Habari za Punde

CCM Zanzibar yapongeza uteuzi wa Maalim Seif kuwa Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar

NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar  Dk.Abdulla Juma  Saadalla, akizungumza na Waandishi wa Habari juu ya mwenendo wa kisiasa nchini.

 NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar  Dk.Abdulla Juma  Saadalla, akizungumza na Waandishi wa Habari juu ya mwenendo wa kisiasa nchini.


NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.

CHAMA cha Mapinduzi (CCM) kimempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi DK. Hussein Ali Mwinyi kwa kutimiza matakwa makubwa ya katiba ya Zanzibar kwa kumchagua Maalim Seif Sharif Hamad kuwa Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar.

Kimesema, kitendo hicho kimedhihirisha nia ya dhati ya Rais wa Zanzibar na Chama cha Mapinduzi katika kutii matakwa ya kikatiba kwenye uongozi wa nchi.

Hayo yalisemwa jana na Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi DK. Abdulla Juma Sadala (Mabodi) wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye Ofisi kuu za Chama hicho Kisiwandui Mjini Unguja.

Alisema, kama ilivyoeleza katiba kwenye ibara ya tisa kuwa Zanzibar itaendeshwa katika muono na mwenendo wa serikali ya kitaifa, na kwa kuwa DK. Mwinyi ameapa kwa katiba ya Zanzibar basi ilimbidi kabisa kutimiza matakwa hayo ya kikatiba.

Aidha alisema, ni wazi kwamba jambo hilo limethibitisha kauli zake za kuwa yeye ni muumini wa utawala bora, umoja wa wazanzibar na mwenye kuthamini haki na wajibu wa viongozi na wananchi wa Tanzania hususani Zanzibar.

 

"Tunachukua nafasi hii kumpongeza Rais kwa kuthibitisha na kutimiza matakwa hayo kwa sababu ametoa kiu za wananchi na za wale ambao walikuwa hawana uhakika wanini kinaendelea," alisema.

Mbali na hayo Mabodi alisema, Chama kinaunga mkono jitihada za Rais Mwinyi, hususani mawaziri alowateua katika kuleta mageuzi makubwa ya kiutendaji.

"Kwa kweli mageuzi haya wengi wetu hatukutegemea kutokea kwa haraka kama hivi, DK. Mwinyi amechagua Mawaziri ambao wanafanya kazi usiku na mchana katika mfumo mkubwa sana ambao ulipotea kwa muda mrefu," alisema.

Mabodi alisema, kuongoza kwa kushuhidia mwenyewe kinachofanyika ni jambo pekee ambalo Rais hataweza kudanganywa wala kuzungushwa kwani kwenye ukweli ataona ukweli na uongo pia ataona.

Lakini vile vile alisema, Chama kinaamini kuwa viongozi waandamizi wengine watafata njia hiyo adhimu ili iwe njia bora na ndiyo reli muhimu ya utendaji wa kazi katika ngazi zote.

"Hakika tunampongeza Rais kwa kuchagua viongozi wepesi kujituma, kufatilia na kutoa maamuzi na wakati mwengine maamuzi huwa magumu lakini yasiyo na muhali," alisema.

Aidha alisema, ndani ya Chama cha Mapinduzi kuna Halmashauri za chama katika ngazi za tawi, wadi, jimbo, wilaya, mkoa na Taifa na kwmaba ngazi zote hizo kwa mpangilio maalumzitaendelea kuisimamia serikali katika majukumu yake waliyopewa na chama ili wananchi wafaidi matunda ya Mapinduzi.

DK. Mabodi pia alisema, Chama kinamuhidi Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi DK. Hussein Ali Mwinyi kuwa kitamuunga mkono katika harakati zake zote za mageuzi, yeye binafsi na viongozi waandamizi aliowachagua wa ngazi zote.

Alisema, wanaamini kwamba viongozi wa Chama cha upinzani watashirikiana na Rais wa Zanzibar na viongozi wengine wote katika mafanikio makubwa ya kimaendeleo ya wazanzibar kwa ujumla.

Mbali na hayo Mabodi alisema, CCM inapinga vikali sana hatua zozote ambazo itakuwa zinachukuliwa katika kudhoofisha mwenendo wa kutoleta maendeleo kwa wananchi.

Aidha alisema, CCM kitaunga mkono jitihada za kubainisha ubadhirifu wowote wenye chembe chembe za ufisadi kila inapogundulika, na kuwaomba wananchama na wananchi wote kwa ujumla kuibua bila kusima maswala yoyote yenye vituko vya ubadhilifu, uonevu na ufisadi.

Alisema, ili kuleta maendeleo ya pamoja na ili kuwa na uongozi shirikishi na maendeleo yenye kujumuisha watu wote maswala haya lazima kwa pamoja kuyapinga.

 

"Chama chetu kinaamini kwamba umoja wa wazanzibar ndiyo nguzo pekee ya kudumisha amani na utulivu na maendeleo ya kishindo yanayotegemewa kutokea kwa muda mfupi yataletwa na umoja wetu, na uwajibikaji," alisema.

Aidha alisema, Chama cha Mapinduzi kinawaasa na kuwahusia wazanzibar wote kwa ujumla walio ndani na nje ya nchi kuunga mkono jitihada za serikali ya awamu ya nane kushirikiana kaye katika kuleta maendeleo ya kiuchumi na ya kijamii.

Aliwasihi wananchi kuendeleza umoja wa kindugu na mashirikiano huku wakijipanga kuanza upya safari ya kuijenga Zanzibar mpya kupitia falsafa ya Uchumi wa Buluu(Blue Economy). 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.