Habari za Punde

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Mhe. Samia Suluhu Aendelea na Ziara Yake ya Kichama Wilaya ya Mjini Unguja.


MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) Taifa ambaye pia ni Makamu wa Rais wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan,amesema ushindi wa CCM katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu ndio njia pekee ya kulinda Muungano na Mapinduzi ya Zanzibar ya Mwaka 1964.

Amesema kila mwana CCM anatakiwa kulinda tunu hizo zilizoasisiwa na aliyekuwa Rais wa kwanza wa Zanzibar marehemu Abeid Amani Karume na Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hayati Mwl.Julius Kambarage Nyerere.

Hayo aliyaeleza wakati akizungumza na Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Mjini huko katika ukumbi wa Mikutano wa Mkoa huo uliopo Amani Unguja.

Akihitimisha ziara hiyo ya kichama ya siku tatu katika mikoa minne ya CCM iliyopo Unguja, mhe.Samia aliwambia viongozi hao kuwa suala la ushindi wa CCM linatakiwa kupewa kipaumbele.

Katika maelezo yake Samia,aliwataka wajumbe hao kuwa makini katika kupitisha wagombea na kwamba wanapaswa kuzingatia kanuni za uteuzi wa wagombea uongozi katika vyombo vya dola, uongozi na maadili.

Amesema Kamati za siasa zinawapitisha wagombea na kwamba baadaye wanapokuja katika nafasi za uongozi na kutowajibika wanalalamika kwa kudai kuwa hawaonekani majimboni na hawawajibiki.

"Mkishawapitisha hao wagombea ambao wanatumia fedha mnaanza kulalamika tangu aingie amelitupa jimbo ndio kaja mara hii lakini hawa watu mnawapitisha wenyewe na sisi huku juu mmetuletea na alama nzuri tunasema hawa ndio wanaoaminika kwenye kamati zao warudisheni,"alisema

Makamu wa Rais aliwataka wajipange vizuri katika kupitisha wagombea hao kuhakikisha wanafuata miongozo ya kanuni za uteuzi wa wagombea uongozi katika vyombo vya dola na katiba ya chama katika kuwapata wagombea.

Alisema kwa kuzingatia miongozo hiyo itasaidia kuwapata wagombea wenye sifa za kuwatumikia wananchi na kwamba kufuata misingi hiyo ni vigumu sana kuwapata wagombea ambao wanaotumia rushwa ndani ya chama.

" Huu ndio muda wa kuzisoma kwa kina kanuni hizo ili mzijue na ikifika muda muweze kufanya maamuzi sahihi yatakayosaidia vikao vya juu kutoa kurejesha watu wenye sifa zinazoendana na matakwa ya wananchi", alisema

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mjini Unguja,Talib Ali Talib alisema umejipanga kuhakikisha wanashinda na majimbo yote yanakwenda CCM.  

Alisema uongozi wa mkoa huo umejipanga na makundi mbalimbali ya jumuiya za chama ili kujipanga yema kwa jailli ya uchaguzi mkuu kwa lengo la kuipatia ushindi wa kishindo CCM.

Naye Katibu wa CCM Mkoa huo Abdallah Mwinyi akisoma taarifa ya kazi za Chama na jumuiya,alieleza kuwa wanashirikiana vizuri na jumuiya zote za chama katika masuala mbali mbali ya kiutendaji.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.