Habari za Punde

Taarifa ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar kwa Vyombo vya Habari Kuhusu Matayarisho ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020


TUME YA UCHAGUZI YA ZANZIBAR


Taarifa ya Tume ya Uchaguzi kwa Vyombo vya Habari Kuhusu Matayarisho ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020.
 

Ndugu Waandishi wa Habari, Tume ya Uchaguzi inatarajia kuendesha Uchaguzi Mkuu mwaka 2020 ambapo wananchi wa Zanzibar watapata fursa ya kumchagua Rais wa Zanzibar, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Madiwani. Maandalizi ya uchaguzi huo yamegawika katika sehemu tatu kubwa ambazo ni:
i)             Upatikanaji wa Vifaa mbali mbali vya Uchaguzi,
ii)            Uandikishaji wa Wapiga Kura Wapya na uhakiki wa taarifa za Wapiga Kura
iii)           Kazi ya kufanya Mapitio ya Idadi, Majina na Mipaka ya Majimbo ya Uchaguzi
Ndugu Waandishi wa habari, Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ipo katika hatua za mwisho za upatikanaji wa vifaa vya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020. Nachukua nafasi hii kuwafahamisha kuwa Tume imekamilisha uchapishaji wa nyaraka, uagiziaji na ununuzi wa vifaa na mbali mbali vya uchaguzi na baadhi ya vifaa hivyo vimeshakabidhiwa Afisi ya Tume ya Uchaguzi.

Ndugu Waandishi wa habari, Kazi ya uandikishaji wa Wapiga Kura Wapya na Uhakiki wa taarifa za Wapiga Kura waliokuwemo katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ilianza tarehe 18/1/2020 katika Wilaya ya Micheweni kisiwani Pemba na kukamilika tarehe 15/3/2020 katika Wilaya ya Mjini.  Katika kazi hii Tume iliandikisha wapiga kura wapya waliofikia umri wa kupiga kura.  Aidha, ilifanya uhakiki wa wapiga kura waliokuwemo katika Daftari la wapiga kura tangu  lilipoanzishwa mwaka 2005 na wapiga kura wengine ambao waliandikishwa kwa nyakati mbalimbali kati ya mwaka 2010, 2013 na 2015. Lengo la uhakiki wa wapiga kura ni kufahamu wapiga kura ambao wamepoteza sifa za kuwemo katika Daftari na kuwafuta waliokosa sifa.

Ndugu Waandishi wa Habari. Kazi ya uandikishaji na uhakiki wa taarifa za wapiga kura kwa ujumla ilikwenda vizuri sana ingawa kulikuwepo na tatizo la baadhi ya Wananchi kukosa kuandikishwa au kuhakikiwa taarifa zao kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kukosa Vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi.

Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar tayari imefanya tathmini ya kazi ya Uandikishaji ili kufahamu kwa kiasi gani zoezi hilo limetekelezwa.  Hivi sasa Tume inaandaa utaratibu utakao wawezesha wananchi wenye sifa ambao walikosa fursa ya kuandikisha na kuhakiki taarifa zao ili wapate nafasi ya kushiriki kikamilifu  katika Uchaguzi Mkuu ujao.

Aidha, Afisi za Tume ya Uchaguzi za Wilaya hivi sasa zinapokea maombi ya wapiga kura wanaotaka kufanyiwa uhamisho wa taarifa zao kutoka vituo vya majimbo waliyopiga kura katika uchaguzi uliopita kwenda katika vituo vya majimbo ambayo wanaishi hivi sasa ambako watakuwa wametimiza sifa ya ukaazi katika vituo vya majimbo hayo.

 Kazi hiyo itaendelea na itasita miezi mitatu kabla ya upigaji wa kura. Tume inawaomba wale wote wanaotaka kufanya uhamisho wa taarifa zao kufanya hivyo muda huu; vyenginevyo watalazimika kwenda kupiga kura katika vituo vyao vya zamani.

Ndugu waandishi wa Habari, Katika zoezi la awali  la uandikishaji wa wapiga kura wapya na uhakiki wa wapiga kura, Takwimu za awali zinaonesha kwamba jumla ya wapiga kura 413,444 walipatiwa huduma hiyo vituoni na kati ya hao wanaume walikuwa ni 199,327 na wanawake ni 214,117. (Inasisitizwa kuwa takwimu hizi ni za awali).

Ndugu Waandishi wa Habari, Kazi nyengine ambayo Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar inawajibika kuifanya katika kipindi hiki cha maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 ni kupitia (review) idadi, majina na mipaka ya majimbo ya Uchaguzi. Kazi hii itafanywa na Tume kwa maelekezo ya kifungu cha 120(4) cha Katiba ya Zanzibar ambacho kimeipa uwezo Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar katika kipindi cha miaka 8 hadi 10 au wakati mwengine wowote, kuchunguza idadi ya mipaka na majina ya majimbo hayo kwa kiwango kile ambacho Tume inahisi kuwa ni wajibu kuangaliwa upya na inaweza kubadili idadi, mipaka na majina ya majimbo hayo kadiri itakavyoona inafaa.

Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar mara ya mwisho ilifanya mapitio kama haya ya majimbo mwaka 2015 kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2015, mapitio ambayo yalipelekea kuongezwa kwa majimbo ya uchaguzi kutoka 50 yaliyokuwepo kabla na kuwa majimbo 54 yaliyotumiwa kwa uchaguzi wa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Madiwani. Tume inawajibika kufanyia tena mapitio ya majimbo haya miaka mitano baada ya zoezi la mwaka 2015 kutokana na malalamiko katika baadhi ya majimbo ambako kuna wadi ambazo Shehia zake zinahudumiwa na majimbo mawili tofauti kinyume na utaratibu. Kwa kawaida kila jimbo linaundwa na wadi mbili mpaka tatu ambapo kila wadi inaundwa na shehia mbali mbali zilizomo katika eneo la uchaguzi. Katika kazi ya mapitio ya majimbo ya mwaka 2015, kuna mkanganyiko ulijitokeza katika wadi na majimbo ya  uchaguzi Unguja na Pemba. Kutokana na hali hiyo, Tume imeamua kabla ya Uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka 2020 ifanye mapitio ya majimbo na ikiwezekana kwa mamlaka iliyo nayo ifanye marekebisho yanayostahiki kwa eneo ambalo linastahiki kufanyiwa marekebisho yanayofaa.

Ndugu Waandishi wa Habari, Mapitio ya idadi na mipaka ya majimbo ya uchaguzi ni kazi shirikishi ingawaje mamlaka ya kufanya kazi hiyo kisheria ni ya Tume ya Uchaguzi.  Hata hivyo, Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kwa kuthamini uwepo mkubwa wa wadau wa uchaguzi vikiwemo vyama vya siasa, Asasi za kiraia na mtu mmoja mmoja, inatoa nafasi kwa wadau wote kushiriki kikamilifu kutoa maoni na maono yao kwa njia ya barua au mawasiliano yoyote kwa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar juu ya hali ya majimbo kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020. Maoni na maono hayo yatapokelewa katika Ofisi zote za Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar Unguja na Pemba wakati wowote baada ya kutoka kwa taarifa hii.

Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ilipanga kuchukua maoni ya wadau juu ya suala hili kwa kufanya mikutano mbali mbali na wadau. Hata hivyo, kutokana na maradhi ya homa ya mapafu (COVID 19) yanayosababishwa na virusi vya CORONA yaliopo nchini na kutokana na agizo lilitolewa na Serikali juu ya kujikinga na maradhi hayo kwa kuepuka mikusanyiko ya watu, Tume haitoandaa mikutano ya maoni, badala yake itapokea maoni na maono hayo kwa njia ya barua katika Afisi Kuu ya Tume ya Uchaguzi iliyopo Maisara Unguja, Afisi ya Tume ya Uchaguzi Pemba iliyopo Chake Chake au katika Afisi za Wilaya za Tume zilizopo katika Wilaya zote za Unguja na Pemba.

Ndugu Waandishi wa Habari, Baada ya maelezo hayo ambayo yamegusa mambo matatu muhimu yanayofanywa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar katika kipindi hiki cha matayarisho ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, nachukua nafasi hii kuishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kutupa misaada mbalimbali iliyotuwezesha kufanikisha maandalizi ya Uchaguzi Mkuu ujao. Ni imani yangu kubwa kuwa wakati mtakapokuwa mnatayarisha taarifa zenu kwa umma mtakuwa makini kuyaeleza vyema yale yote ambayo nimeyasema katika taarifa hii.
Nawashukuru nyote kwa kunisikiliza. 

Ahsante sana


JAJI MKUU (Mst) HAMID MAHMOUD HAMID
MWENYEKITI
TUME YA UCHAGUZI YA ZANZIBAR
ZANZIBAR










No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.