Habari za Punde

WHO yakabidhi dawa na vifaa vya Tiba Bohari Kuu ya Dawa Maruhubi

Mwakilishi Mkaazi wa WHO Zanzibar (wapili kulia) Dkt. Andemichael Ghirmany akimkabidhi Kaimu Waziri wa Afya Simai Muhammed Said msaada wa dawa pamoja na vifaa tiba katika Bohari Kuu ya Dawa Maruhubi Mjini Zanzibar.
Mwakilishi Mkaazi wa WHO Zanzibar Dkt. Andemichael Ghirmany  akitoa maelezo ya Shirika hilo katika hafla ya kukabidhi msaada wa dawa na vifaa tiba uliofanyika Bohari Kuu ya Dawa Maruhubi.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee Jinsia na Watoto Dkt. Omar Dadi Shajak akimkaribisha Kaimu Waziri wa Afya Zanzibar, ambae pia ni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Simai Muhammed Saida kuzungumza na wafanyakazi wa Bohari Kuu ya Dawa
Kaimu Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee Jinsia na Watoto Simai Muhammed Said akizungumza na wafanyakazi wa Bohari Kuu ya Dawa mara baada ya makabidhiano ya dawa pamoja na vifaa tiba Ofisi kwao Maruhubi Mjini Zanzibar.

Kaimu Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee Jinsia na Watoto ( katikati ) Simai Muhammed Saidaakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa bohari kuu ya dawa, viongozi wa Wizara na maafisa wa WHO.

Picha na Makame Mshenga.


Na Ramadhani Ali – Maelezo                          


Kaimu Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee Jinsia na Watoto Simai Mohammed Said amewasisitiza wananchi kuchukua tahadhari na kufuata masharti ya usafi ili kujikinga na maradhi ya kuambukiza.


Waziri Simai ambae pia ni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali alieleza hayo Bohari Kuu ya Dawa Maruhubi baada ya kupokea msaada wa dawa za kujikinga na maradhi ya kupumua na maradhi ya kuambukiza zilizotolewa na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 261.


Alisema kipindi hiki kumekuwepo na ongezeko la maradhi mengi ikiwemo tatizo la kupua, kuumwa na kifua, kichwa, mafua, kuharisha na Typhod hivyo kila mmoja anawajibu wa kujilinda na kujiepusha kuwaambukiza watu mwengine.


Alikumbusha umuhimu wa kunawa mikono mara kwa mara kuwa ni jambo la msingi na kujiepusha kuweka mikusanyiko hasa wakati wa kunagalia wagonjwa hospitali.


Aliwataka wafanyakazi wa Bohari Kuu ya Dawa na wafanyakazi wengine wanaoshughulikia usambazaji wa dawa kuwa waaminifu kwani kumejitokeza tuhuma baadhi ya dawa zinazoagiziwa na Serikali zinauzwa katika hospitali binafsi.


Aidha aliutaka uongozi wa Bohari Kuu ya Dwa kuandaa mfumo ulio uwazi zaidi wa kusambaza dawa katika hospitali mbali mbali ili kila hatua zinapopita hadi kufikia kwa mgonjwa zionekane ili kuondosha upoteaji wa dawa hizo.


Akikabidhi msaada huo, Mwakilishi Mkaazi wa WHO Zanzibar Dkt. Andemichael Ghirmany alisema Shirika hilo litaendelea kuunga mkono Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika juhudi zake za kuimarisha huduma za afya.


Alisema zaidi ya nchi 26 zikiwemo sita kutoka Afrika tayari zimetangaza kutokea kwa awamu ya pili maradhi ya Corona na sio nchi hizo pekee ambazo zina virusi vya maradhi hayo hivyo suala la tahadhari na kujiandaa ni jambo la msingi muhimu.

Aliishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa mashirikiano yake makubwa na Mashirika ya Umoja wa Mataifa hasa WHO katika kuimarisha kanuni za afya za kimataifa.


 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.