Na Miza Kona Maelezo
Wizara ya Afya Zanzibar imeanza kutoa huduma za uchunguzi virusi vya maradhi ya Corona kwa wananchi na wageni wanaoingia na kutoka nchini kwa kutumia mashine maalum ya kuchunguzia maradhi ya mripuko.
Akizungumza na Waandishi wa habari, Mkurugenzi Huduma za Uchunguzi wa Maradhi katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja Dk. Msafiri Marijani amesema kifaa hicho kinauwezo wa kuuchunguza zaidi ya sampuli 90 kwa wakati mmoja na kutoa majibu masaa 24.
Ameeleza kuwa Wizara tayari imeshatoa mafunzo kwa wafanyakazi sita kutoka kwa wataalamu walioleta mashine hiyo kwa ajili ya matumizi ya kifaa hicho hadi sasa imeshachunguza sampuli 260 na kutoa majibu sahihi.
Dk. Marijani amesema mashine hiyo pia itasaidia kuchunguza maradhi mbali mbali ya mripuko ikiwemo ebola na
chikungunya ikiwa yatatokezea nchini
Aidha ameishukuru Serikali na washirika wa Maendeleo kwa kusaidia kifaa hicho na kuweza kupunguza usumbufu wa kupeleka sampuli nje ya Zanzibar.
Kifaa hicho kiliwasili nchini mwezi Mei mwaka huu kutokana na kuingia kwa mripuko wa maradhi ya Corona na kuanza kutumika mwezi huu.
No comments:
Post a Comment