Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi Akutana na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC )

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi (kushoto) akizungumza na Viongozi wa Tume ya Uchaguzi  Zanzibar (ZEC) alipokutana nao leo Ikulu Jijini Zanzibar kwa ajili ya kuwashukuru na kuwapongeza kwa kazi ya kufanikisha vyema  Uchaguzi Mkuu uliopita hivi karibuni.[Picha na Ikulu]. 10/11/2020.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi (katikati) akimsikiliza  Mkuu wa Brigedi ya Nyuki Zanzibar Fadhil Omar Nondo (aliyesimama) alipokuwa akitoa neno la kumshukuru mbele ya Rais mara baada ya Viongozi Wakuu wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama walipofika Ikulu Jijini Zanzibar leo kwa ajili ya  kupongezwa kwa  kufanikisha kusimamia vyema kwa  Zoezi la Uchaguzi Mkuu uliopita hivi karibuni.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi (kulia) akiagana na Mwenyekiti wa  Tume ya Uchaguzi  Zanzibar (ZEC) Mhe.Jaji Mkuu Mstaafu Hamid Mahmoud Hamid baada ya mazungumzo na kuishukuru na kuipongeza Tume ya Uchaguzi  Zanzibar (ZEC) leo Ikulu Jijini Zanzibar kwa  kufanikisha vyema  Uchaguzi Mkuu uliopita
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi (katikati) akizungumza na Viongozi wa Tume ya Uchaguzi  Zanzibar (ZEC) alipokutana nao leo Ikulu Jijini Zanzibar kwa ajili ya kuwashukuru   na kuwapongeza kwa kazi ya kufanikisha vyema  Uchaguzi Mkuu uliopita hivi karibuni.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi (katikati) akizungumza na Viongozi Wakuu wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama leo Ikulu Jijini Zanzibar kwa ajili ya kuwashukuru  na kuwapongeza kwa  kufanikisha kusimamia vyema kwa  Zoezi la Uchaguzi Mkuu uliopita hivi karibuni.[Picha na Ikulu].10/11/2020.

STATE HOUSE ZANZIBAR

OFFICE OF THE PRESS SECRETARY

PRESS RELEASE

Zanzibar                                                                  10.11.2020

---

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ametoa shukurani na pongezi kwa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), kwa kufanikisha vyema Uchaguzi Mkuu uliopita wa mwaka 2020.

Shukurani hizo na pongezi amezitoa leo Ikulu Jijini Zanzibar wakati alipokutana na uongozi wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), wakiwemo Makamishna wa Tume hiyo wakiongozwa na Mwenyekiti wake  Jaji Mstaafu Hamid Mahmoud pamoja na Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi Thabit Idarous Faina.

Katika maelezo yake Rais Dk. Hussein Mwinyi aliueleza uongozi huo wa Tume ya Uchaguzi (ZEC) kwamba ameona haja ya kuwaita viongozi hao baada ya kukamilika mchakato wa uchaguzi kwa azma ya kuwashukuru na kuwapongeza kwa kazi kubwa na nzuri waliyoifanya.

Alieleza kuwa Tume hiyo imetekeleza vyema kazi zake hivyo, kuna kila sababu ya kuishukuru na kuipongeza kwa mafanikio hayo makubwa yaliopatikana licha ya baadhi ya changamoto zilizojitokea katika kipindi hicho cha uchaguzi.

Hivyo, Rais Dk. Hussein aliwaahidi viongozi hao kuwa ataendelea kutoa ushirikiano wake kwao na kusisitiza kwamba milango yake iko wazi akimaanisha kwamba yuko tayari kushirikiana nao na kuwasikiliza wakati wowote.

Nao viongozi hao wa Tume ya Uchaguzi (ZEC) walimpongeza Rais Dk. Hussein kwa uungwana wake mkubwa alioufanya wa kuwaita na kuwapongeza sambamba na kuwashukuru kwa kazi kubwa ya kufanikisha uchaguzi mkuu uliopita.

Viongozi hao wa (ZEC), kwa upande wao walichukua fursa hiyo kumpongeza Rais Dk. Hussein Mwinyi kwa kuchaguliwa kwa kura nyingi na kumshukuru kwa kumaliza kazi hiyo nzito kwa salama.

Waliongeza kuwa wananchi wote wamefurahi kwa ushindi mkubwa alioupata Rais Dk. Hussein Mwinyi na kueleza jinsi walivyoupokea ushindi huo kwa matumaini makubwa, baraka na matarajio kutoka kwa kiongozi  huyo.

Pamoja na hayo, viongozi hao walimuombea kwa MwenyeziMungu Rais Dk. Hussein Mwinyi kuyatekeleza vyema yote aliyowaahidi wananchi wakati wa Kampeni huku wakisisitiza kuwa wataendelea kushirikiana nae kwani kazi waliyopewa na Taifa wamejitahidi kuimamilisha ipasavyo.

Viongozi hao pia, walieleza mashirikiano makubwa waliyoyapata kutoka kwa uongozi wa vikosi vya ulinzi na usalama hali ambayo ilipelekea uchaguzi huo kufanyika kwa amani, utulivu na usalama mkubwa.

Mwenyekiti wa Tume hiyo Uchaguzi alitoa pongezi zake maalum kwa Rais Dk. Hussein Mwinyi na kueleza kwamba ushindi wa kishindo alioupata umetokana na Sera na hotuba zake alizokuwa akizitoa kwa wananchi ambao wamepata matumaini makubwa.

Nae Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee alitoa pongezi kwa viongozi wote wa Tume hiyo ya Uchaguzi Zanzibar (NEC), na kueleza kwamba mashirikiano waliyoyaonesha ndio yalikuwa chachu ya mafanikio yaliopatikana

Wakati huo huo, Rais Dk. Hussein Mwinyi alikutana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Zanzibar na kuvipongeza vikosi vyote vya Ulinzi na Usalama kwa kazi nzuri waliyoifanya katika kipindi chote cha kabla, wakati wa uchaguzi na baada ya uchaguzi.

Uongozi wa Kamati hiyo kwa upande wao nao walitoa pongezi kwa Rais Dk. Hussein kwa kuwaita na kwenda kuwapongeza na kuwashukuru jambo ambalo walieleza kufarajika nalo kutokana na kuwajali na kuwathamini.

Hivyo, viongozi hao wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama walimuahidi Rais Dk. Hussein Mwinyi kwamba wataendeleza utu wao, uaminifu na nidhamu waliyonayo kwa hali ya juu zaidi sambamba na kufuata maelekezo kutoka kwa viongozi wao wakuu.

Walieleza kwamba ushindi huo umeonesha ni namna gani wananchi wanaimani na Rais wao wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Mwinyi, Serikali yao ya Awamu ya Nane anayoiongoza pamoja na chama kilichoshika hatamu.

Pia, viongozi hao wa Vikosi vya ulinsi walipongeza mashirikiano makubwa waliyoyapata kutoka kwa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), wakati wote wa uchaguzi Mkuu uliopita wa 2020.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

1 comment:

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.