Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhajj Dk. Ali Mohamed Shein, akiweka mchanga katika kaburi lililowekwa mwili wa aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Mpendae kupitia CCM Marehemu Salim Hassan Abdallah Turky, yaliofanyika katika makaburi ya Fuoni Kijitoupele Jijini Zanzibar Wilaya ya Magharibi "B" Unguja.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj
Dk. Ali Mohamed Shein leo ameongoza
mazishi ya Mwanasiasa Mkongwe na Mgombea nafasi ya Ubunge Jimbo la Mpendae
Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Salim Hassan Abdullah Turky yaliyofanyika
katika makaburi ya Kijitoupele Mkoa wa Mjini Magharibi.
Viongozi mbali mbali
wa vyama vya siasa, dini, serikali na sekta
binafsi pamoja na wananchi, wafanyabiashara, ndugu na jamaa walihudhuria katika mazishi hayo akiwemo Makamo wa Pili wa
Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd, Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Mungano wa
Tanzania Ali Hassan Mwinyi.
Wengine ni Makamo wa
Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Mohamed Gharib Bilal, Mgombea
nafasi ya Urais wa Zanzibar kupitia CCM Dk. Hussein Ali Hassan Mwinyi, Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabih
pamoja na Naibu Kadhi Mkuu wa Zanzibar
Sheikh Hassan Othman Ngwali.
Mapema Alhaj Dk. Shein
aliungana na viongozi, ndugu, jamaa, marafiki na wananchi mbali mbali katika dua
na sala ya kumsalia Marehemu Salim
Hassan Abdullah Turky (Mr. White) katika
Msikiti wa “Noor Muhammad” uliopo Mombasa
Mjini Unguja.
Akisoma wasifu wa
Marehemu huko Kijitoupele katika eneo la makaburi alipozikwa Marehemu, Waziri
Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mohammed Aboud Mohammed alisema
kuwa Marehemu Salim Hassan Abdullah Turky (Mr. White), aliyezaliwa Februari 11 mwaka
1963 amefariki dunia usiku wa kuamkia leo Septemba 15, 2020 huko katika
Hospitali ya Tasakhtaa Global Jijini Zanzibar.
Waziri Aboud alieleza
kuwa Marehemu Salim Turky alikuwa mfanyabiashara maarufu Zanzibar na muda mrefu
hapa nchini ambapo ameanza shughuli zake za Biashara tangu miaka ya 1980 kwa
kujishughulisha na uagiziaji na uuzaji wa bidhaa mbali mbali.
Aliongeza kuwa katika
mwaka 1990 alijiunga na kuwa Mjumbe wa Jumuiya ya Wafanyabiashara na Wakulima
Zanzibar (Zanzibar National Chamber of Commence) na mwaka 2006 aliteuliwa kuwa
Mdhamini wa Jumuiya hiyo hadi kifo chake.
Aidha, alisema kuwa katika
shughuli zake za biashara Marehemu alikuwa ni mwanzilishi na Mwenyekiti wa
“Turky Group of Company”, Kampuni ambayo inajishughulisha na Biashara za
Utalii, mafuta na gesi, huduma za afya, viwanda, usafirishaji wa Baharini na
kadhalika.
Kwa maelezo ya Waziri
Aboud katika harakati za siasa tokea mwaka 1992 Marehemu alishiriki kikamilifu
katika shughuli za kisiasa nchini ambapo alikuwa mpenzi thabiti wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM), ambapo katika mwaka 2010-2020 alikuwa Mbunge wa kuchaguliwa na
Wananchi katika Jimbo la Mpendae.
Alisema kuwa Katika
kuelekea uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 Marehemu alikuwa tayari ameteuliwa na (CCM)
kuwa Mgombea wa kiti cha Ubunge katika Jimbo la Mpendae.
Aidha, Waziri Aboud
alisema kuwa katika shughuli za Kibunge Marehemu aliteuliwa kuwa Mjumbe wa
Kamati ya Kudumu ya Viwanda na Biashara na Kamati ya Kudumu ya Ardhi Maliasili
na Utalii katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kutokana na umahiri
wake wa kufanyakazi kwa bidii katika Bunge, alisema kuwa Marehemu aliteuliwa
kuwa Kamishna wa Tume ya Huduma za Bunge pamoja na kuwa Mjumbe katika mradi wa
Umoja wa Mataifa wa Huduma za Bunge (Legislative Support Project) unaosimamiwa
na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Mpango wa Maendeleo (UNDP).
Sambamba na hayo,
katika masuala mazima ya kujitolea katika jamii, Waziri Aboud akisoma wasifu wa
Marehemu Turky alisema kuwa mbali na kuwa mfanyabiashara na mwanasiasa pia
alijitolea katika kusaidia masuala mbali mb ali ya kijamii bila ya kujali
itikadi yake ya kisiasa ambapo aliweza kuwasidia watu mbali mbali kutokana na
mahitaji yao.
Wasifu huo ulieleza
kuwa Marehemu pia, alijitolea kikamilifu katika kuunga mkono juhudi za Serikali
za kupambana na umasikini na kukuza uchumi.
Waziri Aboud alisema
kuwa Marehemu atakumbukwa katika juhudi za kukuza sekta ya michezo na elimu
ambapo katika mwaka 1993 alichaguliwa kuwa Meneja wa timu ya mpira wa miguu ya
“Shangani Football Club” na ilifanikiwa kuchukua kombe la ubingwa wa ligi Kuu
ya Zanzibar na mwaka 1995 alikuwa ni miongoni mwa waanzilishi wa Skuli ya Sunni
Madrassa Jamat iliyopo Mkunazini.
Hivi karibuni katika
Mkutano wa uzinduzi wa Kampeni za (CCM) zilizofanyika katika viwanja vya
Kimandamaiti maarufu viwanja vya Demokrasia, Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar
na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein
alimnadi Marehemu Turky pamoja na wagombea nafasi wengine za uongozi ndani ya chama
hicho.
Marehemu Turky ameacha
kizuka na watoto watatu, Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahala pema peponi,
Amin.
Rajab
Mkasaba, Ikulu
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment