Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Atembelea Shirika la Utangazaji Zanzibar ZBC na Gazeti la Zanzibar leo.

Mhariri Mtendaji wa Mashirika ya Serikali Nd. Yussu Khamis Yussuf akimpatia maelezo Mheshimiwa Hemed juu ya utendaji wa Chumba cya Habari cha  Gazeti la Zanzibar Leo hapo Kikwajuni.

Na.Othman Khamis.OMPR.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla alisema Vyombo vya Habari vya Serikali vinapaswa kurejea kwenye hadhi yake ya asili iliyozoeleka katika kupasha Habari sambamba na kutoa Taaluma ili iwafikie vyema Walengwa katika kiwango cha Kitaifa na Kimataifa.

Alisema mikakati imara katika suala zima la uzalishaji wa vipindi, Makala, Habari na hata matukio ya kila siku yaliyochangia vyombo hivyo kuwa na Wasikilizaji, Watazamaji na Wasomaji wengi kipindi hichi cha upangaji wa Safu ya Serikali ndio njia pekee ya kuitangaza Zanzibar kuwa kioo cha Dunia.

Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla alitoa kauli hiyo alipofanya ziara mahsusi ya kuangalia Uwajibikaji kwa Watendaji wa Shirika la Utangazaji Zanzibar {ZBC – TV} Karume Haouse, ZBC – Redio Rahaleo pamoja na Shirika la Magazeti ya Serikali liliopo Kikwajuni Mjini Zanzibar.

Alisema yapo mambo mengi mazuri yanayofanywa na Watendaji wa vyombo hivyo vya Habari vya Serikali yanayotokana na uchapakazi wao mahiri ambao Serikali Kuu inaridhika nao licha ya baadhi ya changanmoto zinazowakabili hasa sula zima la vifaa vinavyokwenda na wakati wa sasa.

Mheshimiwa Hemed Suleiman amewathibitishia Watendaji wa vyombo hivyo vya Habari ambavyo ndio mdomo wa Serikali kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko makini na tayari kuweka msukumo katika kuona uwajibikaji wao wa kila siku unapiga hatua kila wakati.

Hata hivyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliuagiza Uongozi wa Shirika la Utangazaji Zanzibar { ZBC - Redio na TV} pamoja ule wa Shirika la Magazeti ya Serikali kupitia Maafisa wao wa Utumishi na Wahasibu kuandaa utaratibu maalum wa kulipa maposho ya Watendaji wao hata kama yamekuwa na muda mrefu wa zaidi ya Miaka Miwili sasa.

Alisema haipendezi kuona baadhi ya Viongozi wanaosimamia maslahi ya Watendaji wao wamekuwa wazito na kutumia visingizio vingi katika ulipaji wa maslahi yao ikiwemo muda wa ziara wa saa za Kazi na hata zile stahiki zinazodaiwa na baadhi ya Watendaji waliopanda daraja baada ya kumaliza masomo ya muda mrefu.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliuagiza Uongozi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo kufuatilia masuala hayo licha ya Tume iliyoundwa na Wizara hiyo kuchunguza vianzio vya Mapato vya Shirika la Utangazaji Zanzibar.

Halkadhalika Mheshimiwa Hemed Suleiman pia aliutaka Uongozi huo kufuatilia Mikataba iliyopo baina ya Shirika la Utangazaji Zanzibar {ZBC} na Serikai ya Jamuhuri ya Watu wa China ya kulifanyia Matengenezo makubwa Jengo la Studio za Redio liliopo Rahaleo.

Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kamwe hairidhishwi na hali halisi iliyopo ndani ya jengo hilo ambayo haitoi taswira nzuri hasa Studio zake ambazo muda mwingi zimekuwa zikipokea Wageni mbali mbali wanaoshiriki kwenye Vipindi na matukio tofauti.

Akizungumzia Shirika la Magazeti ya Serikali Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman aliridhika na mfumo mzuri uliowekwa na Uongozi wa Shirika hilo katika kuwajengea mazingira ya Kitaaluma Wafanyakazi wake.

Hata hivyo Mheshimiwa Hemed aliutahadharisha Uongozi huo kuendelea kuwajengea mazingira mazuri ya Taaluma wale watendaji wao ambao kiwango chao cha Elimu bado kiko chini.

Alifahamisha kwamba Waandishi wa Habari wakiwa kioo cha jamii Mahali popote pale wanalazimika kubadilika kwa kujitambua umuhimu wao kwa wale wanaowahudumia katika kuwapasha Habari.

Mapema baadhi ya Wafanyazi wa Taasisi hizo za Habari za Redio, TV na Magazeti ya Serikali walimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar matatizo na changamoto wanazopambana nazo katika uwajibikaji wa majukumu yao ya kazi ya kila Siku.

Walisema miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na ucheleweshwaji wa maposho yao hasa katika muda wa ziada wa kazi na siku za mapumziko, vifaa vya kisasa vya Kazi zinavyokwenda na wakati wa sasa wa Teknolojia Ulimwenguni pamoja na fursa za Masomo zinazooana na Teknolojia hiyo.

Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Utangazaji Zanzibar {ZBC} ambae pia ni Mhariri Mtendaji wa Shirika la Magazeti ya Serikali  Ndugu Yussuf Khamis Yussuf akimuongoza Makamu wa Pili wa Rais wa ZanzibarMh. Hemed Suleiman Abdulla alipofanya ziara maalum kwenye vyombo vya Habari vya Serikali mapema asubuhi.

Makamu wa Pili wa Rais wa ZanzibarMh. Hemed Suleiman Abdulla akivitembelea baadhi ya vitengo vya Shirika la Magazeti ya Serikali Kikwajuni alipokuwa katika ziara ya Vyombo vya Habari vya Serikali.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdulla akiuagiuza Uongozi wa Vyombo vya  Habari vya Serikali kuhakikisha haki za Wafanyakazi wao hasa masuala ya maposho yanapatikana ili kuwarejeshea Imani watendaji wao.
Kaimu Fundi Mkuu wa Shuirika la Utangazaji Zanzibar {ZBC- Redio} Mhandisi Joseph Lazaro akimpatia maelezo Makamu wa Pili wa Rais wa ZanzibarMh. Hemed Suleiman Abdulla wakati akizikagua Studio za Redio Rahaleo Mjini Zanzibar.
Kaimu Mkurugenzi wa ZBC Nd. Yussuf Khamis Yussuf akimpatia maelezo Mheshimiwa Hemed juu ya mfumo mzima wa matangazo ya Shirika la Utama Utangazaji Zanzibar  katika studio za Televishini Karume House.
Baadhi ya Watendaji wa Studio za ZBC Televisheni wakiendelea na mtangazo yao walipokuwa hewani kwenye kipindi cha Ukweli si uvumi kilichopata umaarufu kwa watazamaji waliowengi.
Picha na – OMPR – ZNZ.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.