Habari za Punde

Wananchi Jimbo la Welezo watakiwa kulinda miundombinu ya maji safi na salama isihujumiwe

MBUNGE wa jimbo la Welezo Mhe. Maulid Saleh Ali, akishirikiana na wananchi kuchimba mitaro ya kupitisha mipira ya kusambaza maji safi na salama katika jimbo la Welezo.

 BAADHI ya Wananchi, mafundi wa ZAWA na viongozi wa jimbo la Welezo akiwemo Mbunge wa jimbo hilo Maulid Saleh Ali, wakishauriana masuala mbalimbali ya kuimarisha huduma za maji katika jimbo hilo.


NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.

MBUNGE wa jimbo la Welezo Mhe. Maulid Saleh Ali amewashauri wananchi wa jimbo hilo kulinda miundombinu ya maji safi na salama isihujumiwe.

Ushauri huo ameutoa wakati akishirikiana na wananchi kuchimba mitaro ya kupitisha mipira ya maji safi na salama katika jimbo hilo, alisema miundombinu hiyo inahitaji ulinzi wa kutosha kutoka kwa wananchi wenyewe.

Alisema miundombinu hiyo ikilindwa vizuri itaendelea kutoa huduma ya maji hatua itakayosaidia wananchi kupata maji kwa uhakika na kumaliza changamoto hiyo.

Mhe.Maulid aliwahakikishia wananchi wa jimbo hilo kwamba  atashirikiana na viongozi mbalimbali wa chama na serikali kutatua changamoto zinazowakabili wananchi hao hasa ya upungufu wa maji safi na salama.

‘’Ahadi yangu kwa wananchi wa jimbo hili ni kwamba tutajitahidi kutatua changamoto zenu hatua kwa hatua ili kila mwananchi apate huduma bora za kijamii na kiuchumi, kwani mlituamini na kutupatia ridhaa ili tuwaletee maendeleo’’. Alisema Mhe.Maulid.

Pamoja na hayo aliwasihi wananchi kujenga utamaduni wa kujitokeza kwa wingi kushiriki katika shughuli za maendeleo ya jimbo hilo kwa kutoa nguvu kazi ili kuharakisha harakati za maendeleo.

Alisema maji ni huduma muhimu inayotakiwa kupatikana muda wote kutokana na mahitaji yake kuwa ni ya lazima kwa  wananchi.

Alitoa wito kwa wananchi hao pindi watakapopata huduma ya maji kwa uhakika waanze kulipia ili kusaidia gharama za uendeshaji zinafanywa na mamlaka ya maji Zanzibar(ZAWA).

Akizungumzia utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020/2025 alisema kwa upande wa jimbo hilo viongozi wake wamejipanga vizuri katika kuwapelekea wananchi huduma muhimu zikiwemo miradi mbalimbali ya maendeleo itakayowanufaisha wananchi wa makundi yote.

Alieleza kwamba maendeleo hayo yatafikiwa kutokana na uwepo wa ushirikiano baina ya viongozi wa jimbo,wananchi na serikali kwa ujumla.

Naye Diwani wa Wadi ya Welezo Ramadhan Ali juma,alisema jimbo hilo linakabiliwa na tatizo la upungufu wa maji kwa muda mrefu  ambalo kwa sasa linatafutiwa ufumbuzi wa kudumu.

Alisema katika harakati hizo za kurejesha huduma za maji katika jimbo hilo hakuna mwananchi aliyechangishwa fedha bali gharama zote za matengenezo zimetolewa na uongozi wa jimbo kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maji Zanzibar.

Kwa upande wake Sheha wa Shehia ya Welezo Mohamed Amour Khamis, alifafanua kwamba tatizo la ukosefu wa maji katika jimbo hilo linatokana na uchakavu wa mipira ya maji ambapo kwa sasa wameweka mipira mipya ya kusambaza maji hayo.

Naye mkaazi wa jimbo hilo Juma Soud Juma, alisema wananchi wataendelea kuwa walinzi na waangalizi wa miundombinu hiyo isihujumiwe na baadhi ya watu wasiopenda maendeleo.

Akitoa ufafanuzi wa kitaalamu fundi kutoka mamlaka ya Maji Zanzibar(ZAWA)Talib Abdallah Mohamed, alikemea tabia ya baadhi ya watu wasiokuwa waaminifu wanaunga maji kinyume na taratibu katika laini za maji na kusababisha ukosefu wa maji kwa wananchi wengi.

Alisema wao hao wakibainika watachukuliwa hatua za kisheria kwani wanachofanya ni wizi na uharibifu wa miundombinu ya umma kwani serikali inatumia fedha nyingi kununua vifaa mbalimbali vya maji na vinaharibiwa na watu wachache kwa maslahi yao binafsi.

Aidha aliahidi kuwa matengenezo hayo yatakamilika muda wowote kuanzia sasa na kutoa fursa ya upatikanaji wa maji bila usumbufu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.