Habari za Punde

Kamati ya Waandishi wa Habari Zanzibar Imeridhishwa na Uongozi wa Awamu ya Nane wa Dk, Hussein Ali Mwinyi.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla akizungumza na Kamati maalum ya waandishi wa habari Zanzibar iliongozwa na viongozi kutoka taasisi tofauti za Vyombo vya habari, walipofika Ofisini kwake kwa mazungumzo na kujitambulisha leo.
Kamati maalum ya waandishi wa habari iliongozwa na viongozi kutoka taasisi tofauti waliofika Afisini kwake Vuga jijini Zanzibar kwa ajili ya kujitambusha.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla akimsikiliza Mwenyekiti wa Kamati ya wanahabari Zanzibar Bw.Farouk Karim wakati wa mazungumzo yao yaliofanyika katika Ofisi yake Vuga Jijini Zanzibar leo walipofika kujitambulisha na kufanya mazungumzo. 
Afisa Uhusiano kutoka Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) Bw.Mussa Yussuf akitoa shukrani kwa niaba ya kamati hiyo baada ya kumaliza mazungumzo yao na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla yaliofanyika Ofisini kwake Vuga Jijini Zanzibar.


Na.Kassim Salum OMPR.

Serikali ya awamu ya nane inayoongozwa na Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi itaendelea kuthamini mchango mzuri unaotolewa na waandishi wa habari Zanzibar katika kuawahabarisha wananchi juu ya matukio mbali mbali yanayoendelea nchini.

Makamu wa Pili wa Rais Mhe. Hemed Suleiman Abdulla alieleza hayo wakati akizungmza na Kamati maalum ya waandishi wa habari iliongozwa na viongozi kutoka taasisi tofauti waliofika Afisini kwake Vuga jijini Zanzibar kwa ajili ya kujitambusha.

Alieleza kuwa, ndani ya kipindi cha siku mia moja (100) tangu serikali ya awamu ya nane iingie madarakani waandishi wa habari wamefanya kazi nzuri katika kuyatangaza masuala ya msingi yanayolenga kuimarisha ustawi wa wananchi wake.

Mhe. Hemed aliwaomba viongozi hao kutoka taasisi za habari nchini kuendelea kufanya kazi ya kuwapasha habari wananchi juu ya wajibu na majukumu yao katika kuisaidia serikali kutimiza azma yake ya kuleta maendeleo.

Alisema kutokana na mchango unaotolewa na wandishi wa habari katika kutoa taarifa zake kwa haraka imeibua shauku mara dufu kwa wananchi katika kufuatilia vyombo vya habari kwa lengo la kupata taarifa sahihi dhidi ya hatua zinazochukuliwa na serikali yao.

Akigusia suala la wafanyabishara Makamu wa Pili wa Rais aliwaomba waandishi kutumia kalamu zao vizuri katika kuwaelimisha wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla juu ya wajibu wao na umuhimu wa  kulipa kodi kwa maendeleo ya taifa.

Aliwaomba wafanyabiashara kuweka mbele uzalendo kwa kujali Afya za wananchi wa Zanzibar kwa kujenga utamaduni wa kuingiza bidhaa zenye ubora na kuepuka udanganyifu kwani serikali hatokuwa na muhali dhidi ya mfanyabiashara yoyote atakaekiuka miongozo iliowekwa na serikali.

“Hii Zanzibar sio Dump la kutupa bidhaa zilizopitwa na wakati, nawashauri sana ndugu zangu wafanyabiashara tutangulize mbele Afya za wazanzibar” Alisema Mhe. Hemed

Pamoja na mambo mengine Mhe. Hemed alisema kwa sasa serikali ipo katika mchakato wa kuzipitia sharia na kuzifanyia marekebisho ili kuweka wepesi wa utekelezaji wa azma ya serikali, hivyo amewashauri waandishi hao wasisite kuandika mapendekezo yao na kuyawasilisha kwa waziri mwenye dhamana ili ayawalishe serikali kwa ajili ya kufanyiwa marekebisho.

“Niwaombee ndugu zangu wandishi wa habari mutoe maoni yenu na muyawasilishe kwa waziri mwenye dhamana ili serikali iyafanyie marekebisho kupitia chombo chake cha kutunga sharia” Alieleza Mhe. Hemed

Vile vile, Makamu wa Pili wa Rais aliwataka wanahabari hao kuondoa hofu juu ya ahadi zote zilizotolewa na serikali ya awamu ya nane katika utekelezaji wa ahadi zake kutokana na nia njema iliyonayo katika kuwatumikia wananchi wake hasa katika kutatua changamoto zinazoikabili jamii akitolea mfano changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama, miundombinu ya barabara pamoja na huduma za Afya.

“Niwahakikishie Waandishi wa habari serikali hii ya awamu ya nane inayoongozwa na Rais Dk. Hussein Mwinyi itatimiza ahadi zake zote ilizoziahidi kipindi cha uchaguzi pamoja na ahadi nyenginezo” Alisisitiza Makamu wa Pili wa Rais.

Akizungumza kwa niaba ya wanakamati  Mwenyekiti wa Kamati ya wanahabari Zanzibar Farouk Karim alimueleza Makamu wa Pili wa Rais kwamba Waandishi wa habari Zanzibar wanafurahishwa na muelekeo wa serikali ya awamu ya nane ilioanza nao hasa katika muktadha mzima wa kurejesha nidhamu kwa watumishi wa serikali pamoja na watumishi katika sekta zinazojitegemea.

Bw. Farouk alisema ndani ya siku mia moja serikali imerudisha nidhamu kwa kusimamia vyema matumizi mazuri ya fedha pamoja na kuziba mianya iliokuwa ikitumiwa na watumishi wasiokuwa waaminifu.

Pia Mwenyekiti huyo alitumia fursa hiyo kumualika Makamu wa Pili wa Rais katika kongamano la wanahabari linatarajiwa kufanyika Machi 01, mwaka huu ambapo Rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa baraza la mapinduzi anatarajiwa kuwa mgeni rasmi likijumuisha na viongozi wengine waandamizi wa serikali.

Kwa upande wake Afisa Uhusiano kutoka Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) Mussa Yussuf akitoa shukrani kwa niaba ya kamati iliofika kujitambulisha kwa Makamu wa Pili wa Rais alimuomba Mhe. Makamu wa Pili kuwahimiza maafisa habari waliopo katika taasisi nyengine za serikali kutoa taarifa kwa wananchi kwa lengo la kujenga uwelewa juu ya masula muhimu yanayotekelezwa na serikali yao.

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.