Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais Mhe Hemed akutana na kufanya mazungumzo na Uongozi wa Bodi ya Jumuiya ya Makampuni yanayotoa huduma ya Utalii Zanzibar {ZATO}.

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla akizungumza na Uongozi wa Bodi ya Jumuiya ya Makampuni  yanayotoa huduma ya Utalii Zanzibar {ZATO} Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Bodi ya Jumuiya ya Makampuni  yanayotoa huduma ya Utalii Zanzibar {ZATO} baada ya kumaliza mazungumzo yao.

Picha na – OMPR – ZNZ.

Na Othman Khamis, OMPR

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuheshimu jitihada kubwa zinazochukuliwa na Taasisi na Watu waliojikubalisha kujitolea Kizalendo katika kuona Taifa linapiga hatua kubwa Kiuchumi na hatimae kuleta Ustawi  kwa Wananchi walio wengi Nchini.

Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla Ofisini kwake Vuga wakati alipofanya mazungumzo na Uongozi wa Bodi ya Jumuiya ya Makampuni  yanayotoa huduma ya Utalii Zanzibar {ZATO}.

Mheshimiwa Hemed alisema haipendezi kuona wapo Watu waliojitolea  kuijengea Heshima Serikali na Nchi baadae wakaonekana kama hawana thamani kwa sababu ya utashi wa baadhi ya Watendaji wa Umma wenye kuzingatia Zaidi maslahi yao  binafsi.

Alisema yule mwenye dhamana ya Umma akitolea mfano wa Sekta ya Utalii ambayo kwa sasa ndio ngao ya Uchumi wa Taifa na haoni uchungu wala umuhimu wa jukumu alilopewa, Serikali haitosita kuachana naye katika kuamua kubakia na jukumu hilo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameonyesha kufarajika kwake na jitihada kubwa zinazochukuliwa na Viongozi na Watendaji wa Jumuiya ya Makampuni  yanayotoa huduma ya Utalii Zanzibar {ZATO} ndani ya Sekta ya Utalii na kuahidi kwamba Serikali itaangalia njia itakayosaidia Jumuiya hiyo kwa vile tayari imeshaonyesha Uzalendo mkubwa wa kuitangaza Zanzibar Kiutalii.

Alisema kwa vile Taifa limeshajihakikishia kuimarisha Sekta ya Uchumi wa Buluu ambapo na Utalii ukiwa sehemu ya Uchumi huo, kamwe halitaweza kuendelea kubakia na Sheria na Kanuni zisizo Rafiki katika mifumo halisi ya uendeshaji wa Sekta hizo.

Akitoa Ufafanuzi wa kundi la Mapapasi wanaotembeza Watalii Mh. Hemed alisema mfumo unaotumiwa hivi sasa unalikosesha Taifa Mapato kutokana na msongamano wa Kundi hilo na Taifa litalazimika lichukuwe hatua za haraka kuanza kuziba mwanya huo.

Mapema Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Jumuiya ya Makampuni  yanayotoa huduma ya Utalii Zanzibar {ZATO} Hassan Mzee alisema Jumuiya hiyo hivi sasa iko sehemu nzuri Kimkakati hasa katika Kanuni naTaratibu zilizopo zinazowapasa Wazalendo kupata ajira ambayo kwa sasa zinachukuliwa na Wageni.

Alisema Zato ni Wawekezaji Wazawa iliyoanzishwa kuepuka washindikizaji ambapo kutokana na Mikakati yake inahitaji kuungwa mkono ya wadau pamoja na Serikali ili ifanikishe malengo yake.

Wakichangia Kikao hicho nao Wajumbe wa Bodi hiyo wamefafanua mambo mbali mbali yanayochangia kuvuja kwa Mapato ya Taifa ikiwemo changamoto kubwa ya ukosefu wa ushirikiano  kwa baadhi ya Taasisi ndani ya Miundombinu ya Sekta ya Utalii ambapo baadhi yake hushindwa kuwajibika ipasavyo.

Walipendekeza uwepo wa vibali vitakavyotumika na wadau wote wa Sekta ya Utalii katika mfumo wa Teknolojia ya Kisasa itakayoweka wazi masuala yote ikiwemo Udhibiti wa Mapato pamoja pamoja na Mapapasi wa Kigeni wanaotumia fursa hiyo kinyume na Sheria za Utalii zilizopo Nchini.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.