Habari za Punde

Ustawi wa Sekta ya Kilimo Unahitaji Uwepo wa Amani na Utulivu Ndani ya Taifa - Balozi Seif.

Na.Othman Khamis.OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema ustawi wa sekta ya Kilimo unahitaji uwepo wa amani na utulivu ndani ya Taifa ili Wananchi wanaotegemea Sekta hiyo wapate maendeleo yatakayochangia pia pato la Taifa.
Alisema bila ya amani na utulivu hakuna Mwananchi atakayethubutu kwenda shambani, baharini, au msituni kutafuta riziki na hatimae atashindwa kupata mahitaji yake muhimu na ya kila siku ikiwemo chakula, elimu na hata matibabu.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo wakati akiyafunga Maonyesho ya Tatu ya Kilimo yaliyokuwa yakifanyika katika Uwanja wa Maonyesho wa Chamanangwe uliopo Mkoa wa Kaskazini Pemba ambayo huadhimikshwa ifikapo Mwezi wa Nane wa Kila Mwaka.
Alisema haikamiliki kujivunia kwamba Taifa limesheheni uwepo wa  Amani bali hii iliyopo ni vyema ikaambatana na maendeleo ya kudumu katika sekta zote zikiwemo; Kilimo, Afya, Elimu, Maji, Biashara, Miundombinu, pamoja  na Mawasiliano.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif ameupongeza Uongozi  wa Wizara  ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi kwa  kusimamia na hatimae kufanikisha  shughuli  hiyo  muhimu ya maonyesho ya Kilimo.
Alisema umahiri wa Uongozi huo umepelekea wananchi wengi kujitokeza kwa wingi na kushiriki kikamilifu katika maadhimisho hayo sambamba na kupata fursa ya kuuza bidhaa wanazo zitengeneza wenyewe.
Balozi Seif alibainisha kwamba vijana mbali mbali wajasiriamali wakiwemo pia kina mama wameweza kujifunza mambo tofauti ya kukuza mitaji yao iliyosaidia kujiongezea kipato katika kipindi kidogo cha Maonyesho.
Alifahamisha kwamba mambo hayo yanatimiza ile dhamira ya Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo, na Uvuvi ya kuwa maonyesho ya Kilimo ni njia moja wapo ya kuwafikia wananchi waliowengi kwa muda mfupi katika kutoa elimu pamoja na kuonyesha teknolojia mpya za uzalishaji.
Balozi Seif alieleza kuwa hiyo pia inakwenda sambamba na kutangaza fursa mbali mbali zilizopo za kutoa ajira pamoja na kusambaza maendeleo na mafanikio mbali mbali yaliyofikiwa katika kuendeleza sekta ya kilimo nchini.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  alielezea matarajio yake kwamba elimu na taaluma waliyoipata Wananchi hao wataitumia vyema ili kuongeza uzalishaji katika shughuli zao za kilimo, ufugaji, uvuvi pamoja na kuchangamkia fursa zilizopo hususan kwa vijana ili kuleta maendeleo kwa kuinua pato la mwananchi na hatimae kukuza uchumi wa Taifa.
Akigusia Taifa kukabiliwa na Uchaguzi Mkuu ifikapo Mwezi Oktoba Mwaka huu Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema ni jukumu la kila Mwananchi kuhakikisha kwamba anatumia haki yake ya kidemokrasia bila ya kushawishiwa hali inayoweza kupelekea vurugu zilizo na maslahi kwa walio wengi.
Alisema maisha bado yataendelea kuwepo mara baada ya Uchaguzi. Hivyo Watanzania wanapaswa kuelewa kwamba wao wote ni ndugu wanaowajibika kuepuka mifarakano na badala yake wazingatie upendo na kufuata sheria za Nchi.
“ Tuwe watii wa sheria za nchi ipasavyo katika kipindi chote cha Uchaguzi kwani suala la kuilinda Amani ya nchi hii ni jukumu letu sote na halichagui, sura, rangi, dini wala kabila”. Alisisitiza Balozi Seif.
Akitoa Taarifa ya Maonyesho hayo Naibu Kagtibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Maliasikli, Mifugo na Uvuvi Nd. Omar alisema maonyesho ya Mwaka huu yamehudhuriwa na Washiriki 189 kutoka Taasisi na Mashirika ya Umma, Binafsi wa Pemba, Unguja na Baadhi kutoka Tanzania Bara.
Nd. Omar alisema inapendeza kuona Wananchi na Wanafunzi kutoka maeneo mbali mbali ya Kisiwa cha Pemba wamehudhuria Maonyesho hayo kuona pamoja na kujifunza mambo mbali mbali ndani ya ek\ta ya Kikimo.
Alisema wakati maonyesho yanafikia ukingoni kwa mujibu wa tafiti za kitaalamu zimedhihirisha kwamba mwaka huu hakukuwa na cvhangamoto kubwa zilizojitokeza kufuatia Wakulima na Wananchi wengi kufuata miongozo ya Kilimo.
Akimkaribisha Mgeni Rasmi kuyafunga Maonyesho hayo ya Nane Nane yaliyoongezwa siku moja ya ziada Waziori wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na uavuvi Mheshimiwa Mmanga Mjengo Mjawiri alivishukuru vyombo vya Ulinzi pamoja na wale wa  Halmashauri kwa umakini wao uloiopelekea kufanikiwa kwaMaonyesho hayo.
Ujumbe wa Mwaka huu wa Maonyesho ya Tatu ya Kilimo unasema "TUDUMISHE AMANI NA UTULIVU KWA MAENDELEO YA SEKTA YA KILIMO ZANZIBAR"

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.