Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed aendelea na ziara ya kuzitembelea Taasisi na Idara zilizo chini ya Afisi yake

Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya Bibi Kheriyangu Mgeni Khamis akimpatia Taarifa za Tume hiyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdulla alipofanya ziara kwenye Taasisi hiyo.
Mh. Hemed akipata maelezo kutoka moja ya Vitengo vya Kazi vya Tume ya Taifa ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya Zanzibar hapo Kilimani Mjini Zanzibar.

 Mkurugenzi wa Idara ya Watu wenye Ulemavu Zanzibar Bibi Abeda Rashid Abdulla akitoa Taarifa ya Utendaji kazi wa Idara hiyo wakati walipotembelewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman akiwa katika ziara ya kuzitembelea Taasisi na Idara zilizo chini ya Afisi yake.

Picha na – OMPR – ZNZ.


Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inapendelea kuona Watu wenye Ulemavu Nchini wanakuwa mfano bora katika Uwajibikaji ndani ya Taifa hasa ikizingatiwa kwamba jitihada zao wanazochukuwa zimelenga kujikomboa katika harakati zao za Kimaisha za kila siku.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdulla alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na Uongozi wa Idara ya Watu Wenye Ulemavu hapo Makao Makuu ya Idara hiyo yaliyopo Migombani wakati akiwa kwenye ziara ya kuzitembelea Idara na Taasisi zilizo chini ya Afisi yake.

Alisema Watu Wenye Ulemavu wana nguvu na uwezo mkubwa wa kufanya kazi kama walivyo Watu wengine kwenye uwajibikaji, lakini kinachohitajika kwa Jamii inayowazunguuka ni kukubali kuwapa dhamana kwa mujibu wa Maarifa, Elimu na Vipaji walivyobarikiwa.

Hata hivyo Mh. Hemed alisema Watu hao wamekuwa wakikabiliwa na changamoto mbali mbali ndani ya Jamii hasa lile la kudhalilishwa kijinsia na matokeo yake hubaguliwa na kudharauliwa mambo yanayokwenda kinyume na haki za Binaadamu.

Alisema wakati Serikali ikiendelea na wajibu wake katika kuzingatia utatuzi wa changamoto za Watu hao wenye Mahitaji Maalum, Wananchi pamoja na Taasisi za Kijamii lazima zifikie maamuzi ya kuondosha manyanyaso hayo kwa kuwapatia fursa wanazostahiki ili nao wajihisi kuwa sehemu ya Jamii.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amefarajika na mafanikio makubwa yaliyopatikana ndani ya Idara ya Watu wenye Ulemavu na kuwashukuru Watendaji kwa kazi kubwa wanazozifanya katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.

Mheshimiwa Hemed ameuhakikishia Uongozi na Watendaji wa Idara hiyo kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itajikita katika kuiongezea nguvu Taasisi hiyo inayosimamia Watu wenye Mahitaji Maalum ili iendelee kuwajibika kama ilivyopangiwa.

Akitoa Taarifa Mkurugenzi wa Idara ya Watu wenye Ulemavu Zanzibar Bibi Abeda Rashid Abdulla alisema Watendaji wa Idara hiyo wamebadilika kimfumo kuelekea katika teknolojia ya Kisasa ya Habari na Mawasiliano yanayowapa uharaka wa kutekeleza majukumu yao.

Bibi Abeda alisema Mfumo huo umewawezesha Watendaji wa Idara hiyo kusajili Watu wenye Ulemavu katika maeneo mbali mbali ya Unguja na Pemba kuanzia ngazi ya Shehia jambo ambalo lilikuwa ikichukuwa muda mrefu na wakati mwengine ipo changamoto ya kuyafikia baadhi ya maeneo hasa Vijijini.

Alisema yapo mafanikio makubwa yanayoendelea kuifaidisha Idara na Watendaji wake akitolea mfano Jumuiya za Watu wenye Ulemavu zilizojengewa uwezo wa kusajili moja kwa moja Watu wenye Ulemavu kwenye maeneo yote.

Mkurugenzi huyo wa Idara ya Watu wenye Ulemavu alitanabahisha wazi kwamba tatizo la uhaba wa Gari za kufuatilia masuala mbali mbali ya Idara hiyo limekuwa changamoto kubwa inayochelewesha baadhi ya Kazi za Taasisi hiyo.

Mapema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla alitembelea Tume ya Taifa ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya Zanzibar  iliyopo Kilimani ambapo Mkurugenzi Mtendaji wa Tume hiyo Bibi Kheriyangu Mgeni Khamis alisema wapo Vijana Elfu 3,161 waliofanikiwa kuacha kutumia Dawa za kulevya hadi Mwaka 2019.

Bibi Kheriyangu alisema marekebisho ya baadhi ya Sheria na kanuni kwa ushirikiano wa pamoja wa Kitaifa, Kikanda na Kimataifa ndio iliyopelekea mafanikio hayo ya kuiokoa nguvu kazi ya Vijana kuendelea kutumbukia ndani ya janga la matumizi ya Dawa za Kulevya.

Alisema ni jambo la faraja kuona Sheria nambari Tisa nayo imefanyiwa marekebisho kwa kuipa Mamlaka Tume ya Taifa ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya kutaifisha Mali na Fedha za Watu wanaojihusisha na Biashara ya Dawa za Kulevya.

Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdulla alisema Viongozi na Watendaji wanapaswa kuendelea kushirikiana kwa karibu katika kuhakikisha mapambano dhidi ya kukabiliana na wimbi la Dawa za Kulevya yanafanikiwa.

Alisema kasi ya utumiaji wa dawa za Kulevya Nchini inaweza  kupungua kwa kiasi kikubwa endapo wale watakaojihusisha na Uingizaji, Usambazaji na Uuuzaji wa Dawa za Kulevya watataifishwa mali zao.

Mheshimiwa Hemed aliwataka Watendaji kujiepusha na ushawishi  unaotokana na ulaghai wa baadhi ya wahusika wa Biashara ya Dawa za Kulevya kwa vile wasipozingatia hayo wanaweza kuwa Watumwa watakaporidhia hali hiyo mbaya.

Alisema Uadilifu, Uaminifu na Uzalendo ni mambo yanayopaswa kuzingatiwa na wale wote wanaopewa dhamana ya kuzisimamia Kesi zote zinazowakabili Wafanya biashara wa Dawa za Kulevya.

 

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.