Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Alhajj Dk. Ali Mohamed Shein, akihutubia katika hafla ya Baraza la Eid Alhajj katika Ukumbi wa Mitihani Skuli ya Sekondari Bumbwini Wilaya ya Kaskazini "B" Unguja kwa mwaka huu limefanyika Kitaifa katika Wilaya hiyo.
BISMILLAH
RAHMAN RAHIM
Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan;
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi;
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar,
Mama Fatma Karume,
Mheshimiwa Shamsi Vuai Nahodha;
Waziri Kiongozi Mstaafu,
Mheshimiwa Khamis Juma Maalim;
Waziri wa Katiba na Sheria,
Mheshimiwa Sheikh Saleh Omar Kabi;
Mufti wa Zanzibar,
Mheshimiwa Zubeir Ali Maulid;
Spika wa Baraza la Wawakilishi,
Mheshimiwa Omar Othman Makungu;
Jaji Mkuu wa Zanzibar,
Sheikh Khamis Haji Khamis;
Kadhi Mkuu wa Zanzibar,
Waheshimiwa Mawaziri na Manaibu Mawaziri,
Mheshimiwa Hussein Ali Hassan Mwinyi;
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, ambaye pia, ni Mgombea Urais
wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),
Abdalla Juma Mabodi;
Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar,
Dkt. Abdulhamid Yahya Mzee;
Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu
Kiongozi,
Waheshimiwa Wabunge na Wajumbe wa Baraza la
Wawakilishi Wastaafu,
Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya,
Wheshimiwa Washauri wa Rais,
Masheikh wote mliohudhuria,
Makatibu Wakuu na Manaibu Makatibu Wakuu wa Wizara mbali mbali,
Waheshimiwa Mabalozi,
Viongozi mbali mbali wa Serikali,
Viongozi wa Vyama vya Siasa,
Wageni Waalikwa,
Ndugu Wananchi,
Mabibi na Mabwana.
Assalamu Aleikum Warahmatullahi Wabarakatuh
IDD MUBARAK
Namshukuru
Mwenyezi Mungu Mtukufu, Azza Wa Jalla, Mwenye Hekima, Ujuzi na Muweza wa kila
jambo, ambaye kwa kudra zake, ametujaaliya uhai na afya njema; ambayo ndio
yaliyotuwezesha kujumuika hapa leo, katika Baraza hili la Idd kwa kusherehekea
Sikukuu hii ya ya Idd el Hajj.
Tunamuomba Yeye amshushie Rehema na Amani Mtukufu wa daraja, Mtume wetu
Muhammad (S.A.W), Aali na Sahaba zake pamoja na waumini wote waliofuata mwendo
wake mwema. Allah, Subhanahu Wa Taala
atujaalie na sisi uwezo wa kuyafanya mambo ya kheri na atuepushe na shari na maovu, ili tufanikiwe hapa
duniani na kesho mbele ya haki.
Tunamshukuru
Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia uhai na afya njema na tukaweza kuishuhudia na
kuisherehekea sikukuu ya Idd el Hajj ya mwaka huu kwa furaha kubwa, kwani kuna
baadhi ya waumini wenzetu ambao tulishereheka nao katika Sikukuu kama hii mwaka
jana, lakini kwa mapenzi yake Allah, ameshawaita mbele ya haki. Tunamuomba
Allah, Subhanahu Wa Taala, awarehemu wote na awasamehe makosa yao wenzetu hao, sisi tulioko nyuma yao atupe khatima njema.
Ndugu Wananchi,
Sherehe hizi za
Idd el Hajj za mwaka huu, zimetufikia sisi Watanzania tukiwa bado tumo katika hali ya msiba mkubwa
wa kuondokewa na kiongozi wetu Mpendwa wa Kitaifa, Rais Mstaafu wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania wa Awamu ya Tatu, Marehemu Mheshimiwa Benjamin William
Mkapa, ambaye kifo chake kilichotokea usiku wa tarehe 23 Julai, 2020, kuamkia
Ijumaa iliyopita huko Dar es Salaam.
Wananchi wa Zanzibar tuliungana na Watanzania wenzetu katika wiki ya
maombolezo ya Kitaifa kama ilivyotangazwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli baada ya kutokea kifo hicho. Marehemu Rais Mstaaafu alizikwa nyumbani kwao
Lupaso, Masasi juzi tarehe 29 Julai, 2020 na maombolezo ya Kitaifa yamemalizika
jana.
Marehemu Mzee
Benjamin Mkapa ataendelea kukumbukwa nchini mwetu, Barani Afrika na duniani
kote, kwa uongozi wake uliojaa busara, hekima na upendo. Tutamkumbuka kwa tabia yake ya ucheshi na
uzalendo, ufanyaji kazi kwa bidii na nidhamu kubwa, ukweli na uwazi, sifa
ambazo zimeweza kuendeleza umoja na mshikamano wa Watanzania wote kwa kipindi
chote cha uongozi wake Serikalini, kwenye Chama cha Mapinduzi (CCM) na kwenye
nyadhifa mbali mbali alizoshika nje ya nchi yetu.
Hata wananchi
katika mataifa mbali mbali duniani walifaidika na busara na hekima zake pale
ambapo alishughulikia masuala muhimu ya upatanishi na usuluhishi wa mizozo,
migogoro na changamoto nyengine ilizokuwa zikitishia hali ya amani
ulimwenguni. Kutokana na thamani kubwa
aliyonayo Mheshimiwa Benjamin Mkapa kwetu sote Watanzania, tunamuomba Mwenyezi
Mungu amuweke mahali pema, na awape subira na ustahamilivu wafiwa na Watanzania
wote katika kipindi hiki kigumu. Ninakuombeni
tusimame kwa muda wa dakika moja, kwa ajili ya kumkumbuka kiongozi wetu huyu
mpendwa.
Ndugu Wananchi,
Natanguliza shukurani zangu za dhati kwa Mufti wa
Zanzibar na watendaji wa Ofisi yake, kwa
kushirikiana vizuri na Kamati ya Kitaifa
ya Sala na Baraza la Idd pamoja na Uongozi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja na Wilaya zake kwa
maandalizi mazuri ya shughuli hii. Nimefurahi kuona kwamba katika Baraza hili wamehudhuria viongozi na baadhi
ya wananchi wengine wakiwawakilisha wenzao kutoka kwenye Wilaya zote za Unguja
na Pemba. Ndugu zetu hao wamekuja kwa
ajili ya kuifanikisha hafla hii ya
Baraza la Idd el Hajj, ambalo litakuwa la mwisho katika uongozi wangu mwaka huu. Nimefurahi sana kwa mahudhurio haya makubwa
na maandalizi ya aina yake. Nakupongezeni sana. Vile vile, natoa shukurani zangu za dhati kwa wageni
waalikwa wote kwa kuhudhuria kwa wingi katika shughuli hii. Kadhalika, nawapongeza Makamanda na Viongozi wa
Vikosi vyetu vya Ulinzi na Usalama,
wapiganaji wote, Vyombo vya Habari na wananchi wote wanaotusikiliza
kupitia vyombo mbali mbali kwa kuwa pamoja nasi katika shughuli hii. Kwenu nyote nasema, ahsanteni sana.
Leo tupo hapa Bumbwini
katika Wilaya ya Kaskazini B,
Mkoa wa Kaskazini Unguja, kwa ajili ya shughuli hii muhimu ya Baraza la
Idd. Leo asubuhi, tulijumuika pamoja na wananchi
wa Mkoa huu katika Sala ya Idd- el- Hajj ambayo imesaliwa katika kiwanja cha Misuka,
kilichopo eneo la Mahonda, na sasa tuko hapa kwa ajili ya Baraza la Idd.
Tunaendelea na utekelezaji wa utaratibu maalum tulioupanga wa kusherehekea
Sikukuu ya Idd- el- Hajj katika kila Wilaya kwa ratiba maalum
iliyoandaliwa. Utaratibu huu ulitekelezwa
katika Wilaya zote kumi na mwaka huu tunaukamilisha katika Wilaya hii ya
Kaskazini “B”.
Utaratibu huu umeanzishwa, ili kutoa fursa kwa wananchi
katika maeneo mbali mbali waweze kuisherehekea siku hii muhimu pamoja na
viongozi wao. Hapana shaka kwamba utaratibu huu umeweza kuimarisha mapenzi miongoni mwetu na umeongeza imani ya umoja na
mshikamano wetu. Kwa hivyo, mafanikio
haya tuliyoyapta ni makubwa na tunayo kila sababu ya jambo hili zuri
tuliendeleze.
Ndugu Wananchi,
Leo ni siku ya furaha, Waislamu na wananchi wote wa
Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa jumla, tunaungana na Waislamu wenzetu
waliopo katika nchi mbali mbali kwa
ajili ya kuisherekea siku hii ya Idd el Hajj. Kama tunavyofahamu kwamba, ibada hii ambayo ni
nguzo ya tano ya Kiislamu, huwa inatekelezwa na maelfu ya mahujaji wa rangi,
wasifu na hadhi tafauti kutoka kwenye mataifa mbali mbali duniani, ambao wote
hukusanyika katika nyumba tukufu ya Al-Kaaba, huko Makka kwa lengo moja tu, la
kuitikia wito wa Mwenyezi Mungu Subahanahu Wa Taala.
Ibada hii ina uzito maalum katika Dini ya Kiislamu na
Mwenyezi Mungu, Subhaanahu Wa Taala ametueleza uzito huo katika sehemu ya
mwisho ya Aya ya 97 ya Surat Al-Imran, yenye tafsiri isemayo:
“….Na Mwenyezi Mungu,
amewawajibishia watu wafanye Hijja
katika Nyumba hiyo; yule awezaye kufunga safari kwenda huko. Na atakayekanusha
(asiende, na hali ya kuwa anaweza) basi Mwenyezi Mungu si muhitaji kwa kuwahitajia
walimwengu”.
Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwawezesha Waislamu
wenzetu walioko Saudi Arabia kuitikia wito wake wa kuitekeleza ibada hii
muhimu, kwa mwaka huu na leo tunaungana nao baada ya kuikamilisha. Tunamuomba
Mwenyezi Mungu Subhanahu Wataala azikubali Hijja zao na ibada zao zote
walizozifanya katika Mji Mtukufu wa Makka na Madina na sehemu mbali mbali kabla
na baada ya Hijja.
Ndugu Wananchi,
Sote tunafahamu kwamba, hapa Zanzibar na Tanzania nzima
kwa jumla, walikuwepo waumini wenzetu ambao mwaka huu walidhamiria kwenda
kuitekeleza ibada hii, kama ilivyo kawaida. Hata hivyo, kwa bahati mbaya,
safari ya kwenda huko kwa ajili ya kuitekeleza ibada hii haikuwezekana kutokana
na kuzuka kwa janga la maradhi ya COVID-19, yanayosababishwa na virusi vya
Korona. Maradhi ya COVID-19 yaliyoleta,
athari katika nchi nyingi duniani pamoja na Saudi Arabia.
Habari tunazoendelea kuzipata kutoka nchi nyengine kupitia
katika vyombo vya habari na kutoka kwa baadhi ya wanaosafiri, kwamba, hadi sasa
maradhi ya COVID-19, yanaendelea kuwepo katika mataifa mbali mbali. Kwa hivyo, kutokana
na kuwepo maradhi hayo, Serikali ya Saudi Arabia kupitia Wizara yake ya Hijja
na Umra, ndipo ilipoamua kuendelea kuchukua tahadhari, kwa kuwazuia mahujaji
kutoka nje ya nchi hio wasiingie nchini humo katika msimu huu wa ibada.
Naamini kwamba Umoja wa Taasisi zinazoshughulikia masuala
ya Hijja, kwa mashirikiano na Taasisi za Serikali zinazosimamia Hijja, hapa Zanzibar (UTAHIZA), na Taasisi
zote zinazosafirisha mahujaji zimeshaandaa utaratibu mzuri wa namna ya
kuwahudumia wale mahujaji ambao wamekosa kwenda Hijja mwaka huu.
Ndugu Wananchi,
Natoa shukurani zangu za
dhati kwa wananchi wote wa Zanzibar na Tanzania nzima kwa jumla kwa
kuendelea kushirikiana na Serikali zetu zote mbili, Serikali ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika mapambano dhidi ya Maradhi ya COVID
19. Natoa pongezi kwa Kamati mbali mbali zilizoundwa katika ngazi ya Taifa,
Mikoa, Wilaya na maeneo mengine yote, kwa ajili ya kupambana na maradhi haya.
Umoja na mashirikiano tuliyoonesha na tuliyonayo katika kutii sheria, kufuata
miongozo ya madaktari na wataalamu wa afya pamoja na viongozi, vimetuwezesha
kupata mafanikio katika kuyadhibiti maradhi haya.
Ujasiri wetu wa
kuondosha hofu zisizo na msingi juu ya maradhi haya, uzalendo wetu
na kutokana na dua tunazoziomba tumeweza
kupata mafanikio makubwa tunayoyashuhudia katika kupambana na maradhi haya.
Mwenyezi Mungu amezipokea dua zetu. Sote tumefurahi kwa taarifa tulizopewa
kwamba hadi kufikia tarehe 10 Juni, 2020, vituo vyetu vyote vilivyofunguliwa
maalum kwa wagonjwa wa maradhi haya havikuwa na mgonjwa hata mmoja hadi hivi
leo. Kutokana na matokeo hayo, Serikali ililazimika iregeze masharti
tuliyoyaweka dhidi ya COVID- 19, hatua kwa hatua na hivi sasa hali yetu imekuwa
bora zaidi, na ndipo Serikali ikaamua kuziruhusu huduma zote zinazohitajika
katika maisha ya kawaida ziendelee; huku sote tunatakiwa tuendelee kuchukua
tahadhari za kujikinga.
Tunapaswa tujifunze kutokana na athari na madhara tuliyoyapata
wakati maradhi haya yalipoingia nchini na hatua madhubuti tulizozichukua. Tulilazimika
tujinyime na tuyakose mambo muhimu tunayoyahitaji katika maisha yetu ya siku
zote. Lakini tulifanya hivyo, ili
kuyanusuru maisha yetu kwa kujikinga na COVID-19. Tuliendelea kumuomba Mwenyezi Mungu wakati
wote, ili atuondoshee maradhi haya na atuzidishie afya njema, baraka na
atujaalie kila la kheri hapa duniani na kesho akhera.
Kwa hivyo, tutaendelea kuomba dua kwa wingi na tutashikamana
na subira kila tunapokutana na mitihani ya maisha, kama Mwenyezi Mungu
alivyotuelekeza katika Aya ya 153 ya Surat Al Baqarah yenye tafsiri isemayo:
“Enyi
mlioamini! (Jisaidieni katika mambo
yenu) kwa subira na sala, bila ya shaka Mwenyezi Mungu yu pamoja na wanaosubiri”.
Taarifa za maradhi ya COVID 19 bado zinaendelea kutolewa
kila siku katika vyombo vya habari. Bila ya shaka, kuna mambo mengi ya
kujifunza kutokana na taarifa hizo, na
tuendelee kuchukua tahadhari kwa kuzingatia elimu ya kinga tuliyoipata, lakini tusisitishe
shughuli za ujenzi wa Taifa na nyengine muhimu ikiwemo za kutafuta riziki kwa
ajili ya familia zetu. Vile vile, tushikamane na mafundisho ya Kuran Tukufu,
ili tuweze kumtanguliza Mwenyezi Mungu kwa kila jambo letu na kuondoa khofu,
kwani Mola wetu Mtukufu, anatukataza kutanguliza khofu kwa mambo tunayotaka kuyafanya, kama
alivyotufahamisha hivyo katika Aya ya 51
ya Surat Tawba yenye tafsiri isemayo:
“Halitatusibu, ila alilotuandikia Mwenyezi
Mungu. Yeye ni Mola wetu”
Ndugu Wananchi,
Uislamu unatufundisha kuwa kwa kila ibada tunayoifanya,
tuzingatie mafundisho yake na tujitahidi kuyatekeleza katika maisha yetu ya
kila siku. Miongoni mwa mafunzo makubwa
yanayopatikana katika utekelezaji wa ibada ya Hijja, ni utii wa sheria pamoja
na kuimarisha umoja na mshikamano katika hali ya amani na utulivu. Ni vyema
sote tuuone umuhimu wa kufungamana na mambo haya katika kuiletea nchi yetu
maendeleo, kwani mambo haya ndio msingi mkubwa wa mafanikio.
Sikukuu hii inaambatana na kisa cha Nabii Ibrahim (AS)
kilichoelezwa katika Kuran Tukufu, pale
alipooteshwa usingizini na Mola wake Muumba kuwa anamchinja mwanawe wa
pekee, ambaye ni Ismail (AS). Kwa vile, ndoto za Mitume zilikuwa ni maamrisho
kutoka kwa Allah, Nabii Ibrahim (AS) ilimlazimu ayatekeleze maamrisho hayo, na
akamjuilisha mwanawe kuhusu utekelezaji wa amri ile. Naye Ismail (AS),
aliridhia bila ya usumbufu. Haya yanathibitika katika Aya ya 102 ya Surat
Saaffaat yenye tafsiri isemayo:
“Basi alipofika makamo ya kwenda na kurudi pamoja naye, alimwambia: “Ee mwanangu! Hakika
nimeona katika ndoto ya kwamba ninakuchinja. Basi fikiri waonaje? ”Akasema: “Ee
baba yangu! Fanya unayoamrishwa,
utanikuta Insha Allah miongoni mwa wanaosubiri”.
Ndugu Wananchi,
Kuanzia Aya hii ya 102 mpaka Aya ya 110 ya Surat Saaffaat,
Mwenyezi Mungu Mtukufu anatuelezea tukio hili la Nabii Ibrahim (AS) na mwanawe
Ismail, ambapo anatuonesha jinsi alivyowapa waja wake hao mtihani huo mzito,
ili kuwapima imani yao juu Yake; na alipohakikisha kwamba wao walikuwa ni watu
wenye imani thabiti Kwake, aliigeuza amri hio na alimpa Nabii Ibrahim mnyama
amchinje, badala ya kumchinja mwanawe Ismail.
Mwenyezi Mungu Mtukufu anatufundisha kwamba kipimo cha
imani na utu wa mtu ni miongoni mwa mambo muhimu katika uongozi. Kadhalika,
anatufundisha umuhimu wa kutii sheria, pamoja na kushirikiana na kushauriana
katika kupitisha maamuzi mazito. Vile vile, tunajifunza utii wa mtoto kwa mzazi
wake na umuhimu wa kiongozi kuwa muadilifu.
Ni wajibu wetu viongozi na wazazi tuzitii na tuzifuate sheria
pamoja na kuwashirikisha
tunaowaongoza katika mambo muhimu ya
maisha yanayotuhusu sote moja kwa moja. Bila ya shaka, kuna fadhila kubwa
kutoka kwa Mola wetu kwa kuzitii amri zake na hutupa yale mambo yaliyo mepesi,
tunapokua na imani ya kweli ya kufuata maamrisho yake.
Jambo jengine, kubwa tunalojifunza katika ibada ya Hijja
ni usawa wa binaadamu mbele ya sheria na mbele
ya Mwenyezi Mungu. Waislamu wa
makabila mbali mbali na wenye vyeo na
uwezo wa fedha na mali uliotofautiana,
hukusanyika pamoja wakiongozwa na sheria zisitofautisha vyeo, hadhi na mali zao katika kukamilisha
ibada ya Hijja. Kwa hivyo, katika ibada hii ya Hijja tunajifunza mengi kuhusu usawa mbele ya sheria na umuhimu
wake katika kutekeleza na kufanikisha mambo mbali mbali katika maisha ya mwanaadamu.
Ndugu Wananchi,
Hivi sasa tunaelekea
kwenye Uchaguzi Mkuu utakaofanyika katika mwezi wa Oktoba mwaka huu, kwa hivyo,
tunapaswa tukumbuke wakati wote kwamba
msingi wa mafanikio yote tuliyoyapata katika awamu zote ni juhudi zetu za
pamoja katika kufanya kazi, kuilinda hali ya amani na utulivu; pamoja na
kudumisha umoja na mshikamano. Kwa
hivyo, tuendelee kushirikiana, ili tuhakikishe kwamba, Uchaguzi Mkuu utakaofanyika katika mwezi Oktoba mwaka huu unafanyika
kwa amani na utulivu, ili Serikali ya
Awamu ya Nane itakapoingia madarakani, iweze kuyashughulikia maendeleo ya nchi
yetu kwa ufanisi zaidi. Lazima
tuhakikishe kwamba hatokei mtu, au kundi lolote likajaribu kuharibu amani ya
nchi yetu, kupandikiza chuki, uhasama na fitina miongoni mwetu na ndani ya
jamii yetu. Nawanasihi viongozi wa vyama vyote vya siasa na wagombea wao,
wakati ukifika, wajinadi kwa wapiga kura
kwa kutangaza Ilani, sera na mipango ya vyama vyao. Ni lazima wahubiri amani, umoja na mshikamano
kwa maneno na vitendo, wakijuwa kwamba,
lengo lao ni kujinadi, ili wachaguliwe kwa ajili ya kuiletea maendeleo nchi
yetu na kutoa huduma bora kwa wananchi. Ni wajibu wetu tuzingatie, tuziheshimu
na tuzitii sheria na miongozo ya Uchaguzi inayotolewa na Tume zetu mbili za
Uchaguzi (ZEC na NEC).
Ni jukumu letu tushikamane
kwa kuishi kwa mapenzi baina yetu na tufanyekazi kwa pamoja. Suala la kudumisha umoja ndani ya jamii,
ikiwa ni msingi wa mafanikio limehimizwa
sana katika Uislamu. Mwenyezi Mungu Mtukufu anatwambia katika Quran Tukufu,
sehemu ya Aya ya 103 ya Surat Aali- Imran kwa tafsiri isemayo:
“Na shikamaneni kwa kamba (dini) ya Mwenyezi Mungu nyote,
wala msifarikiane”.
Ili tuweze
kuudumisha na kuuendeleza umoja ni lazima tujiepushe na tabia mbaya kama
kudharauliana, kusengenyana, kuhusudiana, kuhasimiana na kushawishiana katika
kufanya hujuma dhidi ya wananchi wenzetu na Serikali yetu, na badala yake
tuhimizane katika kufanya mambo mema.
Vile vile, Allah, Subhanahu Wa Taala, anatuhimiza tuishi kwa kupendana
na kusaidiana katika Quran Tukufu,
sehemu ya mwisho ya Aya ya 2 ya Surat Al- Maidah, kwa tafsiri isemayo:
“…Na saidianeni katika wema na taqwa, wala msisaidiane
katika dhambi na uadui….”
Nawapongeza
wananchi wote kwa kuendelea kuishi pamoja, na huku tunajiandaa kuzikaribisha
shughuli za uchaguzi katika hali ya utulivu, umoja na maelewano mazuri. Hadi
sasa, nchi yetu iko shwari, harakati za
kisiasa, kiuchumi na kijamii zinaendelea vizuri. Ni mategemeo yangu kwamba
hali hii itadumu hadi siku ya
uchaguzi na baada ya uchaguzi. Tukifanya
hivyo, tutatoa fursa nzuri kwa Serikali
ya Mapanduzi ya Zanzibar ya Awamu ya
Nane ya kuanza utekelezaji wa mipango yake ya maendeleo kwa wepesi, hamasa
zaidi na ari kubwa, ili hatimae iweze kupata mafanikio makubwa zaidi. Hii ndio dhamira
na matakwa ya watu wa Zanzibar.
Wazanzibari wanataka maendeleo na kamwe hawataki fujo wala watu
wagombane.
Ndugu Wananchi,
Ni dhahiri kwamba,
licha ya mafanikio tuliyoyapata katika kipindi cha miaka kumi, iliyopita,
lakini bado tunahitaji kuongeza kasi ya kuzifanyia kazi changamoto tunazoendelea kukabiliana nazo,
ambazo baadhi yake, zinaonekana huenda zikahatarisha hali ya amani. Kwa mfano, bado hatujafanikiwa kulitatua
tatizo la vitendo vya ukatili na udhalilishaji dhidi ya wanawake na watoto. Ingawa
tulizindua Mpango Kazi wa Zanzibar wa
Miaka Mitano wa Kupambana na Vitendo vya Ukatili na Udhalilishaji dhidi ya
Wanawake na Watoto hapo Agosti, 2017 na utekelezaji wake utaendelea hadi mwaka
2022. Kadhalika, tulikuwa nao mpango
uliofanana nao kabla ya hapo, lakini, bado tatizo la udhalilishaji wa watoto na
kijinsia linaendelea kujitokeza katika sehemu mbali mbali za Unguja na Pemba.
Tunaendelea kusikia matukio ya unyanyasaji na udhalilishaji katika vipindi vya mawio vya ZBC Redio. Vile
vile, matukio kama hayo yanaripotiwa
mara kwa mara katika vituo vya polisi. Kadhalika, wamejitokeza vijana
wanaowasumbua wananchi, hasa wanawake kwa kuwavamia, kuwapiga na kuwanyang’anya
vitu vyao.
Kadhalika, zipo taarifa za kuongezeka kwa vitendo vya
wizi wa mifugo na mazao pamoja na
uchimbaji ovyo wa mchanga katika maeneo yasiyoruhusiwa. Kwa hakika wananchi wamechoshwa na vitendo
hivi na vyenginevyo na inaonekana kama wanaanza kukata tamaa. Kwa hivyo, ni jukumu la vyombo vya ulinzi na
usalama kwa kushirikiana na jamii, vikundi vya ulinzi shirikishi, tuwachukulie
hatua za kisheria vijana hao na watu wengine wanaotenda uovu huo, ili tuhakikishe
kwamba vitendo hivyo tunavikomesha na
wananchi wanaendelea kuishi kwa amani. Tumesema
sana kwa muda mrefu sana ni lazima kazi hii ifanywe na iwe endelevu. Watu wanasikitika kwenye jamii yetu na
wengine wanadiriki hata kuilamu Serikali kuhusu vitendo hivi. Tutekelezeni wajibu wetu, kwani huruma hailei
mwana. Sote tuwe tayari, kujitokeza mahakamani kila inapohitajika kwa ajili ya
kutoa ushahidi kwa wale watakaoshuhudia vitendo vibaya vikitendwa ndani ya jamii yetu.
Malezi bora ndio
msingi wa kumuandaa mtoto na maisha ya baadae. Tuendelee kushirikiana katika
kuwasomesha na kuwapa malezi bora watoto wetu. Tuhakikishe wanatumia vizuri
fursa za elimu zilizoandaliwa na Serikali yao kwa ajili yao. Wazazi na
walezi tufanye juhudi za makusudi katika kuwasomesha watoto wote, hasa wale
wanaojiandaa na mitihani mwaka huu, tukizingatia kwamba mfumo na mtiririko wa
masomo yao umeathiriwa kutokana na
kufungwa skuli na madrasa kwa kipindi kirefu
kwasababu ya maradhi ya COVID 19.
Wazee wanatuhimiza kwamba “Udongo
upate ulimaji na Kambare Mkunje angali mbichi”.
Ndugu Wananchi,
Utaratibu huu wa kusali sala ya Idd na
shughuli za Baraza la Idd unanipa fursa nyengine ya kuyaona maendeleo na
kuzifahamu changamoto za ndani zinazojitokeza katika Wilaya zetu na Mikoa yetu. Nimefurahi kupata fursa ya kuona ukumbi huu
mpya na wa kisasa uliojengwa ndani ya Wilaya hii. Natoa pongezi kwa viongozi
na wananchi wa Jimbo la Bumbwini kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya
Kaskazini “B” pamoja na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kwa ujenzi wa ukumbi huu mzuri na wa kisasa wenye
nafasi na uwezo wa kukidhi mahitaji ya shughuli mbali mbali za kiserikali
na kijamii. Haya ndio maendeleo
tunayoyataka. Hongereni sana.
Nimepata habari kwamba, Wazee wa Bumbwini,
mmeunda Kamati maalum iliyojumuisha vijana kwa ajili ya kufuatilia kero na
changamoto zinazoendelea kujitokeza katika Jimbo hili na hata katika ngazi ya
Wilaya. Ninafahamu kwamba, Kamati mliyoiunda
inaendelea kushirikiana vizuri na
uongozi wa Wilaya na Mkoa katika kutafuta uwezekano wa kujenga skuli mpya ya Sekondari ya Bumbwini katika
eneo la Bumbwini Gongoni, kwenye kijiji
kipya, kwa ajili ya kutatua changamoto ya msongamano wa wanafunzi uliopo katika
Skuli ya Bumbwini, Sekondari na Msingi.
Naziunga mkono jitihada hizi na nakupongezeni kwa juhudi zenu hizo.
Nauagiza Uongozi wa Wizara ya Elimu, ushirikiane na uongozi wa Wilaya ya Kaskazini “B” na Mkoa huu wa
Kaskazini kwa ajili ya kulikagua eneo
hilo, na baadae iwasilishwe taarifa itakayotoa mapendekezo na mpango wa kuufanikisha
ujenzi wa skuli hiyo. Napenda nikumbushe kwamba, dhamira ya Serikali
hivi sasa ni kujenga Skuli za ghorofa, ili tuwe na matumizi bora ya ardhi. Ni
vyema suala hili nalo likazingatiwa katika ujenzi wa skuli hio. Ni kweli skuli
mpya katika eneo jipya inahitajika, tukiangalia nje tunaona jinsi, msikiti
na makazi ya watu yalivyokaribiana na majengo ya skuli.
Kadhalika, nimesikia kilio cha wananchi wa
Wilaya ya Kaskazini “B” cha kutaka kuwa na Hospitali yenu ya Wilaya kama ilivyo
katika Wilaya nyengine hivi sasa. Huu ni wivu ambao wengi tunaupenda yaani wivu
wa maendeleo, ambao wananchi sote tunapaswa tuwe nao. Ni dhamira ya Serikali ya
kuwa na Hospitali za Wilaya, Skuli za Wilaya, Viwanja vya Michezo vya Wilaya na
mambo mengine. Haya ni masuala muhimu katika utekelezaji wa Mpango wa Ugatuzi
na kwa maendeleo yetu ya baadae.
Nina taarifa kwamba, tayari mmeanza
kulifikiria eneo kubwa la wazi lilioko
karibu na Skuli ya Pangatupu kwa ajili
ya ujenzi wa Hospitali hio. Kwa hivyo, uongozi wa Mkoa wenu na
Halmashauri ya Wilaya ya Kaskazini “B” uanze mazungumzo na Wizara ya Afya na
Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za
Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ, kuhusu ujenzi wa Hosptali hio
katika eneo la Pangatupu mnalillofikiria. Ikithibitika kwamba eneo hilo linafaa
kwa kuzingatia mipango miji na vijiji iliyopo na maendeleo ya muda mrefu ya
Mkoa huu, basi nauagiza uongozi wa Mkoa uanze mradi huo japo kwa kujenga jengo moja dogo kama ni kielelezo cha
utekelezaji wa dhamira hio, na muweze kupata ardhi itakayohitajika kwa kazi
hio. Mkifanya hivyo, bila ya shaka, Serikali ya Awamu ya Nane, itaweza kuuandaa
mpango huu katika mipango yake baadae.
Maendeleo ya Taifa lolote hupatikana kwa
utaratibu wa hatua kwa hatua. Ndiyo maana,
kumekuwa na usemi maarufu wa
Warumi uliotafsiriwa kwa Kiingereza, usemao “Rome wasn't built in a day”, kwa maana ya kwamba “Jiji la Roma (nchini Italia) halikujengwa kwa siku
moja. Nakuhakikishieni kwamba suala hili mkiliendeleza na kulifanyia kazi kwa
moyo mmoja, basi Wilaya ya Kaskazini “B” itakuwa na hospiali ya Wilaya baada ya
miaka michache ijayo. Ninakuhimizeni mlifanyie
kazi wazo hilo, nami naliunga mkono kwa moyo wangu wote. Serikali inawaunga mkono, jiandaeni na jipangeni.
Mambo mbali mbali ya maendeleo yamefanyika katika Mkoa
huu kwenye kipindi cha miaka kumi ya uongozi wangu. Hata hivyo, ninaamini kwamba bado yapo mambo
kadhaa yanayopaswa yatekelezwe. Lakini ninamaliza
muda wangu wa uongozi, nikiwa nimeridhika sana
na mafanikio makubwa tuliyoyapata katika kuimarisha miundombinu mbali
mbali katika Mkoa huu, na Mikoa mengine ya Unguja na Pemba. Nadhani, sitokosea nikisema kwamba Mkoa huu
wa Kaskazini Unguja hivi sasa unaongoza hapa Zanzibar kwa
kuwa na barabara mpya, nzuri na za kisasa. Haya ni matunda ya juhudi
zetu za pamoja. Natoa pongezi zangu za
dhati, kwa wananchi waliokubali bila ya masharti kuondosha vitu na mali zao kwa
ajili ya kupisha miradi ya ujenzi wa barabara tuliyoitekeleza katika Mikoa yote
ya Unguja na Pemba.
Tuhakikishe kwamba tunazitumia barabara zetu kwa kuongeza
kasi ya maendeleo. Barabara hizi, ziwe ni neema kwa wakulima, wafugaji, wavuvi, wafanyabiashara,
wafanyakazi, wanafunzi, watalii, wawekezaji na wananchi wote kwa jumla.
Kwa upande mwengine, nafahamu kwamba, siwezi
kuja Bumbwini na niondoke bila ya kukumbushiwa juu ya mpango wa Serikali wa
kuimaliza barabara ya Makoba-Kiongwe pamoja na ujenzi wa Barabara ya Bumbwini
Mahonda. Nataka nikuhakikishieni
kwamba hizi ni ahadi za Serikali na kwa vyo vyote vile tutazitekeleza. Barabara
hii ya Bumbwini-Mahonda ni muhimu katika kutekeleza dhamira yenu ya ujenzi wa
hopitali ya Wilaya, kuendeleza ujenzi wa
bandari ya mafuta na gesi ya Mangapwani, pamoja na kuliunganisha eneo la
Pangatupu na Zingwezingwe na maeneo
mengine ya Wilaya hii.
Nimepata taarifa juu changamoto zilizopo kwa Wananchi wa
Wilaya hii baada ya kuporomoka kwa daraja la Mperura linalounganisha eneo la Bumbiwini Misufini na Pangatupu. Serikali
inaandaa mipango ya kulifanyia
matengenezo daraja lenu hilo, na panapomajaliwa, baada ya kipindi kifupi
kijacho daraja hilo litatengenezwa na litaweza kupitika vizuri.
Ndugu Wananchi,
Miongoni mwa miji
ya Zanzibar inayoendelea kukuwa kwa kasi hivi sasa ni Mji wa Nungwi ambao upo
kwenye Mkoa huu wa Kaskazini. Mji huu umebahatika kuwa na mazingira mazuri,
fukwe za kupendeza na kama walivyo watu wa Zanzibar, wakaazi wake ni wakarimu.
Kwa jumla Visiwa vyetu vya Unguja na
Pemba vinasifika kwa kuwa na mazingira
mazuri na fukwe za kuvutia. Sijui kama wananchi wengi wa Zanzibar, wanajua
kwamba, mitandao mingi inayotangaza utalii inausifu na kuutangaza ufukwe wa
Nungwi kuwa ni miongoni mwa fukwe 20 bora duniani. Kwa hivyo, tunakazi kubwa ya
kuuendeleza mji wa Nungwi hivi sasa. Tujifunze kutokana na shida tunazozipata
hivi sasa katika utoaji wa huduma katika
maeneo tuliyojenga bila ya kuzingatia mipango miji. Tusijikwae hapo hapo kila
mara.
Kwa kutambua umuhimu wa Mji huu wa Nungwi, Serikali
imeamua kujenga Kiwanja cha Ndege
kidogo, katika eneo la Kigunda karibu na mji wa Nungwi, kiwanja hicho hivi sasa
kimeshafikia hatua nzuri. Katika
Shamshara za Maadhimisho ya Sherehe za Mapinduzi Matukufu, tarehe 10
Januari, 2020 kiwanja hiki kiliwekewa
jiwe la msingi na Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Mheshimiwa Mgeni Hassan
Juma. Hivi sasa kinatumika kwa safari za
ndege ndogo ndogo za utalii na hapo baadae kitatiwa lami na kitakuwa cha kisasa.
Imani yangu ni kwamba kitakapomalizika kiwanja hicho
kitazidi kufungua milango ya maendeleo na kuharakisha kasi ya ukuaji Mji wa Matemwe.
Kwa hivyo, kwa mara
nyengine, nawahimiza viongozi wa Mikoa na
Wilaya zote za Unguja na Pemba mhakikishe kwamba Miji yote mipya
tunayoijenga, inaendelezwa kwa kuzingatia utekelezaji wa mipango miji. Migogoro ya ardhi iliyopo na
itakayojitokeza itatueni kwa kuzingatia sheria na kanuni za Serikali ziliopo.
Ndugu Wananchi,
Sote tunafahamu kwamba baada ya kufanyika Uchaguzi Mkuu
wa mwaka huu wa 2020, na kupatikana Rais mwengine wa Zanzibar, kwa mujibu
wa Katiba ya Zanzibar ya 1984, ndio
itakuwa mwisho wa uongozi wangu sitoongeza hata dakika moja seuze sekunde moja.
Kwa hivyo, hapana shaka kwamba, shughuli hii ya Baraza hili la Idd el Hajj tunayoifanya leo, Mwenyezi Mungu akipenda itakuwa ni ya mwisho
kwangu kuhudhuria na kutoa hutoba nikiwa
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi. Nikialikwa kama mgeni mwalikwa nitahudhuria
na nina uhakika nitaalikwaKwa hivyo, natoa shukurani zangu za dhati kwa wananchi wote wa Zanzibar
na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jumla, kwa mapenzi makubwa
mliyoonesha kwangu na kwa kuiunga mkono
Serikali yetu katika kuyatekeleza majukumu yetu kwa vipindi vyote viwili vya
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba. Kwa furaha kubwa ninawashukuru
wananchi wote kwa kuendelea kuniunga mkono wakati wote, katika utekelezaji wa
mipango yetu mbali mbali na kudumisha amani, mshikamano na upendo miongoni mwa wananchi
wa Zanzibar.
Kwa pamoja, tumeweza kuyapanga na kuyatekeleza mambo
mengi mazuri na makubwa kwa maendeleo ya nchi yetu. Tumeshirikiana kwa dhati
kwa hali ya juu katika kuzitafutia ufumbuzi changamoto mbali mbali zilizokuwa
zikijitokeza. Ni hivi karibuni tu nilipokuwa nikilihutubia Baraza la Tisa la
Wawakilishi la Zanzibar, tarehe 20 Juni, 2020, nilielezea kwa kina mafanikio tuliyoyapata na changamoto
zilizojitokeza katika kuijenga nchi yetu.
Ndugu
Wananchi,
Namalizia hotuba yangu, kwa kutoa shukurani zangu za
dhati na naipongeza sana Kamati ya Kitaifa ya Sala na Baraza la Idd kwa
kushirikiana vyema na uongozi wa Mkoa, Wilaya na wananchi wote kwa ajili
ya kuzifanikisha sherehe hizi. Natoa
shukurani zangu za dhati kwa wananchi wa Mkoa wa Kaskazini, ambao ndiyo wenyeji
wetu katika sikukuu hii kwa mwaka huu wa
2020. Mashirikiano mazuri ya wananchi wa Mkoa huu ni kielelezo cha umoja,
mshikamano na mapenzi kwa Serikali yenu, pamoja na uzalendo wa nchi yenu.
Hongereni sana.
Vile vile, natoa shukurani kwa Vyombo vya Habari ambavyo
vimewawezesha wananchi kuyafuatilia matangazo ya Baraza hili la Idd katika
maeneo yao. Nawashukuru na nawapongeza Makamanda, Viongozi na wapiganaji wa Vikosi
vya Ulinzi na Usalama kwa uwajibikaji wao kwenye shughuli yetu hii adhimu na
nyenginezo. Kadhalika,
nakupongezeni na nakutakieni wananchi nyote kheri na baraka katika
kuisherehekea sikukuu hii ya Idd el Hajj. Namuomba Allah Subhaanahu Wa Taala
aturejeshe nyumbani sote kwa salama na furaha.
Asanteni sana.
WAKULLU AAMUN WA ANTUM BIKHEIR.
No comments:
Post a Comment