Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe Hemed Suleiman Abdulla Atowa Mkono wa Pole Kwa Familia ya Marehemu Abubakar Khamis Bakar.

Katibu wa Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Khalid Ali Mfaume wa kwanza Kulia aliyesimama akisoma dua wakati Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdulla alipofika Mbweni kuifariji Familia ya Mwanasiasa Mkongwe wa Zanzibar Marehemu Abubakar Khamis Bakar.


Na.Othman Khamis.OMPR.                                                                                                                        

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdallah ametoa mkopo wa pole na kuifariji Familia ya Mwanasiasa Mkongwe wa Zanzibar Bwana Abubakar Khamis Bakar aliyefariki Dunia baada ya kuugua kwa muda mfupi na kuzikwa kwenye makaburi ya Familia Kianga Wilaya ya Magharibi A.

Marehemu Abubakari Khamis Bakar aliyesomea  fani ya Sheria pia ni Mwakilishi Mteule wa Baraza la Wawakilishi katika Uchaguzi Mkuu uliopita hivi karibuni Jimbo la Pandani Mkoa wa Kaskazini Pemba kupitia Chama cha ACT Wazalendo.

Akiifariji Familia hiyo hapo Nyumbani kwake Mbweni pembezoni mwa Jiji la Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla alisema kifo cha Marehemu Abubakar Khamis kiecha pengo sio tu kwa chama chake bali ni kwa Wananchi wote wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

Alisema hii inatokana na mchango wake wa kushiriki katika Kamati za Maridhiano ya Kitaifa yaliyopelekea Zanzibar kuwa na mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa uliotokana na hitilafu za Kisiasa zilizovikumba Vuisiwa vya Zanzibar kwa muda mrefu.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliitaka na kuiomba familia hiyo ya Marehemu Abubakar kuwa na moyo wa subra katika kipindi hichi kigumu cha msiba wa Mpendwa wao.

Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar nayo imeguswa na Msiba huo ambao utaendelea kukumbukwa kwa muda mrefu.

Akitoa shukrani kwa niaba ya Familia ya Marehemu Mwanasiasa huyo Mkongwe wa Zanzibar Mwanafamilia Omar Makame kupitia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliishukuru Serikali ya Mapinduzi  kwa kuwafariji Wanafamilia hao kutokana na msiba huo mzito kwao.

Bwana Omar kupitia fursa hiyo aliiomba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na ile ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kuendelea kuhakikisha kwamba ule Umoja na Mshikamano uliopo ndani ya Maisha ya Wananchi unaendelea kuimarika.

Alisema Wananchi bado wana  tabia ya kuishi kwa pamoja kunakotokana na Historia ya hulka yao inayopaswa kuendelea kulindwa na Serikali ili maisha yao yaendelee kama kawaida.

Marehemu Abubaka Khamis Bakar ameacha Kizuka Mmoja, Watoto Watano na Wajukuu 11.

Allah amjaalie Marehemu Abubakar Khamis Bakar safari njema aliyotangulia mbele ya haki. Amin.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.