Habari za Punde

Jamii yaaswa kuwa karibu na watoto wao kujua nyendo zao

 Na Mwashungi Tahir       Maelezo          23/2/2021.

JAMII imetakiwa  kuwa karibu na watoto wao katika kujua nyendo zao zote ikiwemo wakati wa kwenda skuli au madrasa ili kuepukana na vitendo vya udhalilishajiambavyo hivisasa vimeshamiri .

Ameyasema hayo Mkaguzi wa Polisi Makao Makuu ya polisi Zanzibar Dawati la Jinsia na watoto Mussa Khamis Abdullah huko kwenye  uwasilishaji wa ripoti ya udhalilishaji na kuiomba jamii kuwataka  vijana wenye umri wa miaka 15/17 kuacha ushawishi wa kujiingiza kwenye mahusiano ili kuweza kuepuka vitendo vya udhalilishaji.

Hivyo amesema jitihada zinahitajika zaidi kwa jamii  katika utoaji wa elimu kwa vijana ambao ni changamoto kutokana na umri wao kujiingiza katika mahusiano  hasa ukiangaliya hivi sasa Serikali inakemea vikali vitendo hivyo.

Jumla ya matukio 122 ya ukatili na udhalilishaji  wa kijinsia  yameripotiwa mwezi wa January 2021 ambao wengi wao walikuwa ni watoto ambao ni asilimia 83.6 na wanawake ni asilimia 16.4.

Ameyasema hayo Mtakwimu Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Kitengo cha Makosa ya Jinai, Madai na Jinsia Ramla Hassan Pandu wakati alipokuwa akiwasilisha kwa waandishi wa habari ripoti ya takwimu za ukatili na udhalilishaji kwa wanawake na watoto January 2021 huko katika ukumbi wa Mtakwimu Mkuu ulioko Mazizini Zanzibar.

Aidha amesema mlinganisho wa idadi wa matukio kwa mwezi uliopita umeongezeka kwa asilimia 20.8 kutoka matukio 101 kwa mwezi wa Desemba 2020 hadi 122mwezi wa January 2021.

Hivyo amesema Wilaya ya Magharibi “A “ imeripotiwa kuwa na matukio mengi ukilinganisha na wilaya nyengine  matukio 28, ikifuatiwa na Wilaya ya  Mjini matukio 18, na Wilaya ya Kusini ina idadi ndogo katika zote kwa matukio 3.

Ramla amesema kwa upande wa Kaskazini “A” ilikuwa na idadi kubwa ya matukio ya kubaka ukilinganisha na wilaya nyengine ambapo jumla ya matukio 12 asilimia 17.7ya matukio ya kubaka yameripotiwa, kwa wanawake jumla ya matukio 10 ya kubaka  , kwa wasichana ni matukio 51 sawa na asilimia 83.6.

Pia amesema matukio 116 yapo chini ya upelelezi wa Polisi na matukio 6 yapo katika hatua nyengine . matukio matano 5 yapo mahakamani  na tukio moja limefungwa na Polisi.

Amesema takwimu zinazohusu aina ya matukio ya ukatili na udhalilishaji wa kujinsia kwa wanawake na watoto yameanishwa katika matukio makuu sita ikiwemo kubaka, kulawiti, kuingiliwa kinyume cha maumbile, kutorosha , shambulio la aibu na shambulio.

Kwa upande wake Hakimu wa Mkoa na Mwenyekiti wa Mahkama ya Watoto Sabra Ali Mohammed  amewataka wazazi na walezi kuwa na tabia ya kuwafatiliya watoto katika nyendo zao ili suala hili la udhalilishaji liweze kumalizika na pia kuwataka wazazi kuacha muhali na kufika mahakamani kwa kutoa ushahidi pale linapotokea tukio.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.