STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar


KIFO cha Marehemu Rais Mstaafu wa
Awamu ya Tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Bejamin William Mkapa kimeacha
pengo kubwa katika uongozi na maendeleo ya Tanzania, Afrika na duniani kote kwa
mchango wake uliooendelea kuhitajika ndani na nje ya mipaka yaTanzania.
Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, aliyasema hayo
leo katika risala aliyoitoa kupitia
vyombo vya habari kufuatia kifo cha Rais
Mstaafu wa Awamu ya Tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Bejamin William
Mkapa, kilichotoke usiku wa kuamkia Ijumaa ya tarehe 24 Julai, 2020.
Katika risala yake hiyo Rais Dk. Shein alisema kuwa Marehemu Mzee
Mkapa alikuwa na uwezo mkubwa wa kubuni mambo mapya ya maendeleo ambapo miongoni
mwa mambo makubwa ambayo aliyaanzisha katika kipindi chake cha uongozi ni
kuunda Mamlaka ya Kodi ya Mapato Tanzania (TRA).
Alisema kuwa aliunda (TRA) ili kuimarisha ukuaji wa uchumi,
kuongeza ukusanyaji wa mapato na kuiwezesha Tanzania kujitegemea ambapo
jitihada zake hizo zilipelekea Tanzania kukua kwa uchumi wake.
“Tulianza kulipa madeni ambapo baadae nchi yetu ilisamehewa madeni
yake, tulianza kuaminiwa na tukawa tunakopesheka”, alisema Dk. Shein.
Aidha alieleza kuwa katika kipindi chake cha miaka kumi uchumi
ulikuwa kutoka asilimia 3.6 hadi 6.7 sambamba na hatua hiyo, alichukua hatua za
kubinafsisha Mashirika ya Umaa ambayo
yalikuwa yakiendeshwa kwa hasara na kuuletea mzigo mkubwa kwa Taifa.
Akimuelezea Marehemu Mkapa, Rais Dk. Shein alisema kuwa vilevile
aliansha Mpango wa Kukuza Uchumi na Kupinguza Umasikini( MKUKUTA),(MKURABITA)
na (TASAF), pamoja na kuanzisha Wakala kadhaa kama vile EWURA,SUMATRA kwa ajili
ya kudhibiti na kutoa huduma bora kwa jamii.
Alieleza kuwa baada ya kustaafu kwake aliansiha Taasisi Isiyo ya
Kiserikali ya Benjamin Mkapa, ambayo
inayoshughulikia masuala ya afya hasa mapambano dhidi ya UKIMWI.
Katika masuala ya kupiga vita rushwa na ufisadi, kiongozi huyo
alianzisha Tume Maalum maaraufu kwa jina la Tume ya Warioba iliokuwa na lengo
la kupendekeza njia bora za kuzuia mianya na vitendo vya rushwa.
Alisema kuwa matokeo ya jitihada hizo ni kuanzisha kwa taasisi ya
kudhibiti na kuzuia rushwa Tanzania (TAKUKURU) na hatimae kupelekea kuundwa kwa
Mahakama maalum ya wahujumu uchumi katika Awamu ya Tano ya Jamhuri ya Mungano
wa Tanzania.
Kutokana na kauli mbiu yake ya “Uwazi na Ukweli”, Rais Mkapa
alianzisha Wizara Maalum inayoshughulikia Utawala Bora, kadhalika alianzisha
vitengo vya habari na Mawasiliano katika Wizara na Mashirika pamoja na
kuanzisha utaratibu wa kuwahutubia wananchi kila mwezi.
Alisema kuwa hatua hizo zimewawezesha wananchi kuyafahamu matokeo
muhimu ya Kitaifa na Kimataifa ambapo pamoja na suala hilo Marehemu Mzee Mkapa
alitambua mapenzi ya Watanzania katika sekta ya michezo kwa hivyo, alihakikisha
anawajengea wananchi kiwanja cha michezo cha kisasa chenye kiwango cha
kimataifa.
Katika uwanja wa siasa, Rais Dk. Shein alisema kuwa Marehemu Mkapa
alikuwa ni mfano wa wanasiasa bora walioweka mbele maslahi ya Taifa na kuongoza
kwa mifano.
Alisema kwua kwa uhodari mkubwa aliokuwa nao Marehemu Rais Mkapa,
aliweza kuendesha siasa za vyama vingi kwa haki na demokrasia ambapo uongozi
wake wa miaka kumi akiwa Rais, uliipatia Tanzania heshima kubwa katika Jumuiya
ya Kimataifa na ndani ya Taifa hili.
“Alipenda mashirikiano na kuheshimu mawazo ya kila mmoja na wakati
wote alikuwa mchangamfu na mwenye tabasam….alikuwa na uwezo mkubwa wa kuhimili
changamoto za uwongo kila zinapotokea”, alisema Dk. Shein.
Aidha, aliongeza kuwa Rais Mkapa alikuwa kiongozi asiyependa
fitina na majungu na siku zote huwapongeza wanaofanya vizuri pamoja na kuwasamehe
wale wanaotubu makosa yao kwake kwa dhati.
Rais Dk. Shein alisema kuwa Rais Dk. Shein alikuwa mstari wa mbele
katika kutetetea na kuzienzi tunu za Taifa zikiwemo umoja wa Watanzania, Mapinduzi
ya Zanzibar na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Katika kuamini kwake umuhimu wa kuendeleza umoja na mshikamano
miongoni mwa mataifa ya Afrika Marehemu Mzee Mkapa alitoa mchango mkubwa katika
kuanzishwa upya kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki ili kuumarisha mtengemano wa
nchi na wananchi wa nchi za Afrika Mashariki.
Rais Dk. Shein alisema kuwa Marehemu Mkapa alikuwa muumini wa
dhati wa amani ya nchi ambapo katika kutilia mkazo umuhimu wa kutunza amani kwa
maendeleo ya Taifa katika moja ya hutoba zake alisisitiza umuhimu huo kwa kusema
“Nchi hii ni nchi yetu sote ni ya watoto wetu na vizazi vyetu
vijavyo. Ikiwa na amani ni amani ya Watanzania wote ikiwa ya vurugu ni vurugu
itakayowaathiri Watanzania wote. Tukivurugana MwenyeziMungu hatotupa ardhi
nyengine,tuamue basi kuijenga Tanzania ya demokrasia ya kweli, Tanzania
inayoheshimu haki za binaadamu, Tanzania inayopiga haraka hatua za maendeleo,
Tanzania ya amani, upendo, umoja na mshikamano”.
Pamoja na hayo, Rais Dk. Shein, alisema kuwa Marehemu Mzee Mkapa
alikuwa na sifa ya kuibua vipaji vya viongozi wachanga, kuwajenga na kuwakuza
na hatimae viongozi hao kutoa mchango mkubwa katika Taifa.
Rais Dk. Shein alisema kuwa yeye mwenyewe binafsi alijifunza mambo
mengi sana na kupata mashirikiano ya hali ya juu kutoka kwa Marehemu Rais Mkapa
kwa kiasi cha kupata weledi mkubwa wa kuyatekeleza majukumu yake katika
uongozi.
Vile vile, Rais Dk. Shein aliwasihi Watanzania kuendelea kuwa
wamoja, kuyaenzi na kuyadumisha yale yote aliyoyaacha Mzee Mkapa huku
akisisitiza kuwa ni vyema kuzingatia fikra na mawazo yake kupitia hotuba zake
mbali mbali pamoja na yale yaliomo katika kitabu chake cha “My Life My Purpose”
(Maisha yangu Kusudi langu).
Rais Dk. Shein aliongeza kuwa kwa niaba ya Wananchi na Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar anaungana na wanafamilia, ndugu, marafiki na Watanzania
wote katika kipindi hichi kigumu cha majonzi na huzuni.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment