Mwenyekiti
wa THBUB, Jaji (Mst) Mathew Mwaimu (kulia) akiongea na Kamishna wa Sekretarieti
ya Maadili ya Utumishi wa Umma, Jaji (Mst) Harold Nsekela (Kushoto)
alipomtembelea ofisini kwake jijini Dodoma jana. Lengo la ziara hiyo ya THBUB ni
kuimarisha ushirikiano na Sekretarieti ya Maadili.
Na Mbaraka Kambona,
Kamishna
wa Sekretarieti ya Maadili ya Utumishi wa Umma, Jaji (Mst) Harold Nsekela
amezishauri taasisi zinazosimamia utawala bora kushirikiana kwa karibu ili
waweze kutekeleza majukumu yao vizuri.
Jaji
Nsekela alitoa rai hiyo katika ofisi yake jijini Dodoma jana alipokutana na
Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Jaji (Mst)
Mathew Mwaimu.
Alisema
kuwa taasisi hizo zimekuwa na mazoea ya kushirikiana kwa ukaribu wakati wa
sherehe za maadhimisho ya siku ya maadili na haki za binadamu, jambo ambalo
alisema kuwa haipaswi kuwa hivyo na badala yake taasisi hizo ziimarishe
ushirikiano huo wakati wote.
Aliongeza
kuwa kufanya kazi kwa ukaribu na kubadilishana taarifa wakati wa kutekeleza
majukumu yao kutasaidia taasisi hizo kuainisha mipaka yao ya kiutendaji ambapo
itawawezesha kujiepusha na muingiliano wa shughuli zao.
“Kuna
umuhimu wa kuwa na ushirikiano wa karibu kati yetu, hii itatusaidia
kubadilishana taarifa ambazo zitatusaidia kutoa huduma kwa wananchi ipasavyo”,
Jaji Nsekela alieleza.
Aliendelea
kusema kuwa kimsingi majukumu ya taasisi hizo yanafanana, kwani zote ni taasisi
za uchunguzi, tofauti iliyopo ni kwamba THBUB inashughulikia masuala ya haki za
binadamu, Sekretarieti ya Maadili inasimamia maadili ya utumishi wa umma,
TAKUKURU wao wanachunguza masuala ya rushwa na ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa hesabu za serikali
inasimamia matumizi ya fedha za umma.
Aliongeza
kuwa kuna haja ya taasisi hizi kubadilishana uzoefu wa mara kwa mara ili kila
mmoja aelewe mipaka ya mwenzake jambo ambalo
litawasaidia kuepuka muingiliano wa majukumu yao.
Aidha,
Jaji Nsekela aliishauri THBUB kuendelea
na utekelezaji wa majukumu yake kwa kuzingatia maadili kwa sababu hiyo ndio
njia pekee itakayowawezesha kutoa huduma kwa wananchi bila malalamiko.
“Katiba imewapa mamlaka ya kulinda na
kuhamasisha haki za binadamu na misingi ya utawala bora nchini, tumieni mamlaka
hayo kwa kutoa huduma bora kwa Wananchi huku mkizingatia maadili”, Jaji Nsekela
alisisitiza
Akiongea
mapema, Jaji Mwaimu alieleza kuwa lengo la ziara yake ni kuimarisha ushirikiano
na Sekretarieti ya Maadili, lakini pia kuwakumbusha wananchi kuwa THBUB ipo kwa
ajili ya kuwasaidia.
Jaji
Mwaimu aliendelea kueleza kuwa katika kipindi cha miaka miwili iliyopita THBUB
imekuwa ikitekeleza majukumu yake bila ya uongozi kwa maana ya Makamishna jambo
ambalo liliathiri utendaji wa taasisi hiyo.
“THBUB
ni huru, hatupaswi kuchukua upande tunaposhughulikia masuala ya uvunjifu wa
haki za binadamu na misingi ya utawala bora, jukumu letu la msingi ni kusaidia
wananchi kupata haki zao”, Jaji Mwaimu ilifafanua
Mwenyekiti
wa THBUB, Jaji (Mst) Mathew Mwaimu (kulia) akimkabidhi Kamishna wa Sekretarieti
ya Maadili ya Utumishi wa Umma, Jaji (Mst) Harold Nsekela (Kushoto) barua ili
kuimarisha ushirikiano baina ya THBUB na Sekretarieti ya Maadili.
Kamishna
wa Sekretarieti ya Maadili ya Utumishi wa Umma, Jaji (Mst) Harold Nsekela
(Kulia) akimsindikiza Mwenyekiti wa THBUB, Jaji (Mst) Mathew Mwaimu (kushoto)
mara baada ya kumaliza mazungumzo yao.
Kamishna
wa Sekretarieti ya Maadili ya Utumishi wa Umma, Jaji (Mst) Harold Nsekela (Kushoto)
akiteta jambo na Kaimu Katibu Mtendaji wa THBUB, Hajjat Fatuma Muya (Kulia)
muda mfupi mara baada ya kumaliza kikao.
No comments:
Post a Comment