Habari za Punde

Warsha ya siku mbili kuwasilisha mawanda na mtiririko wa mtaala wa msingi juu na msingi chini yafanyika Ukumbi wa Taasisi ya Utalii Zanzibar

 Na Maulid Yussuf WEMA

Walimu wa masomo mbalimbali nchini wameishauri Taasisi ya Elimu Zanzibar kuyafanyia kazi Yale yote waliyochangia katika kutengeneza mtaala ulio bora  ili Taifa lipate wataalamu wake nchini.

Wakitoa maoni yao wakati wa warsha ya siku mbili ya kuwasilisha mawanda na mtiririko wa mtaala wa msingi juu na msingi chini katika ukumbi wa Taasisi ya Utalii Maruhubi Unguja miongoni mwa Washiriki hao mwalimu Kinaa Ussi Juma amesema  wamefarijika  kuona katika mtaala huo mpya  kuingizwa maada ya udhalilishaji katika kila somo ili watoto wapate kujifunza vizuri kwani wao ndio wahanga wakuu wa janga hilo.

Aidha wameiomba Taasisi ya Elimu wanapotoa Mafunzo wasitoe kwa walimu wa skuli pekee bali pia watoe na kwa walimu wa Madrasa  ili nao waweze kuwafudisha vizuri  watoto.

Hata hivyo wameishukuru Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar kupitia Taasisi ya elimu, kwa kuandaa warsha hiyo iliyowawezesha kutoa maoni yao uandaaji wa mtaala wa elimu ya maandalizi na msingi.

Pia amewashauri washiriki wenzao kuanza kuyafanyia kazi Yale yote waliyopewa katika warsha hiyo kabla mtaala huo mpya kuanza kufanya kazi.

Nae kaimu Mkuu wa divisheni ya Elimu ya Maandalizi na msingi Bi Patima Kheir Koba amewaomba walimu hao kuyachukua Yale yote waliyoifunza na kuwaelimisha wenzao pamoja na kuyazingatia kwa kuyafanyia kazi watakapo kwenda katika Skuli zao.


Pia Amewaomba wanapokua na mawazo mengine wasisite kuyafikisha katika Taasisi yao ili yaweze kufanyiwa kazi.

Aidha amewashukuru walimu hao kwa kukubali kuacha kazi zo na kufika kushiriki katika kazi hiyo yakitaifa ambayo ndio nguzo muhimu katika kuwatengenezea  mustakbali mzuri watoto wao.

Akighairisha Warsha hiyo, Meneja wa Mtaala na Vifaa kutoka Taasisi ya Elimu Zanzibar mwalimu Abdullah  Mohammed Mussa amesema hatua za utayarishaji bora wa mtaala ndio huo kwani mtaala shirikishi ndio unaokuwa bora zaidi.

Amesema katika kila hatua lazima washirikishwe wadau husika wa mtaala wa elimu wakiwemo walimu hao ili kuleta mafanikio katika mtaala huo, hivyo amewaomba kutosita kutoa maoni yao ili kuweza kufikia malengo.

Amesema uandaaji wa mtaala sio jambo jepesi, na kuwataka walimu hao kutambua kuwa bado wana kazi kubwa sana katika kufikia malengo ya kitaifa.


Amesema rasimu ya mtaala iliyopitiwa nwaka Jana mwezi wa nne na Rais aliemaliza muda wake, alishauri kuingizwa somo la historia ya Tanzania ili kuwasaidia wanafunzi kuijua historia ya nchi yao.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.