Habari za Punde

OFISI ZA ARDHI KILA MKOA ZAANZA RASMI

Watendaji wa sekta ya ardhi katika ofisi ya Ardhi ya mkoa wa Tanga wakiwa wamesimama katika Bango la kutambulisha ofisi ya mkoa huo.


Na Munir Shemweta, WANMM DODOMA
Ofisi za Ardhi za mikoa kuanza rasmi kufanya kazi katika mikoa 26 ya Tanzania Bara mwezi huu wa Mei 2020 ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Pombe Magufuli kuitaka Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuondoa kero na mzigo wa gharama kwa wananchi katika masuala ya ardhi.

Uanzishaji ofisi hizo ni usogezaji huduma za sekta ya ardhi karibu na wananchi sambamba na kuwapunguzia gharama za kufuata huduma hiyo umbali mrefu ambapo huduma za ardhi awali zilikuwa zikitolewa kwenye ofisi za Ardhi za Kanda na Makao Makuu.

Akizungumza leo tarehe 10 Mei 2020 jijini Dodoma kabla ya kuwasilisha Makadirio ya Hotuba yake hapo kesho tarehe 11 Mei 2020, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi alisema Wizara ya Ardhi imeanzisha ofisi za ardhi katika kila Mkoa ili kutoa huduma zote zilizokuwa zinatolewa kwenye ofisi za Kanda au Makao Makuu.

Alisema, kuanzia sasa wananchi watapata huduma zote ndani ya mikoa yao na kubainisha kuwa wananchi wa mikoa ya Kigoma na Katavi hawataenda tena Tabora kuchukua hati kama walivyokuwa wakifanya awali huku wale wa Tanga, Manyara na Arusha wakipata huduma katika mikoa yao badala ya kwenda Moshi na wale wa mikoa ya Iringa, Njombe, na Rukwa wakisalia mikoa husika badala ya kwenda Mbeya.

Aidha, wananchi wa mikoa ya Ruvuma na Lindi sasa hawataenda mkoa wa Mtwara kupata huduma za ardhi na wananchi wa Kagera na Geita nao hawatalazimika kwenda Mwanza  huku wananchi wa mikoa ya Mara na Shinyanga wakisalia mikoa yao kupata huduma za ardhi ambapo sasa hawataenda Simiyu na wale wa Singida na Morogoro wakiepuka kwenda mkoa wa Dodoma kuchukua hati.

Kwa mujibu wa Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi,  Nyaraka zote,  watumishi pamoja na vitendea kazi tayari vipo mikoani na kubainisha kuwa, sasa Taasisi kama mabenki zitaweza kukopesha kwa kasi kwa kuwa dhamana za wakopeshwaji yaani Hati zipo mikoani na Masjala za Hati zimerudishwa kila mkoa.

Waziri huyo mwenye dhamana ya Ardhi alisema, Wasajili wa hati wa mikoa watatoa hati kwa wananchi kupitia ofisi za Ardhi za Wilaya na siyo wananchi kufuata hati kwenye kanda au mkoani na kuongeza kuwa, vifaa mbalimbali vya upimaji vimenunuliwa na kusambazwa ofisi hizo za mikoa ili Halmashauri za Wilaya ziweze kuazima na kupima maeneo yao bila gharama za kuvikodisha.

‘’Tumeanza mkakati wa kununua vifaa kwa kila Wilaya.  Uanzishwaji wa ofisi hizi ni utekelezaji wa maagizo ya Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli aliyetutaka Wizara tuondoe kero na mzigo wa gharama kwa wananchi na wadau mbalimbali wa ardhi’’ alisema Lukuvi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.