Habari za Punde

Dk. Hussein Ali Mwinyi aahidi kutekeleza ahadi yake ya kupambana na rushwa, ubadhilifu wa mali ya umma na uzembe SUZA

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameahidi kutekeleza ahadi yake ya kupambana na rushwa, ubadhilifu wa mali ya umma na uzembe katika Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) ambacho hivi sasa anakiongoza rasmin.

Rais Dk.Mwinyi aliyasema hayo leo katika hotuba yake aliyoitoa katika sherehe za mahafali ya 16 ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), mara baada ya kutawazwa rasmin kuwa Mkuu wa Chuo hicho, hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Dk. Shein, ndani ya kampasi ya Chuo hicho huko Tunguu, Mkoa wa Kusini Unguja. Hafla iliyohudhuriwa na viongozi mbali mbali wa vyama na Serikali akiwemo Makamo wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad.

 

Katika hotuba yake, Rais Dk. Hussein Mwinyi alisema kuwa akiwa Mkuu wa Chuo, atafuatilia kwa karibu makusanyo ya ada, ruzuku kutoka Serikalini na kwa wahisani, matumizi ya thamani ya vitu vinavyonunuliwa pamoja na vianzio mbali mbali.

 

Rais Dk. Mwinyi aliutaka uongozi wa Chuo hicho kusimamia vizuri na kwa umakini na uadilifu rasilimali za chuo, watunze vizuri nyaraka mbali mbali zenye kuonesha mali zinazomilikiwa na chuo zikiwemo hati miliki za ardhi, nyumba na majengo mengineyo huku akihiza haja ya kufanyiwa matengenezo nyumba na majengo ya chuo na nyumba zote zinakaliwa wakati wote.

 

Aliwataka wahadhiri na wafanyakazi kufanya kazi kwa bidii na nidhamu kwa kuzingatia sheria na maadili yanayoongoza kazi zao pamoja na kujiandaa kitaaluma ili wawe wanapanda daraja kwa kulingana na taratibu zilizopo.

 

Alisisitiza umuhimu wa usafi wa mazingira na kuutaka uongozi kuhakikisha unaweka mazingira katika Kampasi zao ili yaweze kuvutia kwa kuwa na miti ya vivuvi na bustani huku akiwataka kujiandaa kwani hivi karibuni atafanya ziara katika Kampasi zote kuangalia hayo yote aliyoyasema.

 

Aidha, Rais Dk. Hussein mwinyi alisema kuwa Rais Mstaafu wa Awamu ya Saba Dk. Ali Mohamed Shein ameonesha njia kwamba Chuo hicho ni miliki ya Watu wa Zanzibar na kinaendeshwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa hivyo ni lazima kifundishe masomo yanayoendana na mahitaji ya wananchi kiuchumi na kijamii.

 

Kwa msingi huo Rais Dk. Mwinyi aliitaka (SUZA) kuwa mfano wa Chuo chenye mitaala na programu mbali mbali za ufundishaji zinazozingatia mahitaji ya nchi pamoja na sera na mipango ya maendeleo ya muda mfupi, muda wakati na muda mrefu.

 

Alieleza kuwa (SUZA)ina kazi kubwa ya kufundisha wataalamu wa kutosha wanaohitajika kusimamia uchumi wa Buluu.

 

Rais Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kumpongeza Rais Mstaafu Dk. Shein kwa kumkabidhi Chuo kikiwa kimepiga hatua kubwa za maendeleo katika kipindi cha miaka 10 cha uongozi wake ambapo miundombinu imeimarika, idadi ya Kampasi na idadi ya wanafunziimeongezeka, wahadhiri na wafanyakazi pamoja na programu zinazofundishwa na hadhi na sifa ya elimu inayotolewa imekuwa.

 

Rais Dk. Hussein ameitaka (SUZA) kuandaa utaratibu mzuri zaidi wa kufanya tafiti na kuweka mkazo wa matumizi ya tafiti katika maeneo mbali mbali yanayohusu uchumi wa Buluu na sekta nyengine za uchumi.

 

Alieleza kuwa ni kazi ya (SUZA) kwa kushirikiana na taasisi nyengine za Elimu ya Juu ikiwemo Tume ya Sayansi na Teknolojia Tanzania (COSTECH) kufanya tathmini ya tafiti zilizofanywa ndani ya kipindi cha 2015-2020 na uhalisia wa tafiti hizo kwa mahitaji ya nchi.

 

Hivyo, alieleza kuwa Zanzibar ina haja ya kuwa na ajenda mpya ya utafiti wa Kitaifa na kusisitiza kuachana na tabia ya kutegemea wahisani hata katia mambo muhimu ya maendeleo wanayoweza kufanywana Wazanzibari wenyewe.

 

Alisisitiza kwamba atahakikisha wataalmu wote walioajiriwa na wanaolipwa mishahara wanatumia taaluma na uzoefu wao kwa faida ya wananchi na wao wenywe kwani chuo hicho ni lazima kiongeze kasi katika kufanya tafiti mbali mbali.

 

Alieleza kuvutiwa na dhamira iliyokuwepo ya kuifanya (SUZA) kuwa ni Oxford ya Kiswahili na iwe chimbuko la wataalamu, waandishi na malenga wa mashairi na kwa kushirikiana na Baraza la Kiswahili la Zanzibar (BAKIZA), iwe ni kitovu cha kutoa Kamusi zinazopendwa na zinazoaminika katika lugha ya Kiswahili.

 

Aidha, ameutaka uongozi wa (SUZA), kuandaa mikakati mizuri ya kulinda lahaja  za Kizanzibari, kuwa wepesi, kubuni misamiati na istilahi zinazohitajika ili kuweza kwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia.

 

Rais Dk. Mwinyi alitoa kazi kwa uongozi wa (SUZA)kushirikiana na uongozi wa (BAKIZA) katika kuandaa mikakati na kufanya jitihada za kutafuta ajira za Kiswahili nje ya nchi kwa ajili ya wataalamu mbali mbali waliopo Zanzibar.

 

“Lazima tuwe na mipango ya kutumia hazina yetu, kiswahili, katika kukuza ajira pamoja na kuhakikisha kwamba tuna mipango imara ya kufundisha na kukieneza katika mataifa mengine”.

 

Pia, alieleza haja ya kwa Chuo hicho kuangalia upya mitaala yake na mbinu za ufundishaji kwani wawekezaji wengi katika sekta ya utalii wanapenda kuajiri wafanyakazi kutoka nje ya Zanzibar jambo ambalo yeye haridhishwi kuona hali hiyo licha ya kuwa wahitimu wengi wanatolewa katika eneo hilo lakini bado vijana hawapati ajira.

 

Kwa wale walioomba mikopo ya elimu ya juu na wakapata, Rais Dk. Mwinyi aliwahimiza wawe tayari kulipa deni liliopo kwa kuzingatia sheria na makubaliano yaliyo katika mikataba waliyoijaza.

 

Aliwapongeza wahitimu wote na kuwataka kujiepusha na vishawishi na anasa vinavyoweza kuathiri masomo yao huku akieleza kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuweka mkazo kwenye sekta ya elimu katika ngazi zote kwa misingi na dhamira ile ile ya waasisi wa Mapinduzi matukufu ya Zanzibar ya Januari 12. 1964.

 

Wakati huo huo, Rais Dk.Mwinyi alimtunuku Shahada ya Heshima ya Udaktari wa Falsafa katika Sayansi za Tiba, Rais Mstaafu wa Zanzibar Awamu ya Saba Dk. Ali Mohamed Shein na kumpongeza huku akisisitiza kwamba wananchi wa Zanzibar wataendelea kumkumbuka kwa ubunifu wake wa kuanzisha mambo mazuri ambayo watu wengi walihisi hayawezekani.

 

Rais Mstaafu Dk. Shein nae wka upande wake akitoa salamu zake za shukurani aliupongeza uongozi wa Chuo hicho kwa kumtunuku Shahada hiyo ambayo itaendelea kumpa hadhi huku akieleza imani yake kwamba Rais Dk. Mwinyi atakiendeleza vyema chuo hicho.

 

Nae Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Simai Mohamed Said alieleza jinsi Wizara yake itakavyoendelea kumuunga mkono Rais Dk. Hussein Mwinyi pamoja na kueleza mikakati mbali mbali iliyowekwa na Wizara hiyo ili iweze kuleta manufaa katika sekta ya elimu.

 

Mapema Makamu Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) Dk. Zakia Mohammed Abubakar alimueleza Rais Dk. Mwinyi kwamba Jamii ya Chuo hicho cha (SUZA), iko tayari kwa moyo mkunjufu kufanya kazi na yeye kwa kufuata kikamilifu ushauri na maelekezo katika kukiendeleza chuo hicho.

 

Aidha, alimpongeza Rais Mstaafu Dk. Ali Moahmed Shein ambaye alikuwa Mkuu wa Chuo tokea mwaka 2010 hadi 2020 kwa juhudi zake kubwa za kukitumikia chuo hicho ambapo kwa juhudi hizo ndipo chuo hicho kikaamua kumtunuku Shahada ya Udaktari wa Falsafa katika Sayansi za Tiba kwa sababu sheria inaruhus kufanya hivyo.

 

Makamu Mkuu huyo wa (SUZA), alieleza kuwa mwaka huu chuo hicho kinawahitimu jumla ya wanafunzi 1524 ambao Rais Dk. Mwinyi  aliwatunuku vyeti vyao kutoka programu 56 zinazofundishwa na  chuo hicho cha (SUZA).

 

Mkuu huyo alieleza kwamba katika wahitimu wa mwaka wa masomo 2019/2020 jumla ya wanafunzi ambao wamefanya vizuri zaidi ni 41 ambao kati yao 24 (52%) ni wanawake na 17 (48%) ni wanaume na wanafunzi bora ni watatu.

 

Katika hafla hiyo, Rais Dk. mwinyi aliwatunuku wanafunzi 244 wa ngazi ya Cheti, 799 kwa ngazi ya Stashahada, 453 kwa ngazi ya Shahada na 28 kwa ngazi ya Uzamili huku akiwakabidhi vyeti na zawadi wanafunzi bora watatu akiwemo Nassra Suleiman Mohammed wa Shahada ya Kwanza aliyepata GPA 4.9, Ali Abdalla Moh’d wa Stashahada aliyepata GPA 5.0 na Hanafi Abdallah Moh’d aliyepata GPA 4.9.

 

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.