Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein Amemtumia Salamu za Pongezi Rais Xi Jinping Kutimiza Miaka 71 ya Taifa Hilo.

 


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amemtumia salamu za pongezi Rais wa Jamhuri ya Watu wa China Xi Jinping kwa kutimiza miaka 71 tokea kuasisiwa Taifa hilo.

Katika salamu hizo, Rais Dk. Shein alimpongeza Rais Xi Jinping kwa kutimiza miaka hiyo 71 ya Taifa hilo tokea kutangazwa rasmi na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Kikomunisti cha Jamhuri ya Watu wa China  Hayati Mao Zedong mnamo Oktoba 1, mwaka 1949.

Rais Dk. Shein katika salamu hizo alieleza kuwa kwa niaba ya Serikali ya Mmapnduzi ya Zanzibar na wananchi wake wote anatoa salamu za pongezi kwa Rais Xi Jinping pamoja na wananchi wa Jamhuri ya Watu wa China kwa kutimiza miaka 71 tokea kuasisiwa kwa taifa hilo.

Salamu hizo zilieleza kuwa wananchi wa Zanzibar wataendeleza umoja na mshikamano walionao kati yao na ndugu zao wa Jamhuri ya Wawatu wa China kwa lengo la kuendeleza uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo kati ya pande mbili hizo.

Aidha, katika salamu hizo Rais Dk. Shein alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na wananchi wake wote wameridhishwa na mafanikio ya kiuchumi na kijamii yaliopatikana na Jamhuri ya Watu wa China  katika miaka 71 chini ya uongozi thabiti na wenye mikakati madhubuti wa Chama cha Kikomunisti cha China (CCP).

Rais Dk. Shein aliongeza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zote kwa pamoja zinajivunia uhusiano na ushirikiano uliopo kati yao na Jamhuri ya Watu wa  China. Hivyo, Rais Dk. alisisitiza kuwa uhusiano na ushirikiano huo wa kihistoria utaendelea kudumishwa na kuimarishwa kwa manufaa ya pande zote mbili.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein alimtakia kiongozi huyo, familia yake pamoja na wananchi wote wa Jamhuri ya Watu wa China afya njema na mafanikio zaidi katika kuuimarisha uchumi wao ambao umekuwa ukiimarika siku hadi siku sambamba na maendeleo yaliopo.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.