Habari za Punde

Ofisa wa PBZ na wenzake wahukumiwa kulipa fidia ya mamilioni kwa kukiri makosa ya Uhujumu uchumi




Ofisa wa Benki ya Zanzibar (PBZ), Maganga Fungameza na wenzake watano wamehukumumiwa kulipa fidia ya Sh milioni 62,852,000 kufuatia kuingia makubaliano na Mkurugenzi wa Mashitaka nchini DPP ya kukiri makosa ya uhujumu uchumi yaliyokuwa yakiwakabili.

Pia Mahakama ya Hakimu mkazi Kisutu imewataka washtakiwa hao kulipa faini ya Sh milioni moja kila mmoja au kutumikia kifungo cha miaka saba jela.

Mbali na Fungameza washitakiwa wengine ni Kassim Ifyuka, Lancy Chamdio, James Ndila, Amos Mollel na
Ayub Shukia wote wafanyabishara.

Akisoma hukumu hiyo leo Julai 27, 2020 Hakimu Mkazi Mwandamizi, Vicky Mwaikambo amesema tayari washitakiwa wameshalipa Sh. Milioni 45 na kwamba kiasi cha  Sh. Milioni 17. watatakiwa kulipa ndani ya miezi mitatu kama ilivyo kwenye makubaliano.

Mapema, kabla ya kutolewa kwa adhabu hiyo, Wakili wa Serikali Mwandamizi,  Ladislaus Komanya alidai washitakiwa walikuwa wanakabiliwa na mashitaka matatu katika kesi ya uhujumu uchumi namba 23/2020 ambayo ni kula njama, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na utakatishaji fedha

Alidai washitakiwa wamefanya makubaliano na wakafutiwa mashitaka ya kula njama na utakatishaji fedha waliyokuwa wakikabiliwa nayo awali na kubakiwa na  mashtaka mawili.

Aidha, wakili Komanya aliiomba mahakama kutoa adhabu kwa washitakiwa kulingana na makubaliano walipoingia na DPP.

Kwa upande wake, wakili wa washitakiwa, Nashon Nkungu aliomba mahakama kuwapa adhabu ndogo washitakiwa kwa sababu wanafamilia zinazowategemea.

Akiwasomea mashitaka mapya, Komanya amedai washtakiwa kwa pamoja na wenzao ambao hawajafikishwa mahakamani wanadaiwa kutenda kosa la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kati ya Desemba 10,2019 na Februari 15,2020 katika maeneo mbalimbali ya Tanzania ambayo ni Forodhani na Malindi (Zanzibar) na  Dar es Salaam.

Amedai, suki hiyo, kìwa makusudi na kwa nia ya kufanya udanganyifu washitakiwa walijipatia Sh  62,852,000 kutoka katika akaunti inayomilikiwa na Pofu Mcha Mtao katika benki ya PBZ kwa kudanganya kwamba fedha hizo ni manunuzi ya kiwanja jambo ambalo si kweli.

Inadaiwa washtakiwa na wenzao katika kipindi hicho katika eneo la Tabata Dar es Salaam na Malindi Zanzibar walifanya vikao kujipatia fedha hizo.

Amedai mshtakiwa Maganga alikuwa mtumishi wa benki na ndiye alitoa taarifa za mteja kwa wenzake na ndiye alihamisha fedha za mteja kwenda kwenye akaunti nyingine ya CRDB akijaribu kuonyesha kuwa akaunti hiyo imefunguliwa kwa ajili ya ununuzi wa kiwanja pia alikiri kuhusika na uhalifu wakati akihojiwa.

Pia mshtakiwa Maganga anadaiwa alipata Sh milioni 10 kama sehemu ya mgao waliokubaliana na kwamba mshitakiwa wa kwanza na wa pili  alihusika kuandaa uhalifu wa kujipatia fedha hizo lakini pia alikutwa na kadi 10 za benki tofauti

Mshtakiwa wa tatu anadaiwa kuhusika kuandaa nyaraka za viwanja na kuzisaini na uchunguzi uliofanywa ulibaini washitakiwa wote walikuwa na uhusiano wa moja kwa moja na maofisa wa benki.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.