Habari za Punde

Kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Jijini Dodoma leo.

 

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Tanzania Bara Mhe Philiph Japhet Mangula akiongoza Kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kilichofanyika katika ukumbi wa Jakaya Kikwete Dodoma leo 30-3-2021, (kulia kwake) Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa  ambae pia ni Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa ambae pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi


KAMATI Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) leo imekaa Jijini Dodoma chini Makamo Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Philip Mangula ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan alihudhuria.

                                    

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ambae ni mjumbe alihudhuria katika kikao hicho pamoja na viongozi wengine akiwemo  Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein na viongozi wengine wa CCM kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.

Katika kikao hicho ambacho Rais wa Jamhuri ya Muunganao wa Tanzania Samia Suluhu Hassan alitumia fursa hiyo kuwasilisha mapendekezo ya jina la Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mteule Dk. Philip Isdor Mpango ambalo baadae lilipelekwa Bungeni kwa ajili ya kwenda kupata baraka za Muhimili huo kwa kuthibitishwa.

Katika hatua za Bunge hilo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Philip Isdor Mpango jina lake liliwasilishwa Bungeni na kupitishwa kwa kupigiwa kura 363  sawa na asilimia 100 za kura zote zilizopigwa.

Baada ya kuokea jina la Dkt. Philip Mpango, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano Job Yustino Ndugai  alilitangazia Bunge jina hilo lililopendekezwa na Rais Samia ambapo mara baada ya tangazo hilo furaha akubwa ailitawala ndani ya Bunge hilo.

Dk. Mpango alipata fursa ya kuzungumza Bungeni hapo mara baada ya jina lake kutangazwa Bungeni alisema kwamba hakutarajia kupata nafasi hiyo kuhu akiahidi kumsaidia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha Tanzania inapiga hatua kimaendeleo sambamba na kupambana na umasikini.

Dk. Mpango alitumia fursa hiyo kumshukuru Rais Samia kwa kuliteua jina lake pamoja na kukishukuru chama chake cha CCM kwa kuridhi jina hilo huku akiwashukuru Wabunge wenziwe ambao wamefanya kazi muda wote wakiongozwa na  Spika Job Yustino Ndugai pamoja na Naibu Spika wa Bunge hilo Dk. Tulia Ackson.

Kabla ya kushika nafasi hiyo ya Makamu wa Rais Dk. Mpango alikwua Waziri wa Fedha na Mipango kwa kipindi cha miaka sita na pia Mbunge wa Jimbo la Buhingwe, Mkoani Kigoma  kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Dk. Mpango amepata nafasi hiyo baada ya aliyekuwa Makamu wa Rais wakati wa uongozi wa Hayati Rais Magufuli Samia Suluhu Hassan kuapishwa kuwa Rais wa  Tanzania kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa  Awamu ya Tano Hayati John Pombe Magufuli na hivyo nafasi ya Makamu wa Rais kuwa wazi.

Makamu wa Rais Mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Philip Mpango anatarajiwa kuapishwa kesho (Machi 31. 2021), hafla ambayo itafanyika kuanzia Alaasiri huko Ikulu ya Chamwino Dodoma.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.