Habari za Punde

Tuunge Mkono Juhudi za JPM kwa Maendeleo Endelevu- Malecela

Na Jonas Kamaleki, Dodoma

Waziri Mkuu Mstaaf Mhe.John Samuel Malecela amewataka watanzania kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli katika juhudi za kujenga  uchumi imara na endelevu.

Mzee Malecela ameyasema hayo hivi karibuni katika mahojiano maalum na Maafisa wa Idara ya Habari (MAELEZO) jijini Dodoma.

“Tumsaidie na kumuunga mkono Rais Magufuli kwa kazi kubwa na nzuri anayofanya ya kujenga uchumi usiyoyumbishwa ili Tanzania izidi kupiga hatua kubwa kimaendeleo”, alisema Malecela.

Alitaja sifa za Rais Magufuli kuwa ni kiongozi bora, mzalendo, mpinga rushwa na ufisadi, mwenye maono na mwenye kujali  wananchi  sambamba na kusimamia  katiba na sheria za nchi.

Katika kuudhimisha miaka 59 ya Uhuru na 58 ya Jamhuri, Mzee Malecela alitoa tathmini yake ya kimaendeleo na kusema kuwa wakati  Tanganyika inapata uhuru uchumi wa nchi ulikuwa chini sana ukitegemea kuuza nje mazao ghafi kama vile kahawa, pamba, chai, mkonge, korosho na pareto. Kwa sasa uchumi umekua kwani hata mazao yanayosafirishwa au kuuzwa nje yanakuwa yamechakatwa hivyo kuyaongezea thamani.

Aidha, alieleza kuwa nchi imepiga hatua kwa kuboresha miundombinu ya barabara, reli na umeme pamoja na kuboresha elimu na huduma za afya.

“Wakati tunapata uhuru tulikuwa na madaktari watanzania watano tu ambao ni Dkt. Kyaruzi, Mtawali, Mwaisela, Mwanjisi na Dkt. Akimu kwa sasa tuna madaktari maelefu kwa maelefu, haya ni maendeleo makubwa yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 59 ya uhuru” alisema Malecela.

Mzee Malecela aliipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa kukuza uchumi na kuiwezesha Tanzania kufikia uchumi wa kati na kuongeza kuwa watanzania inabidi wafanye kazi kwa bidii na kushiriki shughuli zote za maendeleo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.