Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Afanya Ziara Kutembelea Mradi wa Utanuzi wa Ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume Zanzibar

Meneja wa ujenzi wa mradi wa ujenzi wa Jengo la Abirina na eneo la maegesho ya Ndege kwenye Uwanja wa ndege wa Abeid Aman Karume  {Terminal Three} kwa upande wa serikali ya mapinduzi ya Zanzibar Mhandisi Yasir De Costa akimpatia maelezo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipofanya ziara fupi kuangalia maendeleo ya Ujenzi huo.
Muonekano wa haiba nzuri ya Jengo Jipya la Abiria linaloendelea kujengwa kwenye eneo jipya la maegesho ya Ndege { Terminal Three} katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Abeid Aman Karume.
Mhandisi De Costa akimpa matumaini Balozi Seif Ali Iddi ya kukamilika kwa Ujenzi wa Mradi huo katika Miezi Michache ijayo ili ufikie hatua ya kutoa huduma kama ilivyokusudiwa na Serikali.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwapongeza Watendaji wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar na Wahandisi wa Kampuni ya CRJ kutoka China kwa kazi kubwa ya muendelezo wa Ujenzi wa Mradi huo muhimu kwa Taifa.
Baadhi ya Wahandishi wa Ujenzi wa Mradi wa Terminal Three hapo Uwanja wa Ndege wa AAKIA kutoka Nchini China na wale wa Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius K. Nyerere wakifuatilia nasaha za Balozi Seif alipotembelea uwanja hapo.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Na.Othman Khamis.OMPR.
Kazi ya ujenzi wa mradi mkubwa wa eneo la maegegesho ya ndege kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Abeid Amani Karume Zanzibar zimeanza kupamba moto baada ya kusita kwa muda mrefu.
Harakati za umwagaji wa zege katika sehemu za kupakia na kushukia abiria ziko katika hatua nzuri chini ya wahandisi wa kampuni ya kimataifa ya CRJ kutoka nchini China wakisaidiwa na wahandisi na washauri wazalendo waliobobea kutoka uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere wa Dar es Salam.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alishuhudia harakati hizo pale alipofanya ziara maalum ya kukagua maendeleo ya mradi huo utakaokuwa wa kihistoria wakati Zanzibar inakusudia kurejea katika hadhi yake ya kuwa kituo cha biashara duaniani katika ukanda wa mashariki na kusini mwa bara la Afrika.
Meneja wa ujenzi wa mradi huo kwa upande wa serikali ya mapinduzi ya Zanzibar Mhandisi Yasir De Costa alisema kazi ya ujenzi wa mradi huo hivi sasa imeshafikia asilimia 71% na ile asilimia 29% iliobakia inatarajiwa kukamilika ndani ya kipindi cha miezi michache ijao.
Mhandisi De Costa alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba meli iliyobeba zana na vifaa vya kuendeleza mradi huo kutoka Nchini Jamuhuri ya Watu wa China hivi sasa imeshawasili katika bandari ya Zanzibar na utaratibu wa kuvishusha ili vifikishwe katika eneo husika unakamilishwa.
Alisema wahandisi wa mradi huo wamejipangia kumwaga zege urefu wa mita hamsini (50) kwa siku kazi inayokwenda sambamba na ujenzi  wa miundombinu ya misingi ya kupitishia maji machafu pamoja na mikonge ya kupitishia abiria .
“ Muda wowote kuanzia sasa zana hizo zitateremshwa baada ya kukamilika kwa utaratibu wa kuvitoa Banadarini sambamba na kufanya utafiti wa bara bara zitakazopishwa zana hizo kulingana na tahadhari ya wasafiri wengine wa Bara bara”. Alifafanua Mhandisi De Costa.
Alibainisha kwamba ubadilishaji wa maegesho yatakuwa upande wa Kusini wa Jengo la Abiria badala ya ile ya Mbele kwa Mfumo uliokubalika awali mabadiliko yaliyofanywa kuzingatia ushauri wa Wataalamu waliobobea ambao enbeo la mbele litaendelea kutoa huduma za kupita Ndege.
Mhandisi De Costa alifafanua kwamba kutokana na kasi kubwa za ujenzi huo kwa mujibu wa vigezo vya Kimataifa Ndege ya kwanza inaweza kutua na kupata huduma katika eneo hilo jipya ifikapo Mwezi Oktoba Mwaka huu.
Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amewapongeza wafanyakazi wa wizara ya ujenzi pamoja na wale wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege kwa ujenzi huo licha ya kuchelewa lakini kazi inaendelea vizuri na kutia moyo ili ile kiu ya wananchi ifikie kikomo.
Balozi Seif Alisema uwanja wa ndege wa Zanzibar umepata msukosuko wa mtaji wa fedha wa kuendesha Mradi huo hadi pale Viongozi Wakuu walipofikia ufumbuzi kutokana na umakini  waliouonyesha kuhakikisha kwamba Mradi huo unakamilika kama ilivyopangwa.
Alielezea faraja yake kutokana na Uzalendo wa Timu ya Wahandisi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Juluis Kambarage Nyerere ikiongozwa na Mhandisi Mahiri na Jabari Rehema Myeya kusaidia ushauri wa Kitaalamu katika maendeleo ya Ujenzi wa Mradi huo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliutaka Uongozi wa mamlaka ya viwanja vya ndege Zanzibar kujiandaa vyema kwa ajili ya kuhudumia idadi kubwa ya abiria wanaoshuka na kuondoka pale matengenezo ya Mradi huo yatakapokamilika.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.