Habari za Punde

Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Zanzibar ashirikiana na UVITAZ kuwashauri watumiaji wa madawa ya kulevya

Katibu wa Ushirika wa Vijana wenye Taaluma Zanzibar (UVITAZ) Hakimu Omar Kulukulu akizungumza na watumiaji wa madawa ya kulevya juu ya suala zima la kujiunga na Methadol Clinic iliyopo Kidongo Chekundu ili kupata matibabu ya kuweza kuachana na madawa hayo hafla iliyofanyika Jumbi kwa Mapwenti Zanzibar.
Mwenyekiti  wa vijana Taifa Khamis Rashid Kheir akizungumza na watumiaji wa madawa ya kulevya juu ya suala zima la madhara ya madawa ya kulevya huko Jumbi.
Mtumiaji wa madawa ya kulevya Mahmoud Haji Shaka akitoa changamoto zinazowapelekea kuendelea kutumia madawa hayo mara walipotembelewa na Mwenyekiti wa vijana Zanzibar Khamis Rashid Kheir akiambatana na wajumbe wa  Ushirika wa Vijana wenye Taaluma Zanzibar (UVITAZ) huko  Jumbi Zanzibar.
 Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Zanzibar   Khamis Rashid Kheir (katikati)  akiwa na wajumbe wa  Ushirika wa Vijana wenye Taaluma Zanzibar (UVITAZ) katika ziara ya kuwakagua watumiaji wa madawa ya kulevya katika vigenge mbalimbali.

Mraibu Mayunga Shaaban akielezea jinsi alivyoachana na madawa ya kulevya ambayo aliyatumia kwa miaka kumi na tano na kuwataka watumiaji kuachana na madawa hayo huko Jumbi Zanzibar.

Mwenyekiti  wa vijana Taifa Khamis Rashid Kheir akizungumza na watumiaji wa madawa ya kulevya juu ya suala zima la madhara ya madawa ya kulevya huko Jumbi.

PICHA NA FAUZIA MUSSA /MAELEZO ZANZIBAR

Na Sabiha Khamis      Maelezo   26/12/2020.

Baraza la Vijana Zanzibar likishirikiana na Ushirika wa Vijana wenye Taaluma Zanzibar (UVITAZ) amewataka vijana wanaotumia madawa ya kulevya kujiunga na Cliniki ya Methadone Clinic Kidongo Chekundu ili kupata tiba na kuondokana na majanga hayo.

Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Zanzibar Khamis Rashid Kheir wakati wa ziara ya kutembelea vijiwe vya waathirika wa madawa ya kulevya katika maeneo mbali mbali ya Mkoa wa Mjini Magharibi.

Amesema vijana walioathirika madawa ya kulevya wajiunge na kituo cha Kidongo chekundu ili kuweza kutumia dawa ambazo zitawasaidia kupunguza na kuondoa kabisa hamu ya uvutaji wa madawa ya kulevya.

Amesema wahanga wa madawa hayo (waraibu) wana nafasi kubwa ya kuleta maendeleo ya nchi hivyo ipo haja kujiweka tayari kuachana madawa hayo ili kuweza kufanya kazi na kujipatia kipato halali.

“Waraibu wana nafasi ya kujitoa katika janga hili kwani zipo fursa nyingi za kupeleka maisha yao mbele kwa kujinasua na matumizi ya madawa” alisema Mwenyekiti.  

Aidha amesema ingawa kuna changamoto nyingi zinazowakabili wahanga hao lakini Baraza la Vijana Zanzibar lipo tayari kuwasaidia kwa njia moja au nyengine ili kuhakikisha vijana hao wanaachana na uraibu huo pamoja na kujiunga katika Ushirika wa (UVITAZ).

Kwa upande wake Katibu wa (UVITAZ) Hakimu Omar Kulukulu amesema Shirika hilo lipo tayari kuhamasisha vijana walioathirika ili kujitoa katika janga hilo na kupeleka mbele gurudumu la maisha yao.

Amesema Shirika linatoa elimu kwa wahanga wa madawa hayo pamoja na kuwapa nafasi ya kuwaendeleza kwa wale wenye vipaji kwa kuweza kuvitumia vipaji hivyo.

Vile vile amewataka watumiaji hao kufanya uwamuzi wa kuacha madawa hayo ili kuepukana na athari za madawa ya kulevya ikiwemo wizi wa mali za watu na kuishi maisha hatarishi.

Nae mmoja wa wanachama wa (UVITAZ) Mayunga Shaaban ambae pia alikuwa muhanga wa madawa ya kulevya amesema wathirika hawana elimu ya kutosha kuhusina na uachaji wa madawa  hivyo amewataka kujiunga na Kliniki hio ili kujitoa katika janga hilo.

Pia wahanga hao wamesema wapo tayari kuachana na madawa hayo kwani wamepoteza uaminifu katika jamii na maisha yao kuwa katika hatari.

Katika ziara hio ya siku moja Baraza la Vijana na Ushirika wa Vijana wenye Taaluma Zanzibar wametembelea maeneo mbali mbali ya vijiwe vikiwemo Jumbi kwa Sheikh Mapwenti, Kiembe samaki, Amani, Jang’ombe na Kianga.

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.