WAZIRI wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Riziki Pembe Juma amesema Wizara yake itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo ili kuhakikisha sekta hiyo inaendelea kupiga hatua nchini.
Akizungumza katika kikao cha matayarisho ya makabidhiana ya Skuli mpya ya Sekondari Donge baina ya Wizara ya Elimu na wafadhili wa Skuli hiyo huko Donge mkoa wa Kaskazini Unguja amesema Wizara yake
ilionesha mashirikiano mazuri na wafadhili kutoka Indonesia ili kuhakikisha Skuli hiyo inakamilika ikiwa katika kiwango bora na salama kwa Wanafunzi.
Aidha Riziki amesema ili Taifa liongeze kiwango cha ufaulu kinahitaji Kua na Walimu wabunifu na majengo mazuri yatakayokidhi Haja na kuleta ufanisi mzuri wa Elimu.
Hivyo amewataka wazazi kuhakikisha wanawahamasisha watoto wao kusoma kwa bidiii ili kuhakikisha kiwango cha ufaulu kinaongezeka katika Mkoa wao na kurejesha heshima ya Mkoa wao katika Elimu.
Sambamba na hilo Pembe amewashukuru wafadhili wanaomalizia ujenzi huo na kuwataka kujitahidi kufanya matengenezo madogo madogo yaliobaki ili wanafunzi waweze kusoma kwa haraka.
Mapema Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Zanzibar injinia Idrisa Muslim Hija amesema ni jukumu la Wizara ya Elimu kuhakikisha Wanafunzi wanapata Elimu katika mazingira salama, na ndio maana ikaamua kufanya
matengenezo yaliobainika ili kuwa na ubora zaidi.
Nae Mwenyekiti wa kamati ya maendeleo ya Donge Yahya Ali Ussi amesema kamati yake ilikua mstari wa mbele kuhakikisha ujenzi wa Skuli hiyo unaendelea vizuri ili uweze kusaidia kupunguza tatizo la uhaba wa madarasa katika Skuli ya Donge.
Kwa upande wake mwakilishi wa jimbo la Donge Dkt. Khalid Salum Mohammed ameipongeza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar kwa kuonesha mashirikiano mazuri kwa wananchi wa Donge hadi kuhakikisha
ujenzi wa Skuli hiyo unamalizika.
Ujenzi wa Skuli ya Sekondari Donge ulianza 1993 kwa nguvu za wananchi kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu Zanzibar.
No comments:
Post a Comment