Habari za Punde

OFISI YA MUFTI ZANZIBAR YATOA TAMKO DHIDI YA SHEIKH ISSA PONDA

Katibu wa Mufti sheikh Ali Mfaume akizungumza na Waandishi wa habari huko Ofisini kwake Mazizini wakati  akitoa tamko dhidi ya Sheikh Issa Ponda  juu ya kauli ya uchochezi aliyotoa katika jukwaa la siasa,kushoto ni Naibu Mufti Zanzibar Mahmoud Musaa Wadi na kulia ni Mkuu wa Fatwa Zanzibar Sheikh Thabit Nouman Jongo.

Na Sabiha Khamis   Maelezo     20/10/2020.

Viongozi wa dini nchini wametakiwa kutoichanganya dini na siasa jambo ambalo litapelekea uvunjifu wa amani na utulivu katika nchi hasa katika kipindi cha siasa na kuelekea  katika uchaguzi mkuu.

Hayo yamesemwa na Katibu wa Mufti sheikh Khalid Ali Mfaume wakati akizungumza na Waandishi wa Habari Ofisini kwake Mazizini kufuatia kauli ya Katibu Mkuu wa Shuraa ya Maimamu Tanzania Bara Sheikh Issa Ponda aliyoitoa katika majukwaa ya kisiasa akisema maneno yaliyokinyume na taratibu za kidini.

Alisema kuwa sheikh huyo alipanda katika jukwaa la kisiasa na kusema kuwa waislamu watanzania wamekubaliana kumpa kura mgombea urais wa CHADEMA  Tundu Lissu na endapo waumini hao hawatompa kura mgombea huyo mungu hatowaelewa na dua zao hazitokubaliwa, jambo ambalo ni kinyume na taratibu na mandiko ya dini.

Aidha sheikh huyo alinukuliwa kutoa  kauli za kuwataka waumini kutokukaa kimya endapo matokeo ya uchaguzi yatakuja kinyume na matarajio yao ya kisiasa jambo amabalo ni kinyume na taratibu za nchi zilizoekwa.

Ofisi ya Mufti Zanzibar imesema haitambui kabisa makubaliano hayo na wala haikubali kauli hiyo nakuwataka viongozi wa dini kutochanganya  dini na matakwa ya kisiasa kwani ni  kinyume na muongozo wa vitabu vya dini na ni kitendo cha uchochezi na  uvunjifu wa amani.

“Tanzania haikuanzisha mfumo wa vyama vya kisiasa kwa misingi ya kidini na mtazamo wa kwamba dua hazitokubaliwa na Mungu hatotuelewa ni upotoshaji wa kidini na mtazamo huo haukubaliki katika dini” alisema Katibu Mufti.

Aidha alisema kuwa kila raia ana uhuru wa kuchagua kiongozi anaemtaka ambae anahisi atatekeleza mahitaji yake na kwa upande wa dini inawataka viongozi kuhubiri amani, usawa na upendo na kuacha kuhubiri mambo ambayo yatalea utofauti baina ya watu.

Vile vile alieleza kuwa Sheikh Ponda si msemaji wa Waislam Tanzania, mwenye dhamana ya kusimamia Waislamu wote kwa Tanzania bara  ni Mufti wa Tanzania   bara Sheikh Abubakar Zubeir na kwa upande wa Zanzibar Mufti wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabi.

Ofisi ya Mufti Zanzibar imewataka Walimu wa Madrasa kuwapa mapumziko wanafunzi wa madrasa zote kwa muda wa wiki moja kuanzia tarehe 25 mwezi huu hadi tarehe 02 mwezi ujao kutokana na harakati za uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi huu.

Aliwataka wazazi na walezi kuwadhibiti watoto wasizurure ovyo ili kuwaweka katika hali ya amani na kuwaepusha na vitendo viovu.

Aidha aliwataka Maimamu, Masheikh na Makhatibu wa Zanzibar kuitumia Ijumaa kuiombea dua nchi ili ipate amani na ufanyike uchaguzi katika hali ya amani na usalama.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.