipindi chote cha Baraza la Tisa la Wawakilishi. Mashirikiano na utendaji wao umepelekea kufanikisha kwa uweledi utekelezaji wa majukumu ya Serikali na Ilani ya Chama ya Mapinduzi.
65.    Mheshimiwa Spika, kwa umuhimu wa kipekee naomba niwashukuru Wananchi wa Jimbo la Tumbatu kwa kuniamini na kushirikiana nami katika kuliletea maendeleo Jimbo la Tumbatu. Nawaahidi nitaendelea kwa moyo wangu wote kuzidi kushirikiana nao kwa hali na mali kuwaletea maendeleo. Aidha, natumia fursa hii kuwapa pole waathirika wa mvua za masika zinazoendelea kunyesha na kupelekea watu kupoteza maisha, mali na makaazi. Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ iko pamoja nao katika kipindi hiki kigumu. Nachukua fursa hii kutoa wito kwa wananchi kuchukua kila tahadhari
ili kuepukana na athari zaidi zinazoweza kutokea ikiwemo maradhi ya mripuko.

HITIMISHO

66. Mheshimiwa Spika, naomba Waheshimiwa Wajumbe  wa Baraza lako Tukufu waipokee na kuichangia hotuba hii na hatimae waidhinishe kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ kwa mwaka wa fedha 2020/2021 makadirio  ya shilingi 252,697,370,000. Kati ya fedha hizo, shilingi 103,700,900,000 kwa ajili ya mishahara na maposho, shilingi 35,583,810,000 kwa matumizi mengineyo, shilingi 82,516,430,000 ni ruzuku kwa Tume ya Utumishi ya Idara Maalum, Wakala wa Ulinzi wa JKU na Mamlaka za Serikali za Mitaa, shilingi 30,896,230,000 kwa matumizi ya kazi za maendeleo. Aidha, nawaomba Waheshimiwa Wajumbe waidhinishe mchango wa shilingi 1,982,924,000 ikiwa ni mapato yatakayoingizwa katika kuchangia Mfuko Mkuu wa Serikali.  Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.

HAJI O. KHERI       

Waziri wa Nchi - Ofisi ya Rais,       Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.