RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amesema CCM ndio chama pekee chenye
uwezo wa kuongoza Dola na hivyo
amewataka wananchi na wanachama wa chama hicho kutofanya utani kukiweka
madarakani.
Dk. Shein ambae ni Makamo Mwenyekiti
wa CCM Zanzibar, amesema hayo katika mkutano wa Kampeni ya chama hicho uliofanyika
katika uwanja wa Jamhuri Makunduchi, Mkoa wa Kusini Unguja.
Aliwataka wananchi hao kumchaguwa Dk.
Hussein Ali Mwinyi, Wabunge, Wawakilishi na Madiwani wote wa CCM, akibainisha
hatua hiyo itafanikisha azma yake ya kumkabidhi kijiti cha uongozi mgombea
huyo.
Alisema kuna ulazima wa kumchagua Dk.
Hussein Mwinyi, ikiwa ni hatua sahihi katika kudumisha Muungano wa Tanzania pamoja na kuimarisha Mapinduzi ya Zanzibar ya
1964.
Alisema sifa za mgombea huyo hazina
shaka, zikithibitishwa kutokana na historia ya utumishi wake katika nafasi
mbali mbali serikalini.
Alisema umuhimu wa kuendeleza umoja na
mshikamano ni jambo linaloeleweka vyema na mgombea huyo, hivyo akatowa wito kwa
wanachama na wananchi wote kumchagua.
Alisema kwa kushirikiana na Rais John
Pombe Magufuli, viongozi hao watashirikiana kuendeleza Muungano pamoja na
kudumisha Mapinduzi ya 1964.
Rais Dk. Shein aliwataka vijana
kufahamu historia ya Zanzibar kuwa inatokana na Mapinduzi ya 1964, hivyo
akabainisha kuwa maendeleo yote nchini yanatokana na Mapinduzi hayo, hivyo
akasema wana wajibu wa kuyalinda na
kuyadumisha.
Aidha,
aliwataka kukataa rai za baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani
watakaowaomba kuvipigia kura vyama vyao.
Alisema Mapinduzi ndio ngao ya Zanzibar
sambamba na Muungano kuwa muhimili mkuu
wa uhai Taifa hilo, hivyo ni lazima mambo hayo mawili yawepo, akibainisha
Muungano huo umetokana na muungano wa Serikali mbili huru, jambo alilosema limebainishwa
katika Ilani ya CCM.
Aliwataka wananchi na wanachama
waliohudhuria mkutano huo kuwakataa
wapinzani kwa kigezo kuwa watalitia
Taifa kwenye misukosuko na akasisitiza umuhimu wa kudumisha sifa ya Mkoa
huo ya kuwa ngome ya Chama hicho.
Nae, Mgombea wa Kiti cha Urais kupitia
CCM Hussein Ali Mwinyi alisema katika kufanikisha dhana ya Uwajibikaji kazini,
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar awamu ya nane inakusudia kuangalia stahiki zote
za wafanyakazi katika utumishi wa umma.
Alisema Serikali itahakikisha stahiki
zote za wafanyaakazi zinatolewa kwa wakati pamoja na kuimarishwa kwa kuwaongezea mishahara kadri
uchumi utakavyoimarika.
Alisema kuna umuhimu wa haki na wajibu
kwenda sambamba , hivyo Serikali italenga kusimamia haki hizo pamoja na kusimamia
uwajibikaji kikamilifu.
Alieleza kuwa dhamira ya kuimarisha
sekta mbali mbali ikiwemo za kijamii, kunalenga kuhakikisha kila mmoja
anawajibika kwa nafasi yake, hivyo akasisitiza umuhimu wa wafanyakazi
kuondokana na wizi, rushwa na ubadhirifu wa
mali ya umma.
Katika hatua nyengine, Dk. Mwinyi
alieleza vipaumbele vya serikali ya awamu ya nane Mkoani humo kuwa ni pamoja na
kuajiri walimu wa Sayansi na Hesabati ili kuondokana na upungufu wa walimu
katika fani hizo, sambamba na kujikita katika utoaji wa mafunzo katika vyuo vya
amali ili kukidhi soko la ajira.
Alisema katika kuimarisha sekta ya Ustawi
wa jamiii, Serikali itaendeleza kazi nzuri iliofanywa na serikali ya awamu ya
saba kwa kuendelea kuwapatia wazee posho la pensheni jamii la shilingi 20,000
kwa mwezi pamoja na kuangalia uwezekano wa kuwaongezea kadri hali ya uchumi
itakavyoimarika.
Alieleza kuwa makundi ya walemavu na
wanawake nayo yatapewa kipaumbele ili kuleta ustawi wa jamii.
Alisema pamoja na kazi nzuri ya
kuipandisha daraja hospitali ya Makunduchi kuwa ya Wilaya iliofanywa na
serikali ya awamu ya saba, Serikali ya awamu ya nane itaendelea kuiimarisha kwa
kuiongezea wafanyakazi, vifaa pamoja na kuongeza bajeti ya gharama za madawa na
vifaa tiba.
Akigusia changamoto mbali mbali zinazowakabili
wananchi wa Mkoa huo, Dk. Mwinyi alisema Serikali atakayoiongoza itaimarisha
miundombinu ya barabara mbali mbali ziliomo mkoani humo, ikiwemo ile ya Tunguu
– Makunduchi yenye urefu wa kilomita 48 pamoja ya Kitogani – Paje (kilomita 11).
Alisema sekta ya utalii ambayo ni
muhimu katika kuimarisha uchumi itaimarishwa kwa kuhakikisha unawanufaisha
wananchi na kubainisha kuwa utaratibu utaandaliwa ili kuwawezesha vijana kupata
ajira,
Alisema vijana watapatiwa mafunzo ili
kwenda sambamba na mahitaji pamoja na wananchi na wajasiriamali kupata soko la
uhakika katika maeneo hayo kutokana na
bidhaa wanazozalisha.
Alisema Serikali itahakikisha wananachi wote wanapata haki zao, hususan
katika suala la umiliki wa ardhi na hivyo kuondokana na uonevu unaofanywa na
baadhi ya watendaji wasio waaminifu pamoja na kuhakikisha wawekezaji wanalipa
fidia katika maeneo wanayowekeza.
Dk. Mwinyi alisema changamoto za
upatikanji wa huduma za maji safi na
salama, umeme pamoja na afya katika maeneo mbali mbali ya Mkoa huo
zitashughulikiwa na kuzimariha kwa kuongeza wafanyakazi, kuwekewa vifaa, kujenga miundombinu pamoja na kujenga matangi
mapya.
Mapema, Katibu wa CCM Taifa, Dkt. Bashiru
Ali Kakurwa, alisema Mkoa wa Kusini Unguja una rekodi ya kufanya vizuri katika
chaguzi mbali mbali zilizopita, hivyo akawataka wanachama wa Chama hicho
kuendeleza utamaduni huo, kwa kigezo kuwa ni ngome ya CCM.
Alisema mgombea wa Chama hicho Dk. Hussein
Ali Mwinyi ana sifa kubwa miongoni mwa wanachama wote 16 waliogombea nafasi
hiyo, sambamba na kumpongeza kwa kuendeleza utamaduni wa Maraisi waliotangulia
wa kuwatembelea wazee.
Alimpongeza Dk. Shein kwa kuasisi
utoaji wa Pensheni jamii kwa wazee wote waliofikia umri wa miaka 70,
akibainisha hatua hiyo ni jambo kubwa la
kihistoria na kusema Serikali zote mbili zitaendelea kuzisimamia Serikali zake
kuliendeleza jambo hilo.
Aidha, Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja,
Ayoub Mohamed Mahamoud, ambae pi ni Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Mkoa huo, akigusia
utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa kipindi cha 2015-2020, alisema sekta ya Afya
imeimarika sana Mkoani humo, akibanisha kabla ya kipindi hicho wananchi walikuwa
wakipata huduma za afya katika Hospitali ya Cottage, ambapo hivi sasa
imepandishwa daraja na kuwa Hospitali ya Wilaya, hatua iliyoimarisha upatikanaji
wa huduma bora za afya.
Alisema katika kipindi hicho ujenzi wa
Hospitali ha Rufaa katika eneo la Binguni Wilaya Kati umeanza, ikiwa ni juhudi
za Serikali katika kuimarisha sekta ya
afya nchini.
Vile vile alisema sekta ya Elimu nayo
imeimarika, ambapo pamoja na mambo mengine ujenzi wa Chuo cha Amali Makunduchi
ulikamilika na hivyo kuwa tayari kwa ajili ya kuendesha mafunzo mbali mbali
yatakayowawezesha vijana kuweza kujitegemea.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kusini
Unguja, Ramadhan Abdalla Ali “Kichupa” alimhakikishia mgeni rasmi kuwa wanachama wa
Chama hicho katika Majimbo yote matano Mkoani
humo watampigia kura mgombea wa Chama hicho na kupata ushindi mkubwa.
Katika mkutano huo, viongozi mbali
mbali wa CCM walishiriki, akiwemo Rais mstaafu wa Jamuhuri ya Muungano wa
Tanzania mzee Ali Hassan Mwinyi, Makamo
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd, Katibu mkuu wa CCM Taifa Dkt.
Bashiru Ali Kakurwa,Waziri Kiongozi mstaafu Shamsi Vuai Nahodha pamoja na wake
wa Viongozi wakuu.
Abdi Shamna,
Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777476982. Fax: 024
2231822
E-mail: abdya062@gmail.com
No comments:
Post a Comment