Habari za Punde

Wazee waheshimiwe wamefanya mengi kuleta maendeleo - Mabodi

 Na Mwashungi Tahir      Maelezo     9/01/2021.

Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi, Abdullah Juma Mabodi aliwataka wazee kuheshimiwa kwani wamefanya mambo  mengi katika Serikali ya Mapinduzi na kuleta maendeleo.

Aliyasema hayo huko Skuli ya Maandalizi iliyoko katika Jimbo la Magomeni wakati wa zoezi la kupima  afya kwa Baraza la  Wazee kwa lengo la kuboreshwa afya zao ikiwa ni miongoni mwa shamra shamra ya Mapinduzi matukufu ya  1964 kutimiza miaka 57.

Alisema Wazee ndio kila kitu katika jamii, familiya na wao wana mchango mkubwa waliofanya katika ujana wao wa kuiletea nchi maendeleo na kukuza uchumi kwa mambo mbalimbali.

Hivyo alisema hakuna budi kuwatizama na kuhakikisha wanapewa huduma zote zinaostahiki kama jamii ikiwemo kula, malazi bora, kivazi na kuwashughulikia  afya zao.

“Wazee ndio hazina yetu hatuna budi kuwatunza kwa kuwapatia mambo yote yanayostahiki kupatiwa kama walivyotuhudumia sisi”, alisema Naibu katibu mkuu huyo.

Pia alisema kutokana na umuhimu wao mkubwa Marehemu Mzee Abeid Amani Karume  baada ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar 1964 aliwawekea sehemu zao maalum kwa lengo la kupata hifadhi njema ili na wao wajisikie faraja ndani ya nyoyo zao.

Hata hivyo alisema Serikali ya Awamu ya nane ya Dkt Hussein Ali Mwinyi  ameahidi kuendeleza na  kuwaenzi wazee kama vile zilivyoendeleza awamu zote zilizopita kwani  wao ni ndio hazina kubwa nchini.

Mh Mabodi aliwashukuru viongozi wa Jimbo la Magomeni akiwemo Mbunge Mwanahamisi Kassim  na mwakilishi  Jamal Kassim kwa kuweka siku maalum ya kuwapima afya wazee hao ikiwa ni muendelezo waliojiwekea katika jimbo hilo.

Pia aliwataka na viongozi wa majimbo mengine kufuata utaratibu wa kuwawekea wazee kupima afya zao ili waweze kuendelea kuishi wakiwa na afya bora.

Nae Mbunge wa jimbo hilo Mwanakhamisi Kassim alisema wazee ni kiungo muhimu hivyo ni wajibu wetu kuwapima afya zao na kuwapatia matibabu sahihi ili wapate kuishi vizuri.

Akisoma risala ya Baraza la wazee katibu wa baraza hilo Maryam Haji Shehe  alisema wamekuwa na utaratibu wa kuwapima afya zao wazee wote waliofikia umri wa miaka 60 kila mwaka  bila kuwa na ubaguzi wa siasa, rangi wala dini.

Wakielezea changamoto zao wazee hao  wamewataka viongozi wao kuwapatia sehemu ya kudumu ili kuendesha shughuli zao za maisha ikiwemo na kupatiwa mtaji wa kujiendeleza ili waepukane na omba omba.

Zoezi hil limefanyika kwa kupimwa sukari, presha pamoja na huduma za meno.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.