Habari za Punde

WANAOISHI NA VIRUSI VYA UKIMWI WASEMA ARV'S ZA SASA ZINAWAPENDEZESHA

 Na Dixon Busagaga-Kilimanjaro

BARAZA la Taifa la Watu wanaosihi na Virusi vya Ukimwi (NACOPHA) limepongeza hatua ya serikali kuendelea kutoa bure Dawa za kufubaza virusi vya Ukimwi kwa watu wanaoishi na ugonjwa huo ,dawa zinazotajwa kuongeza seli za kupambana na maambukizi (CD4) kwa haraka ukilinganisha na dawa zilizokuwa zikitolewa hapo awali.

Hayo yameelezwa na mwenyekiti wa Baraza la Taifa la watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi nchini (NACOPHA) Leticia Mourice wakati wa kongamano lililoshirikisha viongozi wa dini mbalimbali katika kijiji cha jamii kilichopo uwanja wa Mandela mjini Moshi ambao maadhimisho ya siku ya Ukiwmi Duniani yanafanyika kitaifa.

“Nina ishukuru Serikali kwa kuendelea kutupatia dawa bure ambazo kwa kweli dawa hizo ni nzuri sana ,ni tofauti na zile ambazo tulikuwa tuna meza siku za nyuma ,zinapandisha CD4 haraka ,zinaboresha afya haraka ,yaani pongezi nyingi sana kwa serikali “ alisema Leticia.

Alisema uwepo wa kijiji cha jamii katika maadhimisho ya siku ya ukimwi duniani kumechangia wengi wa washiriki kufahamu mambo mengi kuhusu Ukimwi kutokana na mijadala katika kijiji hicho ambapo pia washiriki walipata nafasi ya kuuliza maswali .

“Naamini kabisa kila mmoja wetu amevuna chochote ,tumekuwa na viongozi  wa dini kwenye mjadala na wamewaeleza vijana na watu wazima kwamba miili yetu ni hekalu na hili hekalu linapaswa kuwa safi na tunapaswa kuitunza miili yetu .”alisema Leticia .

“Sambamba na hilo tumepata maelezo mazuri kabisa kutoka kwa viongozi wetu wa dini ,sasa kutokana na majadiliano haya mnatakiwa kuwa mashujaa wa kusema hapana ,sihitaji,sipendi kwa habari ya ngono isiyo salama na msiende kuwa mashujaa wa kuwa na watu wengi wa kucheza nao shoo.”aliongeza Leticia.

Mkurugenzi wa Tume ya taifa ya kudhibiti Ukimwi (TACAIDS) Dkt Leonard Maboko akatumia jukwaa hilo kuwaeleza viongozi wa dini kuwa mlango uko wazi kwa tume anayoingoza endapo kuna masuala mbalimbali ambayo wanegpenda kuyafahamu zaidi.

Kongamano hilo ni muendeleze wa mambo kadhaa yanayofanyika ikiwa ni muendelezo wa maadhimisho ya siku ya Ukimwi Duniani ambayo kitaifa yanafanyika mjini Moshi katika uwanja wa shule ya msingi Mandela uliopo kata ya Pasua.

Mwisho

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.