Habari za Punde

Jamii Watakiwa Kuchungua Afya Zao Mara Kwa Mara Ili Kujiepusha na Maradhi Yasioambukiza.

Na Khadija Khamis –Maelezo  26\2\2021.

Jamii imetakiwa kujiwekea utamaduni wa kuchunguza afya mara kwa mara ili kujiepusha na maradhi yasioambukiza ikiwemo Saratani ya Matiti,Shingo ya Kizazi pamoja na Tenzi Dume .

Shauri hilo limetolewa na Meneja wa Kitengo cha Maradhi yasioambukiza cha Wizara ya Afya, Omar Abdalla Ali wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Jumuiya ya Watu Wanaoishi na Maradhi Yasiyoambukiza, Mpendae.

Amesema mwanzoni mwa mwezi wa pili kulifanyika zoezi la uchunguzi wa matiti kwa akinamama katika kisiwa cha Pemba hali imeonyesha baadhi ya akina mama wamepata saratani ya matiti bila ya kujijua.

Alisema Kutokana na hali hii ipo haja ya kujiwekea utaratibu wa kupima afya ili kugundua  maradhi  katika hatua ya awali na kupatiwa matibabu kwa haraka .

“Kwa vile dalili zake haziko wazi ni vyema wananchi kuondoa hofu na kuhudhuria katika vituo vya afya kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi” Alisema Meneja huyo.

Alifahamisha kuwa saratani tatu ikiwemo saratani ya matiti, shingo ya kizazi na tenzi dume ndizo zinazoongoza kwa vifo na watu huugua kwa wingi.

Aidha amesema saratani ya shingo ya kizazi huwapata wanawake wengi nchini kutokana na njia ya kujamiiana ambayo husababishwa na maambukizi ya kirusi kinachojulikana kama Human papilloma virus (HPV).

Meneja huyo alielezea vichocheo vinavyopelekea saratani ya shingo ya kizazi ikiwemo kuzaa watoto wengi,utumiaji wa sigara na tumbaku,kufanya tendo la kujamiina na wanaume tofauti,utaratibu mbaya wa kujisafisha sehemu za siri,kuweka kemikali sehemu za siri pamoja na kupata maradhi ya kujamiiana bila ya kutibiwa kikamilifu.

Alishauri ya kwamba iwapo jamii itachunguza saratani ya shingo ya kizazi mapema itasaidia kutibu haraka ugonjwa huo ili kuzuia vifo visivyotarajiwa.

Hata hivyo aliwataka kina baba hasa wale wenye umri wa miaka 40 na kuendelea kujitokeza kwa wingi kupima tenzi dume ili kuepukana na tatizo la mkojo.

Nae Meneja wa Jumuiya ya watu wanaoishi na maradhi yasiyoambukiza Haji Khamis Fundi ameishauri jamii kupima maradhi mbalimbali ili kujua mwenendo afya zao .


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.