Habari za Punde

SMZ Imejipanga Kutekeleza Ahadi Zake Pamoja na Kutoa Huduma Kwa Jamii Wananchi Watakiwa Kuunga Mkono Jitihada Hizo

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla akitoa salamu kwa Waumini wa Dini ya Kiislamu wa Jambiani mara baada ya kumalizika kwa Ibada ya Sala ya Ijumaa.
Waumini wa Dini ya Kiislamu wa Kijiji cha Jambiani  Mbuyuni wakifuatilia Hotuba ya Sala ya Ijumaa iliyotolewa na Sheikh Ali Aboud hayupo pichani.
Baadhi ya Waumini wa Dini ya Kiislamu wakimsikiliza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alipokuwa akitoa salamu baada ya kumalizika kwa Ibada ya Sala ya Ijumaa.

Mheshimiwa Hemed akibadilishana mawazo na Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unaguja Mh. Rashid Adid Rashid na Mkuu wa Wilaia ya Kusini Nd. Rashid Shamsi.

Picha na – OMPR – ZNZ.

Na.Othman Khamis.OMPR.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla alisema wakati Serikali Kuu tayari imeshajipanga kutekeleza Ahadi zake pamoja na kutoka Huduma kwa Jamii, Wananchi wanalazimika kuunga mkono jitihada hizo zinazokusudiwa kufikia lengo.

Mheshimiwa Hemed Suleiman alitoa kauli hiyo wakati akisalimiana na Waumini wa Dini ya Kiislamu mara baada ya kukamilika kwa Ibada ya Sala ya Ijumaa iliyosaliwa katika Msikiti Mkuu wa  Kijiji cha Jambiani Mbuyuni Mkoa wa Kusini Unguja.

Alisema masuala ya Kisiasa wakati huu  yanakuwa ni maamuzi ya Mwanachama husika yakibakia katika moyo wake huku Taifa likijikita kuteremsha Maendeleo kupitia Miradi  mbali mbali ya Kiuchumi inayotiwa saini katika Utekelezaji wake utakaosaidia kutoa ajira kwa makundi mbali mbali ya Jamii Nchini.

Mheshimiwa Hemed Suleiman alieleza kwamba Zanzibar  ina uwezo wa kufanya makubwa kama baadhi ya Watendaji wa Taasisi za Umma wenye tabia ya udokozi wataachana na hulka hiyo mbaya ambayo Serikali imeshatoa indhari ya kutomruhusu Mtu kujinufaisha pekee katika misingi ya wizi na rushwa.

Alifahamisha kwamba hatua ya kuwadhibiti wabadhirifu lisitafsiriwe kisiasa kama baadhi ya Watu wanavyodai bali lieleweke kuwa ni uendeshaji wa mfumo Mmoja wa kuhudumia Wananchi wote bila ya ubaguzi wa aina yoyote.

Akigusia suala la udhalilishaji Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliendelea kuwakumbusha Wananchi kuacha ukimya wa kuliona suala la udhalilishaji  ni jambo la kawaida.

Alisema Kizazi Kipya ambacho ndicho kinachoonekana kukumbwa na kadhia hiyo kinahitaji kuandaliwa mazingira bora ya Ustawi wao utakaowajengea njia sahihi ya kuwa wasimamizi bora wa Taifa lao hapo baadae.

Mheshimiwa Hemed Suleiman alitanabaisha na kuonya kwamba tabia ya mfumo wa masuala hayo ya udhalilishaji kumalizwa Afisi ya Sheha au baadhi ya Vituo vya Polisi yakitangulizwa na Rushwa hayastahiki kupewa nafasi kipindi hichi.

Mapema akitoa  Hutba ya sala ya Ijumaa Imamu wa Msikiti wa Ijumaa wa Jambiani Mbuyuni Sheikh Ali Abou aliwakumbusha Wazazi na Walezi kuendelea kusimamia Malezi ya Watoto wao ili kujinusuru na siku nzito ya kujibu kile walichokichunga.

Sheikh Abou alisema Wazee na Walezi hao ni vyema wakajikita Zaidi katika kuwapatia Elimu Vijana wao itakayokuwa dira na mwanga wa kuwaonyesha njia ya kuepukana na majaribu mengi yaliyowazunguuka.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.