Habari za Punde

Umoja wa Vilabu Zanzibar Kuzungumzia Hatma ya Ligi Kuu ya Zanzibar.


NA MWAJUMA JUMA

UMOJA wa Vilabu Zanzibar unatarajia kukutana Jumamosi ya mwisho wa wiki hii, mada kuu kuzungumzia kuhusu hatma ya ligi.

Umoja huo ambao unajumuisha vilabu vyinavyoshiriki ligi Kuu ya Zanzibar na daraja la kwanza Kanda lakini kwa siku hiyo watakaoshiriki ni makatibu na wenyeviti wa klabu za ligi kuu pekee.

Hata hivyo taarifa za wapi kikao hicho kitafanyika hazijasema lakini taarifa za ndani zinasema kuwa wamewaita na viongozi wa kamati tendaji wa Shirikisho la soka Zanzibar wa Uguja pekee ambao wamewachaguwa kwa kura.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa sharti la kutotajwa jina lake mmoja wa viongozi wa umoja huo alisema kuwa kikao ambacho watakifanya ni cha kujenga lakini kwanza wameweka siri sehemu ya kufanyia.

Alieleza kuwa katika kikao hicho watazungumza namna ligi hiyo ichezwe na mambo mengine yote ambayo ni ya kujenga na tayari wajumbe wa kamati Tendaji wa Shirikisho hilo wameridhia mualiko wao huo.

“Tumekubaliana tufanye kikao na katika kikao hicho itatubidi tuwaite na wajumbe wa kamati tendaji ya Shirkisho hilo wale wote ambao tumewachaguwa”, alisema mtoa habari huyo.

Alisema kuwa ajenda kuu ambayo iliyopo ni kuhusu ligi lakini kwa vile wanakutana na wajumbe wa kamati tendaji itawabidi na ajenda nyengine za kuongea nao ili kuweza kufikia muafaka.

Alifahamisha kwamba katika kikao hicho wana matarajio makubwa ya kuweza kupata kitu ambacho kitaweza kuwa na maana kwa maslahi ya kujenga soka lao.

“Sasa hivi nakupa taarifa ya kukutana hiyo lakini Jumamosi nitafute mara baada ya kumaliza kikao ili nikupe kilichotokea huko lakini nina imani kitaenda sawa na tutatoka na kitu kimoja cha kujenga”, alisisitiza mtoa habari huyo.

Mtoa habari huyo alisema kuwa kikao hicho pia kitaweza kupanga kikao chengine cha kufanyika ambacho kitashirikisha na klabu za Pemba ambacho hicho kitafanyika Pemba.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.