Habari za Punde

Mgombea Urais wa Zanzibar Kwa Tiketi ya CCM Mhe.Dk. Hussein Mwinyi Ameahidi Makubwa Kwa Wananchi wa Zanzibar.

Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Hassan Mwinyi akihutubia katika mkutano wake wa kampeni katika viwanja vya mpira Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja na kuwaomba kura kumchagua kuongoza Zanzibar na kuwaombea Kura Wagombea Ubunge,Uwakilishi Udiwani na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli, mkutano huo wa kampeni umefanyika leo jioni 20/9/2020.

NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.

MGOMBEA Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM Dk.Hussein Ali Mwinyi amesema endapo atachaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar,atahakikisha anatatua migogoro ya ardhi iliyopo baina ya wakaazi na wawekezaji katika sekta ya utalii katika Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Alisema kuna malalamiko mengi ya wananchi wanaoingia mikataba yenye utata baina yao na wawekezaji na kushindwa kupata haki zao kisheria.

Hayo ameyasema wakati akizungumza na maelfu ya wananchi katika mkutano wa hadhara wa kampeni za CCM uliofamyika katika uwanja wa Skuli Nungwi Wilaya ya Kaskazini "A" Unguja.

Alisema Kila mwananchi aliyedhurumiwa ardhi ama mwenye madai baina yake na wawekezaji atahakikisha wanapata haki yake.

Alisema atatafuta ufumbuzi wa mapema kumaliza tatizo la maji katika eneo la Nungwi kwani kwa upande wa Zanzibar Serikali imesambaza maji kwa asilimia 72 hivyo asilimia 28 zilizobaki zitamaliziwa haraka pindi akiingia madarakani.

Alieleza kuwa eneo la Nungwi ni sehemu ya utalii ni lazima liwe na maji ya kutosha.

Atajenga soko la kisasa na kujenga viwanda vya kusindika samaki ili wavuvi wapate soko la uhakika.

Alisema atafanya matengenezo makubwa ya barabara za ndani ili wananchi na watalii wapate urahisi kwa kufanya kazi zao kwa ufanisi.

Alisema lengo ni kuanzisha vyanzo vipya vya kiuchumi kupitia uchumi wa bahari(Blue economy).

Pia kuimarisha sekta ya uwekezaji kwani ndio chimbuko la upatikanaji wa ajira kwa vijana na wananchi kwa ujumla.

Aliahidi wavuvi wa mwambao huo wa Kaskazini Unguja, kupewa nyenzo na vifaa vya kisasa vitakavyowawezezha kufanya kazi zao kwa uhakika.

Alisema kwa Uongozi wake atatunga Sheria Kali ya kuwadhibiti watu wanaofanya vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia.

Alisema yote hayo yatafanyika kwa haraka endapo wananchi watawachagua kwa kura nyingi Wagombea wote wa CCM kuanzia ngazi za Urais hadi Madiwani na Wagombea wote wa viti maalum.

Alisema sekta ya utalii imeendelea kuleta mafanikio makubwa kwani umekuwa ni chachu ya kukuza uchumi na kuongeza Pato la Taifa.

Ameishukru Serikali ya awamu ya saba kwa kusimamia amani na utulivu wa nchi kwani kwa kipindi Cha miaka kumi Zanzibar imeendelea kuwa na utulivu wa kudumu.

"Chama Cha Mapinduzi hakina tabia ya uongo kwani kikiahidi kinatekeleza kwa vitendo, na tumefanya mambo mengi makubwa sana katika nyanja za kimaendeleo.",alisema Dk.Shein. 

Alisema lengo la CCM kushinda ni kulinda umoja,mshikamano na kulinda Mapinduzi ya Zanzibar 1964  na Muungano.

Akizungumza Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein,alisema Serikali ya awamu ya saba chini ya Uongozi wake imetekeleza ipasavyo Ilani ya uchaguzi ya CCM kwa kiwango kikubwa.

Alieleza kuwa uchumi wa Zanzibar umeimarika kwa kiwango kikubwa na kwamba hali za wananchi zimeimarika na kupungua kwa kiwango Cha umaskini.

Alieleza kuwa ameimarisha miundombinu ya barabara,umeme,maji Safi na salama pamoja na kuimarisha miundombinu ya usafiri wa anga na baharini.

Pia alisema ameweka  mazingira rafiki ya kukuza ustawi wa kijamii kwa kujali na kutoa kipaumbele kwa makundi maalum yakiwemo ya watu wenye ulemavu na wazee.

Dk.Shein,aliwatambulisha na kuwaombea kura sambamba na kuwakabidhi Ilani a Uchaguzi ya mwaka 2020/2025  Wagombea wa nafasi mbalimbali wakiwemo Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM Dk.Hussein Ali Mwinyi,Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.John Pombe Magufuli,Mgombea mwenza wa kiti Cha Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan,Wabunge,wawakilishi,Madiwani na Wagombea wa nafasi za Viti maalum.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Mabodi ,alisema CCM imeendelea kufanya kampeni za kisayansi ambapo Mgombea wa tiketi ya CCM Dk.Hussein anawafuata wananchi katika maeneo yao ili kuwaeleza Sera za vipaumbele vyake atavyovitekeleza pale atakapokuwa Rais wa Zanzibar.

"Mgombea wetu Dk.Hussein anaenda mtaa kwa mtaa kuomba kura na kueleza kwa kina Sera za Chama,kusema kweli anatosha na ana sifa za kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la 
Mapinduzi wa Serikali ya awamu ya Name",alieleza Dk.Mabidi.

Aliongeza kuwa kwa mujibu wa ibara ya tano ya Katina ya CCM ya mwaka 1977 ,ushindi wa CCM ni lazima kutokana na utekelezaji mzuri wa Ilani ya CCM ya mwaka 2015/2020.

Dk.Mabodi amesema Ilani mpya imetaja suala zima la kuwaunganisha wananchi wa Zanzibar ili waendelee kuwa wamoja.

Alisema Ilani hiyo imetaja namna CCM itakavyo endelea kuimarisha mfumo wa elimu na sekta mbali mbali za kimkakati.

Aliongeza kuwa katika Ilani hiyo imesisitiza uimarishaji wa uchumi wa Zanzibar na kuanzisha vyanzo vipya vya kiuchumi.

Aliongeza kuwa CCM itaendelea kuhakiki na kuwafuatilia utendaji wa viongozi wanaopewa dhamana ya kuongoza wananchi ili kujiridhisha Kama wanatekeleza kwa vitendo yale yaliyoahidiwa na CCM kwa wananchi.

"Tulindeni amani yetu kwani bila amani hakuna maendeleo yoyote yatakayofanyika hivyo Kila mtu achukue juhudi za kulinda nchi yake kwa kujiepusha na vitendo vya uvunjifu wa Sheria ",alisema Dk.Mabodi.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja Idd Ali Ame, akitoa salamu za Mkoa huo alisema wananchi wa Mkoa huo wanamshukru Sana Dk.Shein kwa Mambo mema aliyowatendea hasa kwa kuwaletea maendeleo katika nyanja za kiuchumi,kijamii na kisiasa.

Amesema kuwa Mkoa huo ni wa Kwanza kwa kuwa na miundombinu Bora ya barabara ambazo zimesaidia kwa kiwango kikubwa wafanyabiashara na wakulima wanaosafirisha mazao na bidhaa mbali mbali kutoka sehemu moja kwenda nyingine.

Alisema katika kipindi Cha Uongozi wa Dk.Shein,Mkoa huo umejengwa shule za msingi,sekondari na Vyuo vya mafunzo ya amali(ufundi) ambapo vijana wa Mkoa huo wameendelea kupata elimu bure.

Amesema vituo vya afya vimejengwa kwa wingi Hali inayosababisha makundi yote ya jamii ndani ya Mkoa huo Wana siha (afya) njema kutokana na kupata lishe na afya nzuri.

"Mgombea wetu anasema yajayo yanagurahisha hakika ushindi wetu hakuna wa kuzuia kwani tayari CCM imetekeleza maendeleo na kuimarisha maisha ya watu",alisema Mwenyekit.

Mkutano huo ulianza saa 3:00 asubuhi ambapo burudani mbalimbali zimetumbuiza huku maelfu ya wananchi wakimiminika katika uwanja huo.

 Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi na wananchi kwa ujumla wamejitokeza kwa wingi katika mkutano wa kampeni za CCM zilizofanyika katika uwanja wa skuli ya Nungwi Wilaya ya Kaskazini 'A' Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Viongozi mbali mbali wa Chama wamehudhuria katika mkutano huo wakuwatambulisha Wagombea wa nafasi mbali mbali za Uongozi katika Mkoa huo.

Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM Dk.Hussein Ali Mwinyi,aliwasili katika viwanja vya Skuli ya Nungwi majira ya saa 7:45.

Pia Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein amewasili kiwanjani hapo saa 8:00 mchana kwa ajili ya kuwatambulisha Wagombea wa CCM.

Viongozi walioudhuria katika mkutano huo ni pamoja na Rais mstaafu wa Tanzania Mzee Ali Hassan Mwinyi,Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd,Spika wa Baraza la wawakilishi,Waziri kiongozi Mhe.Shamsi Vuai Naohodha na Spika wa Baraza la wawakilishi.

wengine walioudhuria ni wajumbe wa kamati kuu ya CCM Taifa ,Wajumbe wa Halmashauri Kuu,wenyeviti,makatibu ,wagombea wa nafasi mbalimbali za Uongozi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.