Habari za Punde

HOTUBA YA MAONI YA KAMATI YA KUDUMU YA FEDHA, BIASHARA NA KILIMO KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA YA FEDHA NA MIPANGO KWA MWAKA WA FEDHA 2020/2021


HOTUBA YA MAONI YA KAMATI YA KUDUMU YA FEDHA, BIASHARA NA KILIMO KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA YA FEDHA NA MIPANGO
KWA MWAKA WA FEDHA 2020/2021

Mheshimiwa Spika,
Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kuendelea kutujaalia uhai na uzima na kutuwezesha kukutana ndani ya Baraza lako Tukufu kwa ajili ya shughuli zetu za upitishaji wa Bajeti. Nashukuru pia kwa kunipatia fursa hii ya kuwasilisha maoni ya Kamati ya Fedha, Biashara na Kilimo kuhusu makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa mwaka 2020/2021.

Mheshimiwa Spika,
Nachukua fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapindhuzi Dkt. Ali Mohamed Shein kwa uongozi wake imara ambao umepelekea nchi yetu kudumu katika hali ya amani na utulivu hadi leo hii. Nawapongeza pia wananchi wote wa Zanzibar kwa kufuata maelekezo ya Wizara ya Afya na miongozo ya viongozi wetu na hatimaye kuyadhibiti maradhi hatari ya Covid - 19 kwa jamii. Namuomba Mola Mtukufu azidi kutunawirisha na kutuondolea janga hili ambalo limeikumba dunia nzima. Azma kubwa tuwe na afya imara ili tuweze kujenga uchumi wa nchi yetu kwa manufaa ya watu wote.

Mheshimiwa Spika,
Naomba sasa niwatambue kwa kuwataja majina Waheshimiwa Wajumbe wa Kamati ya Fedha, Biashara na Kilimo ambao walitoa mchango na ushauri mkubwa katika utekelezaji wa kazi za Kamati kwa Wizara hii, Wajumbe wenyewe ni:-
1.
Mheshimiwa Dkt. Mwinyihaji Makame
 -
Mwenyekiti;
2.
Mheshimiwa Hamida Abdalla Issa
 -
Makamo Mwenyekiti;
3.
Mheshimiwa Ahmada Yahya Abdulwakil
 -
Mjumbe;
4.
Mheshimiwa Moh’d Mgaza Jecha
 -
Mjumbe;
5.
Mheshimiwa Mussa Ali Mussa
 -
Mjumbe;
6.
Mheshimiwa Nadir Abdullatif Yussuf
 -
Mjumbe; na
7.
Mheshimiwa Wanu Hafidh Ameir
 -
Mjumbe.

 

Mheshimiwa Spika,  

Kamati yetu pia inashirikiana vyema na makatibu wetu wawili ambao kwa kiasi kikubwa wamekuwa wakitusaidia kutekeleza majukumu yetu. Makatibu hao ni:

1.
Ndugu Asma Ali Kassim
 -
Katibu
2.
Ndugu Said Khamis Ramadhan
 -
Katibu

Mheshimiwa Spika,
Kamati ya Fedha, Biashara na Kilimo ilikutana na Wizara ya Fedha na Mipango na kujadili mapendekezo ya mapato, matumizi na Miradi ya Maendeleo ya Fungu FOI la Wizara ya Fedha na Mipango, fungu F02 la Mfuko Mkuu wa Serikali na fungu F03 la Tume ya Mipango. Kiujumla, Kamati yetu imeyakubali na kuyaridhia makadirio ya mafungu hayo.

Mheshimiwa Spika,
Jitihada za Wizara kutafuta mapato, kuyatunza vyema na hatimaye kuyatumia ipasavyo ni suala la kupigiwa mfano. Tunawapongeza wafanyakazi wote waliopo kwenye ukusanyaji wa mapato kwa kazi yao nzuri. Kamati yetu inaipongeza Wizara kwa sera nzuri za fedha na kodi ambazo zina mwelekeo wa kuisaidia sekta binafsi kuimarika.

Mheshimiwa Spika,
Tunaipongeza Wizara ya Fedha na Mipango kwa uandaaaji wa bajeti hii. Naomba ifahamike kwamba leo tunazungumzia bajeti ya Wizara na si bajeti ya Taifa. Wizara hii ndio dhamana wa upangaji wa mipango ya maendeleo ya nchi yetu kwa kushirikiana na sekta mbalimbali. Tunaipongeza Wizara kwa kuifanya kazi hiyo kwa ufanisi. Hata hivyo, tunaishauri Wizara kuratibu na kusimamia vyema shughuli za miradi inayosimamiwa na Wizara zaidi ya moja kama suala la mwani, mashamba ya mpira mafuta na uwekezaji kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika,
Aidha, tunaishukuru Wizara ya Fedha na Mipango ambayo ndiyo dhamana wa uwekezaji kwa kuandaa mpango mzuri kwa miradi mikubwa ya makaazi ikiwemo mradi wa Penny Royal, mradi wa ujenzi wa nyumba ziliopo Nyamanzi (Fumba Town Development) pamoja na mradi wa ujenzi wa nyumba za Bakhresa uliopo Fumba. Tunaiomba Serikali yetu sikivu iweke masharti nafuu kwa wanunuzi wa nyumba hizo ili kuwavutia wanunuzi kutoka ndani na nje ya nchi, pia kuimarisha uwekezaji uliokusudiwa.

Mheshimiwa Spika,
Kamati iliarifiwa kuwa jumla ya shilingi Trilioni Moja, Bilioni Mia Tano Arubaini na Tisa, Milioni Mia Tatu na Arubaini, Laki Nane na Ishirini na Nne Elfu zinatarajiwa kukusanywa na Wizara ya Fedha na Mipango kwa mwaka 2020/2021. Kiwango hiki cha mapato ni kikubwa ikilinganishwa na shilingi Trilioni Moja, Bilioni Mia Tatu Thamanini na Tatu, Milioni Arubaini na Tisa, Laki Saba na Thalathini na Tatu Elfu zilizokusanywa mwaka 2019/2020. Ongezeko hilo limetokana na makusanyo ya ada ya ukodishwaji ardhi, mapato ya Bodi ya Uhandisi, Bodi ya Wakandarasi na Bodi ya Uhaulishaji Ardhi kuingizwa Wizara ya Fedha na Mipango kutoka Wizara inayohusika na Ardhi.

Mheshimiwa Spika,
Mabadiliko haya yamefanywa baada ya kubainika kuwa muundo wa Bodi hizo hauko kimamlaka na hivyo kiutaratibu hazina mamlaka ya kutumia fedha hizo. Aidha, Serikali imebaini matumizi yasiyoridhisha ya sehemu ya fedha hizo na kuamua kuziingiza kwenye mfuko mkuu ili kuhifadhiwa vizuri na kufanyiwa matumizi sahihi yaliyopangwa.

Mheshimiwa Spika,
Kamati ya Fedha, Biashara na Kilimo imebaini kwamba kuna upotevu mkubwa wa mapato unaotokana na kutotumika kwa mashine za kiektroniki (EFD Machine) hususan katika vituo vya ununuzi wa mafuta ya vyombo vya usafiri. Kadhalika, kamati yetu inatambua kwamba wananchi wetu wengi hawana uelewa au utamaduni wa kudai risiti baada ya kupatiwa huduma.  Wauzaji nao huwa wagumu kutoa risiti kwa makusudi ili kukwepa kulipa kodi. Kwa mantiki hiyo, Kamati yetu inaitaka Wizara ya Fedha na Mipango kuharakisha ukamilishaji wa mfumo na taratibu za matumizi ya mashine za kielektroniki pamoja na kutoa elimu kwa wananchi na wafanyabiashara kwa ujumla kuhusu umuhimu wake kwa uchumi wetu.

Mheshimiwa Spika,
Kamati hii imegundua kuna mambo mengi mazuri ya maendeleo na yametekelezwa na Wizara za Serikali katika hali ya kuridhisha.  Hata hivyo, Kamati inasisitiza haja ya kuwepo utaratibu mzuri wa ufuatiliaji wa karibu zaidi katika uandaaji wa miradi ya maendeleo na utekelezaji wake. Kuna matokeo kadhaa ya migongano kati ya Wizara zetu katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika sekta zao kutokana na kukosekana kwa uratibu wa karibu wa kazi zinazofanyika
Mheshimiwa Spika,
Kamati yetu imeelezwa kwamba azma ya kuendeleza na kukamilisha ujenzi wa Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Aman Karume (Terminal III) ipo kama ilivyopangwa pamoja na kuibuka kwa janga hili la homa kali ya mapafu (Covid - 19). Kuwepo kwa hali hiyo kumechangia kuongezeka kwa muda wa makabidhiano hadi kufikia mwezi Januari 2021. Tunaipongeza tena Serikali yetu ya Mapinduzi Zanzibar kwa uamuzi wa busara wa kuazimia kumaliza ujenzi wa terminal III kwa fedha zetu wenyewe.

Mheshimiwa Spika,
Kamati yetu inaipongeza Wizara ya Fedha na Mipango na Serikali kwa ujumla kwa kulisimamia ipasavyo deni letu la Taifa kuwa katika hali ya uhimilivu kwani ukilinganisha mwezi Machi, 2019 na Mwezi Machi 2020, deni hilo limepungua kwa asilimia 2.6. Hali hiyo imetokana na kuongezeka kwa asilimia 13.3 ya deni la ndani ambalo Serikali imekopa kupitia Taasisi ziliopo nchini. Kamati yetu inaafiki utaratibu huo kwa vile taratibu za kupatikana na kulipa kwake huwa hauna vikwazo vingi na hata riba yake riba yake ni rafiki na mazingira halisi tuliyonayo.

Mheshimiwa Spika,
Moja kati ya vipaumbele ambavyo Wizara ya Fedha na Mipango imepanga kuvitekeleza katika bajeti ya mwaka 2020/2021 ni uimarishaji wa shughuli za kitengo cha uchumi wa buluu (Blue Economy). Kamati yetu imeridhishwa na hatua hiyo ya Wizara kwa kuibua kipaumbele hicho kwani nchi yetu bado haijazitumia na kunufaika ipasavyo na rasilimali zinazotokana na Uvuvi wa Bahari Kuu, usafiri na usafirishaji Baharini, utalii wa Baharini pamoja na rasilimali za mazao ya baharini hususan mwani ambapo kimaumbile kila kona ya nchi yetu imezungukwa na Bahari. Kwa mantiki hiyo, kama sekta ya Uchumi wa Buluu itafanyiwa kazi kikamilifu kama ilivyopendekezwa na Wizara itaweza kutuongezea mapato maradufu na kuimarisha uchumi pamoja na maisha ya wananchi wetu.

Mheshimiwa Spika,
Kamati yetu imepata malalamiko kutoka kwa wawekezaji kadhaa nchini kwamba baadhi ya fursa za uwekezaji walizopatiwa wengine kabla yao, zimeanza kusita kutolewa na taasisi husika ikiwemo msamaha wa kodi wa asilimia 20 kwa uingizaji wa rasilimali za awali (capital costs). Kamati yetu inashauri lizingatiwe kwa makini suala hilo ili tuweze kuwaengaenga na kuwavutia wawekezaji waweze kuja zaidi nchini kwetu.

Mheshimiwa Spika,
Kwa niaba ya Kamati ya Fedha, Biashara na Kilimo, namtakia mafanikio mema Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango katika utekelezaji wa bajeti yake ya mwaka 2020/2021 kwa Wizara hii na nawaomba Waheshimiwa Wajumbe waichangie, waulize, wahoji, wakosoe na hatimae waipitishe bajeti hii ili kumpa fursa Mheshimiwa Waziri kutekeleza kwa ufanisi yale yote aliyojipangia kwa mwaka ujao wa fedha.

Mheshimiwa Spika,
Kabla sijamaliza hotuba yangu, nitakuwa mwizi wa shukurani kama sitompongeza kwa mara nyengine tena Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein kwa fikra na muono wake wa mbali wa kuendeleza kivitendo azma ya Muasisi wa Mapinduzi yetu Marehemu Mzee Abeid Amani Karume kwa kufanya ujenzi mpya wa Mji wa kisasa katika eneo la Michenzani ambao ulianza mapema katika miaka ya 70.

Mheshimiwa Spika,
Sote ni mashahidi kwamba eneo la Michenzani hivi sasa limebadilika na tunategemea mabadiliko makubwa mara tu baada ya kumalizika ujenzi wa miradi ya maduka ya kisasa (shopping mall), maegesho ya magari pamoja na mradi wa maduka wa kisonge. Kutokana na muone wake Mheshimiwa Rais ambao unatekelezwa kivitendo na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (ZSSF), nimatumaini yetu makubwa tuombe uhai kuiona Michenzani mpya na ya kisasa. Maendeleo ya mfano ya aina hiyo yatatoa dira na sura mpya kwa mji wetu.

Mheshimiwa Spika,
Mwisho lakini sio mwisho kabisa, kwa niaba ya Kamati yangu ya Kudumu ya Fedha, Biashara na Kilimo pamoja na Makatibu wetu tunachukua fursa hii adhimu kuomba radhi kama kutakuwa na kusoro zozote za kiutendaji au vyenginevyo zimejitokeza kwa Waheshimiwa na watendaji wote ambao kwa mujibu wa Kanuni za Baraza la Wawakilishi (Toleo la 2016) Taasisi zao zinasimamiwa na Kamati yetu zilizomo katikai Wizara ya Fedha na Mipango, Wizara ya Biashara na Viwanda pamoja na Wizara ya kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi. Tunawaeleza kwamba hatukuwa na nia ya kuwakwaza isipokuwa michango na ushauri tuliyoitoa ililenga katika kuisimamia Serikali ili iweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo kwa lengo la kuwatumikia wananchi wetu kwa maendeleo na ustawi wa nchi yetu.

Mheshimiwa Spika,
Kwa kumalizia Hotuba yangu naomba kuchukua fursa hii kuwashukuru sana wananchi wa Jimbo la Dimani kwa kuendelea kuniamini nikiwa Mwakilishi waliyonichagua niingie ndani ya Baraza hili tukufu kuwawakilisha. Maagizo, maswali, hoja za kupatiwa ufafanuzi pamoja na maelekezo waliyokuwa wakinipatia, nimejitahidi kuyawasilisha kadiri ya uwezo wangu na mafanikio mengi tumeyapata katika sekta nyingi hususan elimu, afya, maji, umeme, maendeleo katika uvuvi na miundombinu ya barabara. Tunamshukuru sana Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi pamoja na Serikali kwa ujumla kwa ushirikiano waliotupa katika ustawi na maendeleo ya Wananchi wa jimbo la Dimani. Tumeahidiwa na tumeanza kuyaona mengi mazuri na makubwa yameanza kuonekana.
Mheshimiwa Spika,
Naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja na naomba kuwasilisha.

Ahsante sana,

Mhe. Dkt. Mwinyihaji Makame,
Mwenyekiti,
Kamati ya Kudumu ya Fedha, Biashara na Kilimo,
Baraza la Wawakilishi,
Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.