Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi Amewapongeza Wananchi wa Zanzibar kwa Utayari Wao Kuendeleza Umoja na Kuacha Mifarakano.

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Waumini wa Masjid Raudha Daraja bovu Jijini Zanzibar baada ya kumaliza kwa Sala ya Ijumaa iliofanyika katika Masjid hiyo leo.8/1/2021.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyiamewapongeza wananchi wa Zanzibar kwa utayari wao wa kuendeleza umoja na kuacha mifarakano.

Alhaj Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo huko katika Msikiti Raudha uliopo Darajabovu, Jimbo la Shauri Moyo Mkoa wa Mjini Magharibi wakati akitoa salamu zake kwa Waislamu mara baada ya kukamilisha Sala ya Ijumaa

Katika salamu zake hizo Alhaj Dk. Mwinyi alisema kuwa kwa upande wao wakiwa viongozi wa kisiasa tayari wameonesha nia na njia kwa kuingia katika makubailiano ya kujenga Serikali ya Umoja wa Kitaifa lengo ni kuwafanya wafuasi wao wa kiitikadi za kichama kuacha mifarakano na kuwa wamoja.

Alhaj Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kutoa pongezi na shukurani kwa wananchi wa Zanzibar kwa kukamilisha uchaguzi kwa salama na amani kwani ni uzoefu uliopo kwamba wakati wa uchaguzi amani hutoweka.

Akieleza kuhusu umuhimu wa umoja, Alhaj Dk. Mwinyialisema kuwa kuna umuhimu wa kuwepo kwa umoja wa kitaifa kwani vitabu vyote vya dini vimesisitiza suala la umoja hasa ikizingatiwa kwamba umoja hupelekea hata mambo ya kidunia yakiwemo maendeleo kuimarika.

Alisema kuwa amani na umoja ndio msingi wa maendeleo hivyo, kuna kila sababu ya kuidumisha kwa maslahi ya nchi na wananchi wote wa Zanzibar.

Aidha, Alhaj Dk. Mwinyi alisema kuwa katika kampeni za uchaguzi uliopita aliomba kuwa kiongozi kwa lengo la kutaka kuwatumikia wananachi kwa kuwaletea maendeleo yao.

Alisema kuwa Serikali anayoioongoza imejipanga vyema katika kuwaletea wananchi maendeleo ya haraka kutokana na kuwepo kwa amani na umoja wa kitaifa.

Aliongeza kuwa atahakikisha juhudi za makusudi zinachukuliwa katika kutekeleza ahadi zilizoahidiwa kwa azma ya kuyafanya maisha ya Wazanzibari kuwa bora zaidi.

Sambamba na hayo, Alhaj Dk. Mwinyi alisema kuwa huduma zote muhimu za kijamii zilizoahidiwa zikiwemo afya, elimu, maji, barabara na nyenginezo zitatekelezwa na kuwataka wananchi kuendelea kuomba dua ili kupatikana wepesi wa kuyatekeleza.

Alhaj Dk. Mwinyi alilipokea ombi la Waumini wa Msikiti huo wa kutaka kumaliziwa jengo la msikiti wao na kuahidi kuwasaidia ili msikiti huo uweze kusalika vyema na Waumini wote wa eneo hilo waweze kupata nafasi nzuri ya kuweza kufanya ibada zao.

Alhaj Dk. Mwinyi aliushukuru uongozi wa msikiti huo kwa mapokezi makubwa aliyoyapata pamoja na mapenzi yao ya kutaka kusali na yeye japo kwa siku moja.

Mapema Sheikh Ali Fakih Abdallah akitoa hotuba ya sala ya Ijumaa alieleza kwamba hatua na juhudi zilizochukuliwa na Rais Dk. Mwinyi za kuimarisha umoja, mshikamano kwa kuleta maridhiano katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa anayoingoza ambayo imeondosha mifarakano.

Alisema kuwa jambo hilo la kheri lilianza kufanywa na kiongozi wa Waislamu Mtume Muhammad (S.A.W), kwa kuyaungaisha makabila yaliyokuwa hasimu ya wakati huo Aus na Khazraj na hatimae kuwa wamoja.

Waumini hao pia, walimpongeza Alhaj Dk. Mwinyi kwa uongozi wake bora ambao amekuwa akiwajali watu wote wakiwemo wanyonge katika kuwapigania haki zao huku Waumini hao wakitumia fursa hiyo kumuombea dua ili atekeleze vyema majukumu yake ya Urais.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.