Habari za Punde

HOTUBA YA MAONI YA KAMATI YA USTAWI WA JAMII KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA YA AFYA KWA MWAKA WA FEDHA 2020/2021
Mheshimiwa Spika, Kwanza kabisa naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu, Mjuzi wa yote, Muumba na mwenye kurehemu kwa kutujaalia Afya njema  iliyotuwezesha kukutana tena siku ya leo katika Baraza hili Tukufu kwa lengo la kutekeleza majukumu yetu kwa mustakabali ulio bora. Aidha, napenda pia, kukushukuru na kukupongeza wewe binafsi kwa unavyoliongoza Baraza hili kwa hekma busara na upendo wa hali ya juu, tunamuomba Allah (SW) azidi kukuongoza katika mambo ya kheri na In Shaa Allah utaliongoza tena Baraza hili Tukufu kwa kipindi kinachokuja. 

Mheshimiwa Spika, Kwa moyo wa dhati napenda nitoe shukurani na pongezi za pekee kwa Mheshimiwa Raisi wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dkt. Ali Mohammed Shein kwa kipindi chote alichotumikia nchi hii kwa utulivu na upendo wa hali ya juu na kuitekeleza vyema ilani ya Chama cha Mapinduzi, ni dhahiri kwamba Mheshimiwa Rais amefanya mema mengi na yamsingi ambayo daima wananchi wake tutayakumbuka. Tunamuomba mwenyezi mungu amjaalie uzima, maarifa na nguvu kamili za kuweza kumaliza kipindi hichi kwa salama na amani.

Mheshimiwa Spika, Kwa heshima na taadhima nachukua nafasi hii kumpongeza na kumshukuru sana Waziri wa Afya Mheshimiwa Hamad Rashid Mohamed, Naibu Waziri Mheshimiwa Harusi Said Suleiman, Katibu Mkuu pamoja na Watendaji wake wote wa Wizara kwa jitihada kubwa walizozichukua katika kuhakikisha wananchi wa Zanzibar wanapata huduma bora.
Mheshimiwa Spika, Kwa kuwa hichi ni kipindi cha mwisho kukutana sote katika Baraza hili la Tisa naomba niwashukuru wajumbe wa Baraza hili tukufu kwa muda wote ambao tulikuwa pamoja katika kuhakikisha tunawakilisha vyema yale yote tuliagizwa na wananchi wetu ambao walituamini huko majimboni na imani yangu kwa wale wote tutaokuwa nania watatuchagua tena kuwatumikia katika kipindi kinachokuja.
Mheshimiwa Spika, Kwa namna ya pekee napenda kuwashukuru Wajumbe wote wa Kamati ya Ustawi wa Jamii kwa utekelezaji mzuri wa kazi zao, umakini na umahiri mkubwa na ndio sababu kuu iliyopelekea kuijadili bajeti hii  pamoja na kuhoji mambo yote ambayo yalitupa mashaka kwa mantiki ya kuhakikisha fedha wanazoidhinishiwa  Wizara hii na Baraza lako Tukufu zinatumika ipasavyo kama zilivokusudiwa.
Mheshimiwa Spika, Kabla sijaendelea na hotuba hii, kwa heshima kubwa naomba niwatambue Wajumbe wa Kamati ya Ustawi wa Jamii ambao walifanya kazi na kushauri kwa namna moja au nyengine wakati wakutekeleza kazi za Kamati hii kama ifuatavyo:
  1.  
Mheshimiwa Mwanaasha Khamis Juma  
Mwenyekiti
  1.  
Mheshimiwa Nassor Salim Ali
M/Mwenyekiti
  1.  
Mheshimiwa Shehe Hamad Mattar
Mjumbe
  1.  
Mheshimiwa Tatu Mohammed Ussi
Mjumbe
  1.  
Mheshimiwa Yussuf Hassan Iddi
Mjumbe
  1.  
Mheshimimwa Amina Iddi Mabrouk
Mjumbe
  1.  
Mheshimiwa Ramadhan Hamza Chande
MjumbeMheshimiwa Spika, Kamati hii inafanyakazi na Makatibu wawili ambao wamekuwa wakitusaidia kwa kiasi kikubwa na uweledi wa hali ya juu katika kutekeleza majukumu yetu, msaada wa makatibu hao umekuwa ndio chanzo cha mafanikio makubwa ya Kamati hii.  Makatibu hao ni:

1.    Ndg. Aziza Waziri Kheir                                                       Katibu
2.    Ndg. Mwanaisha Mohammed Kheir                                      Katibu
Mheshimiwa Spika, Kamati yetu ya Ustawi wa Jamii miongoni mwa majukumu yake ni kuchambua mapendekezo ya Serikali, kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya kawaida na miradi ya maendeleo ya Wizara ya kila mwaka, hivyo katika kutekeleza jukumu hilo lililoelezwa katika Kanuni za Kudumu za Baraza la Wawakilishi (Toleo la 2020), Kamati yangu ilikaa na kujadili na hatimaye kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya kwa mwaka wa fedha 2020/2021. Nasasa kwa ruhusa yako na kwa niaba ya Kamati, napenda kuwasilisha maoni ya Kamati kuhusiana na Bajeti hiyo.
Mheshimiwa Spika, Kwa mwaka huu wa fedha Wizara ya Afya imepangiwa kutekeleza kazi zake kupitia Programu Kuu Nne ambapo utekelezaji wake utasimamiwa na programu ndogo ndogo ndani yake.
Mheshimiwa Spika, Kamati yetu inaipongeza Wizara ya Afya kwa kuweza kutekeleza kazi zake kwa kiwango kikubwa kufuatia Bajeti iliyoidhinishiwa kwa mwaka uliopita 2019/2020.  Aidha, imefurahishwa na ongezeko la bajeti kwa mwaka wa fedha 2020/2021 ambayo imepangiwa kutumia jumla ya Tsh. 100,236,100,000/- kupitia (Fungu H01). Hata hivyo, Kamati inawapa tahadhari Wizara  kujipanga vizuri zaidi kwa mwaka unaokuja kwa kuhakikisha fedha watazoingiziwa hazipotei na matumizi yake yaende kwa usahihi ili kufikia malengo yote yaliyokusudiwa.
PROGRAMU KUU YA KINGA NA ELIMU YA AFYA
Mheshimiwa Spika, Programu hii inajukumu la kuhakikisha jamii inapata elimu na huduma ya kujikinga na maradhi mbalimbali yakiwemo ya kuambukiza na yasiyo yakuambukiza. Kwa mwaka huu wa fedha 2020/2021 programu ya Kinga na Elimu ya Afya imepangiwa kutumia jumla ya Tsh 28,664,931.000/-, Kamati inaipongeza Wizara kwa ongezeko la bajeti hii ambapo kwa mwaka 2019/2020 Programu ya Kinga na Elimu ya Afya ilipangiwa kutumia jumla ya Tsh. 21,888,822.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kupitia utekelezaji wa shughuli ya huduma za kumaliza Malaria Zanzibar Kamati inaipongeza Wizara kwa kufanikiwa kuondosha maradhi haya kwa asilimia kubwa kabisa kutokana na hatua mbali mbali walizozichukua za kuangamiza mazalio ya mbu na kupiga dawa majumbani. Hata hivyo, Kamati inashauri Wizara kuongeza jitihada za kuelimisha wananchi kufuatia ishara za ongezeko la homa ya malaria siku zahivi karibuni. Hali hii imesababishwa na  mazalio ya mbu wa Malaria yanayotokana na mvua zinazoendelea, kuendelea kugawa vyandarua vilivyotiwa dawa pamoja na jamii kuwa tayari kupuliziwa dawa za kuangamiza maradhi hayo majumbani.
Hospitali ya Micheweni.
Mheshimiwa Spika, Kamati katika mizunguko yake ya ufatiliaji wa utekelezaji wa Bajeti ilifika Hospitali ya Micheweni na kutembelea wodi ya wazazi ambayo ilionekana wazi kuwa na uhaba wa vyumba vya kujifungulia pamoja na uchache wa vitanda. hali  hii imesababisha wazazi watatu kutumia kitanda kimoja. Aidha, Kamati inasikitishwa na taarifa ya kusitishwa kwa ujenzi wa banda moja la wodi ya wazazi kupitia wafadhili wa Milele Foundation ambao walijitolea kulijenga baada ya kukamilisha taratibu zote za ujenzi. Kamati inaishauri Wizara kulifuatilia kwa undani suala hili na baadae kukubiliana na Milele Foundation kwa ajili ya ujenzi wa banda la Mama na Mtoto.
Mheshimiwa Spika, Kamati pia inaishauri Wizara Kupitia bajeti hii ya 2020/2021 kurekebisha mfumo wa upatikanaji wa kibali cha kusafirishia “Oxygen” kinatolewa kimoja tu kwa Pemba nzima. Hali ambayo hupelekea utolewaji wa huduma kutokamilika kwa wakati iwapo “oxygen” hiyo imemalizika. Aidha, hospitali ya Micheweni inakabiliwa na upungufu wa seti za upasuaji kwa mama wajawazito pamoja na vifaa vya kumsaidia hewa mgonjwa “Capnofraphy” ambapo kazi hufanyika kwa kusubiriana, pamoja na kulishughulikia kwa upana wake tatizo la seti za upasuaji wa mama wanaotaka kujifungua ili kuepusha hatari zinazoweza kutokea.
Mheshimiwa Spika, Kufuatia muamko mdogo wa baadhi ya wananchi juu ya huduma za Kliniki Kamati inatoa wito kwa Wizara juu ya umuhimu wa kuongeza bidii za kuwashajihisha wanawake kuwahi kuhudhuria Kliniki pindi wanapojigundua wajawazito ili kama kuna matatizo ambayo tiba yake inaweza kupatikana mapema kuweza kushughulikiwa kuliko kwenda kwa ajili tu ya kupata gamba la kujifungulia.
Huduma za ufatiliaji wa Mienendo ya Maradhi
Mheshimiwa Spika, Kwa upande wa janga la maradhi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Covid 19 Kamati inaipongeza Wizara pamoja na Watendaji wake wote walijitolea na kuwa mstari wa mbele kwa jitihada wanazozichukua kukabiliana na gonjwa hili licha ya changamoto ndogo ndogo zinazojitokeza.
Mheshimiwa Spika, Kamati inaiomba Wizara kuwapa motisha wauguzi wa Corona ili kuweza kufanya kazi zaidi pamoja na kutoa elimu ya kutosha kwa wauguzi waliomo katika hospitali zetu nyengine jinsi ambavyo wataweza kujikinga na kuwauguza washukiwa wa maradhi ili kuepusha vifo vinavyoweza kutokea kwa kuhofia kuambukizwa na maradhi hayo, kupitia bajeti hii ya 2020/2021 naiomba Serikali na Wizara kwa ujumla kuhakikisha Madaktari na wauguzi wote wanaowahudumia wagonjwa wa Maradhi ya Corona ambao wapo katika kambi zilizotengwa kuwarejeshea mfumo wa ulipaji posho lililokuwa likitolewa kwa watendaji hao hapo awali ili kuondoa malalamiko yanayojitokeza katika kipindi hichi.
PROGRAMU KUU YA HUDUMA ZA TIBA
Mheshimiwa Spika, Dhumuni ya Programu Kuu ya Huduma za Tiba ni kutoa huduma za afya katika Hospitali za ngazi za Vijiji hadi mkoa kupitia Mabaraza ya kitaaluma na Bodi, kusimamia miradi mbali mbali ikiwemo Mradi wa Ujenzi wa Hospitali ya kisasa ya Rufaa na kufundishia katika eneo la Binguni.
Hospitali ya Rufaa na Kufundishia Binguni.
Mheshimiwa Spika, Pamoja na kwamba eneo lililotengwa kwa ajili ya Hospitali ya Rufaa na kufundishia huko Binguni limekuwa likitajwa kwa muda mrefu sasa bila ya mafanikio. Kamati imefarijika na maelezo ya Wizara yaliyoelezea dhamira ya kuanza ujenzi wa majengo matatu katika eneo hilo la Binguni likiwemo jengo la Dharura, jengo la Upasuaji na jengo la Uchunguzi wa Maradhi.  
Mheshimiwa Spika, Ifahamike kwamba, Kamati ilifanya ziara mara kadhaa katika eneo hilo hata hivyo haikubahatika kuona hatua za matayarisho ya ujenzi huo hata yale ya kuwalipa fidia wakaazi wa eneo lile lililopimwa kwa ajili ya ujenzi zaidi ya kuwekwa viguzo vya kuzuia uvamizi wa eneo na kuelezwa kwamba michoro ya awamu ya kwanza imeshakamilika baada ya kumalizika kwa hatua za upimaji wa ardhi  licha ya kuingiziwa fedha kwa vipindi tofauti zisizopungua Tsh 10,472,592,000/- kwa ajili ya ujenzi huo na  hadi kufikia mwisho wa mwezi Juni Mwaka huu kiasi cha fedha zilizokua hazijatumika 6,000,000,000/- zitarudishwa Serikalini iwapo hazijatumika.
Mhehimiwa Spika, Kwa mwaka huu 2020/2021 Ujenzi wa Hospitali ya Binguni umepangiwa jumla ya Tsh 5,500,000,000/- Kamati inaiomba Wizara kutoa maelezo ya kutosha juu ya fedha zilizoidhinishwa hapo kablalicha ya kueleza kuwa ujenzi huo utatumia kampuni ya Serikali ambayo itawahusisha Wakandarasi wahandisi wa Vikosi vya Idara Maalumu za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Mheshimiwa Spika, Kwa upande wa Hospitali ya Abdalla Mzee Kamati imekua haifurahishwi na majibu ya Wizara kuhusiana na ujenzi wa nyumba za wafanyakazi katika Hospitali hiyo kutokana na kwamba ujenzi wa nyumba hizo ni wa muda mrefu sasa na hakuna hatua yoyote iliyofikiwa. Aidha, Kamati imechoka kuona hitilafu inayosababishwa na matumizi ya umeme inayopelekea kuharibika kwa vifaa bado inaendelea. Naiomba Wizara kutoa majibu ya kuridhisha kuhusiana na hatua walizofikia baada ya Kamati kutoa maelekezo kwa Wizara kukaa pamoja na Shirika la umeme ZECO ili kujua kilio hicho vipi kitamalizika.
Bohari Kuu ya Dawa Pemba.
Mheshimiwa Spika, Kamati wakati ikiipitia Bajeti hii ilielezwa ujenzi wa Bohari kuu ya dawa Pemba kwenye eneo la Hospitali ya Vitongoji umefikia katika hatua za kukamilika, na ndani ya mwezi huu wa sita jengo hilo linategemewa kukabidhiwa rasmi kwa Wizara. Kamati inaipongeza Wizara ya Afya kwa maendeleo hayo, hii itaifanya Wizara kuondokana na ile shida ya usafirishaji wa dawa kila robo mwaka kisiwani Pemba.
Hospitali ya Chake chake.
Mheshimiwa Spika, Kamati wakati ikipitisha bajeti ya wizara hii ilielezwa kwamba hatua za manunuzi kwa ajili ya ujenzi ya wodi ya mama na mtoto katika Hospitali ya ChakeChake umekamilika. Niseme kwamba, taarifa hii imetushangaza kidogo kwa kuwa hadi tunamaliza mzunguuko wa mwisho wa ufatiliaji wa utekelezaji wa kazi za bajeti, Wizara haikua imepata muwafaka wa ujenzi huu kutokana na kampuni ya RUNs ilishauri kutafuta eneo jengine kwa ajili ya ujenzi huo kwasababu ya ardhi ya hapo haikubalini na ujenzi wa gorofa wanaoutaka na pia, gharama ya fedha walikusudia kutumia kwa ajili ya kazi hiyo ambayo ni kiasi cha B. 1.4 hakitoshelezi, na ikashauriwa kuongezwa kiasi chengine cha fedha kisichopungua Tsh. Bilioni moja.
Mheshimiwa Spika, kwa upande mwengine Wizara iliwaomba Wakala wa Majengo nao kufanya utafiti wa eneo hilo ambapo baada ya kukamilika kwa akazi waliyoagizwa ilitoa ripoti ya kutaka ujenzi huo uendelee kwa misingi ya kusimamisha nguzo imara. Hivyo, Kamati inashauri kwa Wizara kutafuta muwafaka wa ujenzi wa majengo ya Wodi ya Mama na Mtoto yaliopo Hospitalini hapo kwa mujibu wa bajeti wanayoidhinishiwa na kwa kufuata ushauri wa mjenzi ili kuepusha athari zinazoweza kutokea baada ya ujenzi huo kukamilika.
Mheshimiwa Spika, kupitia bajeti hii ya mwaka 2020/2021 Kamati inaiomba Wizara kutoa majibu ya kina mbele ya Baraza hili tukufu kuhusiana na fedha ambazo zimekuwa zikiingizwa katika bajeti zilizopita kwa ajili ya ujenzi huo ili iweze kuidhisha bajeti ya mwaka huu bila ya matatizo yoyote.
PROGRAMU KUU YA UENDESHAJI NA URATIBU WA WIZARA YA AFYA
Mheshimiwa Spika, Kamati inaipongeza Wizara kufuatia ongezeko la bajeti kwa mwaka huu wa Fedha 2020/2021 kupitia programu ya Uendeshaji na Uratibu wa Wizara ya Afya ambayo imepangiwa kutumia jumla ya Tsh. 20,312,959,000/- tofauti na mwaka wa fedha uliopita 2019/2020 ambayo programu hii iliidhinishiwa kutumia jumla ya Tsh. 17,428,825,000/- kwa ajili ya kazi zake za kawaida.

Mheshimiwa Spika, Kamati yetu  kupitia programu hii inaipongeza Wizara ya Afya kwa kupata Sheria mpya ya Utafiti na Wataalamu wa Maabara za Tiba na Sheria ya Taasisi ya Utafiti wa Afya Zanzibar ambazo zote kwa pamoja zimepitishwa katika kikao kilichopita na Tayari Mheshiwa Raisi wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein amezitia saini. Imani yetu kwamba Wizara kupitia Taasisi husika zitafanya kazi kwa uweledi na uwadilifu wa hali ya juu kwa misingi ya Sheria.
PROGRAMU KUU YA HOSPITALI YA MNAZI MMOJA
Mheshimiwa Spika, Kupitia (Fungu H02) la Hospitali ya Mnazi mmoja imepangiwa kutumia jumla ya Tsh. 17,348,600,000/- kwa ajili ya kufundisha wanafunzi wa kada ya afya wa ndani na nje ya Zanzibar na utoaji wa huduma za uchunguzi na matibabu kwa wagonjwa wa rufaa.
Mheshimiwa Spika, Kamati wakati ikifanya ziara katika hospitali ya Mnazi Mmoja iligundua kasoro kadhaa ikiwemo ya Uchakavu wa Chumba cha Upasuaji, upungufu wa vifaa na ukosefu wa mwanga wa kutosha katika chumba cha Upasuaji hali inayopelekea wakati mwengine madaktari kushindwa kufanya kazi za upasuaji. Matatizo mengine ni pamoja na kuharibika kwa AC mara kwa mara na ukosefu wa vyoo kwa ajili ya watu wenye mahitaji maalumu. Kamati inaiomba Wizara katika bajeti hii ya 2020/2021 kupitia changamoto hii ya uchakavu wa chombo cha upasuaji kuharakisha kupatikana kwa Mkandarasi kwa ajili ya ukarabati wa chumba hicho.
Mheshimiwa Spika, Baada ya maoni hayo ya Kamati, napenda kukushukuru kwa mara nyengine tena Mheshimwa Spika, kwa kunipa nafasi ya kuwasilisha maoni ya Kamati yangu kwa niaba ya Kamati pamoja na Wajumbe wa Baraza lako Tukufu kwa kunisikiliza kwa umakini mkubwa, tunaimani Wizara hii inatekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi.
Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa, sasa niwaombe Wajumbe wa Baraza hili Tukufu, waichangie na hatimae waiunge mkono bajeti hii, ili wamuwezeshe Mheshimiwa Waziri kufanikisha na kutekeleza wa yale waliojipangia katika mwaka huu wa Fedha 2020/2021.
Mheshimiwa Spika, Mimi mwenyewe na kwa niaba ya Kamati ya Ustawi wa Jamii, naunga mkono hoja kwa asilimia 100%.
Naomba kuwasilisha.
Ahsante,

……………………
Mhe. Mwanaasha Khamis Juma
Mwenyekiti,
Kamati ya Ustawi wa Jamii,
Baraza la Wawakilishi,
Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.