Habari za Punde

Utamaduni wa kutopima afya umeongeza tatizo la presha ya macho


Na mwandishi wetu



MKUU wa Kitengo cha Maradhi ya Macho Zanzibar Dk. Slim Mohammed Mgeni,amesema tatizo la presha ya macho  linazidi kutokana na wananchi wengi kutokuwa na utamaduni wa kupima afya zao.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi huko Ofisini kwake Mnazimmoja, alisema kuwa hatua hiyo inapelekea kuwa wengi wanaofika hospitali kupatiwa matibabu wanakuwa na tatizo kubwa.

"Niseme tu tatizo hili la presha ya macho linazidi kukuwa kwa sababu wengi miongoni mwetu hatupendi kupima afya zetu, na mtu kama hana tatizo inamaana anakaa  hapimi afya yake pia hapati elimu ya afya", alisema Dk. Slim.

Hivyo alisema presha ya macho mara nyingi inaendana na urithi hivyo mgonjwa anapokwenda ni lazima wakati wa kupewa elimu apate pamoja na familia yake, ili na wao wapime afya zao.

"Watu wanapokuja wanakuwa tayari washapata tatizo hili na kwa vile tatizo hilo linaendana na urithi hivyo katika utoaji wa elimu lazima awe pamoja na familia yake ili na wao waje wapime afya zao", alisema.

Dk. Slim alifahamisha kwamba katika Kipindi cha miaka 10 iliyopita walikuwa hawana vifaa vya uhakika vya kupimia presha ya macho lakini sasa wamepata na wanawagunduwa na kuwapatia matibabu.

Aidha alifahamisha kwamba tatizo la presha ya macho wanapoliwahi wanakuwa wanawakinga watu
wengi wasipate matatizo ya mwisho ya maradhi hayo ambayo ni upofu.

Hivyo alifahamisha kwamba kuwagunduwa mapema na kuwapa matibabu wanakuwa wamewapunguza vipofu wengi wa macho wazi kama pale wanapofanya zile huduma mapema zaidi.

"Tunaipongeza awamu ya saba ya Dk. Ali Mohamed Shein kwani hivi sasa tumepata vifaa vingi vipya na vya kisasa na tunawagunduwa sana wagonjwa wa aina hii", alisema.

Kwa upande wake Mratibu wa Huduma za Macho Zanzibar Dk.Rajab Mohammed Hilal, alisema ukubwa wa tatizo la macho ni wastani wa asilimia moja kwa Zanzibar sawa na watu karibu 10,000 wenye matatizo ya macho
Zanzibar kwa aina tofauti.

Hivyo alisema kati ya hao 10,000 tatizo kubwa la macho linaloongoza katika vituo vyao ni la mtoto wa jicho ambayo inachangiwa na 0.5% ambayo ni sawa na watu karibu 5000 wenye matatizo ya macho ya mtoto wa jicho kulingana na sensa ya idadi ya watu Zanzibar ya mwaka 2012 huku Presha ya macho ikichukuwa nafasi ya pili kwa asilimia 0.4 ikiwa ni karibu ya watu 4000.




Hata hivyo alisema kuwa tatizo la presha ya macho linapowahiwa basi linawakinga watu wengi  wasipate matatizo ya macho ya upofu (macho wazi).

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.