HOTUBA
YA MAONI YA KAMATI YA SHERIA, UTAWALA BORA
NA
IDARA MAALUM KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA
MATUMIZI
YA OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA,
SERIKALI
ZA MITAA NA IDARA MAALUM ZA SMZ KWA
MWAKA
WA FEDHA 2020/2021
Mheshimiwa Spika, kila sifa njema ni za Mwenyezi Mungu, Mwingi
wa Rehma, Muumba wa Mbingu na Ardhi na vyote vilivyomo, kwa kutujaalia kukutana
kwa mara nyengine tena katika Mkutano huu wa Kumi na Tisa wa Baraza laTisa kwa
dhamira ya kujadili Bajeti kuu ya Serikali na taasisi zake katika Baraza lako
Tukufu. Kwani hii ni rehma yake Muumba kwa kutupa pumzi na afya njema ambayo
wenzetu wengine amewanyima fursa hii.
Mheshimiwa Spika, pia, napenda kutumia fursa hii adhimu
kukushukuru na kukupongeza wewe binafsi kwa kunipa nafasi hii ya kusimama mbele
ya Baraza lako Tukufu, kwa lengo la kuwasilisha maoni ya Kamati ya Kudumu ya Sheria, Utawala Bora na Idara Maalumkuhusina na
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha
kwa Wizara ya Nchi, (OR) Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za
SMZ kwa mwaka wa fedha 2020/2021
kama Kanuni za Baraza hili zinavyoelekeza.
Mheshimiwa Spika, aidha, nawapongeza na kuwashukuru kwa
dhati viongozi wa Wizara hii wakiongozwa na Waziri wao Mheshimiwa Haji Omar Kheri,
Naibu Waziri, Mheshimiwa Shamata Shaame Khamis, Katibu Mkuu, Manaibu Katibu
Mkuu, Wakuu wa Mikoa pamoja Afisa Mdhamini Pemba, na watendaji wote kwa
mashirikiano yao makubwa waliyotuonesha katika Kamati yetu na kupelekea
kutekeleza majukumu yetu ipasavyo. Vile vile, shukurani za pekee ziende kwa
Wakuu, Maafisa na Wapiganaji wote wa Idara Maalum za SMZ kwa mashirikiano yao
waliyotupatia kwa kipindi chote cha utekelezaji wa shughuli za Kamati.
Mheshimiwa Spika, sambamba na hayo, natumia nafasi hii
kuishukuru Wizara ya Nchi (OR) Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara
Maalum za SMZ kwa kutumia na kutekeleza vyema ushauri na maagizo ya Kamati
pamoja na kusimamia kwa ukamilifu na ufanisi utekelezaji wa Bajeti yao ya mwaka
2019/2020, jambo hili limewawezesha
kujenga ari ya kuwasilisha mbele ya Kamati yetu, pamoja na Baraza lako Tukufu
Makadirio mapya ya Mapato na Matumizi ya Fedha kwa mwaka wa fedha 2020/2021 ili yapate baraka za Wajumbe
wako,na kwa mnasaba huo, tunaliomba Baraza lako tukufu liridhie na liipitishe Bajeti
hii kwa maslahi ya wananchi na Serikali kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika, aidha, naomba kutoa shukrani na pongezi
za pekee kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi imara wa Rais wetu
mpendwa, Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.
Ali Mohamed Shein katika uongozi wake na kuhakikisha maendeleo ya watu na
ustawi wa jamii nchiniumeimarika pamoja na kusimamia maendeleo ya kiuchumi
kufuatana na misingi na madhumuni yaliyowekwa katika Katiba ya Zanzibar ya
mwaka 1984, kwa kuhakikisha
upatikanaji wa huduma bora unafanikiwa kwa wananchi wote wa Zanzibar.
Mheshimiwa Spika, ni matumaini ya Kamati yangu kuwa,
mafanikio yanayopatikana katika uimarikaji wa uchumi wetu na huduma za kijamii
yanatokana na utekelezaji mzuri wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015/2020.
Mheshimiwa Spika, Bajeti hii imekadiriwa kufanya kazi kwa
kuzingatia malengo ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na inaakisi hali halisi
ya uchumi wetu na harakati za kupunguza umasikini lakini pia kwa kuzingatia
malengo ya Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini Zanzibar (MKUZA III).
Mheshimiwa Spika, pia, nachukua nafasi hii kuwashukuru kwa
kazi kubwa walioifanya Wajumbe wa Kamati yangu wakati tukiwa tunapitia bajeti
hii, kwa kuonesha mashirikiano yao makubwa katika kutekeleza majukumu ya Kamati
hii.
Hivyo, kwa ridhaa yako naomba sasa uwatambue
Wajumbe wa Kamati hii kama ifuatavyo:
1.
|
Mhe. Machano Othman Said
|
Mwenyekiti.
|
2.
|
Mhe. Zulfa Mmaka Omar
|
Makamu Mwenyekiti.
|
3.
|
Mhe. Dkt. Khalid Salum Mohamed
|
Mjumbe.
|
4.
|
Mhe. Ali Khamis Bakar
|
Mjumbe.
|
5.
|
Mhe. Salma Mussa Bilal
|
Mjumbe.
|
6.
|
Mhe. Suleiman Makame Ali
|
Mjumbe.
|
7.
|
Mhe. Maryam Thani Juma
|
Mjumbe.
|
8.
|
Ndg. Haji Jecha Salim
|
Katibu.
|
9.
|
Ndg. Ali Alawy Ali
|
Katibu.
|
Mheshimiwa Spika, Kamati ya Sheria, Utawala Bora na
Iadara Maalum imetumia uweledi wake wa hali ya juu katika kupitia, kuchambua na
kujiridhisha vyema naprogramu zote zilizokusudiwa kufanyiwa kazi kupitia Mafungu
ya Bajeti ya Wizara hii kama ilivyoelezwa katika Kanuni za Baraza la
Wawakilishi, Toleo la mwaka 2016.
Mheshimiwa Spika, ni imani ya Kamati hii kwamba
kupatikana kwa fedha zilizopangwa katika Wizara hii kutasaidia kwa kiasi
kikubwa utekelezaji na ukamilishaji wa malengo yaliyokusudiwa kutekelezwa ikiwa
ni pamoja na kukamilisha miradi iliyotengwa kwa mwaka huu wa fedha 2019/2020 na vile vile kumalizia mradi
mkubwa wa ujenzi wamahanga na nyumba za askari wa Idara Maalum kisiwani Pemba.
PROGRAMU ZA MAKAO MAKUU (FUNGU D 01)
Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza kazi zake kwa mwaka
wa fedha 2019/2020, Kamati yangu
imefanikiwa kutembelea na kujionea shughuli mbali mbali za kawaida na zile za
miradi ya maendeleo ambazo zinasimamiwa na kuratibiwa na Wizara hii kupitia
programu kuu tatu (3) zifuatazo:
(a)
Programu ya usimamizi na uendeshaji wa Ofisi ya Rais, Tawala
za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ;
(b)
Programu ya uratibu wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa;
(c)
Programu ya usimamizi wa utumishi na uratibu wa Idara Maalum
za SMZ.
Mheshimiwa Spika, programu hizi pia ndani yake zimo programu
ndogo ndogo ambazo zina lengo la kukamilisha utekelezaji wa programu kuu hizo katika
maeneo tofauti ya kiutendaji. Aidha, utekelezaji wa programu hizi unakabiliwa
na changamoto mbali mbali kama vile uhaba wa vitendea kazi, uhaba wa vyombo vya
usafiri pamoja na ubovu wa barabara za ndani katika maeneo mengi ambako
kunapelekea barabara hizo kutokupitika au kupitika kwa tabu hasa kwa wale
wanaotumia vyombo vya moto pamoja na uchakavu na uhaba wa madarasa ya kusomea
katika skuli za msingi, matundu ya vyoo, changamoto katika utoaji wa huduma za
uji wa lishe katika skuli za maandalizi na ukosefu wa maji safi na salama katika
baadhi ya vituo vya afya, skuli za msingi na maandalizi.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, Kamati hii inaipongeza
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa juhudi zake za kusimamia vyema na
kuzitatua baadhi ya changamoto hizi ambazo kwa kiasi kikubwa zimeshamiri katika
skuli za msingi na maandalizi zilizopo vijijini.
Mheshimiwa Spika, vile vile, Kamati inatoa pongezi za
dhati kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuhakikisha kuwa huduma za afya
na elimu kwa wananchi zinakuwa bora kwa kusambaza dawa na vifaa tiba
vinavyohitajika pamoja na kusambaza madaftari, vitabu na chaki katika skuli mbali
mbali za Unguja na Pemba.
Mheshimiwa Spika, Kamati inashauri kwa mwaka wa fedha 2019/2020, idara zinazotekeleza miradi
ya maendeleo, zipatiwe fedha za kutosha kwa miradi hiyo ambayo iliainishwa
katika programu za fungu D01 ili
kuweza kutatua changamoto zinazokwamisha utekelezaji wa shughuli zao kwa lengo
la kuleta ufanisi na kuleta maendeleo katika Idara hizo.
Mheshimiwa Spika, Kamati imeridhishwa na kazi nzuri
zinazofanywa na Ofisi kuu kwa kupitia na kuandaa miradi mbali mbali ya
maendeleo ambayo msingi wake ni kuongeza kasi ya maendeleo ya kiuchumi kwa
jamii. Aidha, Kamati imeelezwa kuwepo kwa fedha za mfuko wa barabara za ndani
ambazo hazikutumika katika mwaka wa fedha unaomalizika mwezi Juni, 2020. Kamati inaishauri Serikali kuhusiana
na fedha hizo zilizotengwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara za ndani kuwekewa
mpango maalum wa matumizi katika kila mwaka ili kunusuru fedha nyingi ambazo
zinabakia bila matumizi yaliyokusudiwa.
Mheshimiwa Spika, Kamati inashauri barabara ambazo
zilikusudiwa kujengwa na Halmashauri katika bajeti ya mwaka 2019/2020 na kushindwa kujengwa kutokana
na kutokuwepo kwa mipango madhubuti ya matumizi ya fedha hizo zijengwe katika
bajeti hii ya mwaka 2020/2021.
Mheshimiwa Spika, Kamati inaipongeza Wizara kwa
kusimamia vyema zoezi la uwekaji wa mipaka ya kishehia na kuweza kufanikiwa kwa
kiasi kikubwa na kuondoa changamoto katika maeneo yenye idadi kubwa ya wakaazi
na hivyo kupelekea kutolewa kwa huduma za kijamii kwa ufanisi zaidi kwa mujibu
wa ukubwa wa eneo na idadi ya wakaazi husika.
PROGRAMU ZA IDARA MAALUM ZA SMZ (FUNGU
D 02 – D 06)
Mheshimiwa Spika, Kamati imeridhishwa na juhudi
zinazofanywa na wapiganaji wetu wa vikosi kwa kazi nzito wanazozifanya za
kulinda, kusimamia na kudumisha usalama wa raia na mali zao pamoja na
kuhakikisha uwepo wa amani na utulivu katika nchi yetu. Sambamba na hayo,
Kamati imeridhika na hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa Mahanga ya Kikosi cha
Valantia Ndugukitu pamoja na Jengo la ghorofa mbili (2) la Kikosi cha Zimamoto na Uokozi cha Kijichame kisiwani
Pemba. Ni dhahiri kabisa, juhudi hizo za Serikali zinaonekana kutia moyo na
kuwajali sana vijana wetu na vile vile, Serikali kutekeleza kwa vitendo ahadi
zake zilizotolewa katika Ripoti ya Kamati na Bajeti ya mwaka huu wa fedha 2019/2020.
Mheshimiwa Spika, Kamati inaishauri JKU kuweka utaratibu
wa kuwa na programu za kuwafuatilia vijana ambao wamepata mafunzo kutoka katika
Jeshi laKujenga Uchumi mara tu wanapomaliza mafunzo yao ili kuwafahamu mahali
walipo na shughuli wanazozifanya kwa mujibu wa mafunzo waliyopatiwa. Programu
hizi zitasaidia kufahamuni kwa kiasi gani mafunzo yanayotolewa yanasadifu
mazingira na wakati tulionao.
PROGRAM
KUUZA URATIBU WA TAWALA ZA MIKOA NA
SERIKALI
ZA MITAA (Fungu D 07 – D 11)
Mheshimiwa Spika, katika programu kuu ya Uratibu wa
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, kwa ujumla wake, Kamati ya Sheria,
Utawala Bora na Idara Maalum imeridhishwa na utekelezaji wa programu zinazosimamiwa
na Tawala za Mikoa pamoja Mamlaka ya Serikali za Mitaa zaidi katika ukusanyaji
wa mapato kutokana na baadhi ya Halmashauri kuvuka malengo waliyokusudia.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa dhana ya Ugatuzi ni njema na
inaleta ufanisi kwa watendaji, Kamati inapongeza sana juhudi za Serikali katika
kusimamia vyema Ugatuzi katika taasisi zilizogatuliwa. Aidha, Kamati
imeridhishwa na utendaji wa taasisi hizo katika kuwatumikia wananchi. Hata
hivyo, ni vyema Halmashauri zetu zikajikita zaidi katika utafutaji wa vyanzo
vipya vya mapato ambavyo havitawaumiza wananchi kwa kuyatumia maeneo waliyonayo
na badala yake kuacha kufanyakazi kwa kutegemea ruzuku kutoka Serikali kuu
kwani kutegemea ruzuku kutapelekea kushindwa kufikia malengo ya kuanzishwa kwa
Halmashauri na kuizidishia mzigo Serikali kwa kuzingatia kipindi hiki ambacho
uchumi wa Dunia umeshuka kutokana na athari za janga la ‘Corona’ (Covid – 19).
Mheshimiwa Spika, pamoja na maelezo mazuri ya Wizara juu
ya utekelezaji wa Ugatuzi katika kipindi hiki, Kamati, wakati wa utekelezaji wa
majukumu yake katika Halmashauri hizo, ilielezwa na kubaini kuwepo kwa
changamoto katika baadhi ya sekta zilizogatuliwa hasa sekta ya kilimo na elimu,
kwa kutokutekeleza ipasavyo suala hili la ugatuzi ambapo sekta hizo zimepeleka
baadhi ya watendaji tu bila ya kupeleka fedha za matumizi katika uendeshaji wa
programu zilizokusudiwa. Kwa mfano bajeti ya elimu ya msingi na maandalizi bado
zipo Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, hivyo Halmashauri hulazimika kulipa
maposho ya walimu pamoja na uji wa lishe kwa skuli za maandalizi na
msingi.
Mheshimiwa Spika, Kamati ilifanya ziara maalum Tanzania
Bara kwa kutembelea Halmashauri ya Jiji
la Mwanza na Jiji la Dar es Salaam
kwa lengo la kujifunza namna ya uendeshaji wa Jiji, utekelezaji wa majukumu ya
Taasisi hizo na namna gani wanaweza kukusanya mapato kupitia vyanzo
walivyonavyo kisheria. Hivyo, Kamati inashauri katika utekelezaji mzuri wa
majukumu ya Jiji la Zanzibar, kuainishiwa majukumu yake na vyanzo vya mapato
ambavyo watavitumia ili kujikusanyia mapato kama zilivyo Halmashauri nyengine.
Sambamba na hayo Kamati imeona ipo haja ya kufanywa marekebishho ya Sheria ya
Mamlaka ya Serikali za Mitaa, nambari 8
ya mwaka 2014 ili majukumu ya Jiji na
vyanzo vya mapato viwekwe wazi katika Sheria hii.
Mheshimiwa Spika, kwa ujumla, Serikali imejitahidi sana
katika kunyanyua elimu ya msingi na afya, changamoto iliyopo ni idadi kubwa ya
madarasa mabovu pamoja na uhaba wa matundu ya vyoo kwa skuli za maandalizi na
msingi. Hivyo basi, Kamati inazishauri Halmashauri zetu kwa kupitia waheshimiwa
Madiwani na Wawakilishi kuwashajihisha wananchi kujitolea kwa hali na mali
katika kuongeza idadi ya matundu ya vyoo pamoja na madarasa ili kuweka
mazingira rafiki kwa watoto wetu katika kujipatia elimu bora. Aidha, Serikali
nayo itenge fungu maalum la fedha za kutatua tatizo hilo.
Mheshimiwa Spika, Kamati inaishauri Wizara kupitia Halmashauri,
kuchukuwa hatua za makusudi kuhakikisha kuwa maeneo yote ya miji yanakuwa safi na
salama kwa kuzipatia magari na vifaa vya kuzolea taka Halmashauri ambazo ndizo
zenye jukumu hilo ili ziweze kudhibiti na kuandaa utaratibu wa kukusanya taka za
majumbani na maeneo mengine au kuweka maeneo maalum ya kukusanyia taka ili
wananchi waweze kuondokana na adha hii ya kukosa maeneo ya kutupia taka na
kupelekea taka hizo kuzagaa mitaani.
WAKALA WA USAJILI WA MATUKIO YA KIJAMII
(FUNGU D 12)
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa, nachukuwa fursa hii kwa
kutoa pongezi kwa Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein kwa kumteua ndugu Idrissa Shaaban Zahran kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala ambapo
Kamati ina matumaini makubwa kwamba Mkurugenzi huyo atazimaliza changamoto
zinazoukabili Wakala huo.
Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Wakala wa Usajili wa Matukio
ya Kijamii umeendelea na usajili wa wazanzibari na kuwapatia vitambulisho vyao
pamoja kusajili vizazi, vifo na talaka. Kamati inaishauri Ofisi hii kuwezeshwa
kwa kupatiwa miundombinu ambayo itasaidia kuweza kusajili wazanzibari wote
katika shehia zao pamoja na hospitali mara tu wanapozaliwa pamoja na kutoa
vyeti vya kuzaliwa vyenye ubora zaidi.
HITIMISHO
Mheshimiwa
Spika, kwa kumalizia,
nachukua fursa hii kuiomba jamii katika kipindi hiki cha mvua za masika zinazoendelea
kunyesha kuzidi kuweka usafi wa mazingira yetu kwa kuitunza michirizi ya maji
ya mvua na kuepuka kutupa taka kiholela ndani ya miji yetu, kufanya hivyo
kutasaidia kujikinga na maradhi ya mripuko na malaria ambayo ni hatari kwa nchi
yetu pamoja na kuitunza misingi hiyo ambayo inajengwa kwa kutumia fedha nyingi
za Serikali.
Mheshimiwa
Spika, aidha, katika
kukabiliana na mafuriko yanayotokea karibu kila mwaka katika maeneo mbali mbali
ya Wilaya ya Magharib ‘A’ na ‘B’, Kamati inaishauri Serikali kujenga
mitaro ya kupitishia maji katika maeneo hayo kama vile ilivyofanya katika
maeneo ya Wilaya ya Mjini, Chake Chake, Wete na Mkoani.
Mheshimiwa
Spika, pia, naomba niwashukuru
Makamanda wa Idara Maalum za SMZ, Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Makatibu
Tawala wa Mikoa na Wilaya, Wakurugenzi, Madiwani, Masheha na watendaji wote wa
Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ kwa
utendaji, uzalendo wao na mashirikiano yao katika kutekeleza majukumu ya Kamati
yetu katika kipindi chote cha maisha ya Kamati hii.
Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa, Kamati inawaomba
Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza lako Tukufu wairidhie, waichangie na waipitishe Bajeti
hii na hatimae waidhinishie makadirio ya fedha zilizopangwa kutumiwa kwa mwaka
wa fedha 2020/2021 kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za
Mitaa na Idara Maalum za SMZ.
Mheshimiwa Spika, Naomba Kuunga Mkono Hoja.
Ahsante,
…………..…………………..
(Mhe.
Maryam Thani Juma)
Mjumbe,
Kamati ya Sheria,
Utawala Bora na Idara Maalum,
Baraza la
Wawakilishi,
Zanzibar
No comments:
Post a Comment