Habari za Punde

Jimbo la Magomeni laanza kazi za kujenga barabara za ndani jimboni

 Gari aina ya Katapila na Bulldozer zikiwakazini katika ujenzi wa barabara ya ndani ya Kwamtumwajeni wakati wa uzinduzi wa barabaraza za ndani za jimbo la Magomeni
 Mbunge wa Jimbo la Magomeni Jamal Kassim akizungumza na viongozi wa Shehia za Jimbo la Magomeni katika uzinduzi wa ujenzi wa barabara za ndani na kuwaomba wananchi kuwa wastahamilivu wakati wa ujenzi huo
  Mwakilishi wa Jimbo la Magomeni Rashid Shamsi akiwashukuru wananchi kwa mashirikiano waliotoa kwa viongozi wao ambapo wameweza kuondosha shida nyingi zilizokuwa zikiwakabili
Magari yaliyopakia kifusi yakiwa tayari kumwaga kifusi hicho wakati wa uzinduzi wa ujenzi wa barabara za ndani uliofanyika barabara ya Kwamtumwajeni Magomeni
PICHA NA RAMADHANI ALI MAELEZO

Mwashungi Tahir     Maelezo   8-6-2020.
Mbunge wa Jimbo la Magomeni Jamal Kassim Ali amesema mashirikiano ya pamoja na viongozi wenzake  ndiko kulikopelekea kutimiza malengo ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya kuwahudumia wananchi ndani ya Jimbo hilo.
Ameyasema hayo kwa Mtumwajeni alipokuwa akizungumza na viongozi wa shehia nne Magomeni wakati wa uzinduzi wa ujenzi wa barabara za ndani zilizomo ndani za jimbo hilo.
Amesema ujenzi wa barabara za ndani ni miongoni mwa ahadi alizotoa wakati wa kuomba ridhaa za wanachi kumchangua ili aweze kuwatumikia.
“Miongoni mwa ahadi nilizoweka wakati wa kampeni za kuomba ridhaa zenu ni kushirikiana na viongozi wengine kujenga barabara za ndani ziweze kupitika kwa urahisi,” alieleza Mbunge Jamal Kassim Ali
Amesema barabara ni moja ya miundombinu muhimu kwa wananchi katika kukuza uchumi wa Taifa na kuimarisha hali bora za maisha.
Mbunge wa Magomeni amewaomba wananchi wanaotumia barabara za ndani zinazojengwa kuwa wastahamilivu katika kipindi hichi hadi kazi za ujenzi zitakapokamilika.  
“Wakati ujenzi ukiendelea barabara zitafungwa kwa muda na zitakuwa na vumbi sana hivyo muwe wavumilivu lengo letu ni kutatua changamoto zinazowakabili ikiwemo barabara, maji safi na salama na upungufu wa madarasa ya kusomea,” alisisitiza Mbunge Jamal.
Mbunge wa Magomeni ameipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuimarisha miundo mbinu ya barabara kuu na kuziweka taa na wao wameamua kuboresha barabara za ndani ikiwa ni utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi.
Mwakilishi wa jimbo la Magomeni Rashid Shamsi amewashukuru wananchi kwa mashirikiano makubwa waliowapa ambayo yamesaidia kupunguza kero nyingi zilizokuwa zikilikabili jimbo la Magomeni.
Alisema barabara nyingi za ndani zimekuwa hazipitiki hasa wakati wa mvua za masika lakini ujenzi unaoendelea utakapokamilika utaondosha tatizo hilo.
Barabara maarufu nne za ndani zilizomo ndani ya Jimbo la Magomeni zenye urefu wa kilomita tatu zitajengwa. Barabara hizo ni Kwamtumwajeni, Nyerere, Makada na skuli ya maandalizi na zitagharimu zaidi ya shilingi milioni 28 zitakapokamilika.
IMETOLEWA NA MAELEZO ZANZIBAR

1 comment:

  1. Haya uchaguzi umekaribia, huo ujenzi unafanyika kwa fedha za umma, tusitumie hizo fedha kisiasa please

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.