Habari za Punde

Uwekezaji wa Bilioni 624 Uliofanywa na Grumet Reserve (T) Ltd Unatija - WASEMA TIC

Na Dixon Busagaga,Arusha

 KITUO cha Uwekezaji nchini (TIC) kimeeleza kuridhishwa na uwekezaji uliofanywa na kampuni ya Grumet Reserve (T) Ltd ya jijini Arusha ,uwekezaji ambao unatajwa kuwa zaidi ya Bilioni 624 huku ikiwa miongoni mwa mwekezaji mahiri nchini .

 Mbali na uwekezaji uliofanywa na kampuni ya Grumet Reserve Ltd kupitia Hoteli za kitalii zilizopo katika Hifadhi za taifa kwa ajili ya kuhudumia wageni mashuhuri  na wenye hadhi duniani,kampuni hiyo pia imeendelea kukua na sasa imeanzisha huduma za usafiri wa anga kupitia Grumet Air.

Maafisa kutoka kituo cha uwekezaji (TIC ) makao makuu wametembelea ofisi za kampuni ya Grumet Reserve (T)  Ltd na kufanya mazungumzo na Meneja uendeshaji wa kampuni hiyo Mark Rashid ikiwa ni sehemu kazi ya kituo hicho kuhamasisha na kusaidia wawekezaji wa kigeni na watanzania waweze kutumia fursa zilizopo nchini.

Akizungumzia ziara hiyo Afisa Mhamasishaji Mwandamizi wa kituo cha uwekezaji (TIC) ,Innocent Kahwa amesema katika kitimiza majukumu ya kituo cha uwekezeji wameanza kutembelea miradi ambayo inajulikana kama miradi mahiri ambayo imekuwa ikisajiliwa na kituo hicho.

“Huu mradi unajulikana kama Grumet Reserves Ldt, ni mradi ambao unaendesha lodge ya kitalii uwekezaji wake ukiuweka kwenye fedha za kitanzania thamani yake ni sawa na Billion 624,kwa hiyo kuanzia 2005 mpaka sasa hivi tunaweza kuona ni kiasi gani ambacho kimeweza kuwekezwa na mwekezaji mmoja mahiri ambaye amewekeza hapa nchini.” Alisema Kahwa

“Huyu mwekezaji ni mahiri na anahudumia wateja watalii wakubwa wenye hadhi duniani, unajua katika sekta ya utalii watalii  wamegawanyika wapo wa kiwango cha kawaida, watalii wa kiwango cha kati na watalii wenye kiwango cha juu, kwa hiyo huyu mwekezaji wetu anahudumia watalii wa kiwango cha juu duniani sio kiwango cha juu kwa Tanzania "No" Ni kiwango cha juu duniani” aliongeza Kahwa.


Kahwa alisema kutokana na kutambua ubora wa huduma ambazo zimekuwa zikitolewa na hoteli zilizopo chini ya Grumet Reserve Ltd,kampuni hiyo imekuwa ikipokea tuzo mbalimbali duniani ambazo kwa kiasi kikubwa imekuwa ikiitangaza Tanzania .

 “Kwa mfano mwaka 2011, mwaka 2012, mwaka 2015 na mwaka 2016 iliweza kutambulika kama Hoteli namba moja duniani, na vilevile mwaka 2016 na mwaka huu imeweza kujulikana kuwa ni lodge ya safari namba moja  bora kwa Africa.”alisema Kahwa. 


“Kwa hiyo hii hoteli ni mradi ambao unaotambulika kwa duniani. Yaweza ikawa hapa Tanzania mradi huu watu hawaujui lakini duniani huu umetupa sifa kama nchi.” Aliongeza Kahwa .

Alisema mradi huo umeweza kutoa ajira ya  watu 800 ambao wamekuwa wakifanya shughuli mbalimbali katika kampuni hiyo huku ukilipa kodi na tozo mbalimbali za serikali ambapo tangu kuanza kwake wameweza kulipa kodi Dola Mil 34.1.

Kahwa alisema wakati kampuni hiyo inaanza ilianza na  vitanda 12 katika hoteli yake ambapo kwa sasa vimefikia vitanda 124 na kwamba imekuwa ikijihusisha na uhifadhi ambapo tayari wameingiza wanyama 32 aina Faru  weusi ambao ni kivutio  kikubwa kwa watalii .

“Tunazidi kuhimiza na kushawishi wawekezaji wa aina hii waweze kuwa wengi zaidi kwa sababu wanaongeza pato la kigeni kwa nchi ,wanaongeza mapato,wanatoa ajira na kuitangaza nchi yetu duniani”.alisema Kahwa.

Ziara ya maofisa kutoka kituo cha uwekezaji (TIC) makao makuu imehusisha pia Mwanasheria mwanadamizi wa kituo cha uwekezaji (TIC) Alex Mnyani na Afisa uhamasishaji uwekezaji ,Linda Loom wote kutoka makao makuu ya TIC .

Mradi wa kampuni ya Grumet Reserve (T) Ltd ulisajiliwa kituo cha uwekezaji (TIC)  mwaka 2005,wakati huo ukiwa na thamani ya Dola Milioni 18 na sasa umefikia thamani ya Dola za kimarekani Mil 343 baada ya kufanya vizuri.

 Mwisho .

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.