Habari za Punde

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali afanya ziara ya kushtukiza Chuo cha Kiislamu Kiuyu Pemba

 Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe Simai Mohammed Said alipowasili Chuuo cha Kiislamu kiunyu katika ziara ya kushtukiza leo
 Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe Simai Mohammed Said akiendelea na ukaguzi wa Chuo cha kiislamu kilichopo Kiuyu Pemba ziara ambayo ni kutekeleza maagizo 13 ya Rais wa Zanzibar Dk Hussein Ali Mwinyi
 Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe Simai Mohammed Said alipowasili Skuli ya Sekondari Madungu

Na Mwandishi wetu 

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe Simai Mohammed Said amefanya ziara ya kushtukiza katika Chuo cha Kiisalam kilichopo Kiuyu na kuangalia maendeleo ya uezekaji wa mapaa ya majengo ya Chuo hicho.

Akizungumza katika ziara hiyo, Mhe Simai amesema ni hatua nzuri iliyofikiwa kutokana na hali ilivyokuwa hapo awali kwani paa zilikuwa zinavuja na kuagiza sehemu zilizobaki kuendelea kuzimalizia ili kuwasaidia Wanafunzi kusoma kwa utulivu zaidi.
Mhe Simai ameelezea kutoridhishwa na hali ya usafi katika maeneo ya dakhalia za Chuo hicho na kuutaka uongozi kulisimamia kwa kina ili kuepusha maradhi ya mripuko yanayoweza kutokea.
Pia amewataka Walimu na Wafanyakazi wote wa Wizara hiyo kukubaliana na wakati uliopo na kuwataka kubadilika kwa kufuata sheria na kanuni ziliopo ili kuleta maendeleo katika sekta ya Elimu nchini.
Katika hatua nyengine Mhe Simai akiwa na Afisa Mdhamini Wizara ya Elimu Pemba mwalimu Mohammed Nassor alimpatia maelezo juu ya ujenzi wa uzio wa Chuo hicho ambao ulikuwa umesitishwa kutokana na mgogoro na wananchi ambao kwa sasa upo katika hatua za mwisho kumalizika ili ujenzi wa uzio huo uendelee kwa lengo la kuzuia uvamizi wa eneo la Chuo hicho.
Wakati huo huo Mhe Simai alikagua Walimu wa madarasa ya Msingi wanaoendelea na mitihani yao katika ukumbi wa Chuo hicho pamoja na katika Skuli ya Maandalizi Kiuyu.
Nae Mkuu wa Chuo cha Kiislamu cha Kiuyu mwalimu Mkasha Sharif Hamad amemshukuru Mhe Simai kwa ujio wake ndani ya Chuo hicho na ameahidi kuyafanyia kazi yale yote aliyoyaagiza ili kwenda sambamba na maagizo ya Mhe Rais wa Zanzibar.
Mapema Mhe Simai amefanya ziara katika Skuli ya Sekondari Madungu na kuwapa nasaha Wanafunzi wa kidato cha nne wanaoendelea na mitihani yao kwa kuwataka kufuata sheria zote za mitihani ili waweze kufaulu vizuri.
Pia Mhe Simai alitumia muda huo kwa niaba ya wafanyakazi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, kuwatakia kheir na mafanikio mema Wanafunzi wote katika mitihani yao.
Ziara hiyo ina lengo la kutekeleza maagizo 13 waliopewa Mawaziri wote walioteuliwa wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Mhe Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Hussein Ali Mwinyi wakati alipowaapisha Mawaziri aliowateua.
Mhe Simai anefanya ziara kwa Wanafunzi wa Skuli ya Sekondari Madungu wanaofanya mitihani ya kidato cha nne, Kukagua maendeleo ya uezekaji wa paa la Chuo cha Kiislam Kiuyu, kituo cha Ubunifu wa Sayansi (School hub) ya Kiuyu, pamoja na Chuo cha Mafunzo ya Amali Daya Mtambwe ilichopo Mkoa wa kaskazini Pemba.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.