Habari za Punde

Wajasiriamali Zanzibar wataka kuondolewa vikwazo wanapopeleka bidhaa Bara

Mkurugenzi Idara ya Dawa na Vipodozi wa ZFDA Bora Lichanda akiwaeleza wajasiriamali (hawapo pichani) mchakato wa Taasisi hiyo kuingia makubaliano na Taasisi ya Viwango Tanzania (TBS) ili kurahisisha kazi za upelekaji bidhaa Tanzania Bara bila usumbufu huko Ukumbi wa Mama na Mtoto Kidongechekundu Mjini Zanzibar.
Mfanya Biashara kutoka Kampuni ya Visiwani Enterprises LTD Hassan Nahoza (alievaa kanzu nyeupe) akieleza Changamoto zinazowakabili katika Biashara zao hafla iliyofanyika Ukumbi wa Mama na Mtoto Kidongechekundu Zanzibar.
 Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi kutoka Jumuiya ya Wafanyabiashara Wanawake Zanzibar (ZWCC) Zeyana Ahmed Kassim akitoa ushuhudi wa vikwazo vinavyowakabili wajasiriamali wa Zanzibar wanapopeleka bidhaa zao Tanzania Bara katika mkutano uliofanyika  Ukumbi wa Mama na Mtoto Kidongechekundu Mjini Unguja.

 Afisa Mipango kutoka ZFDA akitoa Ufafanuzi kwa Wafanyabiashara katika Kikao cha pamoja cha Wajasiriamali na Taaasisi hiyo katika Ukumbi wa Mama na Mtoto Kidongechekundu Zanzibar.

Picha na Maryam Kidiko / Maelezo Zanzibar.


Na Rmadhani Ali - Maelezo     09.012021

Wajasiriamali wa Zanzibar wamezishauri Taasisi zinazosimamia usalama wa Chakula na Vipodozi ambazo sio za Muungano kuzitafutia ufumbuzi changamoto zinazowakabili wanaposafirisha bidhaa zao Tanzania Bara.

Wameeleza kilio chao wakati Viongozi wa Wakala wa Chakula na Dawa Zanzibar (ZFDA) walipokutana na Wajasiriamali hao katika Ukumbi wa Mama na Mtoto Kidongochekundu kuwaeleza mchakato wa kuingia makubaliano na Taasisi ya Viwango Tanzania (TBS) ili kuwarahisishia shughuli zao.

Katibu wa Jumuiya ya ya Wasafirishaji bidhaa nchi za nje Khamis Issa amelalamika vitambulisho vya kusafirishia bidhaa vinavyotolewa na Taasisi zinazosimamia usalama wa Chakula  Zanzibar, ZBS na ZFDA havitambuliki Tanzania Bara kwa madai kuwa sio Taasisi za Muungano.

Amezishauri Taasisi za Tanzania Bara na Zanzibar zinazoshughulikia usalama wa bidhaa kukaa pamoja, kushirikiana na kuaminiana katika kujenga umoja na ushirikiano wa pande mbili za Muungano.

Mjasiriamali kutoka Jumuiya ya Wafanyabiashara Wanawake Zanzibar (ZWCC) Zeyana Ahmed Kassim amesema TBS imeandaa mazingira ya kuwasaidia Wajasiriamali wa Tanzania Bara lakini mpango huo haupo kwa Zanzibar. 

Amesema hali hiyo hupelekea baadhi ya wajasiriamali kutoka Zanzibar kuomba kujiunga na Shirika la Viwango Tanzania Bara ili kuepukana na usumbufu wakati wanaposafirisha bidhaa zao.

Amekumbusha kuwa tokea kuingia madarakani Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Hussein Ali Mwinyi amekuwa akisisitiza nia yake ya kusaidi sekta binafsi wakiwemo Wajasiriamali dhana ambayo inahitaji kuungwa mkono na wadau wote.

Awali akizungumza na Wajasiriamali hao, Mkurugenzi Idara ya Dawa na Vipodozi wa ZFDA Bora Lichanda aliwaeleza wajasiriamali walioshiriki mkutano huo kwamba lengo lao ni kuwaondoshea vikwazo wanavyokabiliana navyo katika kutekeleza shughuli zao

Ameahidi kuwa mapendekezo waliotowa kwenye kikao hicho  watayawasilisha kwa wenzao wa Tanzania Bara kabla ya mchakato wa kuingia makubaliano na TBS haujakamilika.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.