Habari za Punde

Wasimamizi wa Uchanguzi Mdogo wa Jimbo la Pandani Pemba na Wadi ya Kinuni Unguja Wapatiwa Mafunzo.

Msimamizi wa Uchaguzi Wilaya ya Kaskazini "B" Bakari Burhani Suleiman akiwasilisha mada katika mafunzo ya Watendaji wa Vituo vya Kupigia Kura uchaguzi Mdogo Wadi ya Kinuni wa tarehe 28 Machi, 2021 yalifanyika Skuli ya Sekondari ya Abeid Amani Karume Kinuni tarehe 25 Machi, 2021.


Na Jaala Makame Haji - ZEC

Watendaji wa Vituo vya Kupiga Kura Uchaguzi Mdogo Jimbo la Pandani na Wadi ya Kinuni wametakiwa kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu muda wote wanapokuwa katika vituo vya kupigia Kura.

Kaimu Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ZEC Ndg.Saadun Ahmed Khamis alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na watendaji wa Uchaguzi katika mafunzo ya uendeshaji wa Uchaguzi huo wa Wadi ya Kinuni yaliyofanyika katika Skuli ya Sekondari ya Abeid Amani Karume Kinuni

Ndg.Saaduni aliwaeleza watendaji hao kuwa Tume kupitia wasimamizi wa Majimbo inategemea kutoa matokeo ya Uchaguzi ndani ya wakati kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar kama ilivyokuwa katika Uchaguzi Mkuu 2020 hivyo ni vyema kuwa makini katika uendeshaji wa Uchaguzi Vituoni.

Mapema akifungua mafunzo kwa watendaji hao Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Pangawe Ndg.Suluh Ali Rashid aliwasisitiza watendaji hao kufuata taratibu na sheria za uendeshaji wa Uchaguzi wakati wanapokuwa katika vituo vya kupigia kura ili kuufanya Uchaguzi huo uwe wa kidemokrasia.

Ndg.Suluhu alisema ,watendaji hao wanapaswa kuzingatia kuwa, Sheria na taratibu za kuendesha Uchaguzi Mkuu hazitofautiani na taratibu za Uchaguzi Mdogo, hivyo ni vyema kutoa huduma sawa kwa Wapiga Kura wanapofika vituoni

Akiwasilisha mada katika Mafunzo hayo Msimamizi wa Uchaguzi Wilaya ya Kaskazini “B” Ndg.Bakari Burhani Suleiman alifahamisha kuwa ,Watendaji wa Vituo wahakikishe kuwa zoezi la kupiga na kuhesabu kura linafanyika kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na miongozo ya Tume.

Bw.Bakari Burhani alielekeza kuwa ni vyema Watendaji wa vituo kushirikiana pamoja katika utekelezaji wa majukumu yao na kupelekea uchaguzi mdogo kumalizika katika hali ya Amani na utulivu kama ilivyokuwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Aidha, Bwana Bakari aliongeza kusema, Wapiga Kura watu wenye ulemavu, wajawazito, Wazee na wanawake wanaonyonyesha wanatakiwa kuingia moja kwa moja katika kituo cha kupigia kura bila kupanga foleni mara wanapofika katika eneo la kupiga kura.

Naye Mohamed Said Mohamed mshiriki wa mafunzo hayo aliishukuru Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kutekeleza matakwa ya Sheria kwa kuitisha Uchaguzi Mdogo wa Jimbo la Pandani na Wadi ya Kinuni ambapo aliahidi kutumia mafunzo waliyopatiwa na Tume kuhakikisha kila mmoja anatumia haki yake kwa kumchagua kiongozi anayemtaka.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.