Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Shein Kuwasawadia Wanafunzi Bora wa Kidatu cha Sita na Cha Nne Viwanja Vya Ikulu Jijini Zanzibar.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein akiwahutubia Wanafunzi Bora wa Kidatu cha Sita na Nne wa Skuli za Sekondari za Unguja na Pemba wakati wa hafla ya chakula maalum alichowaandalia katika viwanja vya Ikulu Jijini Zanzibar na kuwakabidhi zawadi Wanafuzi Bora wa Masomo mbalimbali.
 

SEIRIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Saba iliamua kuifanya elimu kuwa ni moja ya vipaumbele vya Serikali kwa kuiongeza Bajeti ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kutoka TZS Bilioni 47.093 mwaka 2010/2011 hadi kufikia TSZ Bilioni 178.917 mwaka 2019/2020

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameyasema hayo leo katika hafla maalum aliyoiandaa ya kuonana, kula chakula cha mchana pamoja na kuwakabidhi zawadi wanafunzi waliomaliza masomo ya Kidato cha Nne mwaka 2019 na Kidato cha Sita mwaka 2019/2020 na kufaulu kwa kiwango cha daraja la Kwanza katika mitihani yao ya Taifa.

Katika maelezo yake Rais Dk. Shein alisema kuwa kiwango hicho cha Bajeti kumeiwezesha Zanzibar kupata mafanikio makubwa ya maendeleo katika sekta ya  elimu.

Alisema kuwa dhamira njema ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na mipango mizuri iliyowekwa ya kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika sekta ya elimu tayari matunda yake yanaonekana kwa kuongezeka kwa kiwango cha ufaulu wa wanafunzi katika mitihani yao ya ngazi mbali mbali hapa nchini.

Aliongeza kuwa kwa lengo la kufikia dhamira ya kutoa elimu bure lililoongozwa na Jemedari wa Mapinduzi marehemu Mzee Abeid Amani karume tarehe 23 Septemba, 1964 Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Saba ilipoingia madarakani ilifanya kama zilivyofanya Awamu zilizotangulia kwa kuipa kipaumbele elimu.

Rais Dk. Shein alisema kuwa  ufaulu wa wanafunzi katika mitihani yao umeongezeka sana ambapo wanafunzi wa msingi kwenda Sekondari ufaulu umeongezeka kutoka asilimia 84.4 mwaka 2010 na kufikia asilimia 97.5 mwaka 2019.

Kadhalika kwa maelezo ya Dk. Shein ufaulu wa wanafunzi kidato cha Pili katika mitihani ya kuingia kidato cha Tatu umeongezeka kutoka asilimia 58.2 mwaka 2010 na kufikia asilimia 76.8 mwaka 2019.

Ambapo aliongeza kuwa ufaulu wa wanafunzi kwa mitihani ya kidato cha Nne kwa daraja la kwanza na pili umeongezeka mara nne zaidi kutoka asilimia 1.5 mwaka 2010 hadi kufikia asilimia 6.3 mwaka 2019.

Kwa upande wa kidato cha Sita Rais Dk. Shein alisema kuwa ufaulu kwa daraja la kwanza na la pili katika mitihani ya Taifa, kwa mwaka huu wa 2020 umefikia asilimia 33.92 ikilinganishwa na asilimia 7.2 hapo mwaka 2010.

Aidha, Rais Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuwapongeza wanafunzi hao waliofanya vizuri wakiwemo wanafunzi 299 wa kidato cha Nne na wanafunzi 124 wa Kidato cha Sita waliopata daraja la kwanza katika mitihani yao ya Taifa iliyopita.

Rais Dk. Shein aliwapongeza kwa mafanikio hayo ambayo yameleta furaha kwao, kwa walimu, wazazi na walezi wao lakini vile vile kwa Serikali na jamii yote kwa jumla. “Siku zote ushidni ao mafanikio huleta furaha ndio maana leo tupo hapa kuja kufurahi na kupongezana”,alisema Dk. Shein.

Katika maelezo yake, Rais Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Saba imepiga hatua kubwa katika kuimarisha sekta ya elimu hivyo Serikali ya Awamu ya Nane ijayo ije kuendeleza misingi mizuri iliyoachwa “Tumeiwezesha Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali na wao wameweza na wamefanya vizuri”,alisisistiza Rais Dk. Shein.

Aidha, Dk. Shein aliwahimiza wanafunzi hao kuongeza bidii ili waweze kuifanya vyema zaidi katika masomo yao ya hatua iliyo mbele yao sambamba na kuendelea kuwa na nidhamu na kujiwekea malengo ili waweze kufanikiwa zaidi huko mbele waendako.

Akimnukuu Mwandishi wa Marekani aitwae Vincent Peale (1898-1993) ambae aliwahi kuwa Waziri katika nchi hiyo, Rais Dk. Shein alisema kwamba watu wote wanaofanikiwa ni wale wanaojiwekea malengo katika maisha yao.

Aliongeza kuwa hakuna mtu anaefanikiwa katika maisha iwapo mtu huyo hajui anataka nini katika maisha yake na wala hajitambui hivyo aliwataka wautumie vizuri wakati huu walio nao katika umri walionao kwa kuyapanga malengo mazuri ya maisha yao.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa historia fupi ya sekta ya elimu ilivyokuwa kabla ya Mapinduzi matukufu ya Januari 12, 1964 ambapo wanyonge hawakupata fursa ya kusoma wala kuendelea katika elimu ya juu na kwa wale waliopata fursa hiyo walikuwa wachache sana.

Hivyo, aliwaeleza wanafunzi hao kwamba wasiwe na hofu kwani hapa hapa nchini kwao kuna vyuo vikuu ambavyo vinasomesha masomo yote kutokana na kuimarika kwa sekta ya elimu hapa Zanzibar na hata ikiwa kuna uwezekano wa kusoma nje ya Zanzibar, Serikali itahakikisha wanapata fursa hiyo.

Nae Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Riziki Pembe Juma alitoa pongezi kwa Rais Dk. Shein kwa kuiimarisha sekta ya elimu nchini huku akitoa pongezi nyingi kwa kutoa ufadhili wa nafasi 100 kama ni zawadi kwa kidato cha Sita waliofanya vizuri.

Mapema, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Dk. Idris Muslim Hijja alieleza kuwa wanafunzi wa Kidato cha Nne wamefanya mtihani wa kumaliza mnamo Novemba, 2019 na matokeo kutolewa Januari 2020 ambapo jumla ya wanafunzi 18,647 walifaulu kwa madaraja mbali mbali na wanafuzi 299 wamefaulu kwa kiwango cha Daraja la Kwanza.

Aliongeza kuwa jumla ya wanafunzi 2,548 wa Kidato cha Sita walifanya mtihani wao mwezi wa Juni 2020 na matokeo yao kutoka mwezi wa Agositi 2020 wamefaulu kwa madaraja mbali mbali.

Alisema kuwa kati ya wanafunzi hao 2,548 wanafunzi 124 wamefaulu kwa kiwango cha Daraja la Kwanza ambapo katika mwaka huu wa 2020 wanafunzi bora wawili wamepatikana kwa upeo wa Tanzania kwa masomo ya Biashara.

Aliwataja kwua wanafunzi hao ni Abdulrahman Abdalla Mkanjima kwa Tahasusi ya Uchumi, Biashara na Uhasibu (ECA) kutoka Skuli ya Sekondari ya Biashara ambaye yumo katika kundi la wanafunzi 10 bora kwa Tahasusi hiyo na 10 bora kwa wanaume.

Alisema kuwa mwanafunzi mwengine ni Zaidar Bakar Hemed kwa Tahasusi ya Uchumi, Biashara na Uhasibu kutoka Skuli ya Sekondari ya Chasasa ambaye amekuwa miongoni mwa wanafunzi 10 bora kwa wanawake nchini Tanzania.

“Mafanikio haya tunayoyafurahia hii leo pamoja na walimu wazazi na wazee yanachangia pia, na jitihada zako binafsi, kwani Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar unayoiongoza imewezesha sekta ya elimu kufanikiwa kupata miundombinu imara ya majengo, zana na vifaa vya kujifunzia na kufundishia na kuzipatia vitabu skuli zote za Serikali zenye Kitado cha Tano na Sita kwa masomo yote”,alisema Ktibu Mkuu huyo.

Wakati huo huo, Rais Dk. Shein alitoa zawadi kwa  wanafunzi waliofanya vizuri zaidi wa kidato cha Sita na Kidato cha Nne ambapo kwa zawadi za jumla alipata mwanafunzi Abdulrahman Abdalla Mkanjima kutoka skuli ya Sekondari ya Biashara na  Ziada Bakar Hemed kutoka skuli ya Chasasa.

Wengine waliofanya vizuri katika masomo ya Sayansi ni Muslim Hamad Suleiman kutoka skuli ya Lumumba, Abdulrahman Zaidu Mohammed kutoka skuli ya SUZA na Manal Said Mohammed kutoka skuli ya FEZA Zanzibar.

Kwa upande wa masomo ya Sanaa ni Mwanakhamis Thabit Mohammed kutoka Skuli ya Hamamni, Rashid Kendewele kutoka skuli ya Jang’ombe na Mahamud Mohammed Daud kutoka skuli ya Kiponda na kwa upande wa Biashara ni Abdulrahman Abdalla Mkanjima kutoka skuli ya Sekondari ya Biashara, Ziada Bakar Hemed kutoka skuli ya Chasasa na Yussuf Haji Kombo Skuli ya Sekondari ya Biashara.

Kwa upande wa wanafunzi bora Kidato cha Nne mwaka 2019 ni Raudhat Abdalla Mselem kutoka skuli ya Fidel Castro, Khadija Hafidh Said kutoka skuli ya Lumumba na Marco Abdrea Masabuda kutoka Skuli ya Mikindani.

Hafla hiyo, ilihudhuriwa na viongozi mbali mbali wa vyama vya siasa na Serikali akiwemo Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd, Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM Dk. Hussein Ali Hassan Mwinyi, Kaimu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Haroun Ali Suleiman.

Wengine ni  Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahaya Mzee, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Abdallah Juma Mabodi  pamoja na viongozi wengine, wanafunzi, walimu na waalikwa mbali mbali ambao walihudhuria ambapo kikundi cha Taarab asilia cha Rahatul zamaan kilitumbuiza hafla hiyo.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.